Hadithi ya kusisimuwa: Mimba ya jini-16-
ILIPOISHIA:
"Wala usihofu, hawezi kukugusa mpaka mwezi uishe."
"Mmh! Sawa."
"Nina imani swali moja nimekujibu uliza lingine."
"Nafikiri hili ndilo la muhimu, mengine siyo muhimu sana."
"Mustafa yote muhimu, nipo hapa kukufanya uwe huru na kuondoa wasiwasi wote."
ENDELEA…
"Mmh! Anyway, hivi Shehna tulionana wapi kabla na kipi kilichokuvutia kwangu kupelekea kutaka kuzaa na mimi na kuwaacha wanaume wengi wasio na wanawake?"
Shehna kabla ya kujibu alicheka kidogo kisha alitabasamu huku aibu ya kike ikimtawala na kuanza kuchezea kucha na kupeleka vidole mdomoni. Mustafa alitumia muda ule kuusanifu uzuri wa Shehna na kushangaa aibu iliyompata kutokana na swali lake.
"Shehna kama swali langu limekuudhi naomba unisamehe, naweza kubadili swali," Mustafa alijihami.
"Hapana, sivyo hivyo swali lako lazima nilijibu kwa vile nipo hapa kwa ajili ya kuondoa wasiwasi wa moyo wako. Mustafa huwezi kuamini nimekupenda muda mrefu sana hata kabla ya kuwa na Husna.
"Mapenzi yangu hayajaanza leo ni muda mrefu nimekuwa nakupenda. Katika maisha yangu nilitamani uwe mume wangu lakini kuna vikwanzo ambavyo vilisababisha nichelewe kukueleza ukweli wa moyo wangu.
"Bahati nilipata safari ya ghafla na kuondoka bila kukueleza dhamira yangu ungeweza kunisubiri. Niliporudi nilikuta tayari umeoa lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kutaka hata nipate angalau ukumbusho wa sura yako, ndiyo maana nikataka kuzaa na wewe.
"Wakati napanga hivyo, niligundua una maumivu moyoni mwako kutokana na kuchelewa kupata mtoto. Baada ya kufanya uchunguzi, ilionesha umepoteza fedha nyingi kwenda kwa waganga bila mafanikio. Niliamini nikitatua tatizo ambalo limekunyima furaha, utakuwa tayari kunisikiliza na mimi shida yangu.
"Ndipo nilipokutafuta kwa njia ya simu na kukupa maelekezo ambayo mwenyewe uliona maajabu lakini kiburi cha mkeo kikaharibu kila kitu.
"Kwa vile nilipanga baada ya wewe kupata mtoto ndipo na mimi nipate wangu, basi baada ya mkeo kuvuruga ratiba, itabidi unipe kwanza mimi ujautito ndipo nikupe dawa ya kutafuta mtoto mwingine ambayo mkeo anatakiwa kuwa makini kosa lingine litamfanya awe tasa, hatazaa mpaka anakufa.
"Mustafa kama nilivyokueleza mapenzi yangu kwako hayakuanza leo bali muda mrefu, tumeonana sehemu nyingi lakini inaonesha umenisahau. Unakumbuka siku moja tulikutana ukitoka kufanya usaili ambapo ulikuwa mnyonge baada ya kujua amefanya vibaya.
"Nilikueleza kuwa pamoja na kufanya vibaya lazima jina lako litachaguliwa kati ya matano na kubakishwa jijini Dar. Najua ulishangaa lakini baada ya muda, ilitokea kama nilivyokueleza. Unakumbuka ulikutana na nani akakueleza habari zile?"
Maneno yale yalimfanya Mustafa ashtuke na kurudisha kumbukumbu nyuma miaka nane iliyopita. Siku aliyokwenda kufanya usaili wa kazi ambako walitakiwa watu watano katika watu mia moja waliokuwepo. Katika watu waliofanya vibaya katika usaili ule yeye alikuwa mmoja wapo, katika maswali kumi aliyoulizwa alijibu matatu hata nusu hakufika.
Hata waliokuwa wakiwafanyia usaili, walimkatisha tamaa baada ya kumweleza hakuweza kufika nusu tofauti na wenzake zaidi ya sabini waliotangulia. Aliondoka akiwa hana matumaini.
Lakini alipotoka nje ya ofisi ili aelekee nyumbani, aliitwa na msichana aliyekuwa amevaa hijabu iliyomziba mwili mzima na kuonekana macho.
"Mustafa."
"Naam," aligeuka kumtazama aliyeonekana anamfahamu, hakuweza kumuona uso zaidi ya macho.
"Pole."
"Ya nini?"
"Ya kufanya vibaya.'
‘Umejuaje?"
"Mbona umeniangusha kwa nini umeshindwa kujibu maswali yale mepesi?"
"Yaani hata sijui."
Yule msichana aliyarudia maswali yale na kumuuliza:
"Sasa hapa swali gani gumu?"
"Yaani hata mimi nashangaa, basi tena nitajaribu sehemu nyingine."
"Mbona umekata tamaa mapema?"
"Kama nimefanya vibaya huku zaidi ya watu sabini wamefanya vizuri huku nafasi tano tu zinatakiwa, kuna nini hapo?"
"Usiwe na wasiwasi katika hizo nafasi tano, wewe utakuwemo na ndiye utakayebakia Dar."
"Wewe nani?"
"Mustafa shida yako kujua mimi nani au wewe kupata kazi na kuteuliwa kubakia Dar?"
"Shida yangu kupata kazi."
"Basi subiri muda ufike."
"Nitajuaje?"
"Utapigiwa simu."
"Wataijuaje namba yangu ya simu wakati hawakuchukua kwa vile ni mmoja ya watu waliofanya vibaya."
"Namba yako nitawapa."
"Namba yangu umeipata wapi?"
"Mustafa hujawahi kuigawa namba yako?"
"Nimegawa basi nitashukuru japokuwa najua hakuna kitu."
"Siku tukikutana utaniambia."
Itaendelea kesho wakati kama huu.