Hadithi: Nalutuesha

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Jan 31, 2021
7,067
12,439
JANGA

Eeh uliye kwenye mawingu, uliye mkubwa kuliko wote, tunaomba utusalimu kwa mwanga wako ili tujue iwapo u-hai. Eeeh Ingatambo mungu wa nchi yetu, tusaidie. Hiyo ilikuwa ni sala iliyotoka kwa mtindo wa kilio ikitolewa na wakazi wa Serengeti wakiongozwa na waganga wao na machifu.

Ni karibia mwaka wa tatu tangu mvua inyeshe kwa mara ya mwisho kwenye tambarare za Serengeti. Nchi yote ilikuwa imegeuka rangi na kuwa ya kaki kwa ukame. Vumbi lilikuwa limetimka na kujaa angani hadi kuna wakati ilikuwa ni vigumu kuonana. Sehemu nyingine vumbi lilikuwa jeupe kama unga na sehemu nyingine lilikuwa jekundu kama damu. Kuna sehemu nyingine inasemekana vumbi lilikuwa na kina kirefu hadi liliwafika twiga magotini! Kulikuwa hakuna majani hata kwenye mti mmoja.

Hali ilikuwa mbaya hadi miti iliyokuwa kando ya mito na mabwawa ilikuwa imepukutisha majani. Miti yote ilikuwa imebaki na matawi ya juu tu na haikuwa na magome. Baada ya wanyama kula nyasi zote, wakaanza kula majani ya miti na kisha wakaanza kula magome. Urefu na uzoefu wa twiga wa kula majani ya miti haukuwasaidia kitu. Kwanza miti karibu yote ilipukutisha majani na ile iliyobaki na majani iligombaniwa na wanyama wa kila aina. Wanyama walibuni mbinu mbalimbali za kujipatia chakula kutoka kwenye miti. Ilikuwa kitu cha kawaida kukuta wanyama wa aina tofautitofauti, wakubwa kwa wadogo wakishirikiana kuangusha mikwaju, mipogoro na miti mingine mikubwa. Tembo walikuwa wakibandua magome ya mibuyu na kufyonza maji yake. Kila mnyama alibuni mbinu za kujipatia chakula na maji.

Watoto waliozaliwa hawakuwa wakijua chochote kuhusu nyasi. Wengi walijenga picha kuwa nyasi ni nyekundu, nyeupe au kaki, kulingana na rangi ya vumbi kwenye eneo lao. Wengine walifikiri nyasi ni mipogoro midogomidogo, milaini, isiyo na miiba. Wanyama wakubwa nao walikuwa wanajiuliza, iwapo mvua ikija tena, je, nyasi zinaweza kuota kutoka kwenye lile vumbi? walijiuliza iwapo kwenye lile vumbi laini kama unga bado kuna mbegu.

Kwenye mwaka wa kwanza wa ukame, nchi ilikuwa imejaa miiba mitupu. Hii ni sababu miti mingi ya miiba ilikuwa imeangushwa na kutawanywa huku na kule. Ilikuwa kitu cha kawaida kukuta wanyama wakubwa kwa wadogo wakichechemea. Kuna hadithi kuwa hadi nyoka waliacha kutambaa sababu ya miiba! Baada ya mwaka na nusu, miiba hiyo ilikuwa imepigwa na jua kiasi kwamba hata ikikanyagwa inageuka kuwa unga. Wanyama wengi walikuwa wanaugua magonjwa ya upumuaji na macho, ilisadikika ni sababu ya vumbi lenye sumu iliyotoka kwenye miiba iliyosagika.

Kipindi hicho, si tu kwamba mvua haikunyesha, bali hata jua lilionekana kama limeongezwa ukali kuliko kawaida. Pamoja na kuwa kabla ya ukame mvua nyingi sana ilikuwa imenyesha lakini madimbwi, hata yale yanayotegemewa kipindi cha kiangazi yalikauka miezi michache baada ya mvua kuisha. Mito na madimbwi vilikauka kwa kasi ya ajabu. Kulikuwa na upungufu wa maji kila kona. Mwanzoni wanyama walikusanyika kando ya mito na vidimbwi lakini vilikauka baada ya muda mfupi, walianza kuchimbachimba kwenye matope na mchanga hadi kulipokuwa hakuna maji tena. Kutoka hapo wakahamia kwenye magome ya miti, miti yote yenye maji kama mibuyu ililiwa magome yote na kubaki myeupe pee.

Samaki, mamba na viboko walikuwa na hali ngumu zaidi. Samaki walikuwa wanakufa kwa mamia, ndiyo walikuwa wanyama wa kwanzakwanza kufa kwa wingi. Kuna dimbwi moja baada ya samaki kufa sana kutokana na upungufu wa maji na kubaki tope, mamba na viboko wakakaa kikao. Mkuu wa mamba kwenye eneo lile bwana Kinyang akaanza kwa kusema.

"Ndugu zangu, nimewaita hapa tujadili mustakabali wa uhai wetu. Baada ya kujadiliana na kiongozi wa viboko bwana Sapuki, tumefikia muafaka kwamba makao ni muhimu kama tu chakula na maji vilivyo muhimu. Mnyama anaweza kufa kwa kukosa makao kama tu anavyoweza kufa kwa kukosa chakula au maji. Tena inawezekana makao ni muhimu zaidi. Tuchukulie mfano Simba, makao yao ni nchi kavu, je nchi yote hii tukijaza maji, wanaweza ishi kwa muda gani? Sisi makazi yetu ni kwenye maji, hatuwezi ishi muda mrefu bila maji, ili tuwinde tunahitaji maji ya kutuficha, au nyie mmewahi kuona mamba anazunguka zunguka nyikani mchana akikimbiza swala na nyumbu na usiku analala chini ya mbuyu? Kwa jua hili kali, viboko wanaweza kuishi kwa muda gani bila maji? Samaki wanaweza kupumua bila maji? Makazi yetu ni kwenye maji na uhai wetu unategemea maji."

"Ndugu zetu samaki wamekufa kwa mamia sababu hawawezi pumua bila maji, walau sisi tunaweza. Kwa kweli ndugu zetu wamekufa vibaya sana, ni kama kifo cha kukabwa koo la hewa." Akasema Kinyang kwa sauti ya kusikitika huku machozi yakimlengalenga, kisha akaendelea. "Sasa tumefikia muafaka kuwa, dimbwi hili ni muhimu kwa uhai wetu, hivyo hatutamruhusu mnyama, ndege au mdudu yeyote kunywa maji kwenye hili dimbwi. Ingatambo shahidi yetu. "Ni kweli kabisa, na iwe hivyo" ilisikika sauti kubwa ya viboko na mamba. Mamba mmoja kwa jina Ol kinos akanyoosha mkono na kuuliza; "sasa kama tutawakataza kuja kunywa maji, sisi mamba tutapata wapi chakula?" ''tutakula wakaidi," akajibu Kinyang kwa ufupi. Kuanzia siku hiyo, walimfukuza kiumbe yeyote aliyekuja kunywa maji dimbwini, iwe mchana au usiku.
 
Kawaida matatizo yanapotokea kuna baadhi ya wanyama hufaidika. Ndivyo ilivyokuwa kwa wanyama wala nyama wa Serengeti. Mwanzoni wakati wa ukame wanyama wengi walikuwa dhaifu kwa kiu na njaa. Wanyama wala nyama waliwakamata kwa wingi na kwa urahisi. Kwahiyo, wakati wanyama wala nyasi wakikonda na kufa kwa kiu na njaa, wenzao wala nyama walinenepa na kunawiri. Wanyama wengine walijitapa kuwa wameacha kunywa maji bali wanakunywa damu. Waliua wanyama ili wanywe damu tu. Simba, fisi, duma, chui, mbweha na mbwa mwitu 'walikula na kunywa'. Fisi waliacha kula mizoga, walisema eti ni ya baridi. lakini sherehe hii ya wanyama wala nyama haikudumu kwa muda mrefu.

Baada ya miezi kadhaa wanyama wengi walikuwa wamekufa na kutawanyika kiasi kwamba ilikuwa ngumu kuwapata. Wanyama wala nyama walianza kupigana na kuuana ili kupata chakula. Simba walivamia maeneo ya simba wengine ili kufuata mawindo na kuzua mapigano makali. Simba nao walianza kula mizoga. kipindi hicho ilisemwa "Simba mwenye njaa hula mizoga!" Kipindi cha njaa hata nyasi hupotea, hubaki mizoga tu. Baada ya muda wanyama wala nyama nao wakaanza kufa kwa kiu na njaa kama wanyama wala nyasi.

Njaa na ukame huo havikuacha ndege wala wadudu. Ndege ndiyo waliokuwa na hali mbaya zaidi. Kwanza, baada ya nyasi kuadimika, wanyama wengine wakaanza kula viota vya ndege. Ikabidi ndege waache kutengeneza viota vya nyasi na majani bali vya vijiti na miiba. Hivi vilitoboa mayai yao wakati wa kuyageuza na kudhuru vifaranga wao. Pili, ukitoa tatizo la kiu na njaa lililowapata wanyama wote, ndege walikuwa na tatizo jingine kubwa. Wanyama wengine waliwashutumu ndege kuleta ukame kwa kumuudhi Ingatambo. Walisema kwa kuwa ndege ndiyo wanazurura angani, basi wao ndiyo wamemuudhi mungu.

Nadharia iliyokuwa imeenea sana ilikuwa ni hii. Ilisemekana ndege walikuwa wamechukia sana kwa sababu mvua kubwa kabla ya ukame ilikuwa imeua vifaranga wao na kuharibu viota vyao. Ilisemwa kuwa ndege walikaa kikao ili kumfukuza Ingatambo aliyeleta mvua hiyo. Wakaafikiana kuwa wapae hadi kupita mawingu na kisha kwa pamoja wajisaidie ili kinyesi kimuangukie Ingatambo, jambo litalomfanya ahame. Kabla ya hapo ilikuwa ni marufuku kujisaidia ukivuka mawingu na ni ndege wachache tu ndiyo waliruhusiwa kuruka kupita mawingu, na ilikuwa kwa shughuli maalumu kama kupeleka sala. Ndege walikana sana hili shtaka. Walisema "kama ni hivyo basi siku ya tukio kungekuwa na ushahidi wa mvua ya kinyesi." Wengine walisema" ukivuka mawingu, hewa ni nyepesi hivyo si kila ndege anaweza kupaa huko, labda ndege wadogo na wadudu kama vipepeo ndiyo wanaweza," utetezi wao haukufaa kitu. Wanyama waliungana dhidi yao, walikuwa wamepata wakumtupia lawama. Mahakama ya umma ilikuwa imeshaamua ndege ni wakosaji, la sivyo, kwanini mungu achukie?

Ndege walifukuzwa kutoka kwenye madimbwi ya maji, walifukuzwa popote walipotua, wengi walikufa kwa uchovu wa kupaa angani kwa muda mrefu. Viota vyao vilibomolewa, mayai yao yalivunjwa na kuliwa. Walifanyiwa kila aina ya ubinadamu. Hata ndege wasioruka kama mbuni hawakuepuka ubinadamu huo. Mbuni walijitahidi sana kujitetea kuwa wao siyo ndege! Kipindi hicho ndipo kulizuka ubishi mkali iwapo popo ni ndege au ni mnyama. Hata kirukanjia alikuwa na wakati mgumu sana kuthibitisha kwamba yeye si ndege.

Wadudu wanaoruka nao walihusishwa kwenye uhalifu huo dhidi ya Ingatambo, japo wao hawakutendewa vibaya sana kama ndege. Kuna kipindi mchwa nao walihusishwa na huo uhalifu. Ilifafanuliwa kuwa, kwa kuwa baadhi ya mchwa hugeuka kuwa kumbikumbi na kuruka basi nao ni ndege na wanahusika. Ikabidi baraza la waganga na machifu kuingilia kati kutengua hilo na kusema "huko tunafika mbali, tukitafuta sana wachawi, tutajipata wenyewe"

Wadudu watambaao nao walikuwa na shida yao. Inasemekana mchwa waliungua hadi kufa kutokana na joto ndani ya vichuguu vyao. Wakitoka ndani ya vichuguu walikuwa wanakauka ndani ya muda mchache kwa jua. Usiku wanyama walikuwa wanavizia nje ya vichuguu kuwala.

Wakati wa majanga jamii huwa zinabadilika kabisa, uendeshaji wa mambo hubadilika na roho pia hubadilika. Hicho ndicho kipindi tawala huanguka na nyingine kuinuka. Kipindi ambacho roho ya ukatili na ubinafsi huonekana waziwazi. Mfano, hadi leo, huko Serengeti kuna msemo unasema, " mngekuwa mnakula nyama, mngekula wana wenu." Ulianza hivi.

Baada ya njaa kuwa kali sana, wanyama wala nyama wakaanza kulana wao kwa wao. Ikafika kipindi wazazi wakaanza kula watoto wao. Hili jambo liliwashangaza sana wanyama wala nyasi. Waliwashutumu na kuwasema wanyama wala nyama kotekote walikowakuta. Siku moja kwenye kikao cha mgawanyo wa maji na maeneo ya malisho, nguruwe pori mmoja akaanza kujisemesha (baada ya kuwaona simba wakipita mbele yake) "wanangu! wanangu kabisa! hata njaa iniume vipi, siwezi kula wanangu".

Baada ya simba mmoja kuchukizwa na maneno hayo, akamgeukia na kumwambia. "Acha unafiki kujidai kujisemeshasemesha, je nyie kati yenu hakuna wanaogoma kunyonyesha watoto ili wao wasife, si tunasikia kati yenu kuna madume yanaua ndama ili yao yanyonye!? Siyo nyie mnawapa mamba ndama wenu ili mnywe maji? Mnatofauti gani na wanaokula wana wao?" Akasema Simba yule huku akiwa amepandwa na hasira, akamsogelea yule nguruwe na kuendelea kumwambia, "mngekuwa mnakula nyama mngekula wana wenu." Kwa jinsi hasira zilivyompanda yule simba angemrarua yule nguruwe sema sheria za vikao haziruhusu kupigana au kuwinda wakati wa vikao. Rafiki wa nguruwe pori walikaa kimya kwa aibu, nguruwe pori alikuwa akiangalia huku na huku kwa aibu.
 
Wakati wa majanga makubwa kitu kinachofanya mambo yaharibike haraka ni kuvunjika kwa mfumo wa uongozi. Ili jamii isitawi na iwe na amani ni lazima iongozwe kwa sheria na taratibu. Wakati wa majanga hiki ndiyo huwa kitu cha kwanza kuvunjika. Kila mnyama huanza kufanya anachoona ni sahihi, hufanya kitu kinachomfanya aishi bila kujali sheria na taratibu. Wanyama wengine huunda magenge na vikundi, nchi husambaratika kabisa. Hicho ndicho kilichotokea Serengeti kipindi kile cha njaa. Wanyama walijimegea vipande vya maeneo na kujitangazia kuwa ni nchi zao. Hakuna aliyesikiliza chifu wala mganga. Chifu hakutokana na kurithi bali wanyama wababe na katili ndiyo walikuwa machifu.

Kitu kingine kilichotokea kipindi hicho cha njaa ni magonjwa. Wanyama walianza kupata magonjwa makali ya mapafu, huu ugonjwa uliua wanyama wengi sana.
Jambo jingine liliwasumbua wanyama karibu wote wakati wa ukame huo ilikuwa na kung'oka meno. Karibu wanyama wote walikuwa wanakula kwa kumeza. Wanyama wengine walikuwa wakisema.
"Mbona ndege waliosababisha haya majanga meno yao hayang'oki?" wengine wakasema "yale siyo meno, ni aina ya mapembe"

Ndege nao wakasema. "kama sisi ndiyo tumeleta majanga, mbona hatuadhibiwi kwa kung'oka meno.'' Kila tukio lilikuwa na maelezo yake! Kila mtu alieleza inavyomfaa.
 
NALUTUESHA

Nalutuesha alikuwa ni nyumbu mdogo, alizaliwa karibu miaka mitatu iliyopita, siku ya mvua kubwa sana. Msimu wa mwisho wa mvua kabla ya ukame. Kipindi hicho, Serengeti yote ilikuwa ya kijani. Wanyama wote walikuwa wamenawiri. Nalutuesha au Nalu kama ilivyozoeleka kumwita alikuwa mtoto wa nne kwa mama yake. Alikuwa na dada mmoja na kaka wawili. Miezi ya mwanzo ya maisha ya Nalutuesha kulikuwa na chakula tele huko Serengeti. Alitumia muda wake mwingi kujifunza, kucheza na kula.

Mama yake alikuwa mtu mwenye kujua hadithi na mambo mengi sana. Ndiye alimfundisha Nalutuesha kusali kwa Ingatambo. Alimfundisha kuwa binadamu ndiye kiumbe katili kuliko kiumbe yeyote duniani.
Alimfundisha kuhusu wanyama adui, rafiki na wasaliti. Alimfundisha kuwa miaka mingi iliyopita, kondoo, ng'ombe na mbuzi waliwasaliti wanyama wengine na kwenda kuishi na binadamu. Alimwambia wanyama hao wameenda kujiunga na binadamu ili asiwawinde wao bali sisi. Wamempa siri zetu zote, jinsi tunavyoishi na jinsi ya kututega. Ukikutana na kondoo, ng'ombe au mbuzi, kimbia. Usiongee naye, jua kuwa ametumwa na binadamu kufanya upelelezi." "Lakini mama si binadamu anawala?" Akauliza Nalutuesha. "Ndiyo anawala, lakini ni iwapo akitukosa sisi. Binadamu hata akiwa na ng'ombe nyingi vipi, akitaka nyama atakuja kutuwinda sisi, akitukosa ndiyo atachinja ng'ombe wake tena yule mzee au mlemavu, sisi hachagui uwe mtoto, uwe mzee, uwe na mimba, uwe mzima au unaumwa yeye atakuua na kukula, yote ni sababu ya wale wasaliti."
"Basi hao ni wabaya kuliko hata Simba," alisema Nalutuesha kwa huzuni. "Ni wabaya kuliko hata binadamu mwenyewe, hakuna mnyama anaweza kumfanyia mnyama mwenzake ubinadamu lakini wao wamepitiliza" alisema mama yake kwa kusisitiza.

Nalutuesha na mama yake walipendana sana. Hata katika kipindi hiki cha njaa walifurahi walipokuwa pamoja. Licha ya vifo vya kila siku vya ndugu na jamaa bado waliweza kuwa na wakati wa furaha.

Familia ya Nalutuesha waliishi karibu na eneo linaloitwa Nainokanoka, eneo linalopatikana kusini mashariki ya Serengeti. Eneo hili liko kwenye mpaka unaotenganisha Serengeti na nchi ya binadamu. Hili ni eneo la milima mingi, mvua nyingi na baridi kali. Eneo hili ni tofauti sana na Serengeti yote ambayo ni tambarare tupu. Hapo zamani sana, eneo hili lilikuwa ni tambarare nzuri kama sehemu zingine za Serengeti, nini kilitokea? Kwanza kulitokea ufa ardhini, baada ya muda ufa huo ukatanuka na kuwa bonde pana sana. Kisha kwenye bonde hilo ikatokea milipuko ya volkano. Volkano ililipuka kila mahali kwenye eneo hili. Ilitokeza milima mingi sana, midogo na mikubwa. Uji wa volcano uliruka na kusambaa kwenye tambarare ya Serengeti.
Baada ya miaka mingi milipuko mingine ya volkano ikatokea kwenye milima hiyo, vilele vya milima vikafumuka na kusambaratika. Milima mingine ilifumuka na kutokeza mashimo makubwa, marefu na ya kutisha juu yake. Milima mingine ikatokeza mabonde mapana juu yake. Muda ulivyopita mabonde haya yakawa mazuri sana. Mimea ilistawi ndani yake na yakawa na wanyama wengi sana. Kwa sababu yalikuwa juu ya milima yalikuwa na baridi na yalipata mvua ya kutosha. Kulikuwa hakuna ukame huko. Familia ya Nalutuesha waliishi kwenye moja ya mabonde hayo. Bonde waliloishi Nalutuesha na familia yake lilikuwa juu ya mlima mdogo uliokuwa karibu na Nainokanoka. Lilikuwa ni bonde pana kiasi, ingechukua masaa kadhaa kutembea toka upande mmoja wa bonde hadi mwingine. Maji yalitiririka kutoka kwenye kingo za bonde zenye misitu minene na mvua ilinyesha mwaka mzima. Kwasababu bonde hili lilikuwa kwenye mlima mfupi ilikuwa ni rahisi kulifikia, hilo lilifanya liwe na wanyama wengi sana. Wanyama walikuwa wengi kiasi kwamba kuna majira chakula kingi kilichokuwa bondeni kilikuwa hakitoshi.

Ukiacha matatizo madogomadogo, wanyama waliishi vizuri sana mle bondeni. Walipata maji na nyasi za kutosha. Hata ukame ulipokuwa mkali bado kulikuwa na chakula cha kuokoteza bondeni. Baridi na umande vilipunguza makali ya ukame.

Pamoja na uzuri wake, ukame mkuu haukuliacha bonde lile. Mvua ikakoma, vijito vinavyotiririsha maji kuingia bondeni vikakauka na ukungu uliozoeleka kuwepo hapo mwaka mzima ukatoweka.

Mwanzoni ukame ulipokuwa mkali kwenye tambarare za Serengeti wanyama wakaanza kukimbilia eneo hili, walijazana kwenye milima na kwenye mabonde yale mazuri. Walikula kila kitu. Wakaingia mabondeni na kutafuna nyasi zote. Njaa ikaingia kwenye eneo hili.
Wanyama wazawa wa bonde lile wakatafuta suluhisho. Wakakaa vikao siku nyingi wakibishana. Wakatoka na suluhisho, suluhisho kichaa, mkataba na shetani!

Uliwekwa mkataba kati ya simba na wanyama wala nyasi. Ilikuwa kwamba simba watazuia wanyama wengine wanaokula nyasi kuingia bondeni. Pia watazuia wala nyama wengine kama fisi, mbwa mwitu na simba wengine wasiohusika kuingia bondeni. Kwa malipo, simba watakula kwa urahisi wanyama wa bondeni bila kwenda mbali kuwinda. Ilikubaliwa kuwa simba watakula wanyama wengine wote isipokuwa watoto na wajawazito. Waliona hii ni njia pekee ya kuweza kuendelea kuishi. Ulikuwa mkataba wa ajabu lakini ulifanya maisha yawe nafuu bondeni kuliko maeneo mengine.
 
SAFARI NI HATUA

Siku moja alfajiri na mapema, msafara mkubwa sana wa wafugaji ukiwa na ng'ombe, mbuzi na kondoo ulipita karibu na Nainokanoka. Ulikuwa umetokea kusini mashariki ya Serengeti ukielekea kaskazini magharibi. Msafara huo ulikuwa mkubwa sana ukiwa na maelfu ya ng'ombe, mbuzi na kondoo. Pamoja na ukubwa wake ulikuwa ni msafara usiovutia kutazama. Wanyama walikuwa wamekondeana kupita kiasi, mifupa ilikuwa imejitokeza na ilichezacheza walipokuwa wakitembea. Ulikuwa ni msafara unaosonga polepole sana, wanyama walitembea kichovu huku wakigumia kwa njaa na kiu. Haikuweza kupita kilomita moja bila mnyama kuanguka na kushindwa kuinuka sababu ya njaa, kiu au uchovu. Ilifika wakati wafugaji hawakujihangaisha kuwainua wala kuwachinja wanyama walioshindwa kutembea. Kujaribu kuwainua ilikuwa ni kujichelewesha kufika wanakoenda na wakichelewa wangepoteza wanyama wengi zaidi. Siku msafara unapita karibu na Nainokanoka wanyama wa porini karibu wote walikimbia na kujificha mbali. Hakuna mnyama wa Serengeti ambaye alikuwa hajui habari za ukatili wa binadamu. Wanyama walimuogopa binadamu kuliko kitu kingine chochote, pengime kuliko hata Ingatambo.

Japo bonde aliloishi Nalutuesha lilikuwa lina nyasi za hapa na pale lakini wafugaji wale hakusimama kuweka kambi. Ili kuingia bondeni. kulikuwa na kupanda kilima kisha kushuka kilima kikali. Kutokana na hali ya wanyama wao haingekuwa rahisi kuingiza wote na walioingia si wote wangeweza kupanda kilima kikali wakati wa kutoka. Hivyo walipita bila kuweka kambi hapo.

Kulipopambazuka sehemu kubwa kuzunguka bonde kulikuwa kimya kabisa, hakuna mnyama yeyote aliyeonekana. Hili lilimshangaza na kuamsha udadisi wa Nalutuesha. Amezoea kusikia kelele na vilio kutoka nje ya bonde. Siku zote alitamani kujua maisha yakoje nje ya bonde lakini hakuthubutu kutoka. Kelele na vilio vilivyokuwa vikisikika mara kwa mara toka nje ya bonde vilikuwa vya kuogopesha sana. Sehemu kubwa ya maisha yake alikuwa ameishi bondeni. Alitamani sana kuiona Serengeti aliyokuwa amesimuliwa na wazazi wake, Serengeti yenye nyasi mpaka mwisho wa upeo wa macho (japo kwa wakati huo ilikuwa ni vumbi mpaka mwisho wa upeo wa macho). Kitendo cha kutoona wanyama wawindaji kwenye mpaka wa bonde kulimchochea Nalutuesha kwenda kuona walau kwa kuchungulia kile kilichopo nje ya bonde.

Hakujua habari ya msafara wa wafugaji na wanyama kukimbia wafugaji. Baada ya kutafakari sana, udadisi ulimzidi nguvu. Akaona hii ndiyo nafasi yake pekee ya kuona kilichopo nje ya bonde. Akaanza kutembea kwa tahadhari akiangalia huku na huku. Jambo zuri ni kuwa, kulikuwa hakuna vichaka wala nyasi ndefu za kuficha hatari. Alijiambia kuwa akihisi hatari yeyote basi atarudi bondeni kwa kasi kubwa.

Baada ya kupanda kwa muda akafanikiwa kutoka nje kabisa ya bonde bila kuhisi hatari wala kuona mnyama yeyote. Akasimama kwenye mwinuko na kuangalia mbele yake. Hapo aliweza kuona tambarare ya Serengeti. Hamu ilimuisha! Japo zilikuwa nyakati za ukame mkali lakini akili yake bado ilikuwa inategemea kuona tambarare nzuri kama alivyosimuliwa. Nalutuesha alishikwa na butwaa kwa alichokiona, au tuseme kwa ambacho hakuona. Vumbi lilikuwa limetanda juu kiasi kwamba hakuweza kuona kitu chochote mbele yake. Vumbi lilimuingia machoni na kumpa tabu zaidi kuona. Inaonekana msafara wa wafugaji ulikuwa umetibua vumbi zaidi.

Akashuka kidogo kutoka kwenye kingo za bonde. Baada ya kufikicha macho na kuzoea kuona, Nalutuesha aliona mistari mingi mirefu ya alama za kwato ambazo hakuweza kufahamu ni za mnyama gani. Hakuweza kuona mistari hiyo ilipoishia na kwa haraka haraka hakujua uelekeo inakotoka wala inakokwenda. "Bila shaka wanyama walioacha kwato hizi walikuwa wengi sana" alijisemea. Kundi kubwa la wanyama wengi hivyo ni kitu ambacho hakuwahi kukiona ukizingatia hiki kilikuwa ni kipindi cha njaa. Akaangalia kwa makini na kutambua uelekeo wa zile kwato.

Alipotembea mbele kidogo kufuata uelekeo wa kwato akashangaa kuona mbele kuna kitu kinajigeuza. Hapo likamjia wazo la kugeuka na kukimbia maana alifundishwa "usalama kwanza, udadisi baadaye."Kabla hajageuka na kukimbia, akaona kiumbe hicho kikiwa na pembe mbili ndefu sana, pembe za urefu ambao hajawahi kuona. Hapo akasita kidogo kukimbia, alifundishwa kuwa,"ukiwa porini wanyama wenye pembe ni rafiki zako, ogopa wanyama wanaoficha pembe zao."

Ilisadikika kuwa wanyama wote porini waliumbwa na pembe, lakini wanyama wawindaji kama simba walificha pembe zao. Wengine walisema kuwa walizikata ili waonekane wema. Walisema wanyama wala nyasi waliacha pembe zao sababu walikuwa wema kweli, na wanyama wema hawana cha kuficha. Kwa hiyo lengo la wabaya la kutaka kuficha ubaya kwa kukata pembe halikufanikiwa na badala yake liliwafunua zaidi.

Hii habari ya kuficha pembe ilikuwa kubwa sana na ilikuwa chanzo cha ubaguzi. Mfano, pundamilia walishutumiwa na wenzao kuwa wameficha pembe, walitengwa na kudhihakiwa. Wanyama walikuwa wanaongea chinichini kuwa twiga hana pembe halisi. Tembo kwa ubabe alisema kuwa zile alizonazo ni pembe na si meno kama wengi wanavyosema. Kwa kuwa walimuogopa, walikubali kishingo upande. Kiboko alipojaribu kusema na yeye meno yake makubwa ni pembe alipingwa vikali sana. Serengeti wanyama walibaguana kwa tofauti ndogondogo nyingi sana japo waliishi pamoja na kushirikiana.
 
Basi Nalutuesha akasogea zaidi kwa mnyama huyo, alipofika karibu akamuona amelala huku akigumia. Kwanza akadhani labda ni nyumbu lakini akaona kuwa ana rangi na ukubwa tofauti. Mnyama huyo alikuwa na rangi nyeusi na mabaka meupe. Pia alikuwa mkubwa kuliko nyumbu wa kawaida.

"Habari!", akasalimia Nalutuesha kwa sauti ya kutetemeka. Mnyama yule akafungua macho taratibu na kumuangalia Nalutuesha kwa udadisi kama mtu anayejaribu kutambua kitu kisha akajibu, "Habari!" Japo ilikuwa sauti ya uchovu lakini ilikuwa ya kirafiki, hilo likamfanya Nalutuesha ajione salama.

"Naitwa Nalutuesha, ni nyumbu, natokea bonde lililoko juu ya huo mlima hapo nyuma." Yule mnyama akatabasamu huku bado uso wake ukionyesha kuwa alikuwa kwenye maumivu, inaonekana alikuwa amefurahishwa na jinsi Nalutuesha alivyojitambulisha kirasmi, kisha naye akasema.

"Naitwa ng'ombe, natokea Karatu. Niko safarini kuelekea Maasai Mara." Akasema yule mnyama na kukaa kimya kidogo kisha kwa sauti ya chini na ya kinyonge akasema.

"Nilikuwa safarini kuelekea Maasai mara"

"Wewe ni mnyama gani?"akauliza Nalutuesha.

"Ni ng'ombe" akajibu yule ng'ombe kwa mkato huku akikunja sura kwa maumivu kisha akaendelea, "mbona nimekwambia mi naitwa ng'ombe"

"Samahani kwa kutoelewa" akasema Nalutuesha kwa upole "umesema jina lako ni ng'ombe lakini hujasema aina yako?"

"Sisi aina yetu ni ng'ombe na binadamu wanaotufuga wanatuita wote ng'ombe, hatuna jina mojamoja".

Kusikia binadamu Nalutuesha akashtuka na kukumbuka huyu ndiye ng'ombe wa hadithi ya ng'ombe, mbuzi na kondoo! Wanyama wasaliti waliokimbia na kwenda kuishi na binadamu. Wanyama wanaofanya wanyama wengine waliwe na binadamu kwa kuvujisha siri zao. Bila shaka huku kujitia mwema na yuko kwenye maumivu ni sehemu ya mtego.

Nalutuesha akaanza kurudi nyuma polepole akijiandaa kukimbia, ghafla akaona yule mnyama anakohoa kwa nguvu huku akiwa na sura ya mnyama aliye kwenye maumivu makali na damu nyingi ikimtoka mdomoni akohoapo. Huruma ikamuingia Nalutuesha huku akiwaza.

"Huyu mnyama anaumwa kweli". "Nini kimekupata?" akauliza kwa sauti ya kutetemeka kama mwanzo.

Yule mnyama akakohoa tena na kisha akaanza kupumua harakaharaka, baada ya kutulia akasema.

"Usiogope, najua wanyama wengi wa Serengeti mnatuogopa, habari mnazosimuliana juu yetu si za kweli." Akapumzika tena huku akivuta pumzi kwa shida na kisha akaendelea. "Nilikuwa kwenye msafara, tunaelekea Masai Mara, tunakimbia ukame, bahati mbaya nimepatwa na ugonjwa wa mapafu na nimeshindwa kuendelea na safari."

"Inamaana huko Maasai kuna chakula na ma...., Ngoja kwanza..." akashindwa kumalizia Nalutuesha kisha akaendelea.
"unataka kusema nyinyi siyo wasaliti kama inavyosimuliwa?". Aliuliza Nalutuesha harakaharaka kwa shauku.

"Sikiliza nikuambie" akasema yule ng'ombe. "Hizo habari za usaliti ni kuchafuana tu, na kwakweli zinatuudhi sana. Habari yenyewe iko hivi".
 
"Hapo zamani, sisi, kondoo na mbuzi tuliishi porini kama nyinyi." Shida yetu sisi ni kuwa tulikuwa hatuna kasi kama wanyama wengine wa porini". Hatukuwa na kasi ya swala au nyumbu na wala hatukuwa na nguvu za nyati au kifaru. Jambo hili lilifanya wanyama wawindaji watuwinde sana. Japo tulikuwa wengi lakini tuliwindwa hadi tukakaribia kuisha kabisa. Watoto wetu na wanyama wenye mimba waliwindwa na kuuwawa kikatili. Mbaya zaidi, wanyama wengine waligundua mbinu ya kujilinda iliyotuumiza zaidi"

"Swala, nyumbu, kongoni, pundamilia, cheroe na wengineo, wakaanza kuishi karibu na kuchangamana na sisi. Walikuwa wenye urafiki na sisi tukafurahi kuwa karibu nao, kumbe ni mbinu. Walijua wakiishi ....Koh, koh, koh" akakohoa tena ng'ombe yule huku safari hii akitokwa damu nyingi zaidi. Akatulia na kuanza kuvuta pumzi kwa shida, akitoa sauti kama ya mluzi kila avutapo na kutoa pumzi.

Nalutuesha akaingiwa na huruma sana, akaanza kumsogelea lakini yule ng'ombe akatikisa kichwa kumuashiria kuwa asimsogelee. Baada ya kuanza kupumua vizuri akaendelea. "Walijua wakiishi karibu na sisi, na wanyama wawindaji au binadamu wakija basi sisi ndiyo tutakaouwawa kwa sababu watatuzidi kasi ya kukimbia. Kwahiyo hata wakikimbizwa huko walikuwa wanakimbia na kuja kujichanganya na sisi. Tukianza kukimbia wote wao walituacha mbali na sisi ndiyo tuliuwawa. Hila hii iliendelea kwa muda mrefu na wanyama wengi wakaanza kutufanyia hivyo".
"Tuliwindwa hadi tukakaribia kuisha, mwishowe mababu zetu wakaitana na kukaa kikao, baada ya majadiliano ya siku nyingi wakaja na suluhisho. Wakakubaliana kuwa ni bora wakaishi na binadamu!" "Wakasema, mbwa wamenawiri sana kwa kuishi na binadamu na japo binadamu ni mkatili lakini hawezi akawala wakaisha. Binadamu hali kama simba. Pia binadamu atawalinda dhidi ya wanyama wengine, hawatakuwa chakula cha wote. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa sisi kutoka porini na kwenda kuishi na binadamu. Baada ya muda, kondoo na mbuzi nao wakafuata." Nalutuesha akashangaa sana na hakuamini alichokisikia lakini moyoni mwake akajiambia "mnyama anayekaribia kufa hana sababu ya kudanganya"

"Kwahiyo si kweli kuwa sisi tulienda kwa binadamu kwa usaliti. Hila za wanyama wenzetu ndiyo zilichochea tuondoke na maisha yetu kwa binadamu ni mazuri sana. Si unaona anatupeleka Maasai Mara ili tusife njaa? Toka tumeanza kuishi na binadamu tumekuwa wengi mno. Haui watoto wetu wala wanyama wenye mimba. Hatuishi maisha ya kukimbiakimbia tena".

Nalutuesha akakaa chini huku akitafakari habari ngeni alizozisikia. Ghafla akawa amekumbuka jambo la muhimu na kuuliza "kwahiyo huko Maasai Mara kuna chakula na maji ya kutosha?"
"Kawaida huwa vipo " akajibu ng'ombe" lakini kwa ukame huu wa miaka mitatu sina hakika kama vitakuwepo".

"Inamaana umewahi kufika huko?" akauliza Nalutuesha.

"Nimewahi, kama mara tatu hivi, kawaida ukame ukiwa mkali wafugaji hutupeleka huko. Mara nyingi tukiwa tunaenda huko njiani huwa kuna nyasi za hapa na pale za kula lakini safari hii ni vumbi tupu, ndiyo maana wengi tunashindwa kuendelea na safari".

"Mnyama anawezaje kufika huko?" akazidi kuuliza Nalutuesha.

"Bila binadamu wa kukuongoza!?" Akajibu yule ng'ombe kwa kushangaa. "Ni vigumu sana, ni safari ndefu sana kufika huko na kuna hatari za kila aina, mito mikubwa yenye mamba, mabonde na vichaka vyenye simba, fisi na mbwa mwitu. Bila binadamu wa kukuongoza na kukulinda ni ngumu sana kufika. Na kitu kingine ni kuwa njia unayopita wakati wa kwenda siyo unayopita wakati wa kurudi hivyo siyo rahisi kukariri njia. Mimi mwenyewe pamoja na kufika huko na kurudi mara tatu, bado siijui ...., hebu sikiliza kwanza" ghafla yule ng'ombe akakata kuongea huku akitega sikio kwa umakini"

Kwa mbali zilisikika sauti za fisi. Sauti zilikuwa zinaongezeka kwa kasi sana. Ni kama fisi hao walikuwa wanakimbia kuja upande walipo wakina Nalutuesha. Jambo hilo likamfanya Nalutuesha aingiwe na uoga na kuanza kutetemeka muda huo yule ng'ombe alikuwa anakohoa kwa nguvu huku akimuashiria Nalutuesha akimbie haraka.

Nalutuesha akawa anasitasita huku akimuangalia yule ng'ombe kama mnyama ambaye hajui cha kufanya. Yule ng'ombe kwa uso wa hasira huku akiwa bado anakohoa kwa nguvu akamwambia Nalutuesha, "kimbia!".

Hapo Nalutuesha alikimbia mbio ambazo hajawahi kimbia maishani. Alikimbia kwa kasi bila kujua ni wapi anaelekea. Akili yake ilikuwa inamtuma kukimbia mbali na kule sauti za wale fisi zinakotokea. Alikimbia sana na ghafla akajikuta anahisi ladha ya chumvichumvi mdomoni na kuhisi kama analishwa vumbi. Alikuwa ameanguka vibaya sana. Akainuka na kutaka kuendelea kukimbia, hakujali damu zilizokuwa zinatoka mdomoni. Maumivu makali ya kifua kila akivuta pumzi yalimfanya akae chini. Baada ya kutulia kwa dakika kadhaa aliona maumivu ya kifua yakipungua na kasi ya kupumua ikirudi katika hali ya kawaida, lakini maumivu ya mdomo yalizidi kuongezeka. Hakujali sana maumivu, akili yake ilikuwa inawaza kujiokoa tu. Kufika hapo sauti za fisi zilikuwa zimefifia sana, baada ya kuzisikia kwa mbali uoga ulimpungua na akili ikaanza kumjia. Hapo ndipo alipotambua kuwa amekimbia kufuata ile mistari ya nyayo, mbali na bonde.
 
RAFIKI MWENYE MARANGIRANGI

Nalutuesha hakujua aelekee wapi. Njia ya kurudi bondeni tayari ilikuwa imezibwa na fisi. Akiendelea kukaa hapo asubiri nafasi ya kuingia bondeni ni hatari zaidi, kila dakika wanyama watakuwa wanaongezeka. Akaona njia pekee ya kuweza kuwa hai ni kujitahidi kufikia msafara wa wafugaji. Kila walipopita wafugaji wanyama wa porini walitawanyika mbali na msafara na hawakurudi mpaka msafara ufike mbali kabisa. Kufuata msafara wa wafugaji lilikuwa wazo bora zaidi.

Akajikung'uta mavumbi na kuanza kutembea harakaharaka kufuata zile nyayo za wanyama. Alitembea na wakati mwingine ilikimbia ili awe karibu zaidi na ule msafara wa wafugaji, ulinzi wake. Kufikia mchana alikuwa ametembea umbali mrefu lakini hakuweza kuona msafara wa wafugaji. Njiani aliona wanyama wengi wa wafugaji wakiwa wamekufa au wakikaribia kufa. Waliokuwa hai aliwasalimia lakini hakusimama, alijua hawezi kufanya chochote kuwasaidia.

Hadi jioni giza linaingia alikuwa bado hajauona msafara wa wafugaji. Kuna mawazo yalimjia kuwa labda amepita njia isiyo sahihi, lakini zile nyayo na wale wanyama aliokuwa anakutana nao vilimuonyesha kuwa yupo kwenye njia sahihi. Usiku ulipofika hakusimama, alizidi kusonga. Njaa na kiu vilimbana lakini akili yake ilikuwa kufikia usalama kwanza. Alijua kuwa wafugaji wataweka kambi usiku, hivyo akisafiri usiku wote atawakaribia zaidi. Sababu nyingine iliyomfanya asisimame ni kuogopa wanyama wakali, alijua kuwa wale wanyama walioshindwa kuendelea na safari watakuwa kivutio cha wanyama wakali. Iwapo akichelewa kuwafikia wafugaji basi njia yote walimopita wafugaji kutajaa wanyama wakali.

Japo hakuweza kuona vizuri sababu ya giza lakini aliweza kuifuata ile njia ya wafugaji kwa urahisi. Alikuwa amegundua kuwa kwenye njia ya wafugaji vumbi lilikuwa na kina kirefu kuliko sehemu zingine, alitembea eneo lenye vumbi jingi.
Alitembea hadi usiku mwingi, akaanza kukutana na kinyesi kibichi na cha moto, akajua wafugaji na wanyama wao wako karibu, akazidi kukaza mwendo. Muda ulivyozidi kwenda ndivyo njaa na kiu vilivyozidi kumuuma, hakusimama, hofu ilimsukuma mbele, alijua akiukaribia msafara wa wafugaji atakuwa salama.

Alipotazama mbele baada ya akili yake kuacha kutangatanga kwa mawazo akaona mwanga kwa mbali ukiwa kwenye mafungu yaliyo karibukaribu. Hakujua moto ni nini lakini akili yake ilimwambia kuwa wafugaji watakuwa wameweka kambi pale, alikuwa amewakaribia. Alijihisi salama na furaha ikamjia, akakaa chini na kupumzika, usingizi ukamchukua. Alipokuja kushtuka jua lilikuwa limeshatoka. Alipoangalia kule alikoona mwanga jana usiku aliona kuwa palikuwa ni bondeni na pana miti ya hapa na pale. Hakuona wafugaji wala wanyama wao. Wazo lililomjia haraka ni kwenda eneo lile na kula chochote atakachopata, njaa ilikuwa imemuuma hadi kichwa kikawa kinamuuma.

Akatembea harakaharaka kuelekea kule chini. Alipofika kwenye lile eneo aliona kuwa ni bonde zuri ila lilikuwa limechafuka sana. Bonde zima lilikuwa limetapakaa kinyesi, kidimbwi kidogo cha maji kilichokuwepo kilikuwa kimejaa tope tupu. Kulikuwa na wanyama wengi waliokuwa wameshindwa kuendelea na safari, kondoo, mbuzi na ng'ombe. Nalutuesha akaanza kuokoteza majani hapa na pale huku akikwepa wale wanyama na vinyesi hadi alipohisi nafuu ya njaa. Aliwasalimia wale wanyama lakini wengi walikuwa hoi na hata hawakujibu. Alielekea kwenye kile kidimbwi, maji yalikuwa tope tupu lakini aliyanywa kwa pupa na kujisikia kuburudika sana. Baada ya kunywa akaendelea kuokoteza nyasi hadi alipohisi kushiba kabisa. Sehemu zenye miti si salama kwa wanyama kama nyumbu, Nalutuesha alilijua hilo. Akaanza safari ya kufuata msafara wa wafugaji mara moja. Nalutuesha amezoe kuishi bondeni, hakuzoea kutembea umbali mrefu namna hii. Leo alikuwa amechoka sana na kila kiungo kilikuwa kinamuuma. Alitembea polepole sana. Alikuwa anatamani aukute msafara wa wafugaji lakini mwili haukumruhusu. Hadi giza linaingia hakuweza kuwaona wafugaji. Hakusimama, aliendelea kutembea hadi alipochoka kabisa, hapo akajiangusha kwenye vumbi na kulala. Alishtushwa na kelele za kama vitu vinavunjwa. Ilikuwa ni alfajiri na mwanga bado ulikuwa haujatoka wa kutosha. Alifungua macho kwa taabu sana maana yalikuwa mazito kwa usingizi na uchovu. Alipoangalia kule kelele zinakotokea akaona mwili wa ng'ombe umelala umemgeuzia mgongo lakini ulikuwa unachezacheza. Akajikaza kusimama ili aangalie vizuri. Katika kusimama viungo vyake vilipiga kelele kama vinaachana vile. Kelele hizo zikamshtua mnyama aliyekuwa upande wa pili wa ule mzoga wa ng'ombe. Akagonganisha uso na simba mkubwa mwenye manyoya mengi. Mdomo wa simba yule ulikuwa mwekundu kwa damu ya ng'ombe aliyekuwa akimla.

Nguvu chache zilizokuwa zimembakia Nalutuesha zikamuisha. Akaanza kutetemeka, alitaka kukimbia lakini akagundua hata kusimama kunampa shida. Akatulia akimtazama yule simba usoni. Kitu ambacho hakutegemea kikatokea, simba yule akaanza kujifuta zile damu zilizomtapakaa mdomoni na kujitetea kwa maneno ambayo hayaeleweki na yaliyotoka kwa kubabaika huku akiona aibu. Alikuwa kama vile binadamu aliyekamatwa akifanya jambo la aibu huwa.

"Salama" mwisho neno la kueleweka likamtoka simba yule.

"Salama" alijibu Nalutuesha kwa sauti ya kutetemeka huku kapigwa na mshangao. "Sikujua kama upo hapa...., Sikukuona.......samahani kunikuta katika hali kama hii...."
Alisema yule simba kwa kukatikakatika. Sasa Nalutuesha mshangao ukawa umemtoka na akamuangalia yule simba kwa mashaka.

"Naitwa Ole Ngatuny" Alisema yule simba kwa sauti ya kawaida na kuanza kumfuata Nalutuesha huku akiendelea kujifuta mdomo.
"Nimekuwa mpweke kwa muda mrefu sana, nimefurahi kukuona, upweke ni mbaya kama njaa tu," akasema Ole Ngatuny huku akijichekesha. Nalutuesha akatabasamu kuashiria kuwa anakubaliana na maelezo yake.

"Wasaliti wako wengi sana njia hii, sina shida na chakula. Unaelekea wapi?" Kabla Nalutuesha hajajibu Ole Ngatuny akaendelea, "mi natembea tembea kujua nchi, na mambo ya kifamilia pia, si unajua..., sema we bado mdogo, huwezi kujua. Umesema unaenda wapi?" aliongea Ole Ngatuny kwa mfululizo.

Nalutuesha alipigwa na butwaa lakini akajibu "nafuata msafara wa wafugaji hadi unakoenda"
"Basi tuko njia moja, mi sina sehemu rasmi ninayoenda hivyo nimeamua niufuate huu msafara kwa muda kisha nitakata kuelekea kaskazini mashariki, nataka kuijua nchi vizuri, tunaweza kuongozana, sitakukula!" akasema Ole Ngatuny haraka haraka huku akiachia tabasamu pana sana ambalo halikufifia haraka, alikuwa kama amekenua meno.

Nalutuesha hakujua jinsi ya kujibu. Mambo mengi na maneno mengi yalikuwa yamemtokea kwa muda mfupi. Akaishia kutabasamu, sio kwa sababu alikubaliana na maneno ya Ole Ngatuny bali lile tabasamu pana lisilofifia lilikuwa limemchekesha.

Urafiki ukazaliwa, urafiki wa mashaka.
 
Baada ya jua kutoka vizuri wakaanza kutembea kufuata njia ya msafara wa wafugaji. Ole Ngatuny alikuwa akiongea maneno mengi sana na mfululizo. Nalutuesha alikuwa msikilizaji na alizungumza pale alipokuwa ameulizwa maswali tu. Moyo wake ulijaa mashaka na wala hakuwa na furaha lakini hakuwa na jinsi. Aliwaza kukimbia lakini hakuwa na nguvu za kukimbia kumzidi simba yule.

"Unajua hawa wafugaji huwa wanapita njia ambayo wanajua njiani watakutana na sehemu zenye malisho. Hata kwa ukame huu wanajua kutakuwa na mabonde yana nyasi za kuokoteza. Huwa wanaweka kambi hapo. Umetumia akili sana kufuata msafara wao" akasema Ole Ngatuny.

"Jioni au kesho tunaweza fika sehemu kama hiyo, tukifika hapo kula nyasi za kutosha."

"Umetokea wapi?" Aliuliza Nalutuesha kwa uoga.

Ole Ngatuny alifurahi sana kuongeleshwa, hata swali aliloulizwa hakujibu bali alimueleza Nalutuesha kwa kirefu kuwa asimuogope na yuko salama pamoja naye. Akamueleza kuwa hata akiwa na njaa ya kufa hawezi kumdhuru. Aliongea maneno mengine mengi sana.

Hadi kufika jioni Nalutuesha akawa amemzoea na wala hakumuogopa tena. Alikuwa anaongea naye kwa uhuru na alimuuliza maswali mengi ambayo mara nyingi Ole Ngatuny aliyajibu kwa kirefu hadi kwenda nje ya mada. Alipoulizwa kama ni kweli ndege ndiyo wamesababisha ukame ule yeye alijibu kirefu hadi wakajikuta wakiongelea faida za kula matunda na kwanini wanyama wengi wanang'oka meno.

Walitembea kwa wiki nzima. Nalutuesha hakuona sababu ya kuuakaribia msafara wa wafugaji. Alijihisi salama akiwa na Ole Ngatuny. Walikuwa wanauona msafara wa wafugaji kwa mbali lakini hawakuukaribia. Ole Ngatuny alimwambia Nalutuesha kuwa ni vizuri wakaacha umbali kati yao na msafara. Wakifika sehemu na kila mtu kwenda njia yake ndipo aukaribie.

Mara nyingi nyakati za usiku Ole Ngatuny alikuwa akiondoka kwa muda mrefu na kurudi karibu na mapambazuko. Nalutuesha hakujua alikokwenda, akahisi labda amekwenda kutafuta chakula. Siku moja aliona matone ya damu kwenye shavu la Ole Ngatuny, alikuwa hajajifuta vizuri. Hapo ndipo alijua kuwa kumbe kweli alikuwa anaenda kutafuta chakula. Ole Ngatuny alikuwa anaenda kula wanyama walioshindwa kuendelea na msafara. Alipata chakula chake kirahisi sana na wala hakuhitaji kuwinda. Lakini hakutaka Nalutuesha ajue na ndiyo maana alikwenda kula usiku na alikuwa akijifuta damu. Nalutuesha alipogundua hili hakumuuliza wala halikumtisha, alijua kutumbua siri yake kungemfadhaisha Ole Ngatuny.

Toka siku Nalutuesha anywe maji yenye matope kwenye lile eneo ambalo wafugaji waliweka kambi tumbo lake halikuwa sawa. Hakutilia sana maanani lakini leo hali ilikuwa mbaya zaidi, miungurumo ya tumbo ilikuwa imezidi. Akiwa amechoka na tumbo limechafuka, Ole Ngatuny aliendelea kumshambulia kwa hadithi nyingi kwa mfululizo.

"kuna vitu sijakwambia, nilitaka nione kama na wewe haujatumwa. Unajua mimi nimezaliwa katika ukoo wa kifalme. Tulizaliwa watano kwetu, mimi ndiyo mtoto wa mwisho" akasema Ole Ngatuny. "Pamoja na kuwa wa mwisho lakini Ingatambo alinichagua kuwa mrithi wa ufalme. Ndugu zangu hawakupenda kabisa hicho kitu, wakaanza kunipangia hila na njama".

"Ulijuaje kama Ingatambo alikuwa amekuchagua?" akauliza Nalutuesha.

"Alikuwa ananitokea ndotoni na kuniambia, nyakati nyingine nikitulia sehemu peke yangu nikiwa nimetumia klorit au lengashe nilikuwa nasikia sauti ikiniambia kuwa "wewe ndiye mfalme ajaye, wewe ndiye mfalme ajaye," kwa kujirudia.

"Uliwaambia ndugu zako kuwa Ingatambo amekuchagua kuwa mfalme?" Alijikaza kuuliza Nalutuesha japo alikuwa amechoka mwili, amechoka kusikiliza hadithi za Ole Ngatuny na tumbo lake lilikuwa limevurugika.

"Niwaambie! Wee! Ilikuwa siri yangu, sema watakuwa walijua mimi ndiyo mteuliwa, kulingana na maisha niliyokuwa naishi, niliishi kama mteule" halafu kitu kingine, wao walipokuwa wakitumia klorit au lengashe walikuwa hawapati maono. Mnyama anayepata maono anaonekana tu"

"Japo wamefanya njama na hila ila ipo siku nitakuwa mfalme tu, nikiwa mfalme nitakuita unitembelee, naweza hata kukufanya uwe waziri, unapenda kuwa waziri wa nini?"

"Labda wa maji", akajibu Nalutuesha kichovu.

" Maji, basi utakuwa waziri wa maji, tena jina lako linaendana na uwaziri wa maji. Unajua nina mke na watoto?"

"Wako wapi siku hizi"?

"Tumefarakana, ni njama za kaka zangu. Walimdanganya anilishe sumu, machale yakanicheza nikagundua. Tulizozana sana, watoto wakaingilia, nikajua wao na mama yao na ndugu zangu lao ni moja. Basi ukazuka mzozo mkubwa na wanyama wakajaa wakisema eti nilitaka kuua familia! Nikaona bora nijiondokee, ila ipo siku nitarudi kuchukua cheo changu. Wewe vipi wazazi wako na ndugu zako wako wapi?"

Kabla Nalutuesha hajajibu Ole Ngatuny akaendelea.
"Siku moja uje utumie klorit au lengashe ili uone maono yako yanakwambia nini. Hapa inabidi tutafute sehemu tulale, kesho asubuhi tutaendelea".

"Kweli hata mimi nimechoka sana sijisikii vizuri," akajibu Nalutuesha.

Wakasogea kwenye eneo ambalo palikuwa na mkusanyiko wa mawe makubwa na kutafuta upenyo mzuri na kujilaza. Kabla ya kulala, Ole Ngatuny akapanda na kusimama juu ya jiwe kubwa na kuunguruma sana. Nalutuesha alikuwa amezoea kumuona Ole Ngatuny akifanya hivi japo siku ya kwanza aliogopa sana.

"Unajua kwanini nikitaka kulala lazima niungurume?" Aliuliza Ole Ngatuny huku akiteremka kwenye lile jiwe. "Nafukuza maadui" aliuliza na kujibu Ole Ngatuny. "Ndugu zangu wananitumiaga maadui wengi sana. Siku nyingine fisi, siku nyingine mbwa mwitu. Kuna siku walinitumia nyuki, ilikuwa balaa kubwa lakini niliwashinda. Siku ile wale nyuki walinikoma! Nilirusha vumbi hadi nikawa sionekani, hata wakati wakukimbia wale nyuki hawakukimbia kama kundi, kila nyuki alienda njia yake".

"Siku iliyokuwa hatari zaidi ni siku niliyotumiwa radi. Siku hiyo nilijua nakufa." Unaifahamu radi?"

"Mhmh" akaitika Nalutuesha kiusingizisingizi asielewe hata swali lenyewe.

"Radi ni mwanga unaotoka kwa Ingatambo huwa anautumia kutusalimia lakini wanyama wenye hila wanaweza kuweka umeme ndani yake, ukikugusa tu unakufa. Sijui kama unaufahamu umeme ila radi inaweza kuwa hatari sana. Basi siku hiyo nilikuwa peke yangu nyikani, hakuna miti wala wanyama wengine, ghafla radi zikaanza kupiga na kuunguruma. Sasa unajua ukiwa mteule Ingatambo anakulinda na kukupa ujuzi mwingi. Radi ikipiga na kama hilo eneo halina miti basi lala chini, ukisimama tu umekwisha
Nikalala chini, mvua ilinyesha kubwa sana lakini sikuamka hadi mvua na radi vilipoisha. Sitasahau siku ile."

"Unajua...., Nalu, Nalu, umelala? Acha na mimi nilale, kesho tunasafari ndefu"
 
Asubuhi iliyofuata Nalutuesha aliamshwa na maumivu makali sana ya tumbo na kichwa. Huku akiugulia maumivu, akatazama huku na huko lakini hakumuona Ole Ngatuny, kutazama juu akamuona amesimama juu ya lile jiwe alilosimama jana usiku akitazama huku na kule. Alipomuona Nalutuesha kaamka akashuka kutoka kwenye lile jiwe.

"Siku nyingi sijatumia klorit na lengashe, sipati kabisa maono na Ingatambo ameacha kuongea na mimi, hapa nikipata sehemu yenye miti itakuwa safi nizitafute" akasema Ol Ngatuny.

"Vipi mbona umenyong'onyea, upo salama? Changamka leo tunasafari ndefu hadi tupate sehemu yenye miti"

"Tumbo na kichwa vinaniuma" akasema Nalutuesha kwa sauti ya kuugulia, kama anayetaka kulia.

"Nazijua dawa" akasema Ole Ngatuny harakaharaka.

"Tukifika tu sehemu yenye miti nitakutafutia dawa, tuanze safari kabla jua halijawa kali"

"Tumbo linaniuma sana ngoja tusubiri lipoe kidogo," wakakaa pale huku Nalutuesha akijigeuza huku na huku. Wakati huo Ole Ngatuny hakutulia, alikuwa anaenda kulia, anaenda kushoto, anapanda juu ya mawe anashuka, anaangalia jua nk. Ghafla Nalutuesha akaanza kutapika, alitapika sana hadi akaishiwa nguvu na kulala chini, muda huo Ole Ngatuny aliacha kuzunguka na kukaa karibu naye. Baada ya kutapika, maumivu ya tumbo yakapungua, alipopata nguvu kidogo akasema.

"Mfalme we ungetangulia tu, mi nitakufuata polepole." Nalutuesha alikuwa amenza kumwita Ole Ngatuny mfalme na Ole Ngatuny alikuwa anafurahi sana kuitwa hivyo.

"Aah! Hapana utakaa sawa sasa hivi, kutapika kumetoa sumu mwilini, tusubiri, sina haraka yeyote" akajibu Ole Ngatuny huku akikaa na kuegemea jiwe, lile jiwe alilokuwa analipanda na kushuka. Baada ya kama saa moja kupita, Nalutuesha alikuwa anajisikia ahueni. Wakaanza safari. Walitembea mpaka jioni ilipoanza kuingia.

"Unaona miti ile pale? Pale hatuwezi kosa dawa" aliongea Ole Ngatuny huku akimuonyesha Nalutuesha sehemu ya uwanda wa chini iliyokuwa na miti mingi. Wakaanza kutembea harakaharaka kuelekea lile eneo. Nalutuesha alipata maumivu makali ya tumbo lakini alijikaza. Walipofika lile eneo, mara moja Ole Ngatuny akaanza kutafuta huku na kule kwenye miti. Lengo lake apate dawa ya Nalutuesha na aangalie kama anaweza pata klorit au lengashe, akazunguka kwa muda mrefu sana. Alipata dawa ya tumbo lakini hakupata klorit wala lengashe. Alirudi alipokaa Nalutuesha huku amenyong'onyea sana. Akampa magome ya ile dawa na yeye akakaa pembeni kinyonge. "Umekosa klorit?" akauliza Nalutuesha huku akibugia dawa na kuanza kutafuna, Ole Ngatuny akaitika kwa kichwa.

"Nikimaliza kutafuna dawa tuendelee na safari. Labda dawa zako tutazikuta huko mbele."
"Hatuwezi kuendelea na safari mpaka kesho, kwani hujawahi kunywa hiyo dawa?"
"Sijawahi" akajibu Nalutuesha huku akibugia dawa nyingine na kuendelea kutafuna. "Subiri kidogo, utaona inavyofanya kazi" akasema Ole Ngatuny huku akitabasamu na kujilaza.
Jua likazama na wakapitiwa na usingizi.
Nalutuesha akashtuka usingizini tumbo likimuunguruma kwa kelele sana. Wakati huo Ole Ngatuny alikuwa anakoroma kwa usingizi. Akahisi hali ya kutaka kuharisha ikija kwa kasi, akakimbia pembeni na akaharisha vibaya mno. Akarudi eneo walipolala, lakini kitendo cha kujilaza tu, ile hali ikajirudia tena, akakimbia tena kwenda kando. Hali ile iliendelea kwa muda mrefu hadi usiku wa manane ndipo ikakata, lakini ilimuacha Nalutuesha kachoka sana.

Asubuhi kulipokucha Ole Ngatuny akaamka na kumuamsha Nalutuesha. Nalutuesha alikuwa kachoka na macho yamemdumbukia ndani. Ole Ngatuny alipomuona hivyo akatabasamu na kusema.
"Umeona dawa inavyofanya kazi?" Nalutuesha hakujibu bali alitoa tabasamu la kichovu. Japo alikuwa kachoka lakini tumbo lilikuwa limeacha kabisa kumuuma. Akaamka na kuanza kuokoteza chakula hapa na pale. Baada ya kushiba wakaanza safari.
 
Tofauti na jana wakati wanakwenda kulala, leo Ole Ngatuny alikuwa ni mchangamfu sana. Na alikuwa na hamu ya kuendelea na safari kwa matumaini ya kupata klorit na lengesha.

"Hivi ulisema unatokea wapi?" Akauliza Ole Ngatuny.

"Huko karibu na Nainokanoka" akajibu Nalutuesha.
"Sehemu gani pale, mi najua kila sehemu. Ukitaka kuwa mfalme lazima ujue nchi yako" akasema Ole Ngatuny kwa kujidai.

"Nyuma ya Nainokanoka kuna kilima ambacho kina bonde pana ndani yake. Nimezaliwa humo na kukulia humo"

"Olmoti" akasema Ole Ngatuny.

"Eeh!?"akaitika Nalutuesha kwa mshangao.
"Kilima na bonde hilo panaitwa Olmoti. Kwahiyo wewe ni mkazi wa Olmoti. Umeona! Nimekwambia najua maeneo yote".

Nalutuesha na Ole Ngatuny walijenga urafiki mkubwa sana. Kwa muda wa mwezi mmoja walitembea pamoja. Walisaidina na kutiana moyo. Kuna nyakati zilipita hata siku tatu bila kuona nyasi wala maji. Nalutuesha alikuwa hoi. Alikuwa ni mifupa mitupu, midomoni alijaa vidonda, na macho yalikuwa yamemdumbukia ndani, hakuvutia kumtazama. Ole Ngatuny alimtia moyo na nyakati nyingine kumbeba. Ole Ngatuny hakuwa na shida ya njaa japo kiu kilimtesa sana. Njia yote walimopita kulikuwa na ng'ombe, mbuzi na kondoo walioshindwa kuendelea na safari.

Katika kipindi hicho urafiki wao ulikuwa umekua na kuwa mkubwa sana. Waliongea kwa uhuru na furaha. Magumu waliyokutana nayo yalikuwa ni mengi. Walipambana na makundi ya mbwa mwitu na fisi. Walivumilia kiu kali, jua kali, vimbunga vikali na matatizo ya mfumo wa hewa. Msafara wa wafugaji ulikuwa umewaacha sana, waliona tu alama ulizoacha.
Safari yao ya mwezi mmoja ikawa imewafikisha kwenye bonde la mto Grumeti. Mto wenyewe ulikuwa umekauka ukiwa na vidimbwi vidogovidogo hapa na pale. Sehemu hii miti ilikuwa mingi sana lakini ni michache ndiyo ilikuwa na majani. Ng'ombe, mbuzi, na kondoo zilionekana kwa wingi sana eneo hili lakini wanyama wa porini walikuwa hawaonekani. Makundi ya wanyama hao yalikuwa yamejitenga kwenye mafungu. Ilionekana wafugaji wengi walikuwa wameweka kambi hapo. Mbwa walisikika wakibweka kila kona.

Ole Ngatuny na Nalutuesha walichagua sehemu mbali na wanyama hao. Kitu cha kwanza, waliingia mtoni na kunywa maji kwenye kidimbwi hadi kikakauka. Nalutuesha akaanza kuokoteza nyasi hapa na pale. Ole Ngatuny alienda huko kwenye miti akitafutiza, baada ya muda alirudi akiwa na furaha sana.

"Nimezipata!" akasema kwa furaha "nimepata klorit na lengashe, zipo nyingi sana hapa".

Akaanza kubugia vijiti, magome na mizizi aliyobeba kwa pupa. Alikula huku anaongea maneno mengi.
"Sijala siku nyingi sana hizi dawa. Jaribu na wewe kutafuna"
akasema Ole Ngatuny huku akimpatia Nalutuesha kipande cha mzizi.

Nalutuesha alikuwa anajua dawa hizi na zinafanyaje kazi. Huko Olmoti zilikuwa zinatumika sana kwaajili ya kupandisha mori. Ukame ulivyozidi kuwa mkali ndivyo na matumizi ya dawa hizi yalivyozidi. Tatizo ni kuwa wengi waliokuwa wakitumia walikuwa wakipatwa na matatizo ya akili. Bondeni kukawa na vurugu na kutoelewana hadi matumizi yake yakapigwa marufuku. Hakutumia mizizi aliyopewa na akaanza kuingiwa na wasiwasi kwa jinsi Ole Ngatuny alivyokuwa anazitafuna zile dawa kwa pupa.

Ole Ngatuny alitulia chini ya mti huku akiendelea kuongea. "Nalutuesha, tukivuka huu mto tutaenda kama siku mbili kisha tutaachana, nitafuata huu mto kuelekea kaskazini mashariki kisha nitapinda kusini mashariki kuelekea nyumbani. Kabla hatujaachana inabidi nikufundishe mbinu za kujilinda. Unajua kuwa tembo anabeba mimba karibu miaka miwili!, miezi mingi sana, lakini hilo halitakusaidia kitu kwenye kujilinda" alisema Ole Ngatuny huku akitoa tabasamu lake la kukenua. Macho yake yalikuwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu.

"Katika yale meno mawili ya tembo, kuna jino moja ndilo hupenda sana kulitumia. Ukimuangalia vizuri utakuta limeisha na ni fupi kuliko lile jingine. Ukikutana naye na akakushambulia hakikisha unakaa upande wa lile jino refu. Kifaru haoni vizuri ila ananusa sana, ukikutana naye kaa mbali na usitingishike, hatakuona ila hakikisha umekaa upande ambao upepo unakoelekea siyo unakotokea. Chukua tahadhari unapokuwa unakunywa maji mtoni au kwenye madimbwi, mamba wanakuwemo humo wakivizia"

Nalutuesha hakujua mamba ni nini lakini akaendelea kusikiliza kwa makini na kuweka akilini kuwa anatakiwa kuwa makini anapokunywa maji.

"Ukikutana na fisi au mbwa mwitu kimbia kwa nguvu zako zote, kama huwezi basi usionyeshe uoga wala kuwapa mgongo. Ila mbio ndiyo ulinzi wako mkubwa. Umeniambia kuwa wakina ng'ombe siyo wasaliti lakini kuwa makini na binadamu na wale mbwa wao, siyo viumbe wazuri. Nyakati za usiku lala kwa kujificha kabisa, jifiche kiasi hata mnyama akiwa karibu asisikie harufu yako na kama ulivyogundua mwenyewe, endelea kutembea kufuata msafara wa wafugaji," Ole Ngatuny aliongea habari nyingi sana. Nalutuesha aligundua kuwa, kadri Ole Ngatuny anavyoendelea kutafuna zile dawa ndivyo alivyozidi kuongea sana na kuongea habari zisizoeleweka vizuri. Siku ile wakalala vizuri. Kulipokucha wakakuta wafugaji wengi wameondoka na wengine wako katika hatua za mwisho kuondoka. Kufika mchana wafugaji wote na wanyama wao walikuwa wameondoka. Wao hawakuwa na haraka, walipanga wakae kama siku moja zaidi ili wale na kunywa maji kurudisha nguvu. Nalutuesha aliendelea kula na kunywa maji huku Ole Ngatuny akikazana kula zile dawa. Kadri alivyozidi kuzitafuna ndivyo alivyozidi kubadilika, macho yalizidi kuwa mekundu, ikawa ngumu kumuelewa na kuna muda akawa akitetemeka. Pia alianza kula sana, hakujali kujificha wala kujifuta damu vizuri. Usiku ulipofika Ole Ngatuny alikuwa bado akitafuna zile dawa na kula sana wanyama walioshindwa kuendelea na safari. Vitu alivyokuwa anaongea vilikuwa havieleweki na akawa amekuwa mkali. Nalutuesha alikuwa na wasiwasi mkubwa, akamsihi apunguze kutafuna zile dawa lakini Ole Ngatuny alikuwa kama haelewi alichoambiwa, akamjibu kwa habari nyingine kabisa. Usiku wakalala lakini haukuwa usiku mzuri, Ole Ngatuny alitumia muda mwingi kula na kuunguruma.

Asubuhi kulipokucha Nalutuesha aliamka lakini hakumuona Ole Ngatuny. Baada ya kumtafuta huku na huku akamkuta amekaa sehemu akila ng'ombe mkubwa sana. Alikuwa amempa mgongo, Nalutuesha alipomsogelea akageuka ghafla na akawa kama anataka kumshambulia, Nalutuesha akarudi nyuma kwa uoga. Ole Ngatuny akaanza kumsogelea, macho mekundu na meno katoa huku kajaa damu sura yote. Akawa kama hamtambui wala hajawahi kumuona Nalutuesha.

"Ole Ngatuny, mfalme!" Aliita Nalutuesha kwa sauti ya kutetemeka. Ole Ngatuny baada ya kusikia akiitwa hivyo akasimama, akawa kama ameshtushwa toka usingizini, akamuangalia Nalutuesha kwa uso ulioonyesha huzuni, huruma, majuto na aibu kwa wakati mmoja kisha akasema.
"Binti haupo salama pamoja nami, ondoka uende"

"Ni zile dawa, acha kuzitafuna, utakuwa tu sawa" alisema Nalutuesha kwa sauti ya huzuni na matumaini.
"Hapana, kutoka hapa hali itakuwa mbaya zaidi. Dakika moja nitakuwa nakukumbuka, dakika inayofuata, sijawahi kukuona. Pona yako ni kuondoka. Siyo mara ya kwanza hali hii kunitokea na hapa ni mwanzo tu" akasema Ole Ngatuny.
 
Hatati sana... Ngoja tuone...
Mkuu kumbe umeipitia! Ngoja basi tuendelee nayo.

"Ukikaa na kupumzika kido..." Alisema Nalutuesha lakini kabla hajamaliza Ole Ngatuny alimkatiza kwa sauti kubwa na ya kutisha kama vile anaunguruma.

"Ondoka binti, unataka kufa!?"

Hapo Ole Ngatuny akaanza kutetemeka na macho yakaanza kumbadilika. Alikuwa kainua mdomo juu na anaunguruma mfululizo kwa sauti kubwa sana. Macho yale na muungurumo ule ulimuogopesha sana Nalutuesha. Akaanza kuondoka na kuvuka mto huku machozi yakimtoka. Alipofika ng'ambo na kuangalia nyuma hakumuona Ole Ngatuny lakini bado alisikia sauti kubwa ya kuunguruma. Hakuwa na jinsi, Ole Ngatuny mwenye kujali alikuwa amegeuka na kuwa hayawani. Alianza kutembea haraka haraka. Sasa hayuko na Ole Ngatuny, ulinzi wake ilikuwa ni kutembea karibu na msafara wa wafugaji kwa mara nyingine. Mambo waliyopitia na Ole Ngatuny yalimfanya awe na ujasiri wa ajabu. Hakuogopa kitu alisonga kwa kujiamini japo moyo wake ulikuwa mzito na uso ulijaa huzuni sababu ya Ole Ngatuny. Alijua kipindi kama hiki cha kila mtu kwenda njia yake kingetokea lakini namna kilivyotokea ndiyo ilimhuzunisha sana. Alijihisi kuwa na hatia kwa kutoweza kumsaidia rafiki yake wakati alipohitaji msaada wake.

Mawazo ya kujipa moyo yakamjia yakimwambia kuwa Ole Ngatuny anaweza kujisimamia, na hakuna ambalo angeweza kufanya kumsaidia.

Alitembea mchana wote na hata usiku ulipoingia hakusimama. Alikuwa ameshiba na ana nguvu. Aliamua kutumia nguvu zake vizuri kabla taabu ya njaa na kiu haijampata tena. Kufikia asubuhi aliweza kuona wafugaji na wanyama wao kwa mbali. Hapo alipunguza mwendo na kujihisi salama tena.

Kwa muda wa wiki tatu alikuwa akitembea nyuma ya msafara wa wafugaji. Akipumzika walipopumzika na kuendelea na safari walipovunja kambi. Wafugaji walikuwa wakiweka kambi sehemu ambazo kulikuwa na maji, miti na nyasi. Kiuhalisia hakukuwa na maji bali matope wala hakukuwa na nyasi za maana bali za kuokoteza hapa na pale. Mara nyingi maeneo haya yalikuwa pembezoni mwa mito iliyokauka. Kadri walivyokuwa wanasogea maeneo ya kaskazini ndivyo hali ilionekana kuwa afadhali zaidi ya walikotoka. Ilionekana kaskazini ya Serengeti ukame haukuwa mkali sana kama upande wa kusini. Huku aliweza kuona miti yenye majani na madimbwi ya maji.

Leo wafugaji walikuwa wameweka kambi kwenye bonde la mto mpana sana. Mto wenyewe ulikuwa umekauka kabisa lakini kulikuwa na madimbwi ya hapa na pale. Pia kulikuwa na nyasi za kuokoteza. Hapa zilikuwa ni nyingi ukilinganisha na walikotoka.

Nalutuesha alichagua eneo mbali na wafugaji na wanyama wao na kukaa hapo. Hapo alikunywa maji na kuokoteza nyasi na majani ya miti. Usiku alipokuwa amelala alishtushwa usingizini na maumivu makali kwenye mguu mmoja wa nyuma. Ilikuwa ni kama kuna kitu kimemuuma na kukimbia. Sababu ya giza hakuweza kuona chochote. lakini baada ya muda kidogo maumivu yakapungua na akapitiwa tena na usingizi.

Kulipokucha alikuwa na kizunguzungu kikali sana. Macho na mdomo vilikuwa vizito kufunguka. Alipofanikiwa kufungua macho aliona maluweluwe tupu. Aliona miti miwilimiwili ikicheza. Alipotaka kuinuka mwili ulikuwa mzito kama siyo wake, akaendelea kulala. Asubuhi hii hakuhisi maumivu yoyote kwenye ule mguu lakini alipouangalia ulikuwa umevimba sana. Asubuhi hiyo hiyo, wafugaji na wanyama wao wakaanza kuondoka. Kwa jinsi alivyokuwa anaona wawiliwawili walionekana wengi sana. Alijua kuwa muda si mrefu alitakiwa kuwafuata nyuma lakini angewezaje ikiwa hata kufungua macho tu ni shida! Kila alipokuwa akifungua macho, kizunguzungu kilizidi na kichefuchefu kikamshika. Alipotaka kujaribu kuinuka tena alishindwa na aliishia kutapika sana, alipomaliza alikuwa hoi na moyo ulikuwa ukimuenda mbio kuliko kawaida. Baada ya dakika kadhaa akapitiwa na usingizi.

Aliposhtuka, giza lilikuwa limeingia tayari. Eneo lote lilikuwa lilifunikwa na giza zito na kimya kilikuwa kimetanda. Muda huu aliweza kufumbua macho kirahisi na hakuona maluweluwe kama ilivyokuwa asubuhi. Alipojaribu kusimama aliweza lakini sasa maumivu kwenye ule mguu yalikuwa makali sana. Akawaza iwapo aanze safari usiku uleule kufuata msafara wa wafugaji lakini akaogopa kuwa anaweza kupotea na kwenda njia tofauti. Eneo lile lilikuwa na miti mingi sana na kwenye giza lile hakujua msafara wa wafugaji umeelekea upande gani, akaona ni vema asubiri hadi kukuche. Sababu ya kulala mchana wote, usiku huu hakupata usingizi na ulikuwa mrefu sana.

Usiku ulipoenda sana alianza kusikia pilikapilika za wanyama wa porini wakirudi eneo lile. Alijua kuwa muda si mrefu eneo lile litajaa wanyama wa kila aina, wakali na wapole. Hivyo alidhamiria kuanza safari mara tu mwanga utakapoanza kutoka.

Alfajiri na mapema alianza safari. Mwanzo alianza kwa kuchechemea mguu lakini baada ya kitambo kidogo akawa sawa na aliweza kutembea kwa kasi. Siku hii alitembea mchana wote na usiku wote lakini hakuweza kuona msafara wa wafugaji. Njiani alikutana na wanyama wengi sana, waporini na wa kufugwa walioshindwa kuendelea na safari. Bahati yake nzuri, kwa muda wote huu hakukutana na wanyama wakali waliomsumbua. Njiani aliona makundi ya mbwa mwitu na fisi yakila ng'ombe, mbuzi na kondoo lakini hayakujishughulisha naye.

Mchana wa siku ya pili alifika sehemu kulipokuwa na bonde kubwa sana la mto. Hapa njia ya wafugaji ilikuwa imegawanyika na kutoa njia nyingi, inaonekana kila kundi la wafugaji lilifuata njia yake. Sehemu hii kulikuwa na miti mingi sana. Tofauti na alikotoka, hapa miti mingi bado ilikuwa na majani. Kwa kukosa kula kwa muda wa siku mbili Nalutuesha alikuwa na njaa kali ajabu. Pia alikuwa yupo hoi sababu ya kutembea bila kupumzika. Akaacha kufuata njia za wafugaji na kuelekea kwenye lile bonde labda apate chochote cha kula.

Alipoingia kwenye lile eneo, macho yake yakatua kwenye mti mkubwa uliokuwa na matunda mengi juu yake na mengine yameanguka chini. Hakujua ni matunda gani lakini kwa njaa aliyokuwa nayo akakaa chini na kuanza kula kwa pupa.
 
Shunie Smart911

OL MAKAU

Alipokula, alisikia utamu uliochanganyikana na uchachu. Kwa njaa aliyokuwa nayo, ilikuwa ni ladha nzuri ajabu. Utamu ule ulikatishwa na maumivu kwenye vidonda vilivyokuwa mdomoni mwake. Hakujali sana hayo maumivu, aliendelea kula yale matunda kwa kufakamia. Mbegu zingine alikuwa anazimeza! Alikula hadi meno yakaanza kumuuma. Alikula akashiba lakini kiu ya maji ilikuwa imemkaba mara mbili zaidi. Mpaka sasa alikuwa amejifunza kuvumilia kiu na njaa. Akakaa chini kupumzika. Alikuwa anajua kuwa maeneo yenye miti ni hatari lakini kwa jinsi alivyochoka hakutilia maanani wazo hilo. Wazo ni kuwa akiamka aanze kutafuta maji. Bila shaka kwa uwepo wa miti ile na maji yatakuwepo. Akakaa chini na kujilaza huku meno na midomo vikimuuma.

Hakujua alikuwa amelala muda gani lakini alishtushwa na sauti kali za vicheko. Alipofumbua macho akakutana uso kwa uso na uso uliochoka sana. Mdomo ulikuwa umeachamwa na meno makubwa yakiwa mbalimbali yalionekana. Kwa kweli meno ndani ya kinywa cha mnyama yule hayakuzidi mawili.

Sura na kinywa cha yule mnyama vilimtisha sana Nalutuesha. Akarudi nyuma harakaharaka na akatamani angekuwa na uwezo apande juu ya ule mti. Alivyorudi nyuma ndiyo akaona kundi kubwa la fisi wakiwa wameacha midomo wazi, wengi wao wakiwa na mapengo makubwa.

"Tunatakiwa tugawane sawasawa" alisikika fisi mmoja toka kwenye lile kundi "watoto tuwatengee nyama yao." Yule fisi aliyekaribu na Nalutuesha na wenzake wawili hawakujali hiyo sauti, walizidi kumsogelea Nalutuesha, midomo ikiwa wazi. Yule fisi aliyekuwa mbele akarusha mguu wa mbele ili amkamate Nalutuesha lakini akakwepa pembeni. Kule alikokwepea akakutana na fisi mwingine uso kwa uso, huyu alikuwa ameachama mdomo tayari kwa kumng'ata. Nalutuesha akakwepa tena lakini yule fisi akamuwahi na kumkamata pembe moja kwa meno.

Fisi mwingine akamkamata mkia na kumng'ata kwa nguvu. Nalutuesha alihisi maumivu makali hajapata kuyahisi maishani, akapiga kelele na kulia kwa sauti kubwa. Fisi mwingine akawa akivuta mkia na mwingine akivuta pembe. Yule fisi mkubwa mwenye mapengo akamkamata Nalutuesha mguu mmoja wa mbele. Bahati ya Nalutuesha huyu alikuwa na mapengo.

Wakamning'iniza hewani, wakamvuta pande tatu. Alikuwa anahisi anataka kukatika. Yule fisi aliyeuma pembe akauma na kuvuta kwa nguvu hadi pembe ikakatika. Hapo Nalutuesha akaanguka chini huku bado kang'ang'aniwa mkia na mguu. Mkia ukaanza kutoa damu. Mguu uliong'atwa na Mapengo nao ukaanza kuuma maana Mapengo alikuwa anavuta kwa nguvu. Nalutuesha alijua huo ndiyo mwisho wa maisha yake. Picha ya mama yake, ya ndugu zake na ya Ole Ngatuny zikaanza kumjia kichwani kwa kasi. Akapiga kelele na kufurukuta. Akiwa bado anaendelea kuvutwa, fisi wengine wakaanza kumsogelea, yule aliyekata pembe baada ya kugundua alichopata si chakula na yeye akaanza kusogea tena. Wakamsogelea huku midomo wameiachama zaidi.
 
Kabla ya kuendelea tufahamu kwanza haya. Smart911 Shunie

MAANA YA MANENO YA KIMAASAI

Nalutuesha: Aliyezaliwa wakati wa mvua.

Ingatambo: Mawingu, Anga.

Ol-Kinyang, Ol-kinos: Mamba.

Sapuki: Mnene

Ol-Makua, Magua: Kiboko.

Ol Ngatuny: Simba

Ol-Ngonjinia: Fisi
 
Ghafla fisi waliokuwa nyuma wakaanza kupiga kelele na kukimbia. Hawakusimama kushughulika na vurugu za kumla Nalutuesha bali walipitiliza huku wakipiga kelele. Nyuma yao kulikuwa na vumbi kubwa likija kwa kasi huku katikati yake kukiwa na mnyama mkubwa asiyeonekana vizuri. Kufika hapo yule fisi aliyekuwa ameng'ata mkia alikuwa ameshaukata, naye akatimua nao mbio wala asijue anakimbia nini. Mapengo naye baada ya kuona vumbi na mnyama mkubwa ameachama mdomo vinakuja kwa kasi akamuachia Nalutuesha na kuanza kutimua mbio. Nalutuesha akarushwa pembeni ya ule mti akiwa hajui kinachoendelea huku ametapakaa damu na bado ikiendelea kutoka mkiani. Yule mnyama aliendelea kuwakimbiza wale fisi kwa umbali kidogo mpaka wakatokomea kwenye kilima. Akasimama juu ya kilima kile na kuanza kupiga kelele kama vile anawafokea au anawatukana.

Mnyama yule akaanza kushuka huku akiongea maneno kwa hasira na kusonya. Alivyosogea karibu ya ule mti akamuona Nalutuesha. Akakunja uso kwa hasira na kuanza kuhema kwa nguvu. Nalutuesha akainua macho kumtazama, walipogongana macho yule mnyama akaonekana kupungua hasira.

"Nilifikiri fisi" akasema. "Kumbe walikuwa wanataka kukutafuna, nilijua wanakula ukwaju wangu. Nikasema kama fisi wameanza kula ukwaju basi njaa hii ni kiboko! Naitwa Kiboko". Akasema yule mnyama huku anatabasamu.
"We nani mwenzangu? Ukalie huo mkia."

"Eeh" akasema Nalutuesha kwa kushangaa.

"Ukalie huo mkia au niseme kipisi cha mkia ili damu isiendelee kutoka" akasema yule mnyama huku akiangalia ukwaju uliokuwa umesambaa pale chini kwa masikitiko.

Nalutuesha akijegeuza na kukikalia kipisi cha mkia wake, alisikia maumivu makali lakini aliendelea kukikalia.

"Ona wamesambaza ukwaju wangu wote, nakulaje hivi?" akasema yule kiboko kwa masikitiko."Umesema unaitwa nani?"

"Naitwa Nalutuesha" akajibu Nalutuesha huku akishangaa mnyama huyo mkubwa, mwenye meno makubwa na hana pembe lakini anaonekana kama ni mwenye urafiki. Alipomuona kwa mara ya kwanza alikuwa amewaza kuwa amekoswakoswa kuliwa na fisi na sasa anaenda kuliwa na mnyama mwenye meno kama miguu yake, meno ukubwa wa pembe.

"Naweza kukusaidia kukusanya" akasema Nalutuesha. "Aah! Kaa kwanza hadi damu iache kutoka. unatafuta nini huku? Sijawahi ona mnyama wa aina yako huku" akasema yule kiboko huku akikaa chini ya mti karibu na Nalutuesha.

"Nimetoka huko bonde la Olmoti, karibu na Nainokanoka, naelekea Maasai Mara"

"Maasai Mara! Umeshafika, ni hapo tu ng'ambo, ukivuka mto umefika"
"Nalutuesha wenzako umewaacha wapi?" Akaendelea kudadisi kiboko yule.

"Jamii yetu sisi tunaitwa nyumbu ila jina langu ndiyo Nalutuesha"

"Ahaaa" akasema yule kiboko huku akitabasamu. "Mi mwenyewe jina langu kabisakabisa ni Ol Makau, sema wanyama wengine wanatuita wote viboko, hii imepelekea hata kama najitambulisha niseme naitwa kiboko"

Ol Makau, alikuwa ni mwenye kutabasamu muda wote. Mwanzoni tabasamu hilo la mdomo mkubwa huku likionyesha meno makubwa lilimtisha sana Nalutuesha, lakini sasa alikuwa ameanza kulizoea na kuona kuwa linavutia.

Baada ya muda Nalutuesha akawa amekusanya lundo la ukwaju na Ol Makau, aliubugia mara moja na kuanza kuongea huku akimung'unya ukwaju. "Sasa Nalu unataka kwenda Maasai Mara kufanya nini?Wanyama wengi huogopa kwenda huko sababu binadamu na wale wasaliti wamejaa huko, jana limepita kundi kubwa la wasaliti wakiwa na binadamu".

Nalutuesha akataka kumwambia kuwa ng'ombe, mbuzi na kondoo siyo wasaliti lakini akaona haitatosha, akamsimulia hadithi yote ya safari yake na yaliyompata mpaka kufika hapo.

"Aiseee! Pole sana" akasema Ol Makau huku akiwa na sura ya huzuni.

"Kama nia yako ni kwenda huko basi nitakusaidia maana kuna masharti mengi juu ya kuvuka mto. Twende tukapumzike kwenye mikwaju ya kule chini. Tukanywe maji halafu jioni ntakupeleka kwa mabosi kuvuka."
Wakaanza kutembea kuelekea upande wa mtoni.
"Unajua mara ya kwanza nilivyokuona na meno yako makubwa nilijua utanila" alisema Nalutuesha huku akimfuata Ol Makau kwa nyuma.
"Haya si meno, ni pembe sema yametokezea mdomoni, sisi tupo kundi la wanyama wenye pembe" akasema Ol Makau. Nalutuesha alijua kuwa kinachoongelewa si kweli lakini hakuona umuhimu wa kumpinga.

"Unajua kuwa Tembo hana pembe!? Yale unayoona yametokeza nje ni meno, sema wanyama ni wanafiki na wanashindwa kusema waziwazi kuwa tembo hana pembe, wanamuogopa. Ila viboko tukisema na sisi hizi ni pembe na si meno tunapingwa vikali sana. Hili suala la kuwa na pembe na kutokuwa nazo linakuzwa sana kuliko umuhimu wake. Limekuwa chanzo kikubwa cha ubaguzi. Kuwekana kwenye makundi na kubaguana ni mambo ya kijinga sana, unajua wewe saa hizi upo kundi moja na viboko" akasema Ol Makau huku akimgeukia Nalutuesha na kutoa tabasamu pana.

"Kundi gani?"akauliza Nalutuesha.

"Kundi la wanyama wenye mikia mifupi" akasema Makua na kuangua kicheko kikubwa sana.
Nalutuesha aliishia tu kutabasamu.
 
Wakafika kando ya mto, mto ulikuwa na maji ya kutosha lakini yalikuwa yametulia kama vile mto hauendi. Hapo miti ilikuwa na majani mengi na kulikuwa na kivuli kizuri sana.
"Kulikuwa na wanyama wengi sana kando ya mto ila sababu ya kukatazwa kunywa maji na kuwindana wametawanyika" akasema Ol Makau.

Baada ya kunywa maji wakajilaza kwenye kivuli na muda mfupi baadaye Ol Makau akapitiwa na usingizi. Nalutuesha yeye hakupata usingizi bali mawazo yake yalikuwa yakihama huku na kule. Alitamani kuona nyasi ambazo amesikia zipo huko Maasai Mara, akawaza mama yake atakuwaje wakati huo, akawaza hatma ya yule ng'ombe mwenye kikohozi, akamuwaza Ole Ngatuny, akawaza mambo mengi aliyopitia njiani, kiu na njaa, akawaza alivyotaka kuliwa na fisi muda si mrefu. Mawazo yakamchukua hadi akawaza alivyojilaza pale chini ya kivuli akiwaza! Mawazo na uhalisia vikaingiliana. Baadaye naye akapitiwa na usingizi.

Vishindo vya Makau ndivyo vilivyomuamsha Nalutuesha.
"Twende kwanza tukaongee na mamba maana kuvuka hapa unahitaji kupata ruhusa, kama siyo ya Kinyang basi ya Sapuki na muda mwingine ya wote wawili"
Nalutuesha hakujua hao ni nani lakini alimfuata Makau. Wakatembea pembezoni mwa mto hadi kufikia sehemu iliyokuwa na maji mengi kama dimbwi hivi ndani ya mto. Dimbwi hilo lililokuwa limejaa mamba wengi sana.

Ol Makau akasogea karibu na kumuashiria Nalutuesha asisogee. Kabla hajauliza akawa amemuona Kinyang, Akamfuata.

"Kinyang habari mkuu!" Akamsalimia. Kinyang akainuka kumtazama lakini hakuitikia salamu na badala yake akasema "Nasikia umepata rafiki mpya, yuko wapi?" "Mara hii habari imeshafika huku!" Akashangaa Ol Makau japo alijua jinsi ambavyo kulikuwa na umbea pale mtoni.

"Ni kweli, rafiki mwenyewe ni huyu niliyeongozana naye. Huyu rafiki yangu ametoka mbali, mbali kabisa, safari ya miezi miwili kutoka hapa. Anataka kwenda Maasai Mara, anaomba ruhusa ya kuvuka"

"Umemjua leoleo! Halafu ni rafiki yako!" Akasema Kinyang kwa kebehi. "Vyovyote vile, sheria zetu za hapa mtoni unazifahamu. Haturuhusu kiumbe yeyote kunywa maji wala kuvuka hapa. Kama hatuwezi kusimamia sheria tulizojiwekea kutakuwa hakuna haja ya kuwa nazo. Kama wengine wanafuata na wengine hawafuati, zitakuwa sheria gani hizo?"

"Lakini mkuu, tuliweka zile sheria kipindi maji yanaelekea kukauka kabisa. Mvua zimenyesha huko mto utokako na maji yameongezeka. Si tunaweza kupindisha kidogo hizo sheria, hali zimebadilika"

"Kikao kilichoweka sheria ndicho kinaweza kuzivunja. Mimi kama msimamizi wa sheria na taratibu sitaweza kuruhusu hilo" akasema Kinyang kwa msisitizo.

Ol Makau akapandwa na hasira kuona kuwa Kinyang hayumbishwi kwenye msimamo wake. Nalutuesha akataka kusogea kuongea na Kinyang lakini Ol Makau akamzuia. Akatafakari kidogo kisha akasema "mkuu Kinyang, kwa heshima zote, hiki unachofanya hakina tofauti na ubinadamu"

Kusikia maneno hayo, uso wa Kinyang ukabadilika, pumzi nzito zikamtoka, akawa kama amekabwa. Ol Makau kuona hivyo akaanza kurudi nyuma. Mamba waliokuwa karibu na Kinyang wakasogea pembeni kwa utulivu mkubwa kama vile wananyata.

Kinyang akajirusha juu, akawa kama kasimamia mkia, kwa sekunde kadhaa mwili wote ulikuwa juu ya maji umesimama wima. Ni sehemu ndogo tu ya mkia ndiyo ilikuwa ndani ya maji. Alirudi kwenye maji kwa kishindo kikubwa sana.

Nalutuesha aliogopa lakini hakukimbia. Kinyang alikuwa na ukubwa wa kutisha. Ol Makau naye aliingiwa na uoga lakini alijua Kinyang hawezi thubutu kutoka majini kumdhuru. Kinyang akamsogolea Ol Makau mpaka nusu ya mwili wake ikawa imetoka kwenye maji. Kwa sauti ya kutetemeka kwa hasira akasema "nisije kukuona tena hapa na kuanzia leo anza kutembea ukiangalia nyuma." Baada ya maneno hayo Kinyang akaendelea kufoka na kutukana, mamba wengine wakamuashiria Ol Makau kuwa aondoke. Ol Makau na Nalutuesha wakaondoka na kwenda eneo lenye miti wakajilaza hapo, na kwa dakika nyingi hakuna aliyemuongelesha mwenzake.

"Usiwe na shaka, kesho tutavuka" akavunja ukimya Ol Makau. "Ule ni mkwara tu, kesho tutavuka hamna haja ya kuhuzunika, tuendelee na mambo yetu'.

"Hivi unajua kwanini niliwatimua wale fisi kwenye ukwaju wangu?" Aliuliza Ol Makau na kuendelea bila kusubiri jibu. "Nimewahi sikia kuwa japo ukwaju unaumiza meno lakini pia unayafanya yawe imara sana. Kila siku huwa napita kula na ndiyo maana meno yangu hayang'oki kama wanyama wengine, au kama Ole Ngonjinia na familia yake"

"Ole Ngonjinia ndiyo nani?" Akauliza Nalutuesha.

"Yule mapengo aliyetaka kukutafuna chini ya mkwaju"

Hapa wakaendelea kuongea mpaka usiku ukaingia.
"Tulale sasa, kesho tutaenda kwa Sapuki tuone jinsi ya kutatua hili suala la kuvuka. Ila nakuomba kesho tukikutana na Sapuki usicheke, usitabasamu na ikiwezekana hata meno usionyeshe. Huwa hapendi hilo"

Nalutuesha akakubali japo hakujua Sapuki ni nani na kwanini hapendi wanyama wacheke.

Asubuhi kulipokucha wakashika njia kuelekea dimbwi alilokuwa anapatikana Sapuki.

"Ol Makau nasikia jana umemtukana Kinyang!" Alisema kiboko mmoja akiwa matopeni," inabidi ukamuombe msamaha aisee, japo Kinyang si muelewa lakini ulivyomwambia siyo sawa."

"Ndiyo tatizo la hapa, jambo dogo linakuzwa balaa" akajitetea Ol Makau kisha akauliza.

"Sapuki yupo wapi?"

"Geuka nyuma yako" akajibu yule kiboko wa matopeni, Ol Makau alivyogeuka nyuma akakutana uso kwa uso na uso ulionuna wa Sapuki"

"Aaah, Sapuki!, Habari mkuu," akasema Ol Makau huku akijichekesha na kujibaraguza.
"nilikuwa nakutafuta sana, naomba twende pembeni tuongee kidogo"

Nalutuesha kidogo alipuke kwa kicheko lakini alijikaza kwa nguvu zake zote. Hajawahi ona mnyama mnene kama Sapuki. Sapuki alikuwa anaburuza tumbo chini. Shingo yake haikuonekana na ngozi nene ilikuwa inakaribia kuziba macho yake. Alivyokuwa amenuna mashavu yake yalikuwa kama kaficha mipira mikubwa huku na huku mdomoni. Ol Makau alikuwa anaingia kama mara tatu kwa Sapuki. Ili asije akaharibu mambo ikabidi ajifiche nyuma ya Ol Makau. Akilini aliwaza kama kipindi cha njaa Sapuki yuko hivi, vipi kipindi cha chakula tele!?

"Nimepata habari zako, sihitaji hata kukusikiliza. Hivi Makau unafaidika nini na kuleta vurugu mtoni?" akasema Sapuki kwa masikitiko. "Haya kisa cha kumtukana Kinyang ni nini?"

"Sikiliza mkuu, mi Kinyang sijamtukana, nilimfananishia tu. Huyu unamuona hapa ni binti mdogo na anahangaika na maisha yake, anataka tu kuvuka. Na ukiangalia, maji yameongezeka. Ina maana hali ngumu zitufanye tupoteze unyama wetu!?"
 
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom