Hii ndo Hasara ya Mfumo Mbaya wa Elimu

Mikael Aweda

JF-Expert Member
Dec 17, 2010
2,973
3,901
JE WAJUA? UBOVU WA MFUMO WA ELIMU UMECHANGIA UMASKINI WAKO

Mfumo wa elimu Africa na *chui wa makatasi* ( sehemu ya 1)

Na Mikael Aweda

Naanza kwa kuuliza swali la kushtua kidogo. Je, wajua kuwa mfumo wa shule zetu nyingi Afrika unachangia wewe kuwa maskini?? Bila shaka hilo hi swali la kushtua kwako na kwangu.

Leo tutajadili jambo la tatu kwenye utafiti uliofanywa na Umoja wa mataifa Kitengo Cha Maendeleo na Ujasriamali/Biashara (UNCTAD) wakishirikiana na Chuo kikuu maarufu cha Harvard.
Na nifafanue mwanzoni kabisa kwamba elimu na mfumo wa elimu si kitu kimoja, ni vitu viwili tofauti. Mfumo unaweza kuwa mzuri au mbaya.

Kama tulivyojadili kwenye makala za nyuma, kinachotofautisha maskini na tajiri ni TABIA na siyo dini yake, rangi au nchi wanazotoka. Tofauti kati ya nchi tajiri na Masikini Ni idadi ya matajiri na masikini tu, kwa sababu nchi zote zina masikini na matajiri.

Na TABIA ya tatu (siyo kwa umuhimu) iliyogunduliwa kwenye utafiti huo ni UJASIRI NA KUJIAMINI( Self Confidence). Hii ina maana kuwa ujasri au kujiamini kunachangia kufanikiwa kwetu na kinyume chake woga unaleta umaskini.

Ujasiri ni nini?

Kwa mujibu wa utafiti ule mjasriamali ni yule anayeweza kujiamini na kufanya kitu anachotaka kufanya bila kuyumbishwa na mtu yeyote kimtazamo kiasi cha kuweza hata kutofautiana na desturi au mazoea ya jamii yake ya karibu kama wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wanaompinga.

Ni yule aliyeachana na dhana feki ya ' WENGINE WATANISEMAJE'. Hivyo basi mjasiriamali ni yule anayesikliza dhamiri yake na siyo anayesikiliza watu wanaomzunguka.

Sasa turudi kwenye kichwa cha somo letu la leo. Je, shule zetu kwenye nchi za Afrika wanatujengea ujasiri na kujiamini?? Jibu ni hapana.

Shule nyingi za Ki-Afrika wanamwondolea mtoto ujasiri kwa njia ya adhabu anazopewa mtoto. Mwanafunzi akikosea anachapwa. Kila kosa na adhabu yake. Kuanzia asubuhi akifika shuleni mpaka jioni mwanafunzi anakua na shughuli za kimasomo. Akikosea maagizo viboko vinamhusu na mara nyingi hakuna majadiliano. Ukichelewa Shule kiboko. Usipotimiza matarajio ya mwalimu—viboko!
Mara nyingi hakuna uhusiano wa kirafiki kati ya walimu na wanafunzi. Ni kama askari na mtuhumiwa.

Kupitia simulizi hii labda inawezasaidia wengi kuelewa zaidi athari za viboko kwenye harakati za elimu. Kuna binti moja aliyekuwa anachelewa shule Kila siku na kila mwalimu wa zamu alimchapa viboko. Mpaka kila mtu akazoea hivyo. Baada ya miaka 3 mwalimu moja akamwuliza. Kwanini unachelewa? Binti akajibu, “ nyumbani mimi ndiye nimekua mama na baba kwa wadogo zangu. Ndio maana tangu mama alipofariki nikaanza kuchelewa kwa sababu nimeachiwa wadogo zangu peke yangu na niko mbali” Walimu Walijua tatizo wakati wameshasababisha majeraha nafsini mwake.



Lengo la makala haya siyo kufuta adhabu ya Viboko la hasha lakini viboko vya aina gani au kwa namna gani? Na kwa lengo gani? Ukimchapa mtoto baada ya kumwelimisha kosa lake na kumpa nafasi ya kujitetea hakumwondolei kujiamini.
Lakini Kumchapa binti aliyefiwa na wazazi na hana namna ya kijetetea ni kumwumiza kisaikolojia. Wangapi leo wameumizwa kama huyo binti? Mara ngapi mwanafunzi anachapwa bila sababu ya maana?
Mtoto akichapwa bila sababu na bila fursa ya kujitetea unamwumiza unamwondolea kujiamini. Anajaa woga. Anaona duniani hana haki. Anakosa ujasri na kujiamini.



Kwenye Mifumo yetu ya elimu mtoto akifeli somo fulani anachapwa. Hawamwulizi kwanini umefeli? Labda anaumwa au baba na mama wameachana? Labda anaishi kwa ndugu ambako anateseka. Siyo wajibu wa mwalimu? Kazi ya mwalimu ni kuhakikisha unafaulu tu?! Juhudi hizi za kusaka ‘A’ zinaishia kumchosha mtoto na anaishia kuichukia shule. Akichukia shule atanyooshwa kwa viboko mpaka apate ‘A’.

Nimebahatika kuwa nwenyekiti wa shule moja binafsi, na pia mkiti wa shule moja ya serikali kwa takriban miaka minne. Mbinyo ni ule ule, birika tu ndio tofauti.
Kwa uzoefu wangu shule binafsi ndo wanatumia nguvu kubwa kupata ‘A’ kuliko shule za Serikali. Lakini wote ( shule binafsi na za Serikali) kwenye Kila nchi wanataka watoto wapate ‘A’ lakini hawajatathmini faida ya ‘A’ kwa watoto wao na gharama ya hiyo ‘A’ hawaijui. Wangejua gharama yake wangefikiri mara mbili. Nina imani makala haya na nyingine zijazo zitasaidia kuwafungua macho.

Kwenye shule binafsi ‘A’ zinanunuliwa na mwenye shule. Kwa hiyo, Mwalimu anagawa viboko vya kutosha ili apate ‘A’ nyingi na mwisho wa mwaka Christmas yake iwe njema. Watoto wanaumia. Lengo siyo mtoto ni pesa. TAJIRI mwenye shule binafsi anataka ‘A’ nyingi ili shule ipate wanafunzi wengi au aongeze ada, atatue matatizo yake.
Lengo siyo wanao. Lengo Ni biashara. Mtoto anasoma siku saba za wiki na wakati mwingine wanawekwa bweni ili wasome usiku na mchana. Huku wazazi wanakamuliwa fedha za kutosha nao wanajisifia mtoto wao anasoma International. Hawajui gharama. Tunatengeneza Chui wa makaratasi.

Kwenye shule za serikali zetu kila mkuu wa shule, maafisa wilaya mikoa, kanda (inategemea mfumo wa nchi husika) wanataka ‘A’ ili wasifiwe na wakubwa zao, ili wapande vyeo au waongezewe mishahara. Kadhalika, lengo siyo mwanao. Ni vyeo na mishahara iliyonona.

Mwishowe yule mtoto anapata ‘A’. Walimu na mtoto wanashangilia, wazazi wanacheka na jamii inamsifia yule mtoto. Wote tunashangilia tuna chui kumbe chuki wa makaratasi. Tunajitekenya wenyewe na kujichekesha wenyewe kwa hasara yetu. Nitatoa mfano hivi punde.

Kwenye jamii yetu mkoani Manyara siku za nyuma kidogo wakati wa masika nyani walikua wakitusumbua sana kwa kula mazao shambani. Tulilazimika kulinda usiku na mchana. Baadaye watu wakagundua dawa. Wanatengeneza mfano wa mtu na kumpachikia fimbo begani. Usiku kucha nyani hawaendi shambani kwa kuwa kulikua na mlinzi. Kile kinyago au kikaragosi.


Ujanja huu ukitusaidia kwa muda Sana. Baadaye nyani wakawa wajanja. Wakatofautisha kinyago au kikaragosi cha mtu na mtu halisi. Matatizo ya kulinda usiku na mchana yakarudi pale pale.
Kwa maoni yangu, muda wa kuachana na ‘A’ feki umefika. Mabadilko ya dunia yanatuumbua. Ni muda wa kutafuta ‘A’ halisi. Tuboreshe mitaala yetu. Tusiendelee kujitekenya na kujichekesha kwa kusaka ‘A’ feki isiyo na tija.
Leo hii mashirika mengi ya kimataifa hayaangalii vyeti vyako ofisini. Wanaangalia ufanisi wako. Ndio maana siku hizi mwenye shahada mbili anaweza kuwa chini ya mwenye shahada moja.

Tukumbuke kuwa ‘A’ ya darasani inayopatikana kwa gharama kumwumiza mtoto kisaikolojia kwa kumjazia vitu vya kukariri kichwani bila kumjengea ujasri inatufaa nini?
Nani atakwajiri mwanao aliyechapwa viboko vya kutosha ili kumlazimisha kupata ‘A’. Leo amehitimu na ‘A’ chuo kikuu, lakini bosi hawezi kumtuma kwenye kikao kwa sababu hawezi kusimamia mbele za watu?

Nchi inayoongoza kwa elimu bora duniani ya Finland hawana mtihani kwenye shule ya msingi. Mtihani wa kwanza wa kitaifa atakutana nao secondary. Shtuka!

‘A’ nayopatikana kwa mtoto kusoma saa moja asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni na Jumamosi na jumapili lazima asome, ni tatizo. Mtoto anatakiwa muda wa kucheza na kupumzika. Akikosa hivyo vitu kuna vitu amekosa kwenye ukuaji wake. ‘A’ ya darasani haiwezi kufidia vitu hivyo. Mtoto anahitaji kupumzika.

Kwa maoni yangu, ‘A’ ya darasani peke haitoshi. Nyani wameshagundua kikaragosi cha wana--Manyara. Dunia imebadikika. Haitaki ‘A’ za kwenye karasi.

Ukisoma vitabu vya watu walileta mabadilko kwenye dunia hii ni watu wenye ujasiri, siyo waoga.



Mtoto akiondolewa ujasri shuleni anakuwa mwoga wa maisha. Hafanyi kitu cha maana kusaidia familia yake au nchi yake.Anaogopa kukosea.

Matokeo ya mfumo huu sasa tuna watu wazima waliopata 'A' darasani lakini hawezi kumwambia bosi wake hii siyo sawa. Anaogopa, kwa kuwa Ana F ya Somo la ujasri ambalo halipo shuleni.


Tuna wasomi wenye ‘A’ hesabu na Kiingereza ambao hawana ujasri wa kumwambia mwenye-kiti wa serikali ya Mtaa au Kijiji chake kuwa umeiba pesa yetu. Hawajiamini. Wana F ya Ujasri.


Fikiri mtu mzima aliyenyanganywa ujasri shuleni anapata wazo zuri sana la kibiashara na wazo lenyewe geni na kila anayemwambia anamkatisha tamaa kuwa hakifai. Kuanzia wazazi, majirani mpaka marafiki wote. Yeye mwenyewe hana ujasri wanaomzunguka nao wanazidi kukamtisha tama. Matokeo yake analiacha wazo lake na mzunguko wa umaskini unaendelea. Nani anataka ‘A’ inayolea umaskini kwa kuzalisha wasomi wasio na UJASIRI?


Ikumbukwe kuwa kufanikiwa kiujasiriamali maana yake ni kuanguka mara nyingi au kushindwa mara nyingi na kuanza upya na bila kukata tamaa. kuanguka ni sehemu ya mafanikio. Ni hatua moja kwenda mbele. Ni kujifunza.
Kumbuka methali hii ' mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. unavyomjaza mtoto woga ndivyo anavyokuwa mtu mzima mwenye woga wa kila kitu. Mwimbaji moja alisema “woga wako ndio Umaskini wako”. watu waoga ni mzigo kwa nchi yao. Hawana mchango kiuchumi.’ A’ isiyochangia ukuaji wa uchumi nani anaitaka???

Kwenye changamoto hii, hatuwalaumu walimu kwa sababu wao ni zao la mfumo huu. Wanatoa walicho nacho. Kipofu kamwe hawezi kumwongoza kipofu mwenzake. Wanatumbukia shimoni.



Kwa mujibu wa utafiti tajwa hapo juu uliofanywa na Umoja wa Mataifa, Ujasiri na KUJIAMINI ni kati ya TABIA kumi inayotofautisha maskini na tajiri.



Nihitimishe kwa kutoa home work ( kazi ya nyumbani) kwa kila msomaji wetu.
Mosi, nenda ukajitathmini mwenyewe ili ujijue kama wewe ni mwoga au jasiri. Ukishajijua ni mwoga,chukue hatua stahiki.


Soma vitabu vya kuondoa hali hiyo au ingia YouTube, tafuta video zenye masomo yenye mada hiyo.

Pili, fuatilia maendeleo ya ukuaji wa mwanao kimaisha kwa ujumla . siyo zile ‘A’ za shuleni tu. Fanya hivyo hata kama anasoma 'INTERNATIONAL'. Majuto ni mjukuu. Miaka ya chui wa makaratasi imeisha.

Tatu, niwakumbushe walimu, wazazi na na wadau wa elimu kwa ujumla, kuwa ‘A’ ya darasani bila ‘A’ kwenye maisha ya kawaida ni hasara kwa serikali, wazazi, na watoto wenyewe.
Tuwajaze watoto wetu ujasri ili wakafanikiwe kimaisha wao wenyewe na kisha wakawe msaada kwa wazazi na taifa kwa ujumla.

Mikael Aweda
Mobile: 0785 583 330
Email: mpaweda@gmail.com
Facebook: Mikael Aweda
 
Shule ni full walimu kutishia wanafunzi. Kama wamelazimishwa.
Huu mfumo wauondoe.
 
Back
Top Bottom