Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

Ndo nimesoma Hapa Kaka Umeiludia Ep moja mara tatu sema sio mbaya Ngoja Tusubiri.
 
Itakuwa imejichanganya muda wa kucopy
 
Hii hadithi kama movie ya tenet vile matukio yanajirudia naona nimesoma sehemu zile zile mara kumi
 
NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
SEHEMU YA 14

Bi. Semeni alikuwa mchawi kama wachawi wengine, kila mtu aliyekuwa akihamia mtaani ilikuwa ni lazima kumjaribu kuona alikuwa na nguvu gani, hilo ndilo ambalo alitaka kulifanya hata kwa Bazoka ambaye alihamia nyumbani kwake hapo.
Usiku kabisa akajiandaa kwa ajili ya kwenda kufanya uchawi wake kama kawaida, aliondoka kitandani, nafsi ikaenda kuwanga huku mwili wake ukibaki kitandani hapo, akatokea chumbani kwa Bazoka ambaye alikuwa amelala huku akiwa hana lolote lile.
Bi. Semeni alisimama pembeni huku akiwa na mtupu kama alivyozaliwa, uso wake ulikuwa na masizi, kiunoni alikuwa na shanga kubwa na mkononi mwake alikuwa na tunguli, alimsogelea BAzoka pale kitandani alipokuwa na kuanza kumwangalia.
Hakuwa na kinga yoyote ile, hilo likamfanya Bi. Semeni kuanza kumuwangia huku akionekana kuwa na furaha kabisa, alimchezea alivyotaka, alimchukua na kumpeleka huko kwa wenzake, kila mmoja alimsifu kwani kwa kitendo cha kumpeleka mtu mpya kwenye kundi la wachawi kama alivyokuwa amefanya ilikuwa sifa kubwa mno.
Walicheza ngoma zao, walifurahia na baada ya hapo wakawapeleka shambani ambapo walilima na kurudishwa baadaye kabisa.
Sasa moyo wake ukaridhika, alitaka kujihakikishia kama mtu aliyekwenda kupanga kwake alikuwa na nguvu za namna gani, hakuwa na lolote lile, yaani alikuwa mtupu kabisa.
Asubuhi ilipofika, Bazoka akaamka usingizini, alikuwa amechoka mno, haikuwa kawaida, alihisi kama alitoka kufanya kazi nzito, alikuwa akijiuliza lakini hakuata jibu lolote lile.
Akatoa shuka mwilini mwake, kilichomshangaza, miguu yake ilikuwa michafu mno, hapo hakutaka kujiuliza tena, alijua kilichokuwa kimetokea, yaani alichukuliwa usiku wa manane na kwenda kufanyishwa kazi za shambani, na mtu aliyefanya hivyo hakuwa mwingine bali alikuwa Bi. Semeni.
Hakutaka kujali kwani alijua tu mwanamke huyo hakuwa hata na wiki mbili za kuendelea kuishi, akasimama kutoka kitandani na kwenda kuoga, alipomaliza, akatoka ndani na kuelekea ukumbini ambapo akamkuta Bi. Semeni akiendelea na mambo yake.
“Mama! Shikamoo!” alimsalimia huku uso wake ukiwa na tabasamu pana kana kwamba hapakuwa na lolote lile lililotokea.
“Marahaba mwanangu hujambo!” aliitikia.
“Sijambo tu! Pole na kazi!” alimwambia.
“Nashukuru!”
Wakaanza kuongea kwa dakika kadhaa, kila mmoja alionekana kuwa na furaha kumuona mwenzake asubuhi hiyo, baada ya dakika kadhaa, Bazoka akaondoka na kuelekea kwenye biashara zake.
Hakutaka kuwasiliana na mtu yeyote yule kwa kutumia simu, aliitoa laini yake, akanunua nyingine mpya kwani hakutaka mkewe kumpata kabisa, alichokuwa akikifanya ni kuwasiliana naye kwa kutumia WhatsApp tu, alifanya hivyo kwa kuwa alitaka kumuaminisha alikuwa nchini Uganda.
Akataka kuonana na washikaji zake, Bonge na Sultani, hilo halikuwa tatizo, akawapigia simu na baada ya kukubaliana, wakaonana mahali na kuanza kupata kifungua kinywa pamoja.
“Yaani sijakuelewa...” alisema Bonge.
“Nimepanga chumba maeneo ya Magomeni,” alisema Bazoka huku akiwaangalia wote wawili.
“Kwa sababu gani?”
“Si unajua nimeambiwa nimtafute bibi kwa ajili ya kumtoa kafara?”
“Ndiyo!”
“Sasa hiyo nyumba inamilikiwa na huyo bibi, halafu ndani tupo wawili tu,” alisema Bazoka na kuanza kucheka.
“Aisee safi sana, yaani hapo kazi inakuwa rahisi mno!” alisema Sultani.
“Kaka hii kazi si rahisi kama inavyoonekana!”
“Kwa sababu gani?”
“Huyo bibi mchawi sijapata kuona!”
“Bibi mchawi?”
“Ndiyo! Kwanza niliambiwa mtaani!”
“Sasa si unajua stori za mitaani Bazoka...”
“Halafu usiku nikapelekwa shamba kulima!” aliwaambia.
“Ulipelekwa shamba kulima?” aliuliza Bonge huku akishangaa, mshangao wake ukakatishwa na kicheko kikubwa kutoka kwake.
“Hahahaha...”
“Ebwana kwanza uchawi upo,” alisema Bazoka!”
“Ilikuwaje?”
“Yaani sijui! Mi’ niliamka asubuhi, nikajikuta nimechafuka kishenzi, miguu ilikuwa na tope, halafu jana usiku kabla ya kulala nilioga,” aliwaambia.
“Pole sana!”
“Sasa huyo bibi anaulika kweli?” aliwauliza.
Wakaangaliana na kuanza kucheka.
“Sasa mbona mnacheka?” aliuliza kwa mshangao.
“Bazoka! Hizo nguvu zako ni hatari sana, yaani una nguvu huyo bibi haoni ndani, kumbuka ulikwenda kuzimu, sehemu ambayo kila mchawi anapenda sana kwenda,” alisema Sultani.
“Kwa maana hiyo nguvu zangu ni kubwa mno?” aliuliza Bazoka huku akionekana kushangaa.
“Ndiyo!”
“Sasa mbona ilikuwa kirahisi sana kupelekwa shambani kulima mpaka mgongo unauma?” aliuliza.
“Kwa sababu hukuamua kujilinda!”
“Lakini si umesema nina nguvu tayari?”
“Kwani ukishika bunduki halafu mtu akitaka kukuua, hawezi kukuua?”
“Anaweza!”
“Kwa nini akuue na wakati una bunduki mkononi?”
“Kwa sababu sikuitumia!”
“Basi hilo ndilo jibu lake.”
Bazoka akakaa kimya kwanza, maneno aliyoambiwa yalikuwa na maana kubwa, ni kweli alikuwa na silaha lakini hakutaka kuitumia na ndiyo maana ilikuwa ni rahisi sana kwa Bi. Semeni kumfanya kama alivyotaka kufanya.
Hilo lilimuumiza mno lakini pia akaona hata kama alikuwa na silaha huo haukuwa muda muafaka wa kuhama, ilikuwa ni lazima kuhakikisha anafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anamnaliza mwanamke huyo.
Akauliza namna ya kutumia hizo nguvu, akaambiwa kabla ya kulala ilikuwa ni lazima kutamka maneno mawili, Mulfadhir Bilaal na kisha kulala.
Aliambiwa maneno hayo yalikuwa na nguvu kubwa, kila alipokuwa akiyatamka na kulala kulikuwa na nguvu kutoka kuzimu ambazo zilikwenda moja kwa moja mpaka chumbani kwake na kumlinda.
Kulikuwa na majini yaliyokuwa na nguvu kubwa ambayo yalikuwa na kazi kubwa kuhakikisha watumishi wao wanakuwa salama kabisa, hivyo endapo angeyatamka maneno hayo na kuidhinishwa kwamba aliwahi kufika kuzimu na kupewa nguvu, basi moja kwa moja angekuwa na ulinzi tosha ambapo kusingekuwa na mchawi yeyote yule ambaye angembabaisha kwa lolote lile.
“Kumbeeeee...”
“Fanya hivyo!”
Bazoka alikuwa na akili nyingi, hakutaka kuona akimmaliza mwanamke huyo haraka kwa sababu watu wangejua kwamba ni yeye ndiye aliyefanya hivyo kitu ambacho hakutaka kijulikane kabisa.
Siku hiyo aliendelea na biashara zake kama kawaida lakini hakurudi nyumbani kwake wala kuwasiliana na mkewe, alikaa kwa saa kadhaa akampigia simu Frank na kumwambia alitaka kuonana naye
Kwa kuwa tayari walikuwa marafiki, hapakuwa na tatizo, wakaonana maeneo ya Kinondoni, wakawa wanakula huku wakizungumza mambo mbalimbali. Alimuuliza kuhusu mkewe, Sarah, alikuwa akiendelea vizuri na matibabu hospitalini, hali yake ilitengemaa.
“Ebwana Frank sasa nimeamini yule mwanamke mwanga,” alisema Bazoka, Frank kusikia hivyo, akajiweka vizuri kusikiliza alichotaka kuambiwa.
“Ilikuwaje?”
“Kaniwangia usiku, nimeamka viungo inauma mno, halafu miguu michafu kichizi,” alijibu Bazoka huku akianza kutabasamu.
“Acha masihara!”
“Kweli tena! Yaani mimi pale nahama,” alimwambia.
“Ila nilikwambia kaka, ukabisha, umeona sasa?”
“Aisee kweli! Pale nahama, mi sijazoea kukaa nyumba za wachawi kama ile,” alisema Bazoka, alifanya hivyo kwa malengo yake maalumu.
Alizungumza na Frank na baada ya kumaliza kuondoka kurudi nyumbani. Njiani walikuwa wakizungumza mambo mengi, alichomwambia ni kwamba Bi. Semeni hakutakiwa kujua kama alikuwa na usafiri kwani alihisi mambo yangekuwa mabaya zaidi, hivyo aliliweka gari lile sehemu ya kupaki na wao kuanza kutembea kuelekea nyumbani.
Alipofika, Bi. Semeni hakumkuta lakini alikuta milango ikiwa wazi kabisa. Bi. Semeni hakuwa na kawaida ya kufunga milango ya nyumba yake, alikuwa akiiacha wazi na hapakuwa na mwizi yeyote aliyekuwa akisogea kwa sababu kilichotokea mwaka 2016 kilikuwa balaa.
Mwanaka huo wakati vijana wengi wakiwa hawajui kama mwanamke huyo alikuwa nguli kwenye mambo ya uchawi, aliacha milango wazi na kutoka, vijana wawili waliokuwa na tamaa wakaingia na kuiba walipotoka, wakiwa nje, wakasimama huku wakiwa na vitu walivyoiba mikononi mwao.
Walikuwa wakipiga kelele za maumivu makali, wapita njia walikuwa wakiwashangaa, hawakujua kilichokuwa kikiendelea, walisimama tu, hawakupiga hata hatua, yaani miguu yao ni kama iliwekewa gundi, hata kusogeza walishindwa.
Walikuwa wakijisema tu kwamba walikuwa wezi, waliingia ndani ya nyumba hiyo kwa lengo la kuiba lakini walishindwa kutoka. Umati mkubwa wa watu ulikusanyika na kuwaangalia watu hao, hawakutoka mpaka Bi. Semeni aliporudi nyumbani kwake, aliwaangalia, hakutaka kuzungumza kitu chochote kile, akaingia ndani kwake, akatoka na unyoya wa kuku na unga mweusi, akawapulizia na unyoya ule kuwachapa nao, hapohapo wakatoka, wakapiga hatua na kuanza kuomba msamaha.
Kuanzia siku hiyo hapakuwa na mwizi aliyethubutu kuingia ndani ya eneo la nyumba hiyo, kuliogopwa zaidi ya ikulu, kulikuwa na ulinzni mkubwa kuliko sehemu yoyote mtaani hapo, ulinzi ambao haukuonekana kwa macho.
Baada ya kuingia, moja kwa moja Bazoka akaelekea mpaka uani, alipofika huko akaanza kuangalia mazingira ya huko, kulikuwa na ukuta, akaupanda, upande wa pili kulikuwa na kichochoro ambacho aliamini angeweza kupanda ukuta huo na kutumbukia humo ndani.
Alitakiwa kufanya mambo kijasusi sana, kusiwe na mtu yeyote ambaye alitakiwa kugundua kilichokuwa kimetokea, hivyo haraka sana akaelekea chumbani kwake kwani alisikia kama mtu akiwa ameingia ndani ya nyumba hiyo, kabla hajafika chumbani, ukumbini akakutana na Bi. Semeni ambaye naye ndiyo alikuwa amerudi.
“Mama! Kumbe umerudi,” alimwambia huku akimwangalia.
“Ndiyo! Unaendeleaje? Umetoka wapi tena?” alimuuliza huku akimwangalia.
“Nimetoka chooni!”
“Chooni! Cho cha uani? Kivipi na wakati chumbani kwako kuna choo?” aliuliza mwanamke huyo huku akimwangalia kwa mshangao.
“Nilibanwa na haja hata chumbani nilipaona mbali,” alijibu Bazoka huku akijifanya kutabasamu.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Pole sana jamani!” alisema mwanamke huyo.
Moyoni mwake akaanza kuwa na wasiwasi na Bazoka, aliamini kabisa hakuwa ametoka chooni kwani hata mikono yake haikuwa imelowanishwa kwa maji, alihisi kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea lakini hakujua kilikuwa kitu gani.
Kwa kufanyiwa ubaya aliamini asingeweza kumfanyia, sasa kijana huyo alikuwa na jambo gani lililokuwa likiendelea nyuma ya pazia?
“Nitajua tu!” alijisemea, hakujua kama naye Bazoka alijipanga, alitaka kummaliza mapema sana.
Upande wa pili baada ya Frank kuambiwa na Bazoka kile kilichotokea, haraka sana akaanza kuwaambia watu kuhusu hilo, stori zikaanza kusambaa kwamba Bi. Semeni kama kawaida yake alimroga mpangaji wake na muda huo alifikiria kuhama kama wengine walivyofanya.
Watu walicheka lakini walimshangaa mno Bazoka, kwa maelezo ya Frank ni kwamba alimuonya kabla kwamba mwanamke huyo alikuwa mchawi mkubwa lakini jambo la ajabu kabisa, akawa king’ang’anizi na kwenda kupanga nyumbani hapo.
“Ila jamaa mbishi! Mi nilifikiria ana kinga kumbe mweupe kabisa,” alisema Frank huku kwa mbali akitoa kicheko.
“Kwa hiyo ulimwambia?”
“Yaani zaidi ya mara hamsini, cha ajabu eti akaenda kupanga, jamani jamani sisi binadamu wabishi sana,” alisema Frank, hakujua sababu ya mtu huyo kwenda kupanga ndani ya nyumba hiyo, endapo wangejua, basi kila mtu angemshukuru Mungu kwamba hatimaye mwisho wa Bi. Semeni ulikuwa umewadia.

Je, nini kitaendelea?
 
Pamoja
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…