Ndugu zangu Watanzania,
Kumfundisha mtu mzima na mwenye kushika madaraka kitu cha kufanya pale anapokosea si matusi, wala sio dhihaka, ni hekima. Wakati umefika sasa tumsaidie Rais Kikwete cha kufanya. Kwamba gharama za kuweka maswahiba katika madaraka wasio na uwezo nayo, ndio hizi. Kama George Washington alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza angewakumbatia rafiki zake Marekani isingekuwa hivi. Lakini aliwaambia "You are friends of George Washington, not friends of President of United States of America". Kikwete alikumbatia sana marafiki zake, akawapa nafasi japokuwa hawana uwezo. Wao wakawa wanakula "deals" na kurudisha gharama za kuchangia uchaguzi mkuu wa 2005. Nani alikuwa hajui kuwa Nazir Karamagi alipewa Uwaziri kwa kuwa alikuwa mfadhili wa uchaguzi? Nani alikuwa hajui kuwa Anthony Dialo naye alipewa Uwaziri kwa sababu alikuwa akifadhili uchaguzi? Nani hajui kwamba mtu kama Stephen Wassira anaendelea kuwa Waziri kwasababu yeye ndiye alikuwa anaongoza kampeni za kuwamaliza Frederick Sumaye, Dk. Salim Ahmed Salim na Mzee John Malecela kule kanda ya ziwa mwaka 2005?
Matatizo ya watanzania wa leo yanatokana na dhambi ya viongozi wetu. Na dhambi hii itatutesa milele. Gesi ya kusini mwa Tanzania ni kielelezo. Lakini pia tukumbuke namna ambavyo wanyamapori wanauzwa wakiwa hai. Nani aliwahi kutafakari kuhusu mnunuzi wa wanyama hawa?
Kama Watanzania wanazo kumbukumbu, warejee mwaka 2005. Gazeti moja liliwahi kuandika kwamba Bilionea kutoka Ufalme wa Oman alikuwa ametoa dola milioni 40 kusaidia kampeni za Kikwete. Kikwete na watu wake wakatangaza kuwa watalishitaki gazeti hilo (Nadhani ni Radi Tanzania) nchini Uingereza kwasababu gazeti hilo lilinukuu habari iliyochapishwa na Jarida la African Analysis la nchini humo.
Niwakumbushe kuwa ni Salva Rweyemamu ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu aliyetumwa London kufungua mashitaka dhidi ya Radi Tanzania na Jarida hilo la Uingereza na tukatangaziwa hivyo. Waandishi wa Tanzania leo hakuna anayeuliza kuhusu kesi hiyo kama kweli ilifunguliwa. Na kama ilifunguliwa, mashitaka yalikwendaje na kesi imekwishaje?
Lakini Waandishi wetu hawaulizi kwanini mtu yuleyule anayeandikwa kwamba alitoa dola milioni 40 ndiye huyo huyo ambaye alihusika katika mitambo ya kufua umeme wa dharura? Kwanini hawaulizi kwanii wanyama wanaouzwa nje ya nchi wanahusika na ukoo huo wa kifalme?
Watanzania, ni kweli kwamba kuendelea kukumbuka hali ilivyokuwa huko nyuma wakati nchi hii ikiwa na viongozi wasafi, ni kutafuta machozi. Lakini hebu tuanze kuvuta hisia, kama kweli Mwalimu Nyerere angekuwa fisadi, leo hii watoto wake wangeishi maisha ya kifahari sana. Mwalimu aliipenda Tanzania kwanza.
Leo tunaona kuwa watoto wa viongozi wetu ndio matajiri wakubwa. Wanapata wapi pesa zote hizo?
Mradi wa Gesi ambao leo unawatesa watanzania wenzetu ni matokeo ya miradi kandamizi na ya kifisadi. Mradi huu una manufaa kidogo kwa Wamakua, Wamakonde, Wayao na Wamwera kuliko watu wengine. Kusini ilitengwa sana,ilikabwa sana ni vema sasa ikaachwa nayo ipumue.