Hadithi: Bruno the Fisherman

Hadithi: Bruno the Fisherman

BRUNO THE FISHERMA

Mtunzi.Nyemo

Episode 9


“Bruno….Bruno…Bruno….” zilisikika kelele za watu kutoka mitaani, wanawake waliokuwa wakichota maji kisimani wakaacha na kuanza kuelekea kule kelele zile zilipokuwa zimesikika. Kila mtu alikuwa na shauku ya kumuona huyo Bruno aliyekuwa akishangiliwa na watu waliokuwa mitaani.
Watu waliokuwa ndani ya nyumba zao wakatoka na kwenda kushuhudia kile walichokuwa wakikisikia, waliokuwa pembezoni mwa bahari nao wakaelekea kule kujionea kwa macho yao. Kila kona gumzo lilikuwa ni Bruno, alisababisha kasheshe mtaani na ndiyo maana watu walipolisikia jina lake wakatoka kwenda kujionea kwa macho yake.
Bruno alisimama nje ya teksi huku akiwa na mzee Todd, alikuwa akikiangalia kijiji hicho, uso wake ulikuwa na tabasamu pana, hakuamini kama alirudi kijijini humo baada ya kupotea kwa miezi kadhaa. Alikuwa amekonda, hakuwa kama alivyoondoka kipindi cha nyuma.
Watu walimsogelea na kumwangalia, walitaka kuamini kama alikuwa yeye au mtu mwingine. Wengine wakamsogelea na kumshika, walitaka kuona kama alikuwa mtu halisi au mzimu.
Pembeni yake alikuwepo mzee Todd, watu hawakutaka kufahamu kuhusu mzee huyo wa Kizungu, walitaka kufahamu kuhusu Bruno, ilikuwaje mpaka awe hai kipindi hicho?
Wakati watu walipokuwa wakipiga kelele za Bruno, Sharifa alikuwa nyumbani kwao akiendelea na kazi zake kama kawaida. Alikuwa mnyonge, hiyo haikuwa siku hiyo tu, hayo yalikuwa maisha yake ya kila siku.
Akiwa anaosha vyombo akasikia kelele nje huku jina la mpenzi wake likisikika. Alichanganyikiwa, vyombo havikuosheka tena, akasimama, akavalia khanga yake na kutoka ndani huku akikimbia.
Alichanganyikiwa, alitaka kuona kile alichokuwa amekisikia, alikimbia mpaka mahali kulipokuwa na teksi, alipoanga vizuri, alimuona mpenzi wake akiwa amesimama na mwanaume mmoja wa Kizungu, hakutaka kubaki alipokuwa, akaanza kumfuata kwa kumkimbilia, alipomkaribia, akamrukia, wakaanguka chini huku watu wengine wakibaki wakiwa wamepigwa na butwaa.
“Bruno! Bruno...” aliita Sharifa huku machozi ya furaha yakianza kutoka.
Kwake ilikuwa ni vigumu kuamini moja kwa moja kwamba mtu aliyekuwa amemkimbilia na kudondoka naye chini alikuwa Bruno. Alimpenda, alikuwa mwanaume wa ndoto yake ambaye hakutaka kumuacha hata siku moja.
Machozi ya furaha yalikuwa yakimtoka, hakuamini alichokuwa akikiona, wakati mwingine alihisi kama yupo kwenye ndoto. Watu walizidi kukusanyika, kila mtu aliyekuwa akimuona Bruno, hakuyaamini macho yake.
Hazikupita dakika nyingi Abdul akatokea, uso wake ulikuwa kwenye tabasamu pana, alichanganyikiwa kwa furaha, rafiki wake wa kipindi kirefu, aliyepotea, Bruno alikuwa mbele ya macho yake.
Akamsogelea, akamsalimia na kumkumbatia. Siku hiyo ilikuwa ni furaha kijiji kizima, kila mmoja alionekana kuwa na furaha kupita kawaida. Kabla ya kufanya jambo lolote lile, Abdul akamuuliza kilichokuwa kimetokea baharini kwani waliambiwa na akina James kwamba alizama.
“Walinitupa baharini, sikujua lengo lao lilikuwa nini,” alisema Bruno.
“Walikutupa?”
“Ndiyo! Walitaka nife, nahisi walitumwa, ila sitaki kukumbuka, nimesamehe kila kitu,” alisema Bruno huku akiwa na tabasamu.
Mzee Jumanne alikuwa nyumbani kwake, si kwamba hakusikia kelele kuhusu Bruno, alizisikia sana, moyo wake ulijawa na hasira nyingi, hakuamini kama mwanaume huyo alikuwa amerudi kijijini akiwa mzima kabisa.
Mule alipokaa, alishindwa hata kutoka kwenda nje, uso wake ulikuwa na hasira mno na hakukuwa na kitu chochote alichohitaji kusikia kutoka kwa mwanaume huyo.
Aliwahi kumpiga mkwara mwingi kuhusu kuachana na binti yake lakini kijana huyo hakusikia, ilimuuma sana kwa kuwa hakutaka binti yake aolewe na Bruno kisa tu alikuwa masikini.
Kule walipokuwa, Bruno akamtambulisha mzee Todd kwa Abdul kwani aliamini kwamba hakuwa akimfahamu na baada ya hapo wakaanza kwenda nyumbani kwa mzee Jumanne huku Sharifa akiwa pembeni yake.
Walipofika, wakaingia ndani, wakakaribishwa na kukaa kwenye makochi yaliyoonekana kuanza kuchakaa. Mama yake Sharifa alipokuwa akimwangalia Bruno, hakubadilika, alikuwa vilevile kama alivyokuwa kipindi cha nyuma.
Nyumba nzima walimchukia, hawakumpenda kwa kuwa yeye ndiye aliyemfanya Sharifa kukataa kuolewa na kijana kutoka katika familia ya kitajiri mwezi uliopita.
Mzee Jumanne akaitwa, akaelekea sebuleni, alipofika hapo, macho yake yakatua katika nyuso za watu hao, hakucheka wala kuonyesha tabasamu, alitaka kuonekana kwa watu hao kwamba alikuwa akimchukia Bruno kupita mtu yeyote katika dunia hii.
Walikaa na kuzungumza, kitu ambacho Bruno alimwambia mzee Jumanne ni kwamba alitaka kumuoa Sharifa na kuondoka naye kuishi Nairobi ambapo aliamini kwamba biashara zake zingekuwa huko.
“Umuoe Sharifa?” aliuliza mzee huyo.
“Ndiyo!”
“Kivipi? Huna kitu chochote kile, unataka uende kumuua binti yangu kwa njaa? Hakuna ujinga kama huo,” alisema mzee Jumanne huku akionekana kukataa kabisa binti yake kuolewa na Bruno.
“Mzee! Mimi si Bruno niliyeondoka! Hicho ni kitu cha muhimu sana ambacho unatakiwa kukifahamu. Niambie unahitaji nini,” alisema Bruno.
Mzee Jumanne akanyamaza, kwa jinsi Bruno alivyoongea alionekana kujiamini kupita kawaida. Hakujua sababu ni yule Mzungu au la. Alimwangalia, bado muonekano wake haukuonekana kuwa kama mtu mwenye pesa, alimdharau na aliona kabisa kijana huyo hakustahili kuishi na binti yake.
“Baba! Nitakupa kitu chochote utakachohitaji. Nitakununulia boti za kuvulia samaki zaidi ya tano, achana na mitumbwi, hizo sitokununulia kama kujipendekeza, nitakununulia kama zawadi za kunitunzia huyu Sharifa. Na boti hizo zitaingia hapa kesho,” alisema Bruno huku akimwangalia mzee huyo.
Mzee Jumanne hakuamini alichokisikia, akamwangalia Bruno, kwa jinsi alivyokuwa akiongea, alionekana kumaanisha mno lakini kwake ilionekana kama kichekesho fulani hivi. Hakutaka kusema kitu chochote kile, akapuuzia na kunyanyuka kuelekea chumbani kwake.
Bruno hakutaka kujali, yeye pamoja na wenzake wakasimama na kutoka ndani, huko nje walipokwenda, watu walijikusanya nyumbani hapo, kila mtu alitaka kumuona Bruno kwa mara nyingine, walitamani hata kumgusa ili kuona kama alikuwa yeye au mzimu.
“Bado kuna mambo mengi tunahitaji kufanya! Nitakuja ndani ya siku mbili pamoja na hizo boti za mzee,” alisema Bruno.
“Hivi kweli unataka kumnunulia boti?”
“Sharifa! Ninahitaji baba yako awe na furaha, amekuwa akinichukia kwa kipindi kirefu sana kwa sababu ya umasikini wangu. Nataka nafsi yake imsute kwamba yule masikini ndiye ambaye amekuwa msaada mkubwa kwake,” alisema Bruno.
Siku hiyo hawakutaka kukaa kijijini, wakaondoka na kuelekea Nairobi huku wakiwa na Abdul. Walipofika, wakachukua chumba katika hoteli ya kawaida na kutulia humo.
Bruno alikuwa amekwishafika nchini Kenya alipokuwa akihitaji ilikuwa ni zamu ya mzee Todd tu kuondoka na kuelekea nchini Marekani.
Bado mzee huyo alikumbuka wema aliokuwa ametendewa na Bruno, jinsi alivyokuwa amemsaidia kwa kiasi kikubwa, alichomwambia ni kwamba alitaka kumuachia kiasi cha dola milioni mia tatu kwa ajili ya maisha yake.
Hicho kilikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni mia sita. Kilikuwa ni kiasi kikubwa mno ambacho Bruno hakuwahi kufikiria katika maisha yake.
Kiasi hicho cha pesa kilitakiwa kuhamishwa haraka sana kutoka katika akaunti ya mzee huyo na kuingizwa katika akaunti ya Bruno.
Bila kuogopa kitu chochote kile, wakaondoka na kuanza kuelekea katika tawi la Benki ya Barclays. Walipofika huko, Bruno akateremka, akaelekea ndani ya benki hiyo na kuchukua kitabu cha kuandikia hundi na kurudi kwenye taksi ambapo akamwandikia hundi ya kiasi hicho na hivyo pesa hiyo kuanza kuhamishwa kwenda katika akaunti ya Bruno kitu kilichochukua dakika chache tu.
“Bruno! Ninashukuru kwa kila kitu, pamoja na yote hayo, ninahitaji unisaidie kitu kimoja tu,” alisema mzee Todd.
“Usijali! Kitu gani?”
“Nitahitaji uwe shahidi katika kesi yangu inayonikabiri. Wewe ndiye umeona kila kitu kilichokuwa kikiendelea, jinsi nilivyokuwa nimetekwa na kutakiwa kuuawa, najua kwamba dunia inatamani kuona nikiuawa, ninahitaji uwe shahidi wangu, usimulie kila kitu kilichokuwa kimetokea kuanzia ndani ya meli,” alisema mzee huyo.
“Haina shida. Nitakusaidia pale nitakapohitajika,” alisema Bruno.
***
Maofisa wa CIA walikuwa makini kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea kuhusu mzee Todd, hawakutaka kuiambia dunia moja kwa moja kwamba bado walikuwa wakiendelea kumtafuta mzee huyo.
Waliwatuma baadhi ya maofisa nchini Afrika Kusini, walikwenda huko mpaka sehemu ambayo waliamini kwamba mwanaume huyo alikuwepo lakini baada ya kufika, baada ya kupambana sana na watu wa hapo, hawakuweza kumpata.
Wakarudi na kutoa ripoti juu ya kitu kilichokuwa kimetokea, kila mmoja alihuzunika lakini hawakuwa na jinsi. Siku ziliendelea kukatika, waliendelea kumtafuta kila kona lakini hawakufanikiwa kumuona.
Baada ya siku chache wakapewa taarifa kwamba mwanaume huyo alikuwa ametoa kiasi fulani cha pesa katika akaunti yake na kukihamishia katika namba nyingine.
Hilo likawafanya kuwa na hofu kwamba inawezekana mwanaume huyo aliamua kuhamisha pesa hizo kwa kuwa alihitaji kufanya manunuzi yake kwa ajili ya kujilinda.
Waliwasiliana na benki ya Barclays na kuwaambia kuhusu kuifunga akaunti hiyo lakini hilo halikuwezekana kwani kwa masharti makubwa ya benki hiyo, kitu cha kwanza kabisa hakikuruhusu akaunti yoyote ya mtu kufungwa kwa maslahi ya mtu fulani au shirika fulani.
Wakaiacha, baada ya miezi mitano wakapata taarifa tena kwamba kulikuwa na muamala ulikuwa umefanyika katika tawi la benki hiyo lililokuwa chini Kenya.
Hawakutaka kuchelewa, haraka sana wakawasiliana na vijana wao waliokuwa Nairobi na kuwaambia kufuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea huko kwani tayari walikuwa na wasiwasi kwamba mzee Todd alikuwa huko.
Ndani ya dakika tano tu, maofisa wa CIA walikuwa katika tawi la benki hiyo na kuingia ndani, macho yao yalikuwa yakiangalia huku na kule lakini hawakuweza kumuona mzee Todd.
Hilo likawachanganya, wakatoka hapo na kuelekea nje, walipofika huko, wakamuona kijana mmoja akitembea kwa mwendo wa kujiamini kabisa kuifuata teksi moja iliyokuwa ikimsubiri.
Huyo alikuwa mtu pekee ambaye alitoka ndan ya benki hiyo na kufuata teksi, wakahisi kitu na kuanza kuifuatilia. Alipoifikia teksi ile, akafungua mlango na kuingia ndani.
“Kuna nani mwingine ndani ya teksi ile?” aliuliza ofisa mmoja.
“Naona watu kama watatu hivi!”
“hebu twende!”
Walitaka kuiwahi hata kabla haijaondoka mahali hapo. Mikononi walikuwa na bastola zao, walipoifikia tu, wakaushika mlango wa dereva na kumuamuru atulie kama alivyokuwa na kuufungua mlango.
Walinzi waliokuwa mahali hapo walionekana kushtushwa na kilichokuwa kikiendelea, mawazo yao yaliwaambia kwamba watu hao walikuwa majambazi, wakaandaa bunduki zao lakini ofisa mmoja akawaonyeshea kitambulisho ambacho kilionyesha kwamba walikuwa ni maofisa wa CIA.
“Settle down,” (tulieni) alisema mwanaume mmoja na walinzi wote kutulia.
Wakamshusha mzee Todd, akateremka na kuinyoosha mikono yake ambapo moja kwa moja wakamfunga pingu. Haikuonekana kuwa kazi kubwa, mzee huyo hakuonyesha ishara yoyote ya kiburi kwani alijua kabisa kwamba kitu hicho kingetokea na hata kama kisingetokea yeye mwenyewe aliamua kujipeleka katika ubalozi wa Marekani ambapo huko angechukuliwa na kusafirishwa kuelekea nchini Marekani.
Kwa jinsi kitendo kile kilivyokuwa cha haraka na siri kubwa, hakukuwa na mtu yeyote yule ambaye aliona kilichokuwa kimetokea zaidi ya walinzi wawili, wakamchukua mzee huyo tu, wakampakiza ndani ya gari.
“Help me! You have to do what I’ve told you to do,” (nisaidie! Fanya nilichokwambia kufanya) alisema mzee Todd huku akimwangalia Bruno.
“I will!” (nitafanya)

Je, nini kitaendelea?
Tukutane jumanne
 
Nami nipo humu hatimaye baada ya kuianza shusha nondo mgani wetu
 
Hii hadithi yaendelea vizuri au arostos pia
 
Jion ndo ii woyooooooooooo
Mkuu twasubir na tunakusubir mkuu WA kaya
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom