Pole kwa changamoto hizo,lakini hayo ndio maisha na hapo ndipo pa kujifunza, wewe bado kijana, tena wa kiume, komaa tu, yote hayo yanapita na yatakuwa historia. Ushauri wangu;
1) Mkabili tena huyo ndugu yako, kwa heshima na unyenyekevu (kwa mara ya mwisho) mwambie kwamba una hali ngumu na una uhitaji sana wa fedha zakom, hivyo ni muhimu sana kwa sasa akupatie haki yako, akikupatia ni vema, lakini akigoma, basi achana naye, usisimamie tena biashara yake na umwambie ukweli kwamba hutaweza kuendelea kusimamia biashara yake wakati maisha yako yanakuwa magumu kila siku, na kwamba yote unamwachie Mungu. Usimtukane wala usimuambie maneno yoyote makali au mabaya. Usihangaike na kumshitaki popote, wala usifungue kesi ya madai, haitakusaidia na utapoteza muda na hutalipwa chako, wewe mshitakie Mungu, kisha endelea na maisha yako. Kwa maneno mengine ni kwamba, amekupa au hajakupa fedha zako, umeshajifunza vya hivyo, achana naye sasa!
2) Kuhusu kuoa - usikimbilie kuoa au kutaka na kuishi na mwanamke wakati maisha yako hayako sawa, kuwa mkweli kwa nafsi yako, kwamba unahitaji kujipanga upya. Kuna raha gani kuishi na mtu kwenye mazingira ya matatizo? Tena sio mkeo? Muambie ukweli huyo mwanamke wako kwamba, kwa sasa maisha/mambo yako hayako sawa na hutaki yeye aendelee kupata shida akiwa na wewe, wakati anaweza kuishi maisha bora huko nje. Mpe uhuru wa yeye kuondoka, kuendelea na maisha yake ili wewe ujipange na maisha yako. Akiamua kubaki ili mle vumbi wote pamoja, poa, maana hayo ndio mapenzi, lakini huo utakuwa uamuzi wake na utakuweka wewe huru ukiwa na amani. Ila ukila bingo na mambo yako yakinyooka huko mbeleni (Nina hakika yatakunyookea) utambue kwamba uda deni kwa huyo mwanamke - usije kujifanya mjanja, kumsaliti na mambo kama hayo.
3) Tatizo ni wewe, inabidi ubadilike hasa unavyotazama mambo na kuwalaumu wengine kwa makosa yako mwenyewe, kwa maamuzi mabovu uliyoyafanya mwenywe siku za nyuma. Kwanini uliacha kazi yako mwenyewe ya kufundisha na kuja kusimamia shughuli ya ndugu yako? Maana yake ni kwamba uliacha kujitegemea mwenyewe na ukarudi kumtegemea mtu mwingine (Kosa kubwa!), yaani maisha/hatima yako yote ulimuachia mtu mwingine na yeye hana sababu ya kuangalia maisha yako, anayepaswa kuangalia maisha yako ni wewe na sio yeye. Kwa mfano, ungebaki na kazi yako ya kufundisha na ukaendelea na biashara yako, leo ungekuwa wapi? Bila shaka mbali sana! Kwa mtazamo wangu ni kwamba huyo ndugu yako sio tatizo kwako, hiyo biashara yako kudorora nayo sio tatizo, hata kuishi maisha magumu nako sio tatizo kivile. Ni mungu au ulimwengu unakufundisha, kwamba badilisha maisha yako, anza upya, bado kijana, tena umesoma, anza kulitazama tatizo lako kama lako na pambana nalo na kama wewe, acha kulaumu wengine. Angalia ulipojikwalia na sio ulipoangukia. Tatizo liko akilini mwako, kwamba 'matatizo yangu haya, yanasababishwa na fulani', Huyo ndugu yako mtoe kabisa akilini mwako. Chukulia kila kilichotokea ni shule kwako. Ni Mungu na Ulimwengu unakupa fursa nyingine huku ukiwa umepata funzo kubwa la maisha.
Kila la heri