Hadithi: Bruno the Fisherman

Hadithi: Bruno the Fisherman

BRUNO THA FISHERMAN

Mtunzi.Nyemo

Episode 10


Mzee Todd alikuwa ndani ya ndege akipelekwa nchini Marekani. Taarifa za kukamatwa kwake zilikuwa ni za kimyakimya na hakutakiwa mtu yeyote afahamu kama mwanaume huyo alikuwa amekamatwa kwa kuogopa kuvamiwa na wauzaji wa madawa ya kulevya.
Humo ndani ya ndege, hakuwa na raha hata kidogo, alijua kwamba kila kitu kilichokuwa kimefanyika kilikuwa ni mchezo ambao ulichezwa na Maxwell kwa ajili ya kumpoteza.
Hakuona kama angeweza kutoka katika kesi hiyo kubwa. Mbele yake kulikuwa na ugumu lakini watu pekee ambao aliamini kwamba wangeweza kumsaidia kutoa ushahidi walikuwa wawili tu, Innocent na Bruno.
Alikuwa akisafirishwa kuelekea nchini Marekani huku matumaini yake yakiwa kwa watu hao wawili tu. Hakuzungumza kitu chochote kile, alikuwa kimya na kichwa chake kilikuwa kikifikiria ni kwa jinsi gani angeweza kupambana na kesi hiyo ambayo dunia nzima iliamini kwamba kweli madawa ya kulevya yalikutwa chumbani kwake na kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba alihusika katika kuiteketeza familia yake.
Baada ya saa zaidi ya ishirini, hatimaye ndege ikaingia nchini Marekani. Hapo, alikuwa akisubiriwa na maofisa wa CIA ambao walimchukua, wakampakiza ndani ya gari na kuondoka naye.
Walipoona kwamba amefika salama ndiyo taarifa zikaanza kutolewa kwa waandishi wa habari ambao wote hawakuamini kile walichokuwa wamekisikia.
Mwanaume huyo aliwasumbua kwa miezi sita, hawakuwa wamempata japokuwa walimtafuta kila kona, kukamatwa kwake ikawa shangwe, watu kwenye mitandao ya kijamii wakaandika sana kuhusu mwanaume huyo na kila mmoja alikuwa akimuhukumu kwa nafasi yake kama mtuhumiwa ambaye alitakiwa kunyongwa mpaka kufa.
Kwenye vyombo vya habari, ni picha zake tu ndizo zilikuwa zikitawala. Wamarekani walijua kucheza na akili za watu, walijisifia kwamba hakukuwa na mtu yeyote ambaye angethubutu kuichezea nchi hiyo na kutafutwa asipatikane.
Walihitaji watu wao warudishe matumaini kwao kwa mara nyingine kwani kulikuwa na watu wengi ambao walikuwa wakitafutwa na maofisa wa CIA lakini cha ajabu kabisa hawakuwa wakipatikana.
Kitendo cha kumkamata mzee Todd kikawahakikishia kwamba wangesifiwa kila kona kwani wangeonekana mashujaa ambao hawakulala usiku mzima kwa ajili ya mtu huyo.
Mzee Todd akawekwa ndani ya chumba cha mahojiano na kuanza kuulizwa maswali kadhaa. Hakufumbua mdomo wake kujibu swali lolote lile, kila kitu alichoulizwa, aliwaambia kwamba asingeweza kuongea lolote lile mpaka mwanasheria wake kuwa mahali hapo.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, haraka sana mwanasheria wake, Harry Donny akapigiwa simu na ndani ya dakika chache alikuwa ndani ya chumba hicho na mzee Todd kuanza kujibu kila swali alilokuwa akiulizwa.
Aliulizwa zaidi ya maswali hamsini ambayo yote aliyajibu kwa ufasaha na hivyo kesi hiyo kutakiwa kufika mahakamani haraka sana.
Wakati huo kila kona duniani walikuwa wakimzungumzia mzee huyo, kesi yake hiyo nzito ilizua mambo makubwa mno, kila kona, watu wote walitaka kuisikiliza na kuona hatima ya mzee huyo ingekuwa nini.
Asilimia kubwa ya watu walitaka kushuhudia mzee huyo akifungwa kifungo cha miaka mingi gerezani kwani kwa miaka hiyo kulikuwa na idadi kubwa ya vijana waliokuwa wakipotea kutokana na matumizi mabaya ya madawa ya kulevya.
Waandishi wa habari walikuwa wakimiminika mahali hapo huku wakiwa na hamu ya kutaka kuzungumza na mzee huyo au hata kupata picha zake kwani picha nyingi ambazo zilikuwa zikitumika kipindi hicho zilikuwa ni picha za zamani tu.
Hakukuwa na mtu aliyepata nafasi hiyo, waliambiwa kwamba suala la picha walitakiwa kusubiri mpaka siku ambayo angepandishwa mahakamani.
Mwanasheria wake ambaye ndiye huyohuyo angekuwa wakili wake akaanza kumuuliza maswali mengi juu ya kilichokuwa kimetokea. Hakutaka kumficha, alimwambia ukweli kuhusu kila kitu kwamba hakuwa ameweka madawa ya kulevya ndani ya nyumba yake bali kulikuwa na mwanaume aliyeitwa Maxwell ambaye ndiye alikuwa nyuma ya mchezo wote.
Yeye ndiye aliyeratibu kila kitu na hata alipokwenda Afrika, yeye ndiye aliyepanga mipango ya kuuawa lakini ilishindikana baada ya kukutana na kijana aliyejitambulisha kwa jina la Bruno.
“Alisuka mipnago ya kunimaliza, nikasaidiwa kwani nilichukuliwa kwenye meli yake na kupelekwa sehemu kwa lengo la kuuawa ila tukatoroka bandarini,” alisema mzee Todd.
“Na huyo kijana kuna uwezekano wa kupatikana?”
“Ndiyo! Kuna uwezekano, yeye atatoa ushahidi wa kila kitu kilichotokea,” alisema mzee Todd huku akiwa na uhakika wa kumpata Bruno.
“Sawa. Haina shida!”
Walizungumza mambo mengi na baada ya kukamilisha kila kitu, tarehe ya mahakama ikapangwa tayari kwa kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Mzee Todd alikuwa mtu mwenye huzuni tu, kila alipokuwa selo kichwa chake kilikuwa kikiifikiria familia yake tu, hakuamini kama aliipoteza kwa tamaa za mwanaume mmoja tu aliyetaka afutike ndani ya dunia hii.
Alihuzunika mno lakini alijiahidi kwamba kamwe asingelipa kisasi kwa kuwa aliamini kwamba kulikuwa na Mungu ambaye alisema kwenye maandiko yake kwamba visasi vyote vilikuwa juu yake.
Siku ziliendelea kukatika, baada ya siku kadhaa, hatimaye siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ikawadia. Zaidi ya watu elfu tatu walikusanyika katika viunga vya mahakama kwa lengo la kusikiliza kesi hiyo. Hapo, kulikuwa na waandishi wa habari ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
Mashirika makubwa ya habari duniani, CNN, BBC, Sky News na mengi yalikuwa bize kuonyesha moja kwa moja kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika viunga vya mahakama huku wakijaribu kufanya mahojiano na baadhi ya watu waliokuwa mahali hapo.
“Namkumbuka mpenzi wangu, Jericho, alikuwa mtu mwema kabisa lakini baada ya kuanza kutumia madawa ya kulevya, nikampoteza, moyo wangu uliniuma sana, ninapomuona huyo mzee, ninatamani hata nimuue kwa mkono wangu,” alisema msichana mmoja huku akionekana kuwa na hasira mno.
“Nilimpoteza kijana wangu baada ya kuingia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya. Nilimpa kila kitu, hakutaka kusoma, alichanganyikiwa kabisa na madawa. Halafu leo mniambie kwamba huyu mzee aachiwe huru, nadhani nitamuua hata mtaani,” alisema mwanaume mmoja, kwa kumwangalia tu isingekuwa vigumu kuamini kwamba angefanya kile alichokuwa akikisema.
Kila mtu aliyekuwa akihojiwa alimshutumu mzee huyo moja kwa moja, hakukuwa na mtu aliyetaka kumuona mwanaume huyo akiachiwa huru, kila mmoja alitamani kuona akihukumiwa jela kwa kosa alilokuwa amelifanya.
Baada ya saa moja, gari moja lililokuwa likiongozwa na baadhi ya magari ya CIA lilikuwa likiingia mahakamani hapo. Haraka sana waandishi wa habari wakasogea kule lilipokuwa na kuanza kulipiga picha.
Kila mtu aliamini kwamba huyo alikuwa mzee Todd, walipiga picha nyingi mpaka mlango ulipofunguliwa na mwanaume huyo kuteremshwa huku akiwa na pingu mikononi mwake.
Hakuuficha uso wake, alikuwa na uhakika wa kushinda kesi hiyo, alikuwa akiangalia huku na kule, hakutabasamu, alikuwa kwenye hali ya kawaida, alizungukwa na maofisa wa CIA mpaka alipoingizwa ndani ya jengo la mahakama.
Humo ndani, kulikuwa na watu zaidi ya mia saba waliokuwa wamekaa na wengine kusimama, kila mmoja alitaka kujua kile kilichokuwa kikiendelea, siku hiyo ilikuwa ni ya kusikiliza kesi lakini hakukuwa na mtu yeyote yule aliyetaka kukosa kesi hiyo.
Baada ya dakika kadhaa, mzee Todd akapelekwa kizimbani na hakimu kuingia. Kwa heshima kila mtu akasimama, alipokaa tu kwenye kiti chake, akagonga kinyundo na watu wote kukaa.
Kesi ikaanza mara moja. Siku hiyo haikuwa ya kusikiliza mashahidi, haikuwa siku ya kusikilizwa utetezi wake, ilikuwa ni siku ya kusomewa mashtaka, makosa aliyoyafanya na baada ya hapo kesi kuahirishwa mpaka baada ya wiki moja na nusu.
“Ninaiahirisha kesi hii mpaka tarehe 10/08,” alisema hakimu na kugonga kinyundo chake, akasimama na kuondoka mahali hapo.
Watu wakatoka nje lakini hawakutaka kuondoka mahakamani hapo, walitaka kumuona mzee Todd akiondolewa na kupandishwa ndani ya gari lake.
Polisi mmoja akamfuata pale kizimbani, akamchukua na kuanza kuelekea naye nje huku akiwa amemfunga pingu. Kila kona mahali hapo kulikuwa na ulinzi mkali, walijua kwamba mwanaume huyo alikuwa na watu wengi hatari ambao wangeweza kufanya kila liwezekanalo mpaka kuhakikisha wanamtoa mahali hapo.
Walichokuwa wakikifikiria kilikuwa tofauti kabisa, mzee Todd hakuwa na kundi lolote lile, alikuwa yeye kama yeye na hakukuwa na kitu ambacho aliamini kama mashahidi ambao wangeeleza kila kitu kilichokuwa kimetokea na hivyo kushinda kesi hiyo.
Alipotolewa nje, watu wakachukua simu zao na kuanza kumpiga picha, waandishi wa habari walikuwa wakihangaika, hawakutulia, kila mmoja alihakikisha anapata picha ambayo ingeyafanya magazeti yao na tovuti zao kutembelewa na watu wengi.
Mzee huyo hakuuficha uso wake kama watu wengine, hakuona kama alikuwa na hatia na muda wote alikuwa kimya tu, akachukuliwa na kupakizwa ndani ya gari na kuanza kuondolewa mahali hapo.
Wakati akiondolewa, wakili wake, Harry alikuwa akimwangalia, moyo wake ulimuuma mno, alimuonea huruma mteja wake lakini alikuwa na uhakika kwamba hao mashahidi ambao alimtajia basi wangeweza kumsaidia kutoka katika mikono ya kifungo kilichokuwa kikimkabiri.
Baada ya gari lile kuondoka, akalifuata gari lake na kuondoka mahali hapo. Wakati gari likiwa limefika katika Barabara ya Brooklyn, akaangalia kwenye kioo, kwa nyuma kulikuwa na gari lililokuwa likimfuata.
Alikuwa na wasiwasi nalo kwani kila alipokuwa akijaribu kwenda huku na kule, gari lile lilikuwa likimfuata kitu kilichomfanya kuhisi kuwa watu waliokuwa humo walikuwa wabaya ambao wangeweza kumfanya lolote lile.
Akaanza kuliendesha gari kwa mwendo wa kasi, hilo halikuweza kumsaidia kwani gari lake halikuwa na kasi kubwa kama gari lililokuwa likimfukuza kwa nyuma.
Aliendesha lakini hakuweza kuliacha, gari hilo likamfikia na kuanza kuendesha ubavuni mwake. Mwanaume mmoja akatokeza na kumnyooshea bastola na kumtaka asimamishe gari vinginevyo angeanza kumshambulia kwa risasi.
Harry akaogopa, hakutaka kuona akifa, mule ndani ya gari alipokuwa akaanza kutetemeka kwa hofu, akaanza kupunguza mwendo na kusimama.
Gari lile likasimama, wanaume wawili wakateremka na kumfuata huku wakiwa na bastola mikononi mwao, baada ya kulifikia, wakafungua mlango na kumteremsha na kumpeleka ndani ya gari lao.
“Don’t dare to open your fucking mouth,” (usithubutu kufungua wako) alisema mwanaume mmoja huku akimgongagonga na bastola kichwani. Harry akanyamaza, kijasho chembamba kikaanza kumtoka na kuhisi kwamba huo ungekuwa mwisho wake.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho
 
BRUNO THE FISHERMAN

Mtunzi.Nyemo

Episode 11


Maxwell alikuwa nyumbani kwake, moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, kitendo cha vijana wake kushindwa kumteka mzee Todd kilimuhuzunisha kupita kawaida.
Alichanganyikiwa, alijua hatari ambayo ilikuwa mbele yake, alijua kabisa kwamba kama asingefanya kila liwezekanalo kuhakikisha mwanaume huyo anatekwa basi mbele yake kungekuwa na hatari kubwa mno.
Hakutaka kutulia, kila wakati alikuwa akiwasiliana na vijana wake lakini walichokuwa wakimwambia ni kwamba hawakuwa wamefanikiwa kumpata mwanaume huyo.
Hakutaka kuona akikubali, bado aliendelea kuwasisitiza vijana wake kumpata mzee Todd lakini mpaka siku hiyo ambayo alikuwa sebuleni kwake mwanaume huyo hakuwa amekamatwa.
Baada ya dakika kadhaa kukaa sebuleni, macho yake yakatua kwenye taarifa ambayo ilimshtua sana. Kupitia kituco cha televisheni cha CNN kulikuwa na habari ambayo iliyokuwa imefika hivi punde kwamba mzee Todd alikuwa amekamatwa nchini Kenya na muda huo alikuwa amefikishwa makao makuu ya CIA kwa ajili ya kujibu kesi yake iliyokuwa ikimkabiri.
“Amekamatwa! Mungu wangu!” alisema Maxwell huku akisimama na kuangalia vizuri televisheni ile.
Hakuamini alichokuwa akikiangalia, hapohapo akampigia simu mmoja wa vijana wake aliyeitwa Dragon na kumwambia kuhusu taarifa ile kwamba mzee Todd alikuwa amekamatwa hivyo walitakiwa kufanya kila kitu kujua namna kesi hiyo ilivyokuwa ikiendeshwa.
Hilo halikuwa tatizo, vijana wakaanza kufanya kazi yao kufuatilia, walihitaji kujua mambo mengi kuhusu huyo wakili ambaye angemsimamia, walijua kuwa kama kulikuwa na kesi ilikuwa ni lazima kuwa na mashahidi wa kumtetea mzee huyo.
Hao ndiyo waliotaka kuwajua, walitaka kuhakikisha wanawatafuta mashahidi wote na kuwamaliza ili mzee Todd ashindwe kesi hiyo iliyoonekana kuwa ngumu kwa upande wake.
Siku ambayo kesi ilikuwa ikisikilizwa, walikuwa mahakamani hapo, lengo lao lilikuwa ni kuhakikisha wakili anakamatwa na kupelekwa sehemu kwa ajili ya kuulizwa maswali kadhaa.
Hilo likafanyika na muda huo walikuwa na Harry ndani ya gari lao. Walimwambia anyamaze kwani vinginevyo wangeweza kummaliza.
Walikuwa wakizunguka naye tu huku wakimuuliza baadhi ya maswali kuhusu kesi hiyo na hata mashahidi ambao walitakiwa kwenda mahakamani. Harry hakutaka kuwaambia ukweli, alichokisema ni kwamba bado kesi ilikuwa mahakamani na hata mashahidi hawakuwa wamejulikana hivyo walitakiwa kusubiri.
“Unatudanganya! Hebu kifumue kichwa chake,” alisema mwanaume mmoja maneno yaliyomfanya Harry kuogopa.
“Naomba msiniue! Naomba msiniue, mimi ndugu yenu,” alisema Harry huku akianza kulengwa na machozi.
“Muue bwana, anatuchelewesha,” alisema jamaa huyo na mwenzake kukoki bunduki.
“Subiri nawaambieni ukweli,” alisema Harry.
“Tatizo unahisi kwamba tumekuja hapa kucheza na wewe. Sikiliza mshikaji wetu, tumekuja kufanya kazi, ukituzingua, tunakuzingua,” alisema jamaa aliyeshika bastola.
Harry hakutaka kunyamaza, ilikuwa ni lazima awaambie vijana wale kila kitu kilichokuwa kimetokea hasa upande wa mashahidi ambao walitakiwa kwenda mahakamani kutoa ushahidi wao kuhusu kile kilichokuwa kimetokea.
Mtu wa kwanza aliyemtaja alikuwa Innocent, huyo walimfahamu, kummaliza halikuwa jambo gumu hata kidogo na mtu wa pili aliyemtaja aliiitwa Bruno ambaye waliambiwa kuwa alikuwa nchini Kenya.
Walipoambiwa hivyo hawakutaka kumshikilia Harry, wakamuacha na kumuonya kwamba hakutakiwa kumwambia mtu yeyote yule kuhusu kile kilichokuwa kimetokea.
Wakampigia simu Maxwell na kumwambia kila kitu kwamba katika kesi ile kulikuwa na watu wawili ambao kama asingehakikisha wanamalizwa basi angeweza kufungwa.
Akatajiwa majina ya watu hao, alimfahamu Innocent, kwake, huyo hakumsumbua ila mtu ambaye alikisumbua kichwa chake alikuwa Bruno, mwanaume ambaye hakuwahi kumuona na hakujua alifananaje.
“Alisema anaishi Kenya?” aliuliza.
“Ndiyo!”
“Sehemu gani?”
“Mombasa!” alijibu.
Hilo halikuwa tatizo, kwa sababu walijua mahali pa kumpata walihakikisha wanafanya kila liwezekanalo kabla ya wiki mbili na kumuua.
Alichokifanya ni kuwalipa vijana hao kiasi cha dola laki mbili na kuwatuma kwenda nchini Kenya huku wakijifanya watalii na wengine kutakiwa kumuua Innocent hapohapo Marekani.
Baada ya siku mbili, vijana watatu, Kelly, Adson na Tim walikuwa ndani ya ndege wakielekea nchini Kenya. Walipewa maelezo yote juu ya kile walichotakiwa kufanya, kwa Mombasa, hawakujua eneo hilo lilikuwa na ukubwa gani lakini walikuwa na uhakika wa kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku chache kabla ya kurudi nchini Marekani.
***
Kama kudharaulika, Bruno alidharaulika sana, alikejeliwa kila kona, hakupendwa kutokana na umasikini uliokuwa umemtafuna.
Kipindi hicho kila kitu kilionekana kubadilika, hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba mwanaume aliyekuwa ameagiza boti mpya kutoka jijini Nairobi alikuwa Bruno yule ambaye alionekana kuwa si lolote lile.
Mzee Juma alijisikia aibu moyoni mwake, hapokuwa Bruno alimuonyeshea kutokujali lakini hakuwa na raha hata kidogo.
Alihisi kila mtu alikuwa akimcheka baada ya kumpuuza kijana huyo na mwisho wa siku kutaka kumuozesha binti yake kwa mtu mwingine na wakati Bruno alikuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati.
Alizipokea boti zile, machozi yalikuwa yakimtoka, hakuweza kuvumilia, hapohapo akaanza kububujikwa na machozi, hakukuwa na kitu kilichomuuma kama hicho, akaanza kumuomba msamaha Bruno ambaye bila kupepesa macho alimwambia kwamba alimsamehe.
Jina la Bruno likaanza kukua, kila mtu aliyesikia kile kilichotokea alitaka kumshuhudia Bruno mwenyewe, walitaka kuona alifananaje kwani taarifa walizozisikia ni kwamba alikuwa kijana mdogo aliyekuwa na utajiri wa kutisha.
Hakutaka kuishia hapo, alichokifanya ni kuanza kujenga nyumba kubwa hapo kijijini na kuwawekea bomba maji ya kunywa na kufulia, akawa na mipango ya kununua magari lakini pia akanunua jumba kubwa jijini Nairobi na kuanzisha biashara zake nyingi.
Maisha yake yalionekana kama kulala masikini na kuamka tajiri. Hawakujua sababu iliyomfanya mzee Todd kumpa pesa nyingi Bruno ambaye alikuwa akiziendesha kwa kufanya biashara nyingi na kubwa.
Ndani ya wiki moja tu tayari jina lake likawa kubwa na wengi kutabiri kwamba angekuwa bilionea mkubwa sana hapo baadaye.
Kwa kuwa alikuwa masikini na alijua jinsi masikini walivyokuwa na maumivu mioyoni mwao hasa katika kupata matibabu, akaanzisha taasisi yake ya kusaidia wagonjwa wasiojiweza kujilipia aliyoiita Bruno & Shakira Foundation.
Aliwekeza kiasi kikubwa cha pesa, akaanza kuwaita madaktari kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa waliokuwa wakihangaika kupata matibabu.
Alitumia kiasi kikubwa cha pesa lakini hakujali, kwake, moyo wake ulijitolea kumsaidia kila mtu. Hilo likamfanya kujulikana nchini Kenya, watu wakatamani kumuona kwani kwa masikini wasiokuwa na uwezo alionekana kama Mungu.
Umaarufu wake ukawa mkubwa, kwa jinsi alivyokuwa na pesa, alivyosaidia watu kwa kipindi kifupi cha wiki moja na nusu tayari kila kona alikuwa akisikika yeye tu.
Magazeti yakamuandika yeye na mkewe, jinsi walivyokuwa wameyabadilisha maisha ya watu wengi kwa kipindi kifupi. Hawakuringa, hawakujiona, kwao, ni upendo wa dhati tu ndiyo uliokuwa umetawala mioyoni mwao.
Bruno hakuacha kufuatilia kesi ya mzee Todd, tangu siku ya kwanza ilipoanza kusikilizwa, alipokuwa akihojiwa na hata mashahidi walipokuwa wakihitajika alikuwa akifuatilia kila kitu.
Alisahau kabisa kama alitakiwa kuwa shahidi katika kesi hiyo hivyo kuendelea na maisha yake huku akimuomba Mungu ampiganie mzee huyo ili ashinde kesi ile.
Baada ya wiki moja, akapokea ugeni kutoka nchini Marekani. Watu hao walikuwa madaktari kutoka katika Hospitali ya St. Andrew iliyokuwa jijini New York na lengo lao kubwa la kufika nchini Kenya ni kusaidia watu waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa mbalimbali.
Watu hao walikuwa ni Tim na wenzake. Walipofika Nairobi, kitu cha kwanza kilikuwa ni kulisikia sana jina la Bruno. Hawakujua kama mwanaume huyo ndiye waliyekuwa wakimtaka au alikuwa mwingine.
Walifuatilia na kugundua kwamba alikuwa mwenyewe kwani alikuwa akiishi katika Kijiji cha Guolduvai kilichokuwa Mombasa.
Mbali na kulisikia jina lake, wakapewa taarifa nyingi kuhusu mwanaume huyo, taasisi aliyokuwa ameifungua ambayo ilionekana kuwa gumzo kila kona.
Hilo likawasadia na kuona kwamba kama wangejifanya madaktari kutoka nchini Marekani basi ingesaidia sana kukutana na mwanaume huyo na kutimisha lengo lao.
Wakasafiri kutoka Nairobi mpaka Mombasa. Walipofika huko, haraka sana wakamuulizia mwanaume huyo, kumpata halikuwa tatizo hata kidogo, wakaelekezwa na kuanza kumfuatilia kwa ukaribu.
Siku iliyofuata, walikuwa mbele yake. Bruno alipowaona, alifurahia kwa sababu aliamini kwamba watu hao wangemsaidia mno kuwatibu wagonjwa wengine.
Akawakaribisha nyumbani kwake, akawatambulisha kwa mpenzi wake, kwa kifupi akatokea kuwaamini kupita kawaida.
Walizungumza mambo mengi kuhusu matibabu, walimwambia kuhusu ujio wao nchini Kenya, hawakuwa wamefika kwa kuwasaidia watu bali walifika kwa ajili ya kutembelea nchi hiyo kama watalii ila kwa sababu walisikia kuhusu taasisi yake basi nao wakaona kulikuwa na umuhimu wa kutoa msaada ili wachangie baraka.
“Hakika ni Mungu!” alisema Bruno huku akionekana kuwa na furaha kupita kawaida, hakujua kama watu hao walitumwa nchini Kenya kwa lengo la kummaliza kama maagizo kutoka kwa Maxwell..

Je, nini kitaendelea?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom