Hakuna aliye juu ya CHADEMA

Mzee wa nyeupe

New Member
Dec 4, 2013
3
0
KABLA ya kujadili mada hii, nataka niwe mwadilifu na muwazi kwa kutangaza kuwa nina maslahi katika Chadema. Mimi ni mwanachama wa muda mrefu wa Chadema, nilijiunga na chama hiki tangu mwaka 1992, nyumbani kwetu wilayani Kahama, mkoa wa Shinyanga.

Nimewahi kukitumikia chama kama kiongozi wa vijana wa wilaya yetu, ambapo nilipata fursa ya kusafiri vijiji mbalimbali wilayani humo katika juhudi zangu na viongozi wangu wa wilaya katika kukieneza chama.

Wakati huo viongozi na wanachama wa ngazi zote tulitumia fedha na rasilimali zetu binafsi kukitangaza chama, tumelala vijijini na kula chakula na wananchi, wakati mwingine tulikosa hata fedha za kujinunulia chakula vijijini ambako hatukuwa na wanachama wa kutukirimu na ilifikia wakati tulikunywa chai ya rangi na vitumbua viwili na kisha kwenda kulala.

Tulipata taabu kusafiri vijijini, tulitumia fedha kidogo za mauzo ya kadi kukodisha gari au baiskeli, lakini chama kilienea maeneo mengi ambapo wilaya yetu iliongoza kwa kuwa na matawi mengi katika mkoa wetu kiasi cha kuwavutia hata viongozi wa mkoa na taifa, ziara nyingi za viongozi wa kitaifa zilipangwa wilayani kwetu, na hayati Bob Makani akiwa katibu mkuu wakati huo alituzawadia baiskeli tisa kuunga mkono juhudi zetu za kueneza chama.

Kwahiyo, nakifahamu vizuri chama hiki kuliko wanachama na hata viongozi wengi waandamizi wa Chadema waliopo leo, nimetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya chama hiki.

Kwahiyo, leo hii wanapotokea baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema wanajiona kuwa masuper-star ndani ya chama, na kutaka watambuliwe kuwa wao ndio chama na chama ni wao, kwamba bila wao basi chadema haipo au kinakufa, tunalazimika kusimama na kuwapinga kwa nguvu zetu zote na kuwafungulia milango waondoke, wakatafute chama kingine ambako wataabudiwa na kutukuzwa kama miungu.

Kilichonisukuma kuandika makala hii ni propaganda za kipuuzi zinazoenezwa na kundi la waasi na wahaini katika chama waliovuliwa madaraka na Kamati Kuu ya Chadema wiki chache zilizopita, kwamba huo ndio mwisho wa uhai wa Chadema.

Kundi hilo la wasaliti likiongozwa na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Chadema Zitto Kabwe, kwa kusaidiwa na mabwana zao ambao ni viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) limekuwa likisambaza taarifa za uongo na upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii zinazoonyesha kuwa wanachadema wengi wanapinga uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwatimua madarakani Zitto na wafuasi wake Dk. Kitila Mkumbo ambaye alikuwa mjumbe wa kamati kuu, na aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa Arusha Samson Mwigamba.

Watu hawa wamekuwa wakijaribu kuchora picha kwa wanachama na wafuasi wa Chadema kwamba Zitto ndiye nguzo kuu ya kuimarika kwa chama, kwamba Chadema ni Zitto na kwamba bila Zitto hakuna chama.

Wanatumia mifano ya baadhi ya viongozi wanaojiuzulu na wanachama wanaotangaza kujiondoa katika chama hicho kwa madai ya kupinga uamuzi wa Kamati kuu ya Chadema kuwavua madaraka Zitto na wenzake, kama uthibitisho wa hoja yao kuwa Zitto alikuwa mhimili mkuu wa ustawi wa chama.

Hata baadhi ya waandishi wa habari nao wamenasa katika mtego huu wa propaganda ama kwa kutojua au kwa kujua lakini wanatumika na chama tawala kwa kulipwa ujira wa kazi zao na wengine wanafanya hivyo kutokana na uswahiba wao na kiongozi wa wasaliti Zitto kabwe.

Wanahabari hawa wamejigeuza mawakili wa Zitto na wamekuwa wakilaumu na kushutumu uamuzi wa kamati kuu wakiuita kuwa wa kidikteta na uonevu mkubwa, na wamekuwa wakihitimisha malalamiko yao kwa kutabiri kusambaratika kwa Chadema.

Nataka niwaambie watu hawa kuwa wanaota ndoto za mchana, watu hawa wanaonekana hawakijui vizuri chama hiki na hawana uwezo wa kufanya uchambuzi wa siasa za nchi yetu. Nataka niwaambie kuwa hata Zitto akiondoka kabisa katika chama Chadema hakiwezi kufa bali kitabaki imara.

Chadema hakikujengwa na Zitto, Dk. Kitila wala Mwigamba. Chadema hii tishio kwa CCM imejengwa na mwenyekiti wa sasa Freema Mbowe. Ni ubunifu wa Mbowe uliosaidia kuimarika Chadema na hata kufikia kuwa tishio kwa watawala. Ni Mbowe aliyeanzisha sare za chama za kombati, ni Mbowe aliyeanzisha utaratibu wa Chadema kutumia helkopta kufanya kampeni zake za uchaguzi, ni Mbowe aliyeasisi operesheni sangara na programu ya harakati za mabadiliko ya M4C.

Na kuna watu wengi wasiojua kuwa wakati Mbowe na viongozi wengine wa Chadema wakizunguka huku na kule nchini kujenga chama, Zitto amekuwa akitumia muda wake mwingi kujenga jina lake, kutafuta umaarufu na sifa binafsi kwa malengo binafsi.

Halafu inaonekana wazi watu wengi wanaomshabikia Zitto hawajui alikotoka na aliyemtengeneza kuwa mwanasiasa na kiongozi. Ni Mbowe huyu anayetukanwa na kudharauliwa leo aliyemuibua na kumtengeneza zitto kuwa mwanasiasa na kiongozi.

Baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti mwaka 2004, Mbowe alifanya mageuzi makubwa katika muundo wa sekretariati ya chama kwa kuanzisha mfumo wa kurugenzi, na aliwaondoa watumishi karibu wote wa makao makuu ya chama na kuleta timu mpya, miongoni mwao alikuwa Zitto ambaye aliteuliwa na Mbowe kuwa mkurugenzi wa mambo ya nje wa chama.

Mbowe aliendelea kumwamini Zitto na kumpa fursa za kujifunza siasa na uongozi wa kisiasa mpaka kufikia hapo alipo leo. Alimsaidia kwa hali na mali na hata kumsaidia kwa fedha za kumwezesha kuishi akimchukulia kama mdogo wake na kiongozi chipukizi wa chama chake na taifa kwa ujumla, alimpenda kweli kweli yeye na wenzake wakiwemo kina John Mnyika, John Mrema.

Ni mtu mjinga pekee na asiyemjua Zitto alikotoka, anayeweza kusimama leo na kudai eti Mbowe anamchukia Zitto na kwamba eti chuki hiyo inapindukia kiasi kwamba anafanya mipango ya siri ya kutaka kukatisha uhai wake!

Hivi Mbowe kusimamia misingi na katiba na kanuni za chama kama kiongozi mkuu wa chama ni chuki hiyo? Yaani Zitto na wapambe wake wanataka viongozi wa Chadema kuwafumbia macho viongozi na wanachama wakorofi na watovu wa nidhamu? Hivi leo hii Chadema wakiwa hawajapewa madaraka ya kuongoza nchi watashindwa kuwadhibiti wakorofi na watovu wa nidhamu katika chama, kweli wataweza kuwadhibiti mara baada ya kutwaa uongozi wa nchi?

Ni kweli kila mwanachama wa Chadema ana haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika chama au kutoa maoni ya namna chama chake kinapaswa kuendeshwa, hata hivyo lazima mwanachama afuate utaratibu uliowekwa na chama, yaani afuate katiba na kanuni za chama husika, si kiholela tu, maana kundi lolote lisilo na utaratibu ni sawa na kundi la walevi na wahuni.

Uamuzi wa Zitto na wapambe wake kuanzisha harakati za siri za kuuondoa madarakani uongozi wa chama uliochaguliwa kihalali, kujenga makundi ndani ya chama, kuwatukana na kuwazushia uongo viongozi wenzao na kuchochea chuki dhidi ya wanachama kwa viongozi wao, ni mambo yasiyokubalika hata kidogo.

Kufumbia macho au kunyamazia mambo haya ni kuruhusu fujo na ghasia katika chama, na chama cha namna hiyo hakina sifa ya kuwa chama cha siasa, maana chama cha siasa ni serikali inayosubiri kuingia madarakani, huwezi ukakipa madaraka ya kuongoza nchi chama kisicho na utaratibu wa kuendesha mambo yake, chama ambacho wanachama wake hawawaheshimu viongozi wao, na chama ambacho kila mtu ni mkubwa.

Ukikipa madaraka chama ambacho wanachama wake hawana heshima kwa viongozi wao wa chama, kuna hatari ya siku moja kupata serikali ya hovyo hovyo, serikali ya kihuni, serikali lege lege, maana inawezekana tukashuhudia kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, rais wa nchi anapingana na kubishana hadharani na makamu wake wa rais, waziri mkuu wake, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya na hata watendaji wa kata na watendaji wa vijiji.

Demokrasia haimaanishi kwenda bila utaratibu, maana hiyo siyo demokrasia bali ghasia. Na haya ndio matatizo yanayotukumba sisi tulio katika nchi changa kidemokrasia, maana watu wengi hususan viongozi na wanachama wa vyama vya siasa hawaelewi vizuri juu ya dhana hii nzuri na muhimu, wao wanafikiri kuwa demokrasia ni sawa na fungulia mbwa.

Zitto, Dk. Kitila, Mwigamba na wanachama wengine wa chadema wana haki na uhuru wa kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika chama na kukosoa viongozi wa chama wanapoona wamekosea, lakini lazima kufuata katiba, kanuni na taratibu za chama zilizopo.

Wanachama wa Chadema wanatoa maoni yao au kukosoa viongozi wao kupitia vikao vinavyowahusu, ukiwemo mkutano mkuu wa tawi ambako kila mwanachama ni mjumbe, halafu maoni hayo yanafika katika vikao vya juu vya maamuzi ya chama, yaani Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano mkuu wa Taifa wa Chadema kwa kufuata ngazi za vikao vya chama.

Kwa msingi huo Zitto na wenzake walistahili kuvuliwa nafasi zao za uongozi na nitaunga mkono uamuzi mwingine wa chama dhidi yao hata kama ni kuwafukuza uanachama. Hawa wamefukuzwa kutokana na makosa waliyofanya na wamefukuzwa kihalali maana walipewa nafasi ya kujitetea na kusikilizwa kwa haki kabla ya uamuzi wa kuwafukuza. Hii ni hatua muhimu ya kukiandaa chama kushika madaraka ya dola na kuunda serikali adilifu. Chama hakiwezi kuunda serikali yenye watendaji waadilifu kama kinakusanya wahuni, wazushi, waongo na waropokaji.

Kwa wale wanopinga uamuzi wa kikao halali cha chama milango iko wazi, wanaweza kuondoka waende wakatafute chama kingine au waunde chama kipya ambacho watafanya watakavyo, chama ambacho mwanachama akitaka kugombea uongozi anaruhusiwa kunda kundi la siri na kukusanya fedha kutoka vyanzo visivyojulikana ikiwemo kufadhiliwa na viongozi na wanachama wa chama adui.

Lakini wakibaki Chadema watambue kuwa chama hiki hakina super star, watambue kuwa hakuna mwanachama aliye muhimu kuliko chama chenyewe, watambue kuwa hakuna mwanachama aliye mkubwa kuliko chama, watambue kuwa hakuna mwanachama aliye na ushawishi kuliko chama chenyewe, watambue kuwa chadema kimejengwa juu ya misingi ya kuasisiwa kwake na siyo juu ya kichwa cha kiongozi au mwanachama yeyote, hivyo yeyote atakayekiuka misingi ya chama na kuanzisha uasi, uhaini na usaliti atashughulikiwa bila kujali cheo wala hadhi yake.

Mwisho

Makala hii imeandaliwa na George Maziku, Mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, nikiwa nimeifanya kazi hii kwa zaidi ya miaka 10. Wana-Jamii Forum mnapaswa kuchangia au kutoa maoni kwa hoja thabiti na siyo matusi.
 

Lunyungu

JF-Expert Member
Aug 7, 2006
8,863
1,250
Maziku umesema mengi mazuri .Mimi nina imani kabisa kwamba Mbowe hamchukii Zitto .Nina ushahidi mwingi si wa kuambiwa hapana .Pia napenda kukusahihisha Mbowe kafanya mengi lakini M4C imebuniwa na watanzania wapenda Chadema waishio USA .Ukitaka majina nitakupa lakini wote hao wana nia na wana jenga Chadema .Chadema watu wanatoa michango ya aina nyingi kwa njia mbali mbali .
 

Erythrocyte

JF-Expert Member
Nov 6, 2012
80,336
2,000
KAMANDA UMEANDIKA KIUKWELI SANA , NA TENA ANDIKO LAKO LIMEJAA UJASIRI WA HALI YA JUU SANA ! MUNGU akulinde sana mkuu .
 

nguvumali

JF-Expert Member
Sep 3, 2009
4,898
2,000
Tutawang'oa kwa heshima ya waasisi wa chama hiki ...mzee Mtei , hayati Bob Makani; Hayati Brown Ngwilulupi , Na wengine wote. Hatutakubali CDM iyumbe kwakulinda matapeli wachache
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom