MGANGA NA MWANAFUNZI BUBU
Paliondokea mganga stadi mno wa ajabu. Ikawa katika nchi ile hakuwapo mganga kama yeye. Akafanya mali sana. Na watu kadha wa kadha wakataka wajifunze kazi yake, ila huyu mganga hakutaka mwanafunzi anayesema, ila bubu. Maana yake alijua awezi kueleza neno, na ufundi wake hautakwenda mbali, maana hakutaka ufundi wake uenee, wasije wakafaidika watu wengi kwa chumo. Watu walijaribu kumuomba awafundishe hata kwa mali hakutak. Akaondoka mwanamke mmoja aliyekuwa na mtoto wake mmoja tu. Akamwambia, "Mwanangu, wewe ni mwana yatima, baba yako amekufa, na mimi mwanamke siwezi kukufundisha kazi. Nataka usikilize shauri langu. Ipo kazi kwa yule mganga ukiipata utastarehe wewe na mimi. Lakini ina tofauti moja, hatakiwi mtoto ila bubu. Basi mwanangu nataka ujifanye bubu uende kwa fundi ukanyamaze kimya, ukastahimili yote atakayokutenda."
Mtoto akakubali. Mama yake akamchukua akampeleka mpaka kwa mganga akamwambia, "Nimekuletea mwanafunzi."
Akamuuliza, "Huyu mtoto ni bubu?"
Akanena, "Bubu tangu kuzaliwa."
Akamwambia, "Unaona! Hivyo ndivyo nilivyotaka."
Akampokea yule mtoto, mama yake akaenda zake. Yule mganga akamtwaa yule mtoto akamtandika vema kwa bakora, na mtoto kimya. Maana mganga alijua kuwa kama huyu mtoto ni mwongo, akipigwa atalia, "Mama wee! nakufa."
Alipoona hakulia kwa bakora, akatafuta upupu akamtia. Na mtoto akalia kwa kutoa machozi tu, na kujikuna, lakini neno hakutoa. Mganga akaisha mizungu yote ya kutaka kumsemesha. Hakuweza. Hata mganga akayakini kuwa huyu kweli bubu. Akakaa naye.
Akamsabilia kazi zake zote. Kila anapomfanyizia mgonjwa dawa huyu mtoto sharti awepo. Akimtuma hutumika, akimwuliza neno hajibu ila kwa kichwa na mkono.
Wakakaa katika hali hii siku kadha wa kadha.
Siku moja akaja mtu hawezi kichwa, kutaka kuaguliwa.
Mganga akamtazama, akamwambia, Kichwa chako kimepungua, na ukizidi kukaa katika hali hii utafanya wazimu. Na mimi naweza kukufanyizia dawa lakini sharti nitoboe kichwa chako, nitazame yule mgonjwa akakubali. Mganga akatoboa kichwa, akatazama ndani akaona yuko funza mkubwa mweupe kati ya ubongo.
Akafahamu kuwa huyu ndiye anayeharibu ubongo wake, ikawa fundi kutafuta njia ya kumtoa yule funza. Akatufuta kulabu ili aingize katika ubongo ili akamkamate yule funza amtoe. Yule mwanafunzi akatazama akaona ya kuwa Leo mganga anakosea. Ubongo utiwe kulabu mpaka ndani utaharibika. Lakini kusema hapati maana yeye bubu. Lakini tena akawaza kuwa mimi nikinyamaza hata huyu mtu atiwe kulabu atakufa,
Basi akangoja hata mganga alipokuwa karibu kutia kulabu, Akasema, "Fundi unakosea! Huyo funza ukimto kwa namna hiyo, huo ubongo utazidi kuharibika
Twaa moto uweke karibu na kichwa huyo funza atoke mwenyewe kwa joto!"
Yule mganga alipomsikia mwanafunzi wake kusema, alishangaa, "Ah! Kumbe wewe unasema." Akakasirika sana akataka kumfukuza kabisa. Lakini yule mwanafunzi akasema, "tafadhali ufikiri zaidi. Naliweza kukaa kimya kabisa na kukudanganya siku zote ili nipate faida kwa hila, lakini sikupenda mtu huyu afe, wala sikutaka wewe uadhibiwe kwa kosa lako. Kwa hiyo naliacha hila yangu nikasema."
Mganga akasema, "kweli unayosema," Akamsamehe.
Akazidi kumfundisha uganga wake. Wakawa rafiki tokea siku ile wakafanya kazi pamoja wakasaidiana.