Hekaya za Abunuwasi

Hadithi ya ngamia aliyekuwa mvivu

Hapo zamani za kale dunia ilikuwa bado mpya
kabisa. Iliwapasa wanyama wote kufanya kazi nyingi
ili waitengeneze sawa sawa, iwe mahali pazuri pa
kukaa. Farasi akafanya kazi nyingi kabisa ; na
ng’ombe pia, na mbwa, na punda, na ndovu
kadhalika. lla ngamia peke yake hakufanya kazi
yo yote. Alikuwa akipiga uvivu kutwa kucha,
akijitenga mbali na wanyama wengine, na kula
majani jangwani katika upweke.
Wanyama wengine hawakupenda uvivu wake
hata kidogo, kwa maana kazi yao ikazidi, wakanuna.
Mwisho wakamwendea ngamia yule kumwuliza
sababu ya kupiga uvivu yeye peke yake, asifanye
kazi yoyote, dunia ikiwa bado mpya kabisa. Lakini
yeye mkorofi ; kila anapoulizwa hujibu : Nunduuu!
Wala hajibu kitu kingine, wasijue tena la kusema:
Kila mara wao wakimwuliza, yeye hujibu : Nunduuu ! Halafu huwacheka.
Hata mwisho wakachoka. Wakaenda kwa mchawi mkuu wa jangwani, wakamwuliza :
Je, ni haki ngamia yule kupiga uvivu siku zote, Sisi tukifanya
kazi kwa kuwa dunia ni bado mpya kabisa
Akajibu : Si haki kata kidogo.
Wakasema : Basi, umwambie wewe afanye kazi,
kwa sababu Sisi tukimwambia anatucheka tu ; anajibu : nundu, nundu. Hasemi neno jingine. Mchawi akafikiri kidogo, halafu akachukua
mumunye na uvumbi wa dunia mpya, akaenda
zake kumtafuta ngamia yule aliyekuwa mvivu.
Akamkuta jangwani peke yake, akila manyasi ya
nyikani, akiangalia uso wake katika kidimbwi. Kwakuwa ngamia si mvivu tu, lakini ana majivuno vilevile.
Mchawi akamwuliza : Je, bwana ngamia, nasikia nini juu yako, kwamba hutaki kufanya kazi yoyote, hata siku hizi kama dunia ni mpya kabisa
bado
Ngamia akajibu : Nunduuuu !
Mchawi akasema : Nadhani ni afadhali usiseme nundu kila mara. Neno hili litakudhuru. Sasa nataka kujua kama utakwenda kazini sasa hivi, au
kama unakataa
Ngamia akasema : Nunduuu !
Hapo mchawi mkuu wa jangwani akachukuamumunye lake pamoja na uvumbi wa dunia mpya akaanza kucheza na uchawi wake. Na bwana
ngamia akazidi kujiangalia katika kidimbwi, akijifurahisha moyo kwa ajili ya uzuri wake. Ndivyo alivyofanya ukorofi wa kumchokoza mchawi yule.
Lakini alipokuwa akijitazama hivi katika maji ya kidimbwi, akaona kwamba mgongo wake ulianza kuvimba kwa ajili ya uchawi ule. Mgongo wake ukavimba, ukavimba, hata mwisho ukawa nundu kweli kweli. Akajaribu kuiondoa asiweze.
Akanung'unika kwa mchawi, akasema : Sasa umeniharibu kabisa. Sitaweza kufanya kazi yoyote namna hii. Lakini mchawi akajibu : Utaweza
tu. Itakufaa kwa chakula cha akiba, utumie wakati wa kufanya kazi jangwani. Na usipofanya haraka ya kwenda kazini sasa hivi, nitaharibu kichwa chako vile vile.
Ndiyo maana ngamia ana nundu siku hizi, na
kazi anaifanya kwa shida tu, bila kupenda. Na
iwapo anafanya, hana haraka.
 
Back
Top Bottom