Hadithi: "Kivuli cheusi"

HADITHI: KIVULI CHEUSI


SEHEMU YA TANO


TULIPOISHIA......

“lakini afande mimi sijaua” Maneno hayo ya kiudhaifu yakamponyoka Eva. Vanessa alicheka kwa huruma na kumwambia “usiogope, mimi sio afande ndio maana sijajitambulisha kama Afande Vanessa. Naomba uwe huru kuzungumza na mimi” alimpa moyo kisha aliendelea “naomba nifahamu wewe unamfahamu vipi Bertha”

jina lake alikwisha ambiwa na wakazi wawili, watatu wambea walioponyokwa na maneno wasiyoulizwa na mtu ambaye hawamfahamu. Ili mradi ilikuwa ni siku ya majonzi, kila mtu alizungumza lake analolijua kumuhusu Bertha. ‘alikuwa mpole, masikini dada wa watu’ alimsikia mmoja akisema .

huyu naye “aliongea na kumchangamkia kila mtu” wa mwisho kabla hajamuita Eva ndiye akalitaja jina la Bertha “halafu Bertha ni mgeni, hapa hana hata wiki tatu. Yule jamaa yake aliyekuwa naye jana hapo GQ simuoni hapa? ina maana hana taarifa” pia habari hiyo ilimsukuma haswa afanye mahojiano na Eva.

ENDELEA............

Ilimsukuma kufanya mahojiano na Eva kwa kuwa alisikia pia kuwa mtu wa kwanza kugundu mauaji hayo ni mfanyakazi kutoka katika pub ambayo jana alikuwako Bertha.

Pili mtu ambaye alikuwa naye jana ni mwanaume ambaye inasadikika kuwa leo hayupo katika tukio hili.
Akaanzia hapo kupekenyua.

Raymond Chilambo aliipokea simu hiyo akiwa njiani kuelekea nyumbani kwa Bertha. Ilikuwa ni simu nyingine iliyoingia na habari mbaya sana kwake. Simu nyingine baada ya ile ya kwanza iliyompa taarifa juu ya kuuwawa kwa mtoto wake.

Hivyo kila namba ngeni kwake aliipokea kwa hudhuni, ila ambayo anaifahamu hakujisumbua kupokea. Alifahamu fika ni wambea ambao wanataka kumpa umbea wa hapa na pale. Pamoja na kujikaza kama mwanaume, yeye aliuita umbea. Aliuita hivyo kwa kuwa aliamini alikuwa na maadui wengi kuliko marafiki. Marafiki wanaoibuka wakati wa matatizo yake na kujifanya wakimpa pole.

“Raymond chilambo, nikusaidie nini” aliipokea hivyo Sauti ya upande wa pili ikakoroma. “unasema?” aliuliza kwa mshituko bila kufahamu kuwa simu ilikuwa imeshakatika. Aliishia kuhakikisha kama simu ilikuwa hewani “halo halo…” akaambulia patupu. ‘kivuli cheusi?’ akajinong’oneza.
“baba Bertha unasemaje?” Bi Furahiya aliuliza. Raymond hakufahamu kuwa mawazo yalimfanya aweze kuongea kwa sauti, hata kwa ile sauti ya kujinong’oneza. Raymond alichanganyikiwa sana.

Hivyo hakujibu chochote.

Bi Furahiya ndiye alikuwa akiendesha gari, hivyo gari ilienda kwa mwendo wa kawaida sana. Raymond alihisi machozi yakimtoka kila akikumbuka jinsi alivyompenda binti yake. Hakuwa mtoto wake wa pekee, ila kwa Bi Furahiya alikuwa ni wa kwanza na wa pekee. Alikuwa na watoto wakubwa wawili wa kiume ambao aliwapata akiwa sekondari. Aliwakataa kutokana na ugumu wa maisha. Hivyo hakujua taswira zao za ukubwa wala hakuwa na uhakika kama walikuwa hai tena.

Walifika eneo ambalo Bertha alikuwa akiishi. Umati mkubwa wa watu ulimfanya adondoshe chozi. Bi Furahiya alilia kwa uchungu zaidi hata kuwashitua wale wengine ambao walikuwa eneo lile.

Mmoja mmoja alisikika akisema “ni ndugu yake”

Mwingine akapatia kubashiri “huenda akawa ni mama yake”

Wakati ambao Raymond na Furahiya wanaingia eneo hilo, maiti zilikuwa zimeshatolewa eneo la tukio na kupelekwa mochwari. Vanessa alikwisha kunakili hili na lile alilolipata kutoka kwa Eva, Inspecta Nyaluto alikwisha ondoka na Inspekta Jafary Hiza na askari wengine hawakukaa sana, nao walikwisha rudi katika ofisi zao. Walibaki askari wachache waliokuwa wakipekua nyumba hiyo kutazama kama kutakuwa na lolote litakalowasaidia kumpata muuaji.

Raymond na Bi Furahiya wao walielekea hospitali walipoelekezwa kuwa miili ya watoto hao, imepelekwa.
Simu ya Raymond ikaita tena. Raymond aliipokea bila kuongea chochote. Kama walikuwa wakitegana upande wa pili nao haukujibu kitu mpaka simu ilipokatika. Hapo wasiwasi ukamvaa Raymond na uwoga ukamtetemesha. Akaona si jambo la kulinyamazia, ni heri amueleze mke wake.

*********

Moses baada ya kutoka Kwenye kibanda cha simu, alienda bar ya jirani kuivua midabwada aliyoiona kama mzigo kwake. Aliingia katika bar moja ya jirani na kiwanja cha mpira wa miguu huko karume, soko maarufu la mitumba. Hakuna ambaye aligundua hila zake. Aliingia katika bar hiyo kama mteja wa kawaida aliiagiza supu aipendayo, na bia ya baridi. Akiwa katika hali ile ile ya uzee aliyechoka, akanyanyuka na kwenda maliwatoni. Aliporudi mwendo ule wa kuchechemea haukuwepo. Ni nani angefahamu kijana huyu mzuri aliyehifadhiwa katika moja ya suti nadhifu, ndiyo Yule mzee mchafu aliyeagiza supu akiwa na lijimfuko lake lililowavuta wengi, kudhani huenda amebeba kinyesi? Mfuko ule ule ndiyo ulihifadhi suti hiyo na kiatu mchongoko kilichong’ara kwa rangi nyeusi.

Alitembea vizuri na kuwavutia kila aliyekuwemo mahali pale. Kwa bahati mbaya aliyoidhamiria, aliipita meza aliyokaa mwanzo na kwenda kaunta. Akaiagiza bia ya moto, akiwa na tabasamu laini lililomfanya muhudumu amtazame mara ya pili. Hakika alikuwa ni kijana ambaye si mfupi sana wala mrefu wa kutisha lakini mwenye uso wa mvuto. Uso wake bapa ulinyimwa ndevu, kutokana na usafi alionao. Ni vipele vichache ndivyo viliathiri kidevu chake. Aliinywa haraka haraka huku akionekana mzoefu wa maji.

Huyo ndiye Moses mwenye chuki kubwa na ukoo wa Chilambo. Chuki iliyomfanya atumie hila nyingi, hata zikamfanya ajidumbukize katika mahusiano na Bertha ili aweze kumnasa kila aliyehusika katika njama za mauaji ya familia yake. Hakujali ni nani alihusika ama hakuhusika ila kulipiza kisasi kulihusu ukoo mzima ili moyo wake uridhike. Alipokumbuka tukio lile alilolishuhudia mwenyewe kwa macho yake, aliiagiza konyagi chupa kubwa akaifakamia hata jirani yake akaogopa.

Hasira zikampanda alipomkumbuka Raymond. Akataka kuzungumza naye, ndipo alipoamua kumpigia simu. Alimpigia simu wakati ule ambao Raymond na Bi Furahiya walikuwa njiani wakielekea hospitali. Simu iliita, ikapokelewa, lakini Raymond hakuongea chochote. Naye hakuthubutu kuongea. Si alifahamu kuwa Raymond aliitambua vyema sauti yake? Sasa iweje aharibu njama zake? Alizisikia pumzi nzito za Raymond zikipanda na kushuka. Simu ilikuwa hewani kwa nusu dakika mpaka alipoamua kuikata. Funda la pili, likaifuta pombe yote ndani ya chupa na kuondoka zake kwenda alipopajua yeye.

ITAENDELEA!!
 

HADITHI: KIVULI CHEUSI


SEHEMU YA SITA:

TULIPOISHIA...............


Huyo ndiye Moses mwenye chuki kubwa na ukoo wa Chilambo. Chuki iliyomfanya atumie hila nyingi, hata zikamfanya ajidumbukize katika mahusiano na Bertha ili aweze kumnasa kila aliyehusika katika njama za mauaji ya familia yake. Hakujali ni nani alihusika ama hakuhusika ila kulipiza kisasi kulihusu ukoo mzima ili moyo wake uridhike. Alipokumbuka tukio lile alilolishuhudia mwenyewe kwa macho yake, aliiagiza konyagi chupa kubwa akaifakamia hata jirani yake akaogopa.
Hasira zikampanda alipomkumbuka Raymond. Akataka kuzungumza naye, ndipo alipoamua kumpigia simu. Alimpigia simu wakati ule ambao Raymond na Bi Furahiya walikuwa njiani wakielekea hospitali. Simu iliita, ikapokelewa, lakini Raymond hakuongea chochote. Naye hakuthubutu kuongea. Si alifaham
u kuwa Raymond aliitambua vyema sauti yake? Sasa iweje aharibu njama zake? Alizisikia pumzi nzito za Raymond zikipanda na kushuka. Simu ilikuwa hewani kwa nusu dakika mpaka alipoamua kuikata. Funda la pili, likaifuta pombe yote ndani ya chupa na kuondoka zake kwenda alipopajua yeye.

ENDELEA.......................

Baada ya kutoka hospitali, Raymond na Bi Furahiya walielekea nyumbani. Ilikuwa ni karibu na jioni hivyo foleni haikuwa kubwa sana. Walipofika nyumbani walipokelewa na mlinzi wa getini, Majura.

"Majura niache kidogo, leo sipo sawa"

Alitamka Raymond, baada ya kusimamishwa na Majura pale getini. Ilikuwa ni kawaida kwa Raymond, kumuuliza Majura kama kuna mgeni yeyote aliyekuja. Siku hiyo haikuwa siku muafaka ya kumuuliza hayo. Alifahamu fika ni lazima wageni wangekuwa ni wengi kuhani msiba. Msiba ulimchanganya, lakini sauti iliyokoroma kama ‘kivuli cheusi' Sauti iliyojitambulisha wakati alipopokea simu yake kutoka kwenye simu ya kibandani, ikamtisha zaidi.

Alipopita sebuleni, aliwaona watu kadhaa waliokuwa wakilia kwa uchungu, yeye akawapita kama hakuwaona. Aliingia chumbani kwake kivivu, baada ya kuitikia pole zao kwa kichwa. Hakuvua chochote kutoka katika mwili wake mara alipoona kitanda, alijitupa hivyo hivyo na viatu bado vikiwa mguuni.

Akazama kwenye tafakuri nzito, mkono ukiwa kichwani. Aliingalia taa kubwa yenye nakshi za kuvutia kama ingeweza kutoa jibu lolote kati ya maswali yaliyomsumbua. Lakini mawazo yake hayakuwa katika chumba alicholaza mwili wake. Aliukumbuka mchana ambao aliipokea ile simu.

Mara baada ya kuisikia kauli iliyosema "naitamani roho yako" kisha ikakatwa ndiyo ilimuumiza kichwa. Kisha jina la ajabu likajirudia rudia kichwani mwake kama mwangwi "kivuli cheusi" kama angekuwa akihesabu basi angeshindwa kutoa idadi kamili ya alivyolitamka jina hilo akijaribu kuvuta kumbukumbu.
Simu yake ikapata uhai baada ya muda. Haikutokea namba wala jina la mpigaji, kwenye kioo iliandikwa UNKOWN CALLER. Akaipokea akiwa anajua fika ni simu nyingine ya kitisho.

"Nani mwenzangu" hakujitambulisha.

Sauti upande wa pili ikajibu "Najua unanifahamu fika ni mimi Kivuli cheusi" Raymond aliongea akiwa anatetemeka katika sauti yake

"Unahitaji nini? Kama Roho yangu njoo uichukue niachie familia yangu"

"umepata ujumbe wangu kutoka kwa Majura"

"Majura?" Raymond akauliza kwa jazba. Sauti ile upande wa pili ilijibu kwa kicheko cha dharau na kisha kukata simu. Raymond hakujijua kuwa ameshasimama na kukizunguka chumba chake mwenyewe mara ngapi, alichokitambua yeye ni kuwa yupo nje akimfuata Majura, mbio.

"Majura ulikuwa unasemaje?" alimuuliza.

Majura alitoa boksi moja kubwa lililonakshiwa na kumpatia Raymond "pole sana bosi kwa matatizo. Aliileta babu mmoja, huku akisisitiza ni ya muhimu sana uipate usiku wa leo" alisema. Akili ya Raymond haikuwa katika kusikiliza hadithi za Majura.

Alikwishalifungua boksi lile muda mrefu, kilichokuwemo ndani ya boksi kikamfanya kupoteza fahamu.

Kama asingekuwako Majura karibu yake, basi kisogo cha Raymond kingeisalimu ardhi iliyojaa changarawe. Umapepe wa Majura ukamfanya aropoke.

"Nisaidieni jamaani!!!!!" Kila mtu aliyeisikia sauti ya Majura, alitoka mbio kuelekea getini.


ITAENDELEA................
 

HADITHI: KIVULI CHEUSI


SEHEMU YA SABA:



TULIPOISHIA.............


"Majura?" Raymond akauliza kwa jazba. Sauti ile upande wa pili ilijibu kwa kicheko cha dharau na kisha kukata simu. Raymond hakujijua kuwa ameshasimama na kukizunguka chumba chake mwenyewe mara ngapi, alichokitambua yeye ni kuwa yupo nje akimfuata Majura, mbio.

"Majura ulikuwa unasemaje?" alimuuliza.

Majura alitoa boksi moja kubwa lililonakshiwa na kumpatia Raymond "pole sana bosi kwa matatizo. Aliileta babu mmoja, huku akisisitiza ni ya muhimu sana uipate usiku wa leo" alisema. Akili ya Raymond haikuwa katika kusikiliza hadithi za Majura.

Alikwishalifungua boksi lile muda mrefu, kilichokuwemo ndani ya boksi kikamfanya kupoteza fahamu.

Kama asingekuwako Majura karibu yake, basi kisogo cha Raymond kingeisalimu ardhi iliyojaa changarawe. Umapepe wa Majura ukamfanya aropoke.

"Nisaidieni jamaani!!!!!" Kila mtu aliyeisikia sauti ya Majura, alitoka mbio kuelekea getini.


TUENDELEE...............


Vanessa ni mwanamke wa ajabu sana. Aliwashangaza wengi katika uvutaji wake wa sigara. Alizivuta zile sigara kubwa zilizoitwa ‘cigar' Katika ulabu alipendelea haswa zile wine tamu tamu, kama sweet anna na sinzano. Huyo ndiye mpelelezi aliyekataa kujiunga na kikosi maalumu cha usalama wa taifa na kubaki kama mwandishi wa habari wa kujitegemea.

Siyo kwamba hakufuatwa, hata Raisi mwenyewe aliwahi kupoteza dakika zake na kumuandikia barua ya kumomba ajiunge na kikosi hicho. Alikataa bila sababu, lakini sababu aliijuwa mwenyewe. Vanessa aliupenda uhuru wa kufanya kazi zake binafsi. Hakutaka mtu wa kumshinikiza afanye hiki na kile. Magazeti yalimuandika kwa kumtukuza na hata waandishi wengi wa riwaya wakamtaja katika riwaya zao kama mwanamke wa chuma. Akawashinda wanaume katika mapigano na hata upeo wa kufikiria.

Leo alikaa ofisini kwake nyuma ya kiti kikubwa kinachozunguka kama tiara. Glass ya sinzano ilikuwa mkono wa kulia, sigara ikashikwa mkono wa kushoto. Kichwa kikaegemea kiti kikiwa katika tafakuri nzito. Aliwaza kuhusu mauaji ya kutisha.

Mara akakumbuka kitu.

Aliinama kwenye meza yake iliyojaa picha mbali mbali za maiti ya Bertha na Pamela. Akauvuta mtoto wa meza hiyo, kisha kuibuka juu na bahasha iliyohifadhi kitu Fulani. Vanessa aliiangalia bahasha iliyohifadhi nakala moja ya picha ile ya kivuli cheusi aliyojipiga Moses.

Wakati akiitazama picha ile, simu yake ya mezani ikapata uhai.

"Vanessa" ilikuwa ni sauti ya Inspekta Jafary Hiza

"habari yako Hiza?"

"salama, umepata majibu yeyote juu ya mpigaji wa picha hiyo?" Hiza aliuliza
"hapana na bado najiuliza kwanini mtu huyu ameamua kuuacha ushahidi huu kama sehemu ya kuendeleza mauaji yake" alisema Vanessa "sawa, pia majibu ya Postemoterm kuhusu ule mwili wa yule binti mwingine tuliyemkuta pale sebuleni"

Vanessa akauliza "yule aliyeibusu ardhi akielea juu ya mapovu?"

"Acha mzaha Vanessa, Majibu yametoka na yanasema kuwa, alikunywa sumu kali iliyomnyang'anya uhai wake"

Inspekta Hiza alihitimisha hivyo na kuikata simu mara baada ya kuagana. Vanessa akabaki akiwa hajaelewa jambo.

Alijidumbukiza kwenye tafakuri nyingine nzito, hata pombe iliyoanza kumkolea, ikimsaliti na kubaki mweupe. ‘ina maana alianza kufa yeye au Bertha? Ni nani alikuwa wa kwanza kuuwawa? Ni nani alikuwa mlengwa wa mauaji haya?' alijiuliza Vanessa akiishirikisha nafsi yake.

Alisimama akakizunguka chumba chake. Akaongeza kinywaji kwenye glass akakifuta chote. Alienda pale, akarudi kitini alipotaka kukaa wala hakukaa, alikuwa akiwaza tu. Ghafla alitabasamu, tabasamu lililochanua na kuufanya uso wake kuwa mzuri na kuonesha taswira ya umalaika. Hakika Vanessa alipendeza akicheka katika raha. Mashavu yake yakabonyea na kujenga dimples. Alimuita katibu muhtasi wake, alieyemchukulia kama mdogo wake. Yeye aliitwa Naima, mtoto wa kitanga. Binti aliyeiacha shule kutokana na shida za kuilima ardhi iliyonuna kustawisha mazao yake. Aliyetundikwa mimba kabla hajalimaliza darasa la saba na siku ya kujifungua mtoto wake alikataa kutoka akiwa hai. Alifia tumboni baada ya kukosa pumzi. Kipindi hicho Naima alikuwa na miaka kumi na nane.

Alikutana na Vanessa katika harakati zake za kutafuta maisha, alikuwa akiuza mchicha, sukuma wiki na mnafu. Ni nani ambaye hakutokwa na mate alipomtazama Naima? Ni nani ambaye, hakuacha kumsifia alipotazama kifua chake kilichotuna kiuchokozi na kufanyiza mfano wa matiti kifuani mwake? Alikuwa na kiuno kilichobeba mapaja manene na mguu uliofaa kuitwa wa bia. Huyu ndiye Naima mwenye asili ya kiarabu kutoka Tanga, hakutumia mkorogo wowote katika weupe wake.

"nimepata wazo" alimwambia Naima

"wazo gani?"

"kuhusu haya mauaji"

"mauaji ya hawa mabinti wawili waliouwawa huko kiitonyama?" Naima alimuuliza.

"ndiyo. Nimepigiwa simu na Hiza, amenieleza kuwa huyu mmoja" Vanessa alikuwa akiongea huku ameshika picha ya Pamela, akiwa ameyalalia mapovu. "ameuwawa kwa sumu. Hivyo inavyoonyesha, huyu alikuwa wa pili baada ya huyu wa kwanza aliyekatwa kichwa" macho yakamtoka pima Naima na kubaki mdomo wazi. Hakujuwa ni vipi Vanessa akili yake ilifanya kazi haraka hata kutambua hayo yote bila kumfahamu muuaji.

"Inawezekana huyu msichana hakuwa katika njama hizi, ila kihere here chake kilifanya hata akaupoteza uhai" alinyamaza akiyameza mate kwa raha huku akitabasamu kama kawaida yake

"inawezekana huyu aliingilia harakati za muuaji na kutaka kuitoa siri ya mauaji haya"

Naima kicheko kikamponyoka na kumwambia Vanessa "sielewi wewe ni binadamu wa aina gani, nimeanza kukuogopa"

Vannesa akaendelea kumwambia "na ndio maana hata pale eneo la tukio, hatukukuta simu. Inawezekana simu zingetuwezesha kupata ushahidi mwingi. Zilipofuatiliwa namba zilizokuwa zikiingia katika simu ya huyu Bertha.." akashika picha ya Bertha "hakuna historia yeyote. Hivyo inaonekana huyu muuaji kuna mchezo mchafu ameucheza na hawa watu wa mitandao kama sio hawa wajanja wa IT"

XXXXX

Raymond alipokuwa akikimbizwa hospitali, aliipata nafuu. Gari ilikuwa ikienda kasi sana akiwa mapajani mwa Bi Furahiya. Alijishika kichwa na kumtazama mkewe.

"niko wapi?"

Bi Furahiya alishituka kumuona mumewe ameamka, alifurahi sana na kumwambia dereva asimamishe gari. Wote waliokuwemo walishangaa na kumshukuru mungu kwa pamoja.

"mungu mkubwa!!!"

Raymond alitoa amri yakurudishwa nyumbani kwa kuwa alijiona hakuwa na tatizo la kumpeleka hospitali.

"sawa baba Bertha kama ni hivyo, lakini ilikuwa muhimu wewe kwenda kufanyiwa check up.."

"Nimeshasema ulikuwa ni mshituko wa kawaida" Raymond akafoka.

Raymond alikumbuka kila kitu kilichotokea na kuwahadithia kila kitu. Aliwahadithia Bi Furahiya na kaka yake Nyato Chilambo, kuhusu ujio wa lile boksi na alichokiona ndani yake. Boksi lililonakshiwa, lililomfanya apoteze fahamu. Kwa kuwa Bi Furahiya alifahamu yote yanayoendelea, alianza kupatwa na hisia mbaya. Alitetemekwa na mwili sanjari na mapigo ya moyo yaliyomuenda kasi zaidi. Alitamani kulia machozi hayakutoka. Alibaki kuwa mnyonge akisubiri litakalotokea.

Walipokuwa njiani, ndipo gari yao ilipata pancha na kuwalazimu wakae zaidi ya nusu saa eneo hilo la barabara iliyosuswa kupitiwa na magari mara kwa mara. Milango ilikuwa wazi, upepo ukiwapiga. Bi Furahiya alimpatia Raymond barua iliyoandikwa kwa damu. Barua hiyo iliandikwa na Moses. Barua yenye vitisho na masharti ya kuogofya.

Raymond aliisoma huku akitetemeka na moyo kumuenda kasi zaidi. Alitoa onyo. Yeyote aliyeyasikia hayo, asitoe habari hiyo kwa yeyote. Wote wakatii. Tairi likarekebishwa na kuwekwa la spare.
Safari ya kurudi nyumbani ikaendelea

XXXXX



ITAENDELEA..............
 
HADITHI: KIVULI CHEUSI


SEHEMU YA NANE:



TULIPOISHIA.............

Walipokuwa njiani, ndipo gari yao ilipata pancha na kuwalazimu wakae zaidi ya nusu saa eneo hilo la barabara iliyosuswa kupitiwa na magari mara kwa mara. Milango ilikuwa wazi, upepo ukiwapiga. Bi Furahiya alimpatia Raymond barua iliyoandikwa kwa damu. Barua hiyo iliandikwa na Moses. Barua yenye vitisho na masharti ya kuogofya.

Raymond aliisoma huku akitetemeka na moyo kumuenda kasi zaidi. Alitoa onyo. Yeyote aliyeyasikia hayo, asitoe habari hiyo kwa yeyote. Wote wakatii. Tairi likarekebishwa na kuwekwa la spare.
Safari ya kurudi nyumbani ikaendelea

ENDELEA..........



Moses alijirudisha katika mavazi yake yale yale ya kuudhi na taswira ya kishamba iliyomzeesha. Alienda mpaka nyumbani kwa Raymond, kisha akakirudia chumba chake kilichochoka na kuhifadhi kunguni viroboto na kila aina ya wadudu, katika ile guest ya bei nafuu huko Keko magurumbasi.

Kukaa kwake keko magurumbasi, Si kwamba hakuwa na pesa hata aamue kukaa katika chumba kama hicho. Pesa alikuwa nazo nyingi, tena nyingi zilizomkinaisha. Urithi wa kampuni ya baba yake, Mzee Utonga usingemtosha kweli? Usingemtosha kuishi katika hoteli zenye hadhi ya nyota tano? Ale vinono huku akisaza akiwa amezungukwa na walimbwende wenye hadhi ya juu? Mivinyo ya gharama na vyakula vya kutoboa amana ya mwenye kubipu starehe?

Hakuna ambaye hakumjua Moses kipindi yupo chuoni. Huyo ndiye Moses aliyejiita Musolline pale mlimani. Aliyeuvaa umasikini hata akauzoea, akaupenda na aliutamani pale alipokuwa mbali nao. Umasikini uliomuhifadhi mbali na mkono wa polisi pamoja na wale aliowaweka katika harakati zake za kulipiza kisasi.

Alifanya haraka kurudi mafichoni kwake, baada ya kutimiza njama zake. Maficho yaliyomkumbatia kwa kunguni, mbu, viroboto na patasi, waliomganda hapa na pale. Kwa hali ya ulevi, mara moja moja sana; walionesha kumgasi na kujipiga makofi yasiyo na madhara hata ya kuuwa mbu. Jinamizi la kisasi, lilimsukuma kuanza mauaji kwa mpenzi wake. Bertha mpenzi wa kujilazimisha. Hiyo yote ikiwa ni njama ya kutuma salamu kwa wahusika.

Alimuonea huruma sana Yesay kwa kuwa aliumiza hisia zake siku alipomsaliti na kumchukua msichana wake. Bertha kwao kulikuwa na pesa lakini alikuwa na tamaa ya pesa nyingi zaidi. Moses alikuwa nazo za kumchanganya Bertha hata akamsaliti Yesaya wake waliotoka mbali. Bertha hakujua njama za Moses akajisifia kwa wenzake kila alipopita pamoja na Moses.

Moses aliulalia mkono wake akitafakari safari zake za tangu asubuhi, mpaka sasa usiku wa manane akiwa amelewa bwii. Aliikumbuka safari yake ya kwanza, alipoenda katika ile bar. Aliingia kama Mzee aliyechoka na kuagiza supu ya kuku na chapati mbili pamoja na bia ya baridi.

Akacheka

"Niliwaweza kweli" kwa sauti ya chini akasema "Tangu lini nikanywa bia ya baridi mimi?" hakukuwa na wa kumjibu, hivyo alicheka zaidi. Ilishangaza sana alipocheka kwa nguvu hata kikohozi kilichokuwa kikishitua shitua, sasa kikaachia na kujirusha katika kidevu chake. Alijifuta mdomo kwa mkono wake. Mara alibana pua yake, akiiga sauti fulani ya kike.

"shenzi nilijuwa tu huyu babu hawezi kurudi tena" alimuiga yule muhudumu katika ile bar alisimama huku akipepesuka pepesuka kwa ulevi. Hakika alilewa. Alienda kushoto akarudi kulia, lakini alikuwa imara akapiga breki asiibusu ardhi.

Sakafu iliyopoteza hadhi ya kuitwa sakafu kwa mashimo mashimo yaliyojichimba baada ya cement kumomonyoka. Alisonya, kisha akabeua na kuanza tena kucheka. Aliikumbuka safari yake ya kwenda nyumbani kwa Raymond Chilambo na kukutana mlinzi aliyemfahamu fika, "bwana mdogo, Majura" akajisemea.
Aliporudi kutoka kumpa mzigo ule Majura, mzigo uliomuangusha na kumfanya Raymond kupoteza fahamu ndipo akapata wazo, wazo la kuangamiza tena. Alitaka kuangamiza, ili alinde uhuru wake. Ndani ya moyo wake alihisi kabisa hayupo huru na mtu ambaye alihatarisha maisha yake alikuwa ni Omary Kibanga yule muhudumu wa nyumba ya kulala wageni.

Tukio lile la kuokota kitambulisho alijua fika lingemtia katika wakati mgumu endapo serikali ingefikia uamuzi wa kutangaza kumtafuta muuaji wa bertha kupitia katika vyombo vya habari. Alikuwa na hakika hakuna mwenye picha yake, wala taswira; hivyo isingekuwa rahisi kutambulika.

"lakini, lakini.." akiwa katika kuwaza akawakumbuka wahudumu wa pub ya GQ. Eva ndiye muhudumu wa mwisho kumuhudumia yeye na Bertha. Huyo ndiye angeharibu harakati zake za kulipiza kisasi. Katika jeshi la polisi, walikuwako vijana walio na uwezo mkubwa wa kuchora picha kwa kuhadithiwa tu jinsi mtu alivyo. Eva ana uwezo mkubwa wa kuwaongoza vijana hao na sura yake kupatikani.

"Nimuanze nani?" akajiuliza huku akiangalia saa yake. Ilikuwa yapata saa 12:30 usiku. Uhakika wa kumuanza Eva ukapotea. "lazima leo nifute ushahidi wa mmoja" akajisemea huku akifika eneo la maegesho ya bajaji na kuichukua mojawapo ya bajaji nyingi zilizojipanga hapo. Bajaji hiyo hakupenda kuichukua moja kwa moja mpaka keko magurumbasi yalipo maficho yake, Alitumia bajaji tatu mpaka kufika hapo kwenye nyumba ya kulala walala hoi. Mtu wake wa kumtoa kafara ndio kwanza alikuwa anapasha mapafu moto kwa kahawa.

Tabasamu laini likamponyoka Omary.

Nadhani moyoni mwake alipendezwa na utembeaji wa mzee huyu mchafu. Kwa hila za moses na jinsi alivyopenda kubadilisha muonekano wake, ugoro ukamzoea na kumpenda. Meno yake yalikwisha chafuka na kufanana na wazee kabisa. Akalijibu tabasamu la Omary kwa kuonesha meno yake machafu. Meno ambayo kuna wakati alilazimika kulitoa lile jino la dhahabu na kubaki kama pengo

"ha! Babu! Kumbe una. pengo?" Moses akacheka kicheko cha kuudhi. kicheko alichokitia na kikohozi kikavu. Kikafanana kabisa na kicheko cha kizee.

Akafanikiwa kumlaghai Omary, akamjibu "Mjukuu wangu una maswali mengi"

"Ah! Babu unajua siku zote nimekaa na wewe sijawahi kukuona ukiwa na pengo"

Moses akijitia kusikilizia maumivu ya kiuno, Omary akaendelea "Nikajua wazee wa kitongoji washakung'oa" wakacheka kwa pamoja Moses akamlaghai Omary, Omary nae akajaa kwenye hila za Moses.

"nina kiu ya kahawa mjukuu wangu"

Omary kwa upendo, akajibu haraka haraka "anha babu! Lipo birika zima siwezi kumaliza lote acha nikumiminie"

Sekunde ya kugeuka, likawa kosa kwa Omary. Moses alitoa ule unga wa sumu ya nyongo ya mamba na kuimwaga ndani ya kikombe cha kahawa aliyokuwa akiinywa Omary. Omary akageuka na kikombe cha kahawa na kumpatia Moses.

Moses akakohoa kiasi huku akimtupia jicho la wizi Omary. Omary akakifakamia kikombe chote na kukifuta pale pale. Moses naye akainywa kahawa yake funda moja na kuingiza mkono wake ndani ya mfuko wa koti kuukuu na kuibuka na picha ambayo alipiga kivuli chake. Picha ambayo aliipiga mara baada ya kumuua Bertha na Pamela. Alikuwa nazo nyingi mara baada ya kujipiga na kutoa nakala nyingi.

Dakika tatu zikawa nyingi, Omary naye alijinyonga tumbo macho yakamtoka kama anayekufa saa yeyote.

"Babu nakufa" Moses akacheka pia na kumwambia kwa hasira "Pole kwa kujua siri yangu unakufa kwa kufuta ushahidi"

Wakati ambao alikuwa anataka kukata roho, Omary alikuwa anataka kumshika Moses kwa hasira akaambulia kuipokonya picha aliyoishika Moses. Picha ya kivuli cheusi. Roho ya mauti ikatwaa roho yake na kumlaza usingizi wa milele Omary.

Ukawa mwisho wa Omary Kibanga.

Moses alipoyakumbuka yote hayo, akabaki akicheka kilevi. Hivyo ndani ya chumba hicho hakukaa sana, dakika chache baadaye ikawa sawa na hakuwa hata na chembe ya kilevi, pombe ikamkatika. Moses akawa katikati ya mitaa ya kigogo mburahati akitafuta nyumba nyingine ya kujificha. Kule akawa amehama na kila kilicho chake.

XXXXX

ITAENDELEA!!!
 
Duh!
Moses umeanza kuua na wasiohusika sasa, huyo omary kakukosea nini,ungehama tu gesti bila kumuua kijana wa watu
 
Duh!
Moses umeanza kuua na wasiohusika sasa, huyo omary kakukosea nini,ungehama tu gesti bila kumuua kijana wa watu


Omary aliokota kitambulisho cha Moses na kukisoma; hivyo alijua kuwa Omary atamuahribia mambo yake. Amemuua ili kupoteza ushahidi.

Twende pamoja tuone huyu jamaa jinsi alivyo hatari kwa kutoa roho za watu.


MIZAMBWA
INANIUMA SANA!!!
 

HADITHI: KIVULI CHEUSI


SEHEMU YA NANE:



TULIPOISHIA.............



Wakati ambao alikuwa anataka kukata roho, Omary alikuwa anataka kumshika Moses kwa hasira akaambulia kuipokonya picha aliyoishika Moses. Picha ya kivuli cheusi. Roho ya mauti ikatwaa roho yake na kumlaza usingizi wa milele Omary.
Ukawa mwisho wa Omary Kibanga.
Moses alipoyakumbuka yote hayo, akabaki akicheka kilevi. Hivyo ndani ya chumba hicho hakukaa sana, dakika chache baadaye ikawa sawa na hakuwa hata na chembe ya kilevi, pombe ikamkatika. Moses akawa katikati ya mitaa ya kigogo mburahati akitafuta nyumba nyingine ya kujificha. Kule akawa amehama na kila kilicho chake.

ENDELEA.............


XXXXX

Maeneo ya kijitonyama ilipo bar ya GQ, Kulikuwako na pilika pilika za kila aina. Mvua iliyokera haikukoma kunyesha na kusababisha mazingira kuwa machafu kama yalivyokuwa. Vidimbwi vya maji machafu vilikanyagwa na magurudumu ya magari, tope zito likawarukia wapita njia waliokosa uvumilivu wa kusubiri mpaka mvua iishe.

Mmoja wa wapita njia hao, alishushwa kutoka kwenye bajaji na kukumbana na dhahama hiyo. Kiatu chake cha kufuta, kikarushiwa tope zito kisha gari likaendelea kutembea taratibu kama mwanamke mwenye maringo ajitingishaye. Mtu huyu alilitazama gari lile huku akimtusi dereva wake. Akamlipa dereva ujira wake na kukimbilia ndani ya pub hiyo.

Saa 4:26 asubuhi, watu walikuwa wengi sana. Aliangaza huku na kule, akaipata nafasi moja iliyo mafichoni karibu na tawi la mti. Akatembea taratibu kwa mwendo ambao si wake. Nani ambaye angefahamu haukuwa wake kama alikuwa amebadilika kiasi hicho? Aliibuka kutoka mafichoni kwake kigogo akiwa amepunguza vitu viwili ambavyo vilikera wasichana. Kwanza kitambi pili unene ulioanza kumnyemelea. Alitumia wiki chache tu za kufanya hivyo.

Alibadilika kiasi kwamba hakuna ambaye angemkumbuka. Alikuwa mwembamba mwenye kifua kipana cha mazoezi na mwili ulioenda hewani. Nywele zake akanyoa tofauti kama alivyozoeleka. Sasa alinyoa kipara kilichong'arishwa kwa mafuta. Ndevu chache za bandia zilizotengeneza O kwenye mdomo wake, hakuna atakayekubali kuwa huyo alikuwa maeneo hayo wiki chache zilizopita. Akajihifadhi ndani ya suti nzito ya gharama. Hakika Moses akapendeza hata akajipenda alipotazama muonekano wake mpya. Suti hiyo ilimbana na kuwa kama mmoja wa wanamitindo jukwaani akinadi aina ya nguo mpya.

Alikaa huku tabasamu likiendelea kung'ang'ania juu ya mdomo wake. Akachomoa kasha la sigara na kuivuta moja mara baada ya kuipachika mdomoni. Huyo ndiye Moses mwenye kila hila za kulipiza kisasi. Alifanya kazi kwa muda mrefu, akitegemea ipo siku angeanza harakati zake huku akitafuna taratibu fedha zake. Utajiri mwingine mkubwa wa fedha, ulitunisha akaunti yake kutoka kwenye kampuni ya baba yake.
Aliendelea kuangaza angaza huku na kule akimtafuta Eva. Akajisema alipokuwa akimtafuta bila mafanikio yeyote.

"Haiwezekani awe amehama bar"

Akaendelea kuvuta taratibu moshi wa baridi uliokuwa ukitoka kwenye sigara. Kama ujuavyo wahudumu wa kwenye bar zetu za Tanzania, zikachukua dakika nyingi mpaka Moses alipofuatwa kusikilizwa.
"Nikusaidie nini kaka?"

Moses si kwamba hakumuona au hakusikia alichoulizwa, ila msichana huyo alikuwa si mgeni kwake. Msichana huyo ndiye alikuwa akimtafuta. Akajiuliza "ina maana amenisahau? Au haujanifahamu?"
Eva akarudia kwa kuudhika "kaka nakusubiri wewe"

Moses akasema "niletee Ndovu ya moto"wakati ambao Eva alikuwa anaondoka, Moses akapata nafasi ya kuzungumza "ningeomba ukirudi unipe dakika zako tano naahidi kukulipa"

Moses hakuwa msanii wa kubadilisha taswira yake pekee hata lafudhi haikutofautiana kabisa na mfaransa. Ungesema labda ni mkazi wa Rwanda au nchi zilizotawaliwa na mfaransa. Lakini ukweli ni kwamba lugha hiyo aliisomea chuoni kutokana na kukuza uhusiano mzuri wa biashara katika kampuni ya baba yake.
Si kifaransa pekee alikiweza kireno, kichina hata kwa kukuandikia.

Huyo ndiye Moses aliyelelewa na kukuwa katika familia ya Mzee Joram Utonga. Mzee ambaye kwa miaka mingi Moses alifahamu kuwa ndiye baba yake mzazi.

Haikuwa hivyo.

Mzee Utonga alilazimika kumlea baada ya mkewe bi Matopi kunyang'anywa uhai na risasi iliyofumua vibaya kichwa chake. Haijulikani ni nani aliyemuua kwa sababu ushahidi ulikosekana. Mzee Utonga alimfahamu muuaji japo hakuwa na uwezo wala sauti ya kumuadabisha muuaji huyo. Moses akaelezwa asili na ukweli wa maisha yake na Utonga mwenyewe alipokuwa akiyapigania maisha yake kutokana na risasi iliyopenya moja kwa moja na kukifumua kifua chake. Damu nyingi zilimuangukia mikononi Moses. Utonga akatamka kwa shida sana

"mali na kila kitu ni vyako urithi huu nimekuandika we.." hakuweza kumalizia neno lake lakini alifanikiwa kueleza kila kitu, akayafunga macho yake kistaarabu. Moses alilia kwa uchungu sana. Alilia kilio ambacho si rahisi kwa mtu wa kawaida kumbembeleza anyamaze. Alilia si kwa sababu Mzee Utonga amefariki, alilia kwa sababu ni yeye aliyesababisha kifo hicho.

Eva akarudi na kinywaji huku furaha ya kumnasa afrikast asubuhi asubuhi ikizidi kutanua papi zake na kuunda kitu kilichoitwa tabasamu. Eva alimkaribisha
"karibu " Moses aliyejitambulisha kwa jina la Frank, hakujibu ahsante zaidi ya kwenda katika hila yake moja kwa moja.

"Unakaa wapi vile?"

"Kigogo mbuyuni" Eva akajibu bila kufahamu furaha gani aliyompa Moses. kazi ya kutafuta windo lake. Moses alimaliza kile alichopanga kukisema.

"Nahitaji kukaa na wewe jioni ya leo katika ile bar ya jirani na kituo cha kwenda mburahati" akatoa noti 5 za shilingi elfu kumi na kusema kwa ushawishi "tafadhali!"
dhiki ikamlaghai Eva akaingia katika mtego wa Moses akakubali bila hiyana. Hata hivyo hakumkumbuka kabisa.

XXXXX

Vannesa alipokea taarifa za mtu aliyekufa huko Keko Magurumbasi. Inspekta Jafari Hiza ndiye alimpa taarifa hizo kwa hali ya kuchanganyikiwa sana. Zilikuwa ni habari za kushitua, lakini zilikuwa ni ambazo zinaweza kumpa mwanga katika uchunguzi wake. Watu walikuwa ni wengi kama ilivyo sehemu yeyote yenye tukio la kushangaza.

Vannesa alipata shida kujipenyeza kati kati yao mpaka alipofika kwa Jafari Hiza. Hakukuwa na salamu, picha yenye kivuli cheusi ikawekwa mkononi mwake.

"muuaji ni mmoja na lile tukio la msichana Bertha kule kijitonyama"

ilikuwa sauti ya Jafari Hiza iliyozibua masikio yake kwa furaha.

"maiti yako wapi?"

Akaongozwa mpaka ilipo maiti ya kijana Omary. "amekufa kistaarabu" vannesa akataka kucheka akaishia kutabasamu. Akaendelea "hajatema povu wala damu? Ni ajabu"

Inpekta Jafari Hiza akaongea kwa kuhuzika "vannesa sipo tayari kufanya kazi na mtu mwenye mzaha kama wewe naomba ujaribu kuwa serious wakati mwingine" alinyamaza kama aliyejaribu kuangalia huku na huko, kisha akasema kwa utaratibu sana ".. unafanya kazi na jeshi la polisi kwa usiri naomba uiheshimu nafasi hii uliyopendelewa" bado Vannesa akacheka kama hakuambiwa kitu. Baadaye Vanessa akaongea kwa hasira "si nafasi ya upendeleo kufanya kazi na jeshi zembe lenye tama ya pesa kam la polisi. Jeshi lililojaa rushwa na uhaini wa hali ya juu. Sipo hapa kwa ajili ya maslahi ya polisi ali kwa ajili ya roho za raia wema naomba unielewe kwa hilo hiza" kisha kaitazama picha ile, haikuwa na tofauti na ile aliyo nayo ofisini kwake.

Akaachana nayo.

Akaungana na watu wawili watatu waliojikusanya kimakundi kujaribu kusikiliza kama angepata lolote la maana, lakini hakuna lililomsaidia. Alipotaka kuondoka, akavutwa na mtu mmoja aliyekuwa akilia sana kuliko hao waliokuwa wakishangaa. Yeye alikuwa ni kijana aliyekuwa akielekea katika utu uzima. Uso wake ulikomaa kiasi cha kukadiria hajapoteza miaka 45 basi angefikisha 50 kabisa. Alionekana kuwa alikuwa na mengi ya kuzungumza kuliko watu walivyolichukulia swala hilo kiuwepesi. Jicho la mtu wa kawaida lingemuona yeye kaguswa tu kama wengine ambao wangekuwa wamefiwa. Ndio maana askari uchwara walimpita lakini Vannesa aliyebarikiwa ushushu, akamfuata kabisa.

"Habari yako kaka?"
huyo aliyekuwa akilia, akalivuta kamasi laini na kufuta chozi lililomdondoka. Akamtazama aliyemsalimia, 'binti mrembo' akajinong'oneza, kabla hajajibu salamu ya Vannesa.

"si nzuri kama uonavyo"

Vannesa akakaa kitako pembeni ya mtu huyo.

"naitwa Vannesa" yule mtu alimtazama Vannesa kwa kumsahili juu mpaka chini, kwa macho yaliyolowa machozi. "mimi si polisi wala mwandishi wa habari" vannesa alijaribu kujitetea kumtoa hofu "unajua hiki kifo cha Kibanga kimenishangaza sana. Lakini hakuna la maana nililopata zaidi ya kusikia kuwa alichukua msichana wa mtu?" alitia hila zake ili apate chochote kutoka kwa huyo mtu.

Yeye alijulikana kwa jina la Mfaume, mfagizi na aliyehusika kusafisha vyumba vya nyumba hiyo. Mfaume akahamaki kwa hasira "Waache unafki" kikohozi laini kikampitia na kamasi alilivuta, kisha akaendelea. "Omary alikuwa hana tabia za wasichana hata kidogo. Nimekaa naye miaka 10 katika hii biashara tangu keko machungwa mpaka hapa. Mpaka niliwahi kuhisi huyu kijana jogoo hapandi mtungi ila kijana wa watu yupo safi" kilio kikaanza upya. Hakuna lolote aliloongea Mfaume, la kumjengea picha Vannesa katika kuanza upelelezi wake.

Vanessa akaendelea kudadisi."Ina maana ameuwawa na mwendawazimu gani" akajitia kuweka hasira katika sauti yake "Hata amuue kijana mpole kama Omary?"

Mfaume akavuta kamasi, kisha akamuinamia Vannesa. "sikiliza dada yangu hawa polisi watahangaika tu, lakini muuaji amekwisha ondoka na sidhani kama ni rahisi kumpata."

Mapigo ya moyo wa Vannesa yalimuenda kasi kwa furaha, kupata lile alilotarajia. Akatega ufahamu wake wote aweze kupata picha halisi.

Akahoji "ina maana muuaji unamfahamu?"
Mfaume akatingisha kichwa, huku akitabasamu kuonesha alimaanisha alichozungumza.

XXXXX

ITAENDELEA JUMATATU, NAWATAKIA WEEK END NJEMA.............
 
HADITHI: KIVULI CHEUSI


SEHEMU YA TISA:



TULIPOISHIA.............

Vanessa akaendelea kudadisi."Ina maana ameuwawa na mwendawazimu gani" akajitia kuweka hasira katika sauti yake "Hata amuue kijana mpole kama Omary?"

Mfaume akavuta kamasi, kisha akamuinamia Vannesa. "sikiliza dada yangu hawa polisi watahangaika tu, lakini muuaji amekwisha ondoka na sidhani kama ni rahisi kumpata."

Mapigo ya moyo wa Vannesa yalimuenda kasi kwa furaha, kupata lile alilotarajia. Akatega ufahamu wake wote aweze kupata picha halisi.

Akahoji "ina maana muuaji unamfahamu?"
Mfaume akatingisha kichwa, huku akitabasamu kuonesha alimaanisha alichozungumza.

ENDELEA..................


Jirani na kituo cha daladala ziendazo kigogo mburahati na ruhangwa, kulisimama taksi moja aina ya chaser mayai, yenye rangi ya maziwa. Vioo vilivyopandishwa mpaka juu , viliashiria kuwa kipupwe cha kutosha kilipuliza ndani ya gari hilo. Yule ambaye alikuwa kama mteja kwenye gari hiyo, alishusha mguu wa kwanza, hatimaye wa pili mara baada ya kumlipa ujira wake dereva huyu mzee aliyechoka.

Gari lilipoondoka, mteja alionekana kuwa nadhifu kuliko wakazi wa kitongoji hicho. Yeye alivaa suruali iliyokolea upanga kwa moto wa pasi shati iliyobana kifua chake na tai ya teksido.
Alikuwa Moses, nyuma ya miwani ya transparent, alipendeza. Kila jicho lilikuwa upande wake. Kabla hajavuka, Moses alishikwa shati. Alipogeuka kumtazama aliyemshika, alikuwa Eva.

"Frank!?"

Moses alishitushwa sana kumuona Eva akiwa amewahi kiasi hicho. Mshituko mwingine uliongezwa na jina aliloitwa. Nadhani alikwishasahau hata kuwa ni yeye ndiye alimdanganya jina hilo. Baada ya sekunde chache alikumbuka hila zake. Alikumbuka kisasi na roho ya mauaji ikamuingia na kuuchukulia uzuri wa Eva kama kinyago. Tabasamu laini lile linalowachanganya wengi, likamponyoka Moses na kumlaghai Eva.

"sikutegemea kama ungewahi kiasi hiki."

Akamshika mkono Eva, "twende tena ni heri umewahi" Moses alisimamisha taksi nyingine na kumuongoza Eva ndani. Eva alishitushwa, haikua hivyo kama walivyoahidiana asubuhi pale GQ.

Akauliza "mbona umebadilisha sehemu?"

ilimchukua muda Moses kujibu. Lakini lengo na dhumuni hakuhitaji kusumbua maficho yake mapya kwa sasa. Aliwaza endapo angempeleka mbali, huko ndipo ungefanyika msako wa muuaji anayeacha kivuli cheusi.

"Tupeleke kinondoii"

Dereva aligeuza gari na kuelekea alipoagizwa. Moses alikumbuka njia ya kuelekea katika apartment moja nzuri sana maeneo ya Masaki. Mmiliki wake alikuwa ni mholanzi fulani ambaye alimfahamu vizuri. Alifahamu michezo yake michafu aliyoicheza na kumfanya yeye kumiliki apartment kama hizo kumi pembezoni mwa ufukwe wa bahari. Hivyo alikuwa na hakika kwa lolote baya lingetokea, ingebidi mholanzi huyu kumfichia siri hiyo nzito.

Wakaegesha pembezoni mwa jumba la kifahari. Jumba lililomezwa na bustani iliyotota ukijani uliovutia macho. Alimlipa dereva elfu 10, huyu alikuwa ni wa pili alimtoa pale kinondoni a kumfikisha Masaki ilipo apartment hiyo.

Mchezo wake ulikuwa ni ule ule kubadilisha madereva, kupoteza ushahidi. Urefu wa njia na foleni za hapa na pale, ziliwatosha Eva na Moses kuwa wapenzi. Eva akahoji kwa bumbuwazi

"sasa mpenzi" huku akiendelea kushangaa kila kona ya bustani na wafanyakazi waliosimama wakiwatazama wageni hao.

Eva akaendelea "kama una nyumba nzuri kiasi hiki? Kwa nini usiwe na gari ya kutembelea?"

Si kwamba hiyo ilikuwa ni nyumba nzuri pekee kwa Moses. Alikuwa nazo nne zilizobebana na kuitwa ghorofa. Moja ya kijitonyama nyingine upanga na mbili za bunju ambayo moja ndiyo anayoipenda zaidi. Alikuwa na magari ya kifahari ya kutosha.

Hivyo alitabasamu tu na kumuona Eva ni mmoja kati ya wasichana waliokosa elimu ya kutosha kutokana na kushindwa kutambua tofauti ya nyumba na apartment ya kukodisha. Walikaribishwa kwa bashasha kutoka kwa wahudumu waliohakikisha usafi wa nyumba hiyo ukiwa ni wa hadhi ya kimataifa. Moses alivaa pama kubwa na kuwa kama mtalii huku akiwa amemshikilia Eva kiuno chake. Hakika wakaonekana kuwa wapenzi wa kudumu wa muda mrefu.

Wakajitoma ndani.

Huko walikaribishwa na kipupwe cha kiyoyozi kilichomfanya Eva aone hakika maisha ndio hayo. Moses alifahamu kila kona ya nyumba hiyo, hakuwa mgeni kufungua hiki na kile. Akaitoa chupa ya mvinyo wa dodoma.

Eva akaropoka "Anha! Dompo!"akiwa ameishika chupa yake "Naipenda sana"
waliinywa hiyo kisha chupa ya pili wakaimaliza na ya tatu. Eva akawa hoi kwa kilevi aliposhikwa kidogo na Moses, akaita jina la Frank kwa huba.

Moses akambeba na kuingia naye chumbani. Huko kitu kilichofanyika, hakikufaa kutazama. Kichwa kilinyofolewa, mikono na miguu vikatenganishwa na kiwiliwili.

Alikichukua kichwa hicho na kukihifadhi ndani ya friji la chumbani hapo. Mkononi akamuwekea picha aliyotembea nayo siku hiyo, ilikuwa ni picha ya kivuli cheusi. Moses akatokomea baada ya kukamilisha zoezi lake.

Alijua sasa kilichobaki ni mke wa Raymond. Mwanamke aliyesababisha kifo cha mama yake, Bi furahiya.

"Lazima nimuanze yeye ile huyu mshenzi ajue nipo siriazi"

Moses hakufahamu kuwa hakumaliza kufuta kumbukumbu ya taswira yake ya uzee katika kichwa cha Mfaume.

Akacheka sana kwa furaha alipokuwa akitazama taarifa ya habari akiwa ndani ya bar yenye mazingira machafu katika guest aliyolala huko kigogo mburahati.

Taarifa iliyokuwa ikitangaza tukio la kuuwawa kwa kwa muhudumu wa nyumba ya kulala wageni na muuwaji akihusishwa katika matukio ya mauaji ya wasichana wawili.

XXXXX


ITAENDELEA......................
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…