nameless girl
JF-Expert Member
- Apr 22, 2012
- 4,195
- 2,675
1
MLANGO uligongwa tena. Safari hii mgongaji aligonga kwa nguvu zaidi. Kwa mbali, sauti yake ilisikika ikinong’ona, ikiwa na kila dalili ya hofu na wasiwasi, ikisema, “Tafadhali nifungulie… dakika moja tu ya muda wako…”
Joram aligeuka kumtazama Nuru ambaye alikuwa chali, juu ya kitanda, vazi jepesi la kulalia likiwa pazia pekee lililouweka sirini mwili wake laini; unaolazimisha kutazamwa tena na tena. Hata hivyo, halikuwa pazia maridadi kiasi hicho. Wepesi na ulaini wa vazi hilo haukuwa kipingamizi cha haja dhidi ya macho ya Joram ambayo yaliweza kuona waziwazi hazina ya uzuri usiochuja, iliyokuwemo katika umbo hilo; hazina ambayo Joram alikuwa akijifariji kwa kuitazama na kuipapasa; vidole vyake vikistarehe; roho ikiburudika na nafsi yake kuridhika; muda mfupi tu kabla ya yeyote aliyekuwa hapo mlangoni akibisha hajafika.
Macho ya Nuru, ambayo yalikuwa yameanza kulainika kwa mguso wa vidole vya Joram Kiango, vilivyohitimu kugusa, yalirudiwa na uhai yalipoona maswali katika macho ya Joram. Kama aliyejua Joram anauliza nini alitamka kwa upole, “Mfungulie.”
“Anaweza kuwa nani? Na anataka nini saa hizi?”
“Majibu yenye uhakika utayapata hapo baada ya kumfungulia mlango.”
Joram alisita tena, hakuweza kufikiria nani anaweza kufanya ziara chumbani kwake usiku huo, saa sita kasorobo! Zaidi hakuhitaji kabisa kupata mgeni yeyote muda huo alikuwa akijiandaa kwa mara nyingine kufanya ile ziara ya kila siku katika bustani isiyokinaisha iliyofichwa katika umbo la Nuru, safari ambayo kamwe haimchoshi na bado kila anaposafiri inakuwa kana kwamba ni mpya zaidi. Kama jana alisafiri kwa kila kitu kama ndege, leo itakua kana kwamba yuko katika jahazi linalosukwasukwa kwa mawimbi mazito, ambayo badala ya kutisha na kuogofya yanafariji na kusisimua. Na kesho ataivinjari bustani hiyo huku akielekea angani. Kesho kutwa…
Hapana. Si hilo lililomfanya asite kufungua mlango. Hasa ni hisia. Zilikwishamfanya aamini kuwa mgeni huyo hakuleta habari njema. Si kwamba Joram alikuwa mwoga wa habari mbaya, bali alikuwa ameamua kujitenga kwa muda na dunia aliyoizoea, dunia ya Joram Kiango.
Utashangaa kuwa chumba hiki walichokuwemo kilikuwa kidogo chenye kitanda kimoja kikiwa hoteli ya daraja la nne, au mwisho, katika kimojawapo cha vijimitaa kisicho na jina, katika vitongoji vya Tandale; kijihoteli ambacho Joram hata hakujishughulisha kufahamu jina lake ambalo lilimtoka mara baada ya kupatiwa ufunguo!
Joram, ambaye maisha yake yote ni katika miji mikuu na mahoteli ya daraja la kwanza! Joram ambaye sura yake ni maarufu katika magazeti na televisheni zote duniani, akiwa na uzito wa aina yake katika masikio ya karibu kila mtu. Naam, Joram yuleyule ambaye sasa yuko katika chumba hiki chenye kuta zilizochakazwa kwa utandu wa buibui, chumba ambacho kingeweza kutoa harufu ya kutatanisha, endapo mafuta yenye harufu nzuri ya Nuru yasingeibabaisha harufu hiyo! Hata hivyo, hilo halikuwafanya waepuke ukatili wa kunguni na mbu jeuri, wasiosikia dawa, waliokuwa tele katika vyumba vyote vya hoteli hii. Zaidi ya wadudu hao, panya wenye ukubwa wa paka mdogo waliwadhihaki sana kwa kuwatazama kwa macho ya kebehi na kisha kuwarukia kitandani walipoona Joram na Nuru hawajishughulishi nao.
Joram na Nuru walizistahimili kwa sababu moja tu, ya kuepuka kupigiwa hodi kama hizi, ambazo zingeleta mgeni wasiyemhitaji. Hapa alikuwa mafichoni. Na amekuwa katika maficho hayo leo wiki ya pili na siku mbili, tatu, wakati huohuo wakibadili majina haya na yale na kuvaa sura mbalimbali za bandia ili wasifahamike; tabia au mwenendo ambao waliuanza tangu waliporejea kishujaa toka huko Afrika Kusini ambako walifanya yale yaliyofanyika, yale ambayo hayatasahaulika.
Kwa kweli, stahili yao haikuwa kuwa katika chumba hiki, wakati kama huu. Haki yao ilikuwa wawe katika chumba chenye hadhi, miongoni mwa watu wenye hadhi. Ni hilo ambalo Taifa lilihitaji kuwatendea tangu ilipodhihirika kuwa ni wao walioachia lile pigo takatifu ambalo watawala dhalimu wa Afrika Kusini kamwe wasingelitoa mwilini, pigo ambalo baada ya kuandikwa sana magazetini, kutajwa katika redio na televisheni, bado waandishi mbalimbali wamejitokeza kuiweka kumbukumbu hiyo katika vitabu. Hapa nchini mwandishi mmoja hakubaki nyuma, tendo hilo la kishujaa amelitungia kitabu alichokiita Tutarudi na Roho Zetu? Ushujaa huo wa Joram Kiango na yule msichana wa aina yake, Nuru, ulimfanya Rais aamuru Joram atafutwe ili apewe tuzo ya Kitaifa na kutangazwa hadharani kuwa shujaa wa taifa na afrika. Ni kutopenda sifa za aina hiyo kulikowafanya waamue kujificha huku ili wasubiri roho za binadamu ambazo ni nyepesi kusahau mema na mashuhuri kuhifadhi mabaya zitakaposahau mchango wao, ndipo wangejitokeza na kurudia mzunguko wao wa maisha.
Jambo la kushangaza ni kwamba safari hii binadamu hakuelekea kusahau. Uchunguzi wao uliwathibitishia kuwa upelelezi ulikuwa ukiendelea kufanyika nyumba hadi nyumba, kichochoro kwa kichochoro, kuwatafuta chini ya uongozi wa Inspekta Kombora.
Ndipo wakaendelea na ukimbizi huu.
Na sasa mtu anabisha hodi, mtu ambaye kwa vyovyote si mtumishi wa hoteli hiyo. Aliendelea kugonga.
“Mfungulie,” Nuru alisema tena akiinuka na kujitupia mavazi zaidi mwilini mwake.
Joram alivuta taulo akalifunga kiunoni mwake. Kisha, akauendea mlango na kuufungua. Mtu aliyekuwa hapo mlangoni hakuwa na afya nzuri. Joram hakuona kwa nini aligonga mlango wake badala ya mlango wa daktari yeyote aliyekuwa karibu. Hali yake ilimfanya amkaribishe kwa ustaarabu kuliko alivyotegemea. Akamwongoza na kumketisha juu ya kiti hiki kikuu kuu ambacho zamani kingeweza kuitwa kochi. Sura yake ilikuwa ngeni machoni mwa Joram. Alipoanza kusema, sauti yake ilikuwa ngeni vilevile masikoni mwa Joram na Nuru, ambaye sasa alikuwa ameketi kitandani; akimtazama kwa mshangao. Kwa kila hali mgeni huyo alionekana kuwa mtu aliyetoka nje ya nchi, jambo ambalo liliwafanya wamsikilize kwa makini zaidi. Alikuwa hasikiki vizuri.
“Jikaze kidogo… haya… unasemaje?”
Joram alimnong’oneza akiwa amemshika begani.
“Joram… Kiango wewe?” aliuliza kwa udhaifu.
“Ndiye. Unasemaje?”
“Nak… nakufa…” alilalamika.
Ndiyo. Kifo hakikuwa mbali sana na roho yake. Hilo Joram hakuwa na haja ya kuambiwa. Lakini bado hakuona kama hilo lingeweza kumtoa mtu huyo kokote huko alikotoka na kuja kumwambia hivyo mtu ambaye hakuwa na undugu, wala urafiki naye. Hivyo, aliendelea kumshawishi aseme kilichomleta.
“Nimetafuta s… sana wewe. Nak… nakufa… la, la,la… sifi kabla ya kutimiza… kazi… kazi niliyotumwa na… Rais wetu,” aliendela kutokwa na maneno kwa taabu.
“Rais!” Joram aliuliza. “Rais gani?”
“Ra… Ra… Rais wa Pololo… ame… nini… nituma. Nikuite… yuko hata… hatarini…”
Uwezo wa kuzungumza ulionekana kumtoka harakaharaka. Mara akaegamia kiti alichokikalia na kuanza kutapatapa huku akibubujikwa na maneno ambayo hayakuleta maana yoyote katika masikio ya Joram na Nuru. Mara alitulia kimya, macho yenye hofu yakiwa yamemtoka pima, pindi roho ikimkimbia. Dakika iliyofuata alitulia kimya kabisa, katika hali ya utulivu mkubwa; kama ambaye anasubiri tuzo baada ya kuifanya kazi aliyotumwa.
Joram na Nuru walitazamana kwa mshangao. Kwa muda hakuna aliyejua la kusema. Kisha, Joram alitabasamu na kusema polepole, “Nadhani sasa nimekuwa mtu maarufu duniani. Kama mtu anaweza kusafiri toka umbali wa kilometa nyingi kuja kufia katika mikono yangu! Mama yangu ana haki ya kujipongeza kupata mtoto wa aina yangu.”
“Joram!” Nuru alimkatiza. “Hili sio jambo la kufanyia mzaha. Lazima tujue la kufanya. Sasa hivi tuna mzigo mzito mikononi mwetu. Mzoga wa tembo ni mwepesi kuliko maiti ya mtu. Na tuko nayo chumbani. Kumbuka tumepanga kwa majina ya bandia. Hilo peke yake linatosha kututia hatiani. Lazima tuamue la kufanya haraka.”
Joram alitabasamu tena. Safari hii tabasamu lake lilikuwa halisi, likiufurahia ushujaa wa msichana huyu. Msichana wa kawaida sasa hivi angekuwa akitetemeka, machozi yakimtoka. Mwingine angekuwa amezimia au kutapika kwa hofu ya maiti. Huyu alikuwa imara, kama alivyo. Baada ya tabasamu hilo Joram alimrudia marehemu na kumtazama kwa makini zaidi.
Mwili wa marehemu ulionyesha kuwa hakuwa mtu aliyejua sana amani. Alikuwa mkakamavu, mwenye makovu hapa na pale. Hata hivyo, makovu hayo hayakuwa kisa cha kifo chake cha ghafla. Joram aliendela kumkagua. Katika mfuko wake mmoja alipata hati yake ya usafiri. Mfuko wake mwingine ulikuwa na ramani pamoja na pesa chache ambazo jicho la mtu aliyehishiwa lingeziona nyingi sana. Ni katika mfuko wa siri sana, uliofichika mapajani, ambapo Joram alipata bastola ndogo.
Baada ya kuhakikisha kuwa hakuacha kitu chochote katika mwili wa marehemu, alimfunika kwa shuka moja ya chumba hicho. Kisha, alirejea kitandani ambako alianza kuvichunguza vitu vya marehemu kwa dhamira ya kupata chochote ambacho kingeweza kumsaidia katika mkasa huu wa kutatanisha.
Hati yake ya usafiri ilimwonyesha kama mwandishi wa habari, jina lake likiwa wazi kwa herufi kubwakubwa, Patauli Kongomanga. Umri wake ulikuwa miaka arobaini na mbili. Hati hiyo ilikuwa na mihuri ya nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya ambako aliwahi kutembelea. Alikuwa mtu wa safari mara kwa mara. Ni macho yake katika picha hiyo ambayo yalimwonyesha Joram kile alichohitaji kukiona, kuwa kama alikuwa mwandishi wa habari, hakuwa mwandishi wa kawaida. Hiyo ilikuwa kazi yake ya ziada tu. Kazi yake hasa ingekuwa mbali sana na uandishi na karibu zaidi na ukachero. Hilo lilikuwa wazi katika macho ya mtu huyo pichani. Joram asingeshindwa kuyafahamu macho ya watu hao, hasa yanapomtazama mpiga picha. Huwa yana aina yake ya utazamaji ambayo makachero wengi hushindwa kuificha.
Pesa alizokuwa nazo zilikuwa za nchi mbalimbali pamoja na Tanzania. Upande mmoja wa noti zao, ulikuwa na picha ya Rais wao, ikiwa sura ya mtu aliyeshiba, macho ya mtu mwenye njaa. Upande wa pili ulikuwa na picha ya vitu mbalimbali kama mazao mashuhuri, wanyama maarufu; na kadhalika.
Joram alimtazama kwa makini Rais huyo, mtu ambaye inasemekana anamwita! Anamwita kweli? Na anamwitia nini? Na kwanini mtu aliyetumwa kumwita akate roho kabla hajaukamilisha ujumbe wake? Kitu gani hasa kilimwua?
Jibu lisingeweza kuwa karibu kiasi hicho. Alijua kwa vyovyote alikuwa ametumbukia pasi ya hiari katika shimo lenye kiza kinene ambacho kilimhitaji yeye kama Joram Kiango kulivinjari na kupata jibu.
“Utafanya nini?” Nuru, ambaye alikuwa akimtazama kwa utulivu muda wote huo, aliuliza.
“Naona kama sina la kufanya zaidi ya kumtii marehemu. Naitwa na Rais wa Pololo.”
“Utakwenda?”
“Vipi nisiende? Nawaheshimu sana maraisi wetu, hasa wale waliopigania uhuru. Unajua wamebaki wachache sana.”
“Utakwenda!” Nuru aliuliza kwa mshangao. “Una hakika gani kuwa unaitwa? Yawezekana huyo alisema hayo kwa kutapatapa tu pindi roho ikimkimbia. Na kama sivyo, huoni kuwa yaweza kuwa safari ya hatari sana? Kama mjumbe aliyetumwa tu kukuita ameweza kupoteza maisha kabla hata hajaufikisha ujumbe wake kikamilifu, wewe unayeitwa utakuwa katika hali gani?”
Joram alitabasamu kidogo. Akaushika mkono wa Nuru na kuutomasatomasa taratibu. Kisha, akasema, “Tangu lini umeanza kujenga tabia ya uoga? Usinidanganye, unapenda sana kwenda huko vilevile. Huwezi kujua. Pengine naitwa nikawe Waziri Mkuu au Mkuu wa Majeshi. Yawezekana tukapokelewa kwa shangwe na kupewa heshima ya hali ya juu na huduma zote za kifalme. Siwezi kuichezea bahati kama hiyo. Binadamu uishi mara moja tu.”
Nuru alijua wazi kuwa Joram alikuwa hasemi kweli. Katika yote aliyoyategema kwenye ziara kama hiyo heshima ya kifalme haikuwemo kabisa akilini mwake. Akamtazama kwa macho yaliyomfaya amsikie wazi kama anayesema, “Wacha mzaha.”
Hilo lilimfanya Joram acheke tena na tena na kusema polepole, “Hata kama kuna hatari, naamini hatari hizo si mbaya kama kuadhibiwa na kunguni kusimangwa na mende, kuchezewa na panya huku ukiumwa na mbu wasio na huruma. Unajua, Waafrika wengi hadi leo bado tunakufa kwa malaria zaidi ya risasi? Tutaendela kujificha hadi lini tukisubiri kifo cha malaria. Tutakwenda zetu safari hii fupi. Tutakaporudi wanaotutafuta watakuwa wamekwishachoka kama si kutusahau kabisa.”
Aligeuka kuyatazama maiti ambayo bado yalikuwa yamelala juu ya kiti kwa utulivu, yakiwa hayana dalili zozote za kufahamu uzito wa mkasa yaliouweka mikononi mwa wenyeji wake. Kisha, Joram alimgeukia Nuru na kumwuliza kwa sauti nyembamba, “Unafahamu nini juu ya nchi ya Pololo?”