BRUNO THE FISHERMAN-
Mtunzi.Nyemo
Episode 12
Kitendo cha Bruno kuwaamini Wazungu wale kilionekana kuwa kosa kubwa kwa kuwa hawakufika nchini Kenya kutangaza dini au kutoa msaada, walifika mahali hapo kwa kufanya kitu kimoja tu, kumuua yeye na kurudi nchini Marekani.
Kumpata Bruno na kumuua lilionekana kuwa jambo gumu mno, mara nyingi hakuwa akishinda nyumbani, kwa kuwa alikuwa na mambo mengi ya kufuatilia, kazi yake kubwa ilikuwa ni kwenda huku na kule na kuhakikisha hakuna kitu chochote kile kinachoharibika.
Tim na wenzake wakawa kwenye wakati mgumu, kila walipopanga wamteke na kwenda naye sehemu kwa lengo la kufanya mauaji, jambo hilo lilionekana kuwa gumu mno.
Mtu waliyekuwa wakibaki naye alikuwa Sharifa. Yeye ndiye walisaidiana naye kuhakikisha huduma ya afya ilikuwa ikiendelea vizuri na kila mtu kuhudumiwa kama ilivyotakiwa kuhudumiwa.
“Tufanye nini?” aliuliza Adson.
“Hivi kweli imeshindikana kumteka kabisa?” aliuliza Tim huku akiwaangalia wenzake.
“Ni suala gumu sana! Yaani kumuua ni vigumu kuliko hata tulivyokuwa tunajifikiria,” alisema Kelly.
“Kwa hiyo?”
“Kama vipi tumteke mkewe!”
“Halafu?”
“Tumuonye asiende Marekani kwa ajili ya kutoa ushahidi vinginevyo tutamuua mke wake,” alisema Adson.
Hawakutaka kufanya jambo hilo kwa haraka, walitakiwa kusubiri mpaka siku mbili kabla ya kesi ile kuunguruma tena nchini Marekani.
Kumteka Sharifa halikuwa jambo gumu, lilikuwa jepesi mno ambalo lingefanyika ndani ya dakika chache tu na kufanya mambo mengine.
Wakakubaliana na hatimaye kwa pamoja kuanza kuhesabu siku. Hawakumuonyeshea Sharifa tofauti yoyote ile, nyuso zao zilikuwa na tabasamu pana na kila wakati walipokuwa wakiongea waliongea kwa mbwembwe kiasi kwamba msichana huyo akawaona kuwa watu muhimu sana.
“Una mimba?” aliuliza Tim huku akimwangalia Sharifa.
“Umejuaje?”
“Unavyoonekana tu! Kweli au uongo?” aliuliza.
“Kweli!”
“Ooh! Safi sana!”
Hiyo ikawa sababu nyingine kwao kufanikisha kile walichokuwa wakikihitaji, walijua kabisa kwamba mwanamke anapokuwa na mimba ya kwanza, mwanaume huwa anachanganyikiwa na anakuwa radhi kufanya lolote lile lakini si kumpoteza mke wake.
Wakaambiana kilichokuwa kikiendelea na hivyo kusuka mipango yao vizuri. Tim akaanza kuangalia ramani, ilikuwa ni lazima kumteka mwanamke huyo na kukimbia naye mbali kabisa na kijijini hapo.
Sehemu ambayo aliiona kuwa nzuri kukimbilia ilikuwa ni ni Tanga ambapo huko kulikuwa na mapango ya Amboni, wangekaa huko mpaka kipindi ambacho kesi ile inamalizika pasipo Bruno kuelekea nchini Marekani.
“Ni mpango mzuri sana, naamini kama tutafanikiwa, basi tutakuwa tumeshinda vita kubwa mno,” alisema Adson huku akitoa tabasamu pana.
Wakati wao wakiendelea kujadiliana na kupanga mipango yao, upande wa pili watu walizidi kumiminika katika kila kituo ambacho taasisi ya Bruno na mkewe ilianzisha. Madaktari waliokuwa na uwezo waliendelea kufanya kazi yao kama kawaida huku wakipata usimamizi wa karibu kutoka kwa Sharifa.
Kila siku Bruno alikuwa na kazi ya kumpigia simu mke wake na kumuuliza kuhusu maendeleo yake. Kipindi hicho ndicho msichana huyo alipomwambia mpenzi wake kwamba alikuwa mjauzito.
Bruno aliposikia hivyo, hakutaka kuendelea kubaki Nairobi, haraka sana akaondoka na kuelekea Mombasa kwa lengo la kumuona mpenzi wake huyo.
Alipofika, akapokewa kwa mabusu kemkem na kukumbatiwa. Alimwangalia Sharifa machoni na kumuuliza kama kile alichomwambia kilikuwa kweli au alikuwa akimtania tu.
“Ni kweli! Nilikwenda kupima,” alisema Sharifa huku akimwangalia mpenzi wake huyo.
“Wa kike au wa kiume?”
“Bado sijajua! Ila ninachojua atakuwa mtoto mzuri sana,” alisema Sharifa na kumkumbatia Bruno.
Ujauzito huo ulimchanganya Bruno, hakuamini kama naye alikuwa akikaribia kuitwa baba. Kila alipomwangalia Sharifa, msichana huyo alionyesha tabasamu pana huku muda mwingi akilishika tumbo lake.
Mapenzi aliyokuwanayo Bruno ni kama yalikuwa yamechochewa na kuchipuka upya moyoni mwake. Alizidi kumpenda mpenzi wake na kumwambia kwamba angempenda milele hata kama kingetokea kitu gani. Hakukaa sana Mombasa, siku iliyofuata akarudi Nairobi huku Tim na wenzake wakiendelea kupanga mipango yao.
***
Wakati akina Tim wakiwa nchini Kenya, huku Marekani Maxwell alitakiwa kufanya jambo jingine la msingi, kwa kuwa kati ya mashahidi waliokuwa wametajwa alikuwepo Innocent, ilikuwa ni lazima kuhakikisha kijana huyo anauawa mara moja.
Akampigia simu na kumwambia kwamba anataka kuonana naye, kwa kuwa Innocent hakuwa na hofu na alishirikiana na Maxwell kwa mambo mengi, akakubali na kwenda kuonana naye.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ambayo Maxwell alitakiwa kummaliza kijana huyo, hakutaka kuona akiendelea kuishi, ili kwenye kesi ile ionekane kwamba kweli mzee Todd alifanya mauaji hayo, hakuwa na jinsi kuanza na kijana huyo.
Baada ya dakika arobaini na tano Innocent akaibuka nyumbani hapo na kuanza kuzungumza. Hakutaka kumficha, alimwambia ukweli jinsi kesi ilivyokuwa ikiendelea mahakamani na ilitakiwa wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba mzee huyo hachomoki.
Hilo halikuwa tatizo kwa Innocent, akakubaliana naye lakini kwa upande mwingine, akajua kabisa kwamba angeweza kusalitiwa.
Akachukua simu yake na kumtumia ujumbe mfupi kijana aliyekuwa nje, ujumbe ambao alimwambia kuwa alitakiwa kuhakikisha anamchukua Innocent na kwenda naye sehemu kumuua akiwa na wenzake.
Hilo halikuwa tatizo, wakakubaliana na wakati wakiagana na Innocent kutoka nje, wanaume wawili wakamsogelea na kuanza kumzongazonga huku wakiwa na bastola.
Alishangaa, lilikuwa jambo geni kabisa kwake, akahoji lakini akajibiwa kwa kupigwa na kitako cha bastola kichogoni hapohapo akaanguka na kupoteza fahamu.
Wakambeba na kumuingiza ndani ya gari. Hawakutaka kupoteza muda kusubiri mahali hapo, wakaondoka na kuelekea katika jumba moja lililokuwa Manhattan hapohapo jijini New York.
Huko, hawakutaka kuchelewa, wakamuingiza katika chumba cha mateso na kumuweka kitini kisha kumfunga kamba. Aliporudiwa na fahamu, alishangaa kuona akiwa kwenye chumba hicho kilichoonekana kutisha kupita kawaida kutokana na mazingira yake yalivyokuwa.
Hakujua kosa lake lakini hakuwa na budi kuomba msamaha, wanaume hao waliokuwa na miili iliyojazia hawakutaka maswali wala maelezo walichokifanya ni kutekeleza kazi ya bosi wao na hivyo kumpiga risasi kadhaa kifuani na kumpigia simu Maxwell.
“Kazi imekamilika,” alisema jamaa mmoja.
“Amekufa?”
“Kama ulivyotuagiza.”
“Sawa. Ahsanteni! Ngoja niwasiliane na akina Tim nione wamefikia wapi,” alisema Maxwell na kukata simu, hakutaka kupoteza muda, hapohapo akampigia simu Tim kwa lengo la kumuuliza mahali walipofikia.
“Kila kitu tayari,” alisikika Tim kutoka upande wa pili.
“Mmemuua?”
“Hapana! Ila tumemchukua mke wake, hapa tupo tunaelekea nchini Tanzania,” alisema.
“Kufanya nini?”
Tim akaanza kumuelezea kile kilichokuwa kimetokea, walimwambia hali aliyokuwanayo Sharifa kwamba alitakiwa kuchukuliwa na mumewe kupigiwa simu na kuambiwa kwamba hakutakiwa kwenda nchini Marekani kwa gharama yoyote ile.
“Kazi nzuri! Na akija Marekani tu, hakikisheni mnamaliza huyo mke wake, sawa?” alisema na kuuliza.
“Ndiyo mkuu!”
“Kazi njema,” alisema na kukata simu.
JE, nini kitaendelea?