Panya Ronin ameweka rekodi mpya ya kugundua mabomu ya ardhini baada ya kubaini vilipuzi 109 na mabaki mengine 15 ya silaha katika mkoa wa Siem Reap Nchini Cambodia.
Mafanikio haya yamefikiwa kati ya Agosti 2021 na Februari 2025, na kumfanya kuwa panya aliyegundua mabomu mengi zaidi duniani.
Ronin, aliyekuzwa kupitia mpango wa mafunzo wa Shirika la kutoa misaada ya kutegeua mabomu yaliyotegwa ardhini lililo na makao yake nchini Ubelgiji la APOPO, alizaliwa Agosti 13, 2019 Mkoani Morogoro, Tanzania. Ameipiku rekodi ya awali iliyoshikiliwa na panya Magawa, ambaye pia alizaliwa Tanzania. Magawa aligundua mabomu 71 ya ardhini katika kipindi cha utumishi wake wa miaka mitano kabla ya kustaafu mwaka 2021.
Shirika la APOPO limekuwa likiwafundisha panya wa Kiafrika 'African giant pouched rats' kwa zaidi ya miongo miwili ili kuwasaidia watu wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa na mabomu ya ardhini. Panya hawa wanatumia uwezo wao wa harufu kali kugundua vilipuzi vilivyofichwa ardhini bila kuhatarisha maisha yao, kwani uzito wao mdogo hauwezi kusababisha mlipuko.
Kwa mujibu wa Lily Shallom, Meneja wa Mawasiliano wa APOPO, Ronin ameonyesha kiwango cha juu cha umakini na bidii. "Anapenda kazi yake na huiona kama mchezo wa kutatua changamoto," alisema Shallom.
Mbali na kugundua mabomu, baadhi ya panya wa APOPO pia hutumiwa kusaidia utambuzi wa ugonjwa wa kifua kikuu katika hospitali, wakiharakisha mchakato wa uchunguzi katika maeneo yenye rasilimali chache.
Ronin, ambaye kwa sasa ana miaka mitano, anaendelea na kazi yake huku akitunzwa na wataalamu wa APOPO. Imeelezwa kuwa anapendelea vitafunwa vya parachichi, ndizi, na karanga, na hutumia muda wake wa mapumziko kucheza michezo ya kutafuta vitu.
✍️: @Barakadon_
#WasafiDigital