Heko Usalama wa Taifa

Serayamajimbo

Senior Member
Apr 15, 2009
191
38
Happiness Katabazi

KATIKA mchakato wa mageuzi ambayo yamefanyika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, mfumo wa sheria na siasa za nchi, taasisi za dola zimejikuta zikiwa nyuma wakati vuguvugu la mageuzi likienda mbele.

Moja ya tasisisi zilizokumbwa na fukuto hilo ni Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ambayo hapo awali, yaani chini ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, ilikuwa ni taasisi ambayo haikutambulika kisheria kutokana na muundo wake kuwa wa siri na wa gizani mno.

Matokeo ya utendaji wa idara hiyo uliiletea sifa ya kuogopwa sana na kuonekana ni chombo cha majungu, chuki na wauaji wa wananchi wenye misimamo tofauti na watawala wa serikali hizo mbili zilizopita zilizoongozwa na hayati Rais Julius Kambarage Nyerere na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.

Maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wakiwa katika umbile la kiraia ni wanajeshi na; idara hiyo ni chombo nyeti katika uhai wa dola letu.

Ni kweli kiasili, chombo hiki hufanya kazi kwa taratibu za idara zote za usalama wa taifa na kamwe mwanasiasa hawezi kukitumia; hata hivyo mwanasiasa anaweza kumtumia ofisa wa idara hiyo kwa siri kitendo ambacho ni cha ukiukwaji wa maadili.

Nchi inapoingia kwenye matatizo, migogoro ya kisiasa, lawama kubwa huelekezwa kwa taasisi hii kwani ndiyo inayotambua, kubashiri na kutoa ushauri wa nchi inavyoweza kukabiliana na hatari zozote zile za kiusalama na kiulinzi.

Hapa Tanzania, mageuzi ya mwaka 1992 yaliyoanzisha mfumo wa vyama vingi na mabadiliko mengine ya kisheria na Katiba, yalisababisha kuundwa kisheria kwa Idara ya Usalama wa Taifa.

Kutambulika rasmi kisheria hapa nchini kulianza mwaka 1996, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa Na.5 ya mwaka 1996 na kutambulika rasmi kwa jina la Tanzania Intelligence and Security Services (TISS), ambapo kwa sasa idara hiyo inaongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Rashid Othman.

Cheo hicho cha Mkurugenzi Mkuu ni sawa na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa (CDF), David Mwamunyange, na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema.

Kwa mujibu wa sehemu ya nne ya sheria hiyo inayounda (TISS), kazi na mamlaka iliyonayo ni kukusanya habari, kuchunguza na kutathmini habari zote zinazohatarisha usalama wa taifa na hatimaye kuishauri serikali hatua muafaka za kuchukua kwa maslahi ya taifa.

Ni wazi kwamba idara hii imechangia kwa kiasi kukubwa kudhibiti na kuzuia matendo mengi ya kihalifu ambayo yametendeka au yanayotarajia kutendeka kwa kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi na taasisi nyingine husika ambazo mwisho wa siku ndizo zimeshiriki na kufanikisha kushindwa kwa matukio ya kihalifu.

Hivyo hatuna budi kuipongeza TISS kwa kazi nzuri wanayoifanya; haiwezi kuonekana moja kwa moja na wananchi kwa sababu moja ya miiko ya kazi zinazofanywa na idara hii ni siri.

Na idara hii imenyang’anywa mamlaka ya kukamata wahalifu kwani enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere idara hii ilikuwa na mamlaka hayo chini ya ‘Detention Order’ yaani sheria ya kumuweka mtu kizuizini.

Kwa muktadha wa majukumu hayo, idara hiyo ilitakiwa ijiunde upya kutoka kwenye giza na usiri ili ifanye kazi kama chombo cha dola chenye majukumu ya kulinda amani, usalama na demokrasia. Kwa vyovyote vile idara hiyo haiwezi kufuta mfumo wa utaratibu wake wa kufanya kazi zake kwa siri kwa kuwa hiyo ndiyo namna pekee inayowezesha kupata taarifa na habari za kiusalama.

Lakini pia katika dola ya kidemokrasia lazima chombo hiki kivae umbile la uwazi katika utendaji kazi wake ili wananchi wakijue, wajue majukumu yake na waweze kushirikiana nacho pale inapobidi.

Kwa vyovyote vile usalama wa taifa unalindwa na kusalitiwa na wananchi ambao ndiyo wenye nchi; hivyo ni bora wakajua masuala mbalimbali yanayowazunguka.

Idara hiyo isipojijengea haiba ya kupendwa na wananchi, na hasa wazalendo, mwisho wa siku itajikuta inashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa urahisi zaidi.

Hivi sasa lawama nyingi zinahusu kuibwa au kuporwa kwa rasilimali za nchi kunakodaiwa kufanywa na matapeli kwa kushirikiana na baadhi ya wawekezaji. Idara hii inaelekezewa lawama hizo, kuhujumiwa kwa uchumi wa nchi, kuuzwa kwa mashirika ya umma kwa bei chee na sasa mikataba mibovu mbalimbali ambayo dola imeingia na wawekezaji lazima ielekezwe kwenye idara hii. Kwa vyovyote vile kashfa ya ufisadi wa BoT, EPA na ombwe la viongozi bora lazima shutuma zielekezwe kwenye idara hii.

Kumbe basi wajibu wake si kama ilivyosadikiwa hapo zamani; yaani kuwa kazi kubwa ya maofisa wa idara hii ni kubeba mikoba ya viongozi, kuwatayarishia malazi salama viongozi pindi wanaposafiri, kuwakuwadia mabibi viongozi, kuhesabu vizibo kwenye mabaa, majungu, chuki dhidi ya wananchi na viongozi wao.

Kwa hiyo tunapojikuta leo tuna mgogoro wa kisiasa katika vyama vya siasa vya ushindani vikiwa vimehujumiwa visifanye kazi, makundi yanayohasimiana kuibuka ndani ya CCM, ufisadi wa kupindukia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, ni mambo yanayowaelemea maofisa wetu wa idara yetu ya usalama.

Kwa vyovyote vile mbeba lawama wa mwisho ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Yeye ndiye anamteua Mkurugenzi Mkuu wa idara hiyo. Idara hiyo nyeti isipofanya kazi vizuri rais atayumba, ataboronga na dola kwa ujumla itaonekana ni ya hovyo ndani na nje ya nchi.

Wananchi wanailalamikia dola kwamba inawanyanyasa na kuminya haki zao bila fidia ya kutosha. Hii inatoa tahadhari kwamba malalamiko hayo yanatokana na utendaji usioridhisha wa idara hiyo.

Natoa wito kwa viongozi wa idara hii kuamka na kushika nafasi kikamilifu kwenye kazi hiyo nyeti ya usalama kwa maslahi ya taifa letu bila kuyumbishwa na wanasiasa manyang’au na wachumia tumbo.

Hatujasikia idara hii kukosa uwezo au vitendea kazi; kwa hiyo haya mambo madogo madogo yanayotishia usalama wa nchi, hayawezi kutolewa visingizio kwamba haijawezeshwa.

Hivi sasa nchi yetu imekuwa na uhuru mkubwa zaidi wa kutoa maoni ambapo wananchi wamekuwa wakijadili kashfa mbalimbali hadharani kila zinapoibuka pasi mtu kukamatwa, kuwekwa mbaroni na kuteswa; tunaamini Idara ya Usalama wa Taifa inafanya kazi yake kwa maadili yanayostahili. Kwa hili tunaipa heko.

Nchi nyingine maofisa wa idara kama hii hawajaenda shule vizuri na wala hawajui maadili ya kazi zao.

Watanzania wengi wangeishia kuumia na kuteswa kwenye majumba ya siri yenye giza, nge na kila aina ya mateso. Tunasema haya kwa sababu tunajua yanayoendelea kufanywa na idara kama hii katika nchi nyingi za Afrika.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
 
Muungwana heko kwa lipi walilolifanya hata baada ya sheria kubadilishwa? Unwapongeza kwa kazi wasioifanya wao?
 
Ni suala la Kujifunza tu kutoka kwa wenzetu waliofanikiwa zaidi kwenye nyanja hii. Wenzetu wana mpaka websites. Lakini Idara ya usalama wa Taifa wamehakikisha wanakua nyuma kiteknolojia ili tu kutunza siri.

Unapokuwa msiri saaaana....mwishoni siri hizo hugeuka kuwa habari. Watu watasoma ishara tu na kujua kila kinachoendelea. Njia nzuri na bora kabisa ya kuficha jambo ni kuliweka wazi lile linalostahili kuwa wazi. Waangalie Mossad, wana website na inahabarisha wananchi juu ya masuala mbalimbali, lakini hutakaa ujue siri zao....kwa sababu wanakufanya uamini kama mwananchi wa kawaida kuwa unaweza kutumia Internet ukapata habari zao....upo?

Waangalie FSB, CIA, MI5,CSIS, e.t.c mfumo ni uleule, kuondoa udadisi, kuna mambo wanayaweka wazi na inasaidia kulinda 'siri halisi",.. sasa nyinyi mnachanganya ngozi na utumbo, pua na mapafu, uso na ubongo..whats up??. Acha cha nje kiwe nje ili cha ndani kihifadhiwe.

LASTLY IDARA HII NI KATI YA IDARA AMBAZO HAZINA NAMNA YA KUKWEPA KUFANYA KAZI HALISI WANAYOKUSUDIWA KUFANYA. Asili ya Kazi hiyo, inaifanya kuwa na matokeo makubwa mabaya kama vile mlipuko wa bomu pale linapofanyika jambo kinyume na Makusudi sahihi ya kuwa na chombo hiki. YOU https://jamii.app/JFUserGuide UP IT EXPLODES!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!SHAURI YENU!!!!!!
 
mdogo wangu Happiness ameingizwa katika somo ambalo sidhani kama ana uwelewa nalo wa kutosha. TISS ilivyo sasa ni aibu kwa vyombo vya usalama wa taifa duniani. Believe me I know.
 
mdogo wangu Happiness ameingizwa katika somo ambalo sidhani kama ana uwelewa nalo wa kutosha. TISS ilivyo sasa ni aibu kwa vyombo vya usalama wa taifa duniani. Believe me I know.
Kwa kweli ni chombo muhimu sana, ila kwa sasa wanasiasa kwa njaa zao na kutaka umaarufu wameweza watumia wachache ambao hawana maadili ndani ya chombo hicho kuiyumbisha inchi.

Wakati wa mchonga bwana huwezi mrubuni usalama, walikua wazalendo but now nahisi hawatumii njia muafaka wa kuwapata hawa watu, kwani wengi si wazalendo, ni aibu tupu, ndo maana hali ya usalama wa rai every day inaenda vibaya. We siku hizi raia akitoa ripoti kuna muhalifu askari anaenda mwambia fulani ndo kakutaja. Huu si ubaradhuli kabisa. Shame on them.

Nahisi serikali ijipange hapo kwanza kwa kuwaanisha wote ambao si waaminifu then kuwashughulikia na kutumia njia sahihi za kuwapata wazalendo ikibidi kuwafundisha au kuwakumbusha nn uzalendo.
 
yangu macho, kama kuna mahafisa wa ngazi za juu katika jeshi letu wamejiunga na CIA na TISS wapo sijui wanawachunguza au wameamua kufanya butubutu mpira uwende, sijui kwasababu tz hatuna siri
"yangu macho" lakini pengine wanavuta kasi wanapoamka ngoma mdundo, cha muhimu mfumo wake ungegawanywa katika vikundi vidogo vidogo kwani hata CIA wana IU 1 mpaka 10 na kila kikundi kinamfumo wake wa uwajibikaji. yangu macho pengine wanafanya kazi kwa kificho sana mpaka hatujui kama wapo,
 
INASIKITISHA SANA NA SINA IMAN NA CHOMBO ICHI IKIWA KUMTIA HATIAN ZOMBE WALISHINDWA. Hii nchi ipo hatarini. Hata hvyo ninaiman taifa hili ni taifa kubwa duniani nasiku moja mifumo yote tangu usalama wataifa, majeshi yetu yote ya ulinz na usalama yatakuwa ktk ubora wa kimataifa. Hili ni taifa kubwa na kwa hakika nilazima litimie, wahujumu wa taifa hili makabur yao yatakuwa jehanamu na watanzania kushuhudia vitanz vyao hakika umauti utawapata kama sunami. MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE. Amen
 
Happiness You are to shallow, unawapongeza kwa lipi? or you are just propagating for them??????
 
hiki chombo kimepoteza taswira yake kabisa sasa hivi imekuwa ni show mtaani no maadili kabisa kiukweli imeingiliwa kabisa na atuwezi kupata kile tunchotarajia kutoka kwao ona ufisadi,mikataba mibovu, ubinafsishaji, siri zinavuja ovyo, maadili hakuna yani kwishinei kabisa na uzalaendo enzi ya mwl utamjuaje usalama fisadi utamsikia wapi, siri utazipata wapi
 
Mambo mengine ni mazito na wewe Happiness hujui lolote kuhusu usalama na aliyekupa hizo info uweke kwenye gazeti lenu amekudanganya.

Idara ya Usalama wa Taifa tanzania ilikuwa makini enzi za ujamaa leo hakuna kitu pale. Uozo unaouona ktk polisi na jeshini ni uozo huo huo upo idara yetu ya usalama.
 
Uumhh, mwandishi Happiness angeweka bayana yale ambayo yeye anawasifia hawa jamaa au kwa sababu siku hizi hakuna vile vifungo vya nyumbani au kubebwa na kupelekwa kusikojulikana kama tu ukiisema vibaye serikali?
 
mdogo wangu Happiness ameingizwa katika somo ambalo sidhani kama anauwelewa nalo wa kutosha. TISS ilivyo sasa ni aibu kwa vyombo vya usalama wa taifa duniani. Believe me I know.

Mwandishi anashangaza kuandika makala kama hii hasa wakati huu. Huo msukumo sijui ameupata wapi. Labda aliombwa kuwaandikia PR piece itakayowatengenezea taswira chanya katika jamii. Baada ya kuwasikika wakihusika na skandali za EPA, Meremeta, n.k. hadi kumdondosha mama meghji na kumpa PM (mtoto wa mkulima) kigugumizi Bungeni, tunachokiona ni kuwa umuhimu wao sasa umekuwa zaidi katika kusaidia wakuu na maswahiba wao kuhujumu uchumi wa nchi.
 
Hawa jamaa wana mchango wao mkubwa tu kwenye AMANI na UTULIVU tuliyonayo Watanzania. Tunaweza kubishana sana kwa hili. Wakubwa wao tu ndio wamekuwa wakiwaunga mkono hata mafisadi wa wazi kabisa.
 
Kila mtu anao mwono wake katika kutoa sifa pale aliporidhishwa na jambo.

Happiness labda anasifia uwezo wa TISS katika kutunza siri za mienendo michafu ya viongozi na wafanyabiashara wakubwa katika kuhujumu nchi, kutokufatilia mikataba kandamizi na ya kijinga kabisa ambayo maafisa wa serikali wanaisaini kwa niaba ya nchi kwa kutojua au kwa makusudi maalumu.

HEKO anazotoa kama ziko kwa mwelekeo huo, basi hajakosea maana tukiziandika zitafika kurasa mia kadhaa.
 
mimi nadhani labda huyo hapness anazungumzia kwamba sasa hiyo TISS, inatambulika kwa wtu wote sio kama ilivyokuwa zamani ambacho ilikuwa inaonekana ni kitu kama cha kufikirika tu

lakini tukija katika kuipongeza nadhani hapo ni hapana,
KAMA KUNA IDARA AMBAYO INAIANGUSHA HII NCHI NA KURUDISHA MAENDELEO NYUMA BASI ITAKUWA NI HII IDARA, nadhani ndani ya hiyo idara kuna department moja tu ya Siasa, department ya kushughulikia upinzani na mtu yoyote anaeonesha ana misimamo mikali ya kisiasa,
SIDHANI KAMA KUNA KITENGO CHA MAANA KABISA NDANI YA HII IDARA KINACHOSIMAMIA UCHUMI NA MASLAHI YA KWELI YA HILI TAIFA (ISSUE KAMA ZA EPA, RICHMOND, MADINI NA NYINGINEZO ZISINGETOKEA KABISA KWA MASLAHI YA TAIFA HILI)

HAWEZI MTU KUTOKA IRANI na kuja kuitawala nchi bila hao jamaa kuchukua hatua, eti kisa ajagombana na CCM, kwa hiyo hao jamaa wapo na siasa tu, lakini mwisho wa siku huyo MwIrani ka fu*k everywhere, ka corrupt mpaka huo usalama wenyewe

kwa kifupi hao jamaa wapo hapo kwa usalama wa wanasiasa tu
 
Pengine mwandada Katabazi amelazimika kusafisha jina (kwa uoga wake mwenye wa au kwa shinkizo) baada ya makala zake mbili,moja ya 13 February 2008

IDARA YA USALAMA WA TAIFA NI SEHEMU YA UFISADI?
Na Happiness Katabazi

BAADHI ya Watanzania wakiwemo viongozi mbalimbali wastaafu na wale wa vyama vya upinzani,wamekuwa wakiliambia taifa kwamba limepungukiwa na viongozi waadilifu na wakaona kwamba umaskini unaolikabili taifa letu ni wa kujitakia.

Kwakuwa licha ya rasilimali kubwa tulizonazo hatuna viongozi wenye upeo wa kutuonyesha njia ya kuzitumia vyema ili tupate maendeleo.

Badala yake tunaona kuwa tunao viongozi wasiyo waadilifu,mafisadi,wazandiki na wababaishaji wa kutupwa.

Uongozi wa taifa una mfumo wa kitaasisi ambao wengi wanaita ‘system’.Kwa lugha ya kawaida system inamaanisha mfumo wa Idara ya Usalama wa Taifa katika kuchagua na kudhibiti ubora wa viongozi na mwenendo wao.
Moja ya wajibu mkubwa wa Idara ya hiyo ni kulipatia taifa viongozi bora,wazalendo na waliofundwa vya kutosha kutumia madaraka yao kutetea maslahi ya taifa.Lakini wimbi la ufisadi lililojitokeza nchini ni ishara kwamba idara yetu ya usalama wa taifa imeshindwa kazi.

Moja,idara hiyo imegeuka kuwa ni sehemu ya CCM kwahiyo badala ya kutekeleza wajibu wake tulioujata kulingana na Katiba na sheria za nchi, ikiangalia vyama vyote,taasisi zote za kijamii nk.

Baadhi yao wamejifanya ni watendaji wa CCM na wanapotenda hivyo kazi yao kubwa inakuwa ni kuhujumu viongozi walio kwenye vyama shindani kana kwamba hawa si watanzania na ila ni maadui wa nchi.

Pili,kuzuka kwa kundi la wanamtandao ambalo linadaiwa kumuweka madarakani rais Kikwete kunaashiria ushiriki mkubwa wa idara hiyo kupanga mtandao kuhusisha sekta zote za jamii na kuhusisha watendaji muhimu serikali ili wote kwa pamoja watekeleze azimima ya CCM kubaki madarakani.

Inasemakana kwamba nyuma ya ufisadi unafichuliwa yapo makampuni ya kifisadi ambayo hayumkini yalioanzishwa na idara ya usalama wa taifa kukusanya mabilioni ya fedha yaliyotumika na wanamtandao na CCM kwenye uchaguzi wa 2005.

Hakika yeyote anayependa kusema ukweli atakiri kwamba mabilioni ya fedha yaliyotumika kwenye mchakato ndani ya CCM na mabilioni ya fedha yaliyotumika na ccm katika uchaguzi uliopita hayana maelezo au chanzo kingine kama si makampuni hayo ya kifisadi ya kupora fedha za umma.

Sasa tujiulize taasisi hii ina uadilifu kiasi gani na Je aijashiriki katika ufisadi kwa namna yoyote ile?. Ikiwa watetezi wa usalama wa taifa watasema inatenda kazi zake kwa mujibu Katiba na sheria za nchi Je walilala wapi BOT ilipohujumiwa?

Je ilikuwa wapi maslahi ya nchi katika uzalishaji wa umeme yalipohujumiwa katika mradi wa IPTL na Richmond?

Je walikuwepo wapi maslahi ya nchi yalipohujumiwa katika ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara,TTCL, na makampuni mengine mbalimbali ya umma?

Tunachokiona sisi Idara ya Usalama wa taifa isiyojua wajibu wake na ambayo ufisadi ni sehemu kuu ya kazi yake. Pia tunachokiona sisi ni idara hii isiyojua kutetea maslahi ya ya nchi ambayo ipo tayari kuona rasilimali za nchi zikihujumuiwa ili mradi wanafanya hivyo ni marafiki zao.

Kazi kubwa ni kulindana, kupeana vyeo bila kuwa na sifa na pia kuwapiga vita wale wanaojitokeza kupingana na mwenendo wa kifisadi.

Tumefikishana mahala watu sasa wanamwagiwa tindikali,wanahushishwa kwenye ajali za kupangwa na bila shaka siku si nyingi tutashuhudia mauaji ya watu kwa mtindo wa kijambazi unaotumika na Mafia.

Inapotokea kwamba viongozi wa taifa ama serikali wanapata nyadhifa au kuajiliwa kazini kwa sifa za ubabaishaji au kughushi na hilo likafumbiwa macho,basi hakuna usalama wa taifa.

Kwa maana kwamba ikiwa uongozi utawekwa mikononi mwa matapeli walioghushi sifa za elimu basi hatima ya taifa itakuwa hatarini.

Je viongozi wa aina hii wataelewa nini kinachoendelea kuhusiana na mikataba ya biashara ya madini au mikataba ya umma? Kwa hiyo tusishangae serikali yetu inaendeshwa sawa kama viongozi hawajaenda shule kwani siyo kila anayejiita Daktari ni Daktari wa kweli.

Mfano ilikuwaje kampuni ya kihuni ya Richmond kupewa mkataba wa mabilioni ya fedha kununua majenereta ya umeme bila usalama wa taifa kujua?

Je kukosekana kwa umeme Je si jambo nyeti na hatari kwa usalama wa taifa?Au labda idara hii inaona Watanzania wamelala usingizi na wako tayari kufanyiwa vitendo viovu na wako tayari kulipishwa kodi na kubebeshwa gharama kubwa za maisha bila kulalamika au hata kufanya maandamano?

Labda Watanzania wamekuwa wapole mno katika kutetea haki zao.Bila shaka usalama wa taifa utaona ugumu wa maisha wanaopata wananchi pale tutakapokuwa tayari kuandamana na kuwatoa maofisini na kuwafukuza kwa bakora hao mafisadi?

Kwa ujumla , vyombo vyetu vya ulinzi na usalama tulivyonavyo, chombo ambacho akijatufanyia haki ni Idara hii ya usalama wa taifa.Hawa wamelala usingizi wa pono nchi ina hujumiwa,wananchi tunapata taabu .JWTZ,Magereza,JKT na Polisi wanafanyakazi nzuri, tunawapongeza, licha ya kwamba wamekuwa wakilalamika bajeti za wizara zao ni finyu kuliko bajeti ya Idara ya usalama wa Taifa.

Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) chini ya Jenerali Davis Mwamunyange, wanafanyakazi nzuri na ndiyo maana hadi sasa nchi yetu haijavamiwa na maadui.

Polisi chini ya IGP-Said Mwema,nao wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la uhalifu.

Magereza chini Kamishna Mkuu, Agustino Nanyaro nao wamejitahidi, kwani hadi sasa hatujasikia wafungwa wamevunja magereza na kutoraka. JKT na wanajitaidi kuwalea vijana na kuzalisha mali.

Wakati umefika sasa watendaji wa Idara ya Usalama wa Taifa wawajibike kikamilifu bila kumuonea haya kiongozi yeyote, ama sivyo itabidi idara hii ivunjwe tuunde jipya na hilo linawezekana kama tuna uchungu wa kweli na Tanzania yetu.

Mungu ibariki Afrika,Mungu ibariki Tanzania
na makala yake hii ya 22 July 2007
Twahitaji Usalama wa Taifa si Uhasama wa Taifa

Happiness Katabazi

KISWAHILI kama zilivyo lugha nyingine, kina maneno kadhaa ambayo ama yana maana ya kitu kimoja au maana yake inashabihiana.

Mfano wa maneno haya ni hili ‘taifa’ waweza kulifananisha na neno ‘nchi’ na pengine neno ‘dola’. Taifa au dola kama inavyojulikana ni jumuiya ya watu wanaolikalia pande la ardhi yenye mipaka inayotambulika rasmi kwa mataifa au dola nyingine.

Hivyo taifa au dola hufanya mambo yake ndani ya mipaka yake na hutumia vyombo kadhaa kuendesha shughuli hizo na kulinda masilahi ya wanataifa dhidi ya maadui wa ndani na nje.

Wataalamu wanatanabaisha kwamba dola/taifa lina mihimili mitatu (Serikali, Bunge na Mahakama), wengine huongeza mhimili wa nne, yaani vyombo vya habari. Mhimili wa Serikali ndiyo wa kiutendaji na hivyo husimamia vyombo kadhaa katika utendaji huo. Hivi huitwa vyombo vya dola, ambavyo ni pamoja na majeshi ya ulinzi na usalama.

Hapa Tanzania tunalo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linalohusika sana katika kulinda nchi yetu na mipaka yetu dhidi ya maadui wa nje na pale inapobidi kuingia vitani kulinda nchi.

Katika hili twaweza kutoa mfano jinsi JWTZ walivyofanya kazi ya barabara mnamo mwaka 1978/1979 dhidi ya majeshi ya adui Idd Amini Dada wa Uganda (sasa marehemu).

JWTZ katika vita iliyopiganwa mwaka huo walifanya kazi iliyotukuka, kiasi kwamba sitarajii itakuja kusahaulika miongoni mwa Watanzania na katika historia ya nchi hii.

Naam! JWTZ walitimiza wajibu nyeti ambao si mwingine, bali kulihakikishia taifa letu usalama. Tunalo jeshi jingine, Polisi, hawa tunaambiwa siku zote wako kwa ajili ya usalama wetu sisi raia na usalama wa mali zetu tulizojaliwa kuzimiliki.

Nao kazi yao si haba. Mara kadhaa wametuweka salama dhidi ya vibaka wakwapuaji, majambazi wa kutumia silaha, wavunja sheria za nchi na wengineo.

Hata hivyo pamoja na jitihada zao nzuri, matukio ya uhalifu bado yapo nchini na pengine wanashindwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao, mathalani vifaa duni na mengineyo.

Lakini hatuwezi kusita kusema kwamba, vitendo vya baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi si tu ni kero bali vinaondoa maana ya dhana nzima ya wao kuwa chombo cha usalama wa raia na mali.

Kwa muda mrefu baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani (Traffic) wameendelea kuwanyanyasa wenye magari kwa rushwa.

Aidha, udhaifu mwingine wa Jeshi la Polisi umejikita katika namna ambavyo watu fulani wenye mamlaka huamua kukitumia chombo hiki ndivyo sivyo, mathalani, katika matukio kadhaa badala ya polisi kuwalinda raia walitumiwa kuwatesa raia.

Asiyeelewa hili awaulize vijana wa vyuo vikuu walivyotandikwa mara kadhaa na FFU, au wamuulize Profesa Ibrahim Lipumba kisa cha kujeruhiwa mkono wake na askari waliopaswa wamlinde.

Kama hilo halitoshi, kumbukumbu ziwapeleke huko Zanzibar ambako askari polisi walitumika kuwamwagia maji ya ‘washawasha’ raia wema. Polisi wasinielewe vibaya, kazi yao ni nzuri sana ila kasoro za ufisadi na unyanyasaji ni mbaya. Isije ikawa mnatimiza lile neno lililonenwa na nabii akisema ‘chachu kidogo inachachua donge zima’.

Naam!, kwa ujumla twaweza kusema, mipaka yetu ni salama (heko JWTZ), raia tuko salama kiasi chake (asante polisi). Lakini je, kama tutatumia usalama katika maana yake kamili, taifa letu Tanzania liko salama? Na hili si swali la kipima joto hata lijibiwe kwa kusema tu ndiyo, hapana au sijui. Jibu linahitaji fikra pana.

Tangu tukingali watoto wadogo tumekuwa tukisikia uwepo wa chombo kiitwacho Usalama wa Taifa.

Wengi tunaweza kuwa tunafahamu majukumu ya chombo hiki kinadharia tu, maana shughuli kinazozifanya hazionekani moja kwa moja hadharani mara zote.

Yamkini kazi za wanausalama wa taifa hufanyika kwa usiri mkubwa. Ndiyo maana inakuwa hata si rahisi kujua nani mwajiriwa katika chombo hiki.

Watu wanaishia kutuhumiana tu, mara utasikia ‘ooh, fulani ni usalama wa taifa na fulani naye…’ lakini hakuna uthibitisho, ni siri kwelikweli.

Hawa wanaodhaniwa kuwa ni wanausalama wa taifa wako katika vyama vya siasa, taasisi kama vile vyuo vikuu na kwingineko, ambako kama pasipochungwa huenda patahatarisha masilahi ya vigogo.

Kinachoshangaza hapa ni kwamba inakuwaje mtu wa usalama wa taifa afanye kazi ya kudhibiti jitihada za chama fulani kisiweze kushika madaraka ya dola kihalali?

Inakuwaje mtu wa usalama wa taifa atumiwe kudhibiti midomo ya wasomi katika vyuo vikuu wasiseme ukweli, wasiwe na uhuru wa fikra bali wahubiri tu na kukariri yale yaliyo matakwa ya vigogo?

Inakuwaje usalama wa taifa kufanya kazi ya kudhibiti vyombo vya habari ili viandike yale tu ambayo wakubwa wanataka na si vinginevyo!

Inakuwaje usalama wa taifa uone kwamba kazi inayotakiwa ni kuwadhibiti waandishi wa habari wasifanye kazi yao, kama ilivyotokea wiki mbili zilizopita pale Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kati ya wapiga picha hadi Rais Jakaya Kikwete, akaingilia kati!

Katika hili, sina budi kumsifu Rais Kikwete. Ama kwa hakika kitendo chake cha kuwakataza walinzi wasiwazuie waandishi kufanya kazi zao ni cha upeo wa hali ya juu wa uelewa na ni funzo kwa wanausalama ambao wanasahau majukumu yao ya msingi na kujishughulisha na vitu ambavyo wala si hatari kwa usalama wa taifa.

Kudhibiti vyombo vya habari, wasomi na wanasiasa wa kambi ya upinzani, wanausalama wetu mfahamu fika kwamba uko si kulinda usalama wa taifa bali ni kujenga uhasama wa kitaifa.

Usalama wa taifa mkitambua hilo, rejeeni katika shughuli za kimsingi mnazopaswa kuzifanya hususan zama hizi ambapo usalama wa taifa letu na wa wakati ujao unazidi kuwa shakani.

Hamisheni nyenzo zenu pale Chuo Kikuu Mlimani mzielekeze kwenye maofisi ambako wizi wa kalamu unazidi kushamiri, ufisadi unaoota vitambi na uzandiki unastawi kupitia mikataba ya kishenzi inayosainiwa kati ya wezi wa ughaibuni na wenzetu wachache wanaokosa hata lepe la uzalendo, wanaiuza nchi hii kila uchao mchana kweupe na nyie mpo eti usalama wa taifa…usalama upi?

Tuseme hamjasikia hayo yanayotokea katika Benki Kuu ya nchi hii, kwanza mlikuwa wapi hata msiyadhibiti yasitokee? Au mlikuwa Tanzania Daima na MwanaHalisi mkiangalia nani anawaandikia wananchi ukweli ili ashughulikiwe?

Mmelala usingizi upi mpaka madini ya nchi hii na rasilimani nyinginezo vinachotwa na wageni kwa ‘raha zao’. Yamkini mlikuwa kwenye lecture rooms pale Mzumbe au SUA mkidhibiti wahadhiri wasitoe mihadhara ya takwimu za uporaji huo.

Mlikuwa wapi wakati hao wezi wakifanya mambo yanayowahusisha na kashfa nzito pengine kuliko zote nchini (ya BoT, Meremeta Gold Company, Kampuni ya Alex Stewarts, Akaunti ya madeni ya nje, Bank-M na kwingineko?).

Au mlikuwa kwenye mikutano ya hadhara ya ushirikiano wa vyama vya upinzani ili kukusanya ni hoja gani za nguvu wamezijenga mkawaripoti kwa vigogo watafute namna ya kuwajibu?

Ni usalama wa taifa upi mnaoshughulika nao ndani ya nchi ambayo wengi wanazidi kufukarika wachache wananeemeka kwa kasi ya roketi?

Ama hamjui kwamba hapana usalama palipo na wingi wa fukara, maana wajapokata tamaa amani itayeyuka kama barafu wakati wa jua kali.

Yatosha mliojishughulisha na masilahi ya wachache wala nchi, oneni uchungu, rejeeni maadili ya taaluma yenu, liokoeni taifa lenu, watumikieni wananchi, turejesheeni usalama wa taifa.

Watanzania tunautamani usalama wa taifa unaomlenga kila mmoja wetu, unaolenga uhifadhi wa rasilimali zetu na unaolinda haki ya kila mmoja wetu, awe raia huru au raia anayetumikia kifungo (pengine kwa kuvunja sheria au kubambikiziwa, au kushindwa kutoa rushwa kwa hakimu na karani mahakamani).

Katika hilo mawazo yananirejesha kukitazama chombo kingine cha dola, Jeshi la Magereza. Chombo hiki nacho kilipewa jukumu zuri, kuwahifadhi wahalifu wanapotumikia vifungo vyao na kuwafanya warejee katika tabia njema zinazofaa katika jamii (re-socialization). Jukumu hili nalo lililenga usalama wa jamii.

Cha ajabu ni kwamba, wafungwa kadhaa wanapomaliza kutumikia vifungo vyao badala ya kurejea uraiani wakiwa watu wema waliobadilika, wazingativu wa maadili ndiyo kwanza huja na mbinu kali zaidi za uhalifu.

Msomaji usishangae bali tushirikiane kuliambia Jeshi la Magereza litufafanulie; bangi na pengine dawa za kulevya zinapenyaje na ulinzi wenu mkali na kuwafikia wafungwa? Au baadhi yenu mna masilahi katika hiyo miradi?

Inakuwaje huko magereza wafungwa ‘wanashikishana ukuta’ (wanaingiliana kinyume cha maumbile), au kwenu ninyi hiyo ni haki ya mfungwa?

Hao chawa wataisha lini kwenye virago wanavyolalia wafungwa, wataacha lini kulala mzungu wa pili na kwa msongamano katika vyumba vidogo.

Au hamjui kwamba kwa kuwaweka wafungwa katika mazingira ya kinyama namna hiyo ndiyo kwanza mnawajengea moyo wa ‘kihayawani’ na kikatili badala ya kuwarejesha katika uadilifu.

Mtueleze wazi mnakuwa wapi hadi wafungwa wa kike wanapachikwa mimba wakiwa magerezani?

Jeshi la Magereza, ebu jiulizeni leo hao wafungwa mnaowahifadhi wakimaliza vifungo vyao usalama wa taifa utakuwa katika hali gani?

Mama yetu Tanzania, leo wewe si taifa salama, waambie wanao (wananchi) wajue hali uliyonayo, washiriki kilio chako ili tumbo lako lisizidi kuwa shimo tupu lililotolewa utumbo wote (mali asili) kwa manufaa ya wageni; lisiendelee kupata uchungu wa kuzaa wana mafisadi na wahalifu, mwite mwanao serikali akishtue chombo chake Usalama wa Taifa kisiendelee kubweteka ilhali usalama wako unazidi kutokewa.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.
 
Pengine mwandada Katabazi amelazimika kusafisha jina (kwa uoga wake mwenye wa au kwa shinkizo) baada ya makala yake hii ya February 2008
Ni kweli mkuu, baada ya kutuletea makala hiyo aliyo andika awali, kila mwenye akili atamwelewa. Aje hapa atufafanulie tofauti hizo mbili za makala zake zimetokana na nini? Maana zina rangi tofauti, nyeusi na nyeupe.
 
Back
Top Bottom