Gumzo: Mama Mwajey

Donnie Charlie

JF-Expert Member
Joined
Sep 16, 2009
Posts
18,550
Reaction score
21,676
MAMA MWAJEY

HAIKUWA siri kwamba maandazi anayouza Mama Mwantum hayakuwa na tofauti yoyote ya maana pale mtu angeyalinganisha na ya wenziwe.

Tangu unga anaotumia, mafuta anayokaangia mpaka meza anayouzia havikuwa mbali na vya wenziwe wote wanaofanya biashara pale Maandazi Street.

Mama Mwantum hutumia debe chakavu, ambalo juu yake huweka sinia pana ambalo pia juu yake pana vitu - maandazi.
Jambo ambalo halikuwa la kawaida kwa maandazi ya mama Mwantum ni vile wateja wanavyoyapapatikia!

Mama Mwantum hufika Maandazi Street muda ambao wenziwe wote huwa wameshafika na kuanza biashara, lakini biashara zao huenda kwa kusuasua kutokana na baadhi ya wateja kusubiri maandazi ya Mama Mwantum. Anapofika tu, huzungukwa na wateja lukuki wakingoja awauzie.

Na yeye huwa hafanyi papara: huchukua debe lake na kuligeuza kichwa chini miguu juu na kuweka sinia juu yake. Kisha kwa maringo ataanza kupakua shehena kubwa ya maandazi na kuweka juu ya sinia. Hapo wateja utadhani kichaa kimewashika! kila mmoja atadai awe wa kwanza kuuziwa.

"Jamani msifanye fujo! Mkifanya fujo nitaacha kuuza haya maandazi!" Husema Mama Mwantum, kana kwamba yeye ndiye `mfalme', na katu si mteja!

Kwa unyonge kabisa wateja wataacha kufanya fujo na kupanga ka-foleni ka kununua maandazi. Muda wote huo akinamama wenziwe ishirini hivi wanamwangalia kwa macho ya husuda, na kucheka naye jino - pembe.

Baada ya muda mfupi sinia lote linabaki jeupe, na mama Mwantum kujikusanyia vilivyo vyake na kuondoka kwa madaha. Wauza maandazi wenziwe wanamsonya kimoyomoyo.

Kuondoka kwa mama Mwantum ndiko kunakoacha fursa ya wateja wengine kununa kwa wauza maandazi waliobaki.
Hali huwa hivyo kila siku.
Maandazi Street

Siku moja mama Mwajey alienda mtaa wa Maandazi kusogoa kwa shoga yake mama Hayamwezi. Mama Mwajey hufanya biashara hiyohiyo ya Maandazi katika kitongoji cha pili, baada ya kuhamia kutoka Tanga hivi karibuni. Hakuwa na taarifa za mama Mwantum na biashara yake ya Maandazi.

Wakati wanaendelea kusogoa, ghafla aliona sura ya shoga yake inaanza kujaa makunyanzi, na kuanza kuonana kunong'ona maneno fulani na wenziwe.

"Aka babu wee! Tumpashe! hiyo dawa yake aweke maji kidogo ipungue makali na sisi tufanye biashara!" alisema mama Hamyamwezi kwa sauti ya chini na kuwafanya wenzake waporomoe kicheko cha haja!
"Hee! He! Heeeee!! Halo Haloooo!"

Mama Mwantum machale yakamcheza kwamba siyo bure kicheko kile kinamhusu yeye. Lakini akapuuza.
"Waswahili nawafahamu walivyo!" alijisemea kimoyomoyo.

Akapakua shehena yake, na wateja wote wakahamia kwake. Punde si punde, maandazi yote finish! Kwisa kabsaa! Akabeba vilivyo vyake na kujiondokea.

Mama Mwajey alijionea maajabu!
"He! Mbona maandazi ya mwenzenu yanagombewa vile! Au mwenzenu kasomea upishi pale Forodhani chuo cha Utalii" akauliza.
Kikafuata kicheko kikali.

"He! He! Heeee! Halooooo!"
Mama Mwajey akabaki kwenye mataa.
"Labda chuo alichoenda kipo Bagamoyo Mlingotini! Lakini tujuavyo Mama Mwantum ni mwenzetu!" alisema Mama Siwatu, aliyeketi jirani na mama Hamyawezi.

Hawakuongea zaidi.
Wazo la biadhara `kutoka' sawa na ya mama Mwantum lilimvutia sana mama Mwajey!

Hebu fikiri. Unaweka maandazi, yanagombewa, unajiendelea kwenda kwenye shughuli nyingine! Raha iliyoje!
"Lazima nitamwendea mama Mwantum anipe siri ya ulimbo wa urembo!"

Mganga ‘konkodi’

MAMA MWAJEY hakupata taabu kupafahamu nyumbani kwa Mama Mwantum! Ilikuwa ni kukatiza vichochoro viwili vitatu tu na kufika nyumbani kwake.

Jambo aliloliona gumu ni `gea' ya kumuingia Mama Mwantum mpaka akubali kutoa `siri ya urembo' wa maandazi anayouza.
Kwanza kabisa Mama Mwajey alilazimisha urafiki wa karibu kati yake na Mama Mwantum, kila jioni huenda kwake na kusogoa kuhusu hili na lile. Kwenye vikao vya kusukana hupiga soga kuhusu hili au lile na kuporomoa vicheko mara zote.

Baada ya miezi minne, ushoga wao uliota mizizi kiasi cha kumfanya kila mmoja amwamini mwenziwe na kuwa huru kumweleza lolote pasi na kuwa na wasiwasi wowote ule. Ni hali hii aliyoingoja Mama Mwajey muda wote.

Siku moja Mama Mwantum alijiingiza kwenye mtego pale alipotumbukiza suala la biashara ya maandazi kwenye mazungumzo yao.
"Unajua shoga," alianza, "binadamu tuna wivu sana! Yaani wenzangu wote tunaofanya biashara nao pale mtaani hawanipendi kabisa!"
Mama Mwajey akajifanya kushangaa!.

"Lo! Kwa nini Shoga?"
"Aah! si wivu tu? Wananionea gere biashara yangu inavyotoka! Nikiweka maandazi yangu wateja wanayagombea. Hilo nd'o lawakera. Wananionea kijicho!"
"Ala kumbe..."
"Eeeeeh!" akadakia tena Mama Mwantum, "Wivu tu! Eti wanataka dawa ninayoweka niiongeze maji kusudi na wao wapate biashara kidogo! Lakini nani asiyetumia dawa kwenye biashara yake? Majuzi tulikorofishana na Mama Hayawezi shauri ya mambo haya haya!"
"Enhe! Ilikuwaje!"
"Ilikuwa Kasheshe tupu! Isingekuwa Mama Siwema kutuamulia, hadithi ingekuwa nyingine!"
Pakapita kimya.

Kimya kikuu kina mshindo. Mama Mwajey alitumia muda huo kutafakuri jinsi ya kumuingia shogaye.
"Kwani ni mganga yupi aliyekupa dawa hiyo?" aliuliza.
Mama Mwantum akacheka.

"Na wewe unataka? Lakini utayaweza masharti?"
Meno yote ya Mama Mwajey yakawa nje kwa furaha.
"Ndiyo nataka sana! Wala hamna sharti litakalonishinda!"
"Basi shoga! Mganga mwenyewe anaitwa nani sijui, ila ni maarufu kwa jina la Songombingo! Anapatikana kijiji cha Kalambo, nyanda za juu kusini!"
***
Mipango ikasukwa, na baada ya wiki mbili Mama Mwajey na Mama Mwantum wakaelekea kwa mganga.
Nyumba ya mganga yule haikutofautiana na ya wengine. Vikorokoro vyote ya kumpa `imani' mteja vilikuwepo. Kuanzia kwato za Punda mpaka fuu la kichwa lifananalo na mtu.

Mama Mwajey aliiingia ndani peke yake, akimwacha Mama Mwantum nje.
Kibanda cha Mganga kilikuwa kiza. Mwanga hafifu uliopenya kwenye nyufa za kibanda cha Songombingo ndio uliomwezesha Mama Mwajey kuzungumza huku akiona ni wapi mganga ameketi. Hata hivyo hakuweza kuiona vizuri sura yake.

Macho yake yalivinjari kuta za kibanda kile kilichosheheni kila namna ya vimbwanga vya kuonesha kwamba mganga yule ni `rili' na katu siyo `feki'. Mawazo yake yalikatishwa na sauti ya mganga.
"Nini shida yako?"
Mama Mwajey akaketi vizuri.

"Biashara baba! Nafanya biashara ya maandazi!
Nataka biashara yangu itoke kwa kasi kubwa kuliko ya wenzangu. Nikifika tu wateja waanze kupapatikia maandazi ninayouza!"
"Shida hiyo tu?" aliuliza mganga.

"Tawire baba!" alijibu Mama Mwajey.
Mganga alianza kuzungumza maneno ya ajabu ambayo Mama Mwajey hakuweza kuyaelewa. Kisha akasita ghafla kama vile mtu aliyekumbuka jambo fulani.

"Umeshaweka kifungua n'koba?"
Mama Mwajey alifungua pochi lake na kutoa noti mbili za bluu na kuzitumbukiza kwenye chungu kitupu alichooneshwa na mganga.
"Ngapi hizo mama?"
"Elfu ishirini, mzee!"
Mganga akaendelea kuzungumza kwa kasi mpya baada ya "kifungua mkoba" kuwepo kwenye himaya yake.
Aliendelea kupandisha "mori" ambapo sasa alianza kusimama na kuranda huku na kule chumbani kama kwamba "anapandisha" mashetani.

Alianza kupiga mayowe na kusema maneno ya ajabu kwa sauti kubwa. Kisha akashusha sauti, na kuanza kusema kwa sauti ndogo, nene.
Dawa ya biashara
"UNAMFAHAMU Mama Mwantum?" mganga aliuliza. "Ndiyo namfahamu, tena ndiye aliyenielekeza hapa!" alijibu mama Mwajey kwa shauku.
"Vema sana! Yule nilimpa dawa ya kuleta wateja. Si unaona wateja wanavyopaparikia biashara yake?"
"Tawire baba!"

"Eenhe! Na wewe ukifuata masharti nitakayokupa biashara yako itatoka vilevile kama ya mama Mwantum!"
Mganga akaanza kutoa orodha ndefu ya vitakataka vidogodogo anavyovihitaji kwa kazi yake, ikiwa ni pamoja na kucha za mtoto mchanga mwenye umri wa siku moja, chupa tisa z amaji ya Ziwa sipe lililoko kwenye mlima Kilimanjaro na jina la bibi kizee, aliyerudiana na mumewe baada ya kutengana tangu wakiwa vijana.

Yote hayo yalimfanya mama Mwajey kichwa kimuwange, lakini sharti la mwisho ndilo lililomwacha hoi kabisa.
"Ukishavipata vitu hivyo vyote ulete ngozi ya kondoo dume lililouawa kwa radi!"
Mama Mwajey akatoa `kifunga mkoba' cha noti nyingine mbili za buluu.
"Halafu uje nikupe dawa!"
"Tawire baba!"
***
Kazi ya kutafuta vitu alivyovitka mganga haikuwa ndogo. Vitu alivyovitaka mganga vilimfanya mama Mwajey afunge safari huku na kule kutafuta vitu vile.

Wakati fulani ilimbidi avizie makaburini usiku alipoona kitoto kichanga cha siku moja kimezikwa ili aweze kupata kucha zake.
"Mwishowe n'takuwa mwanga! Hivi nikikamatwa nitasema nini mbele ya Baba Mwajey?"
Hata hivyo, baada ya miezi mitano ya gharama kubwa na safari nyingi, hatimaye mama Mwajey alikuwa na vikorokoro vyote vinavyohitajika kwa Mganga.

Kazi ya kuvipata vikorokoro vile haikuwa ndogo. Ilitaka moyo haswa! Tena almanusura ndoa yake ivunjike!
Lakini siku ilifika ambayo begi lake lilisheheni vyote alivyotaka maganga kusudi apewe dawa itakayowapumbaza wateja wa maandazi wayapaparikie maandazi yake.

Alifika kwa mganga Songombingo na kumkabidhi ile "malighafi" ya kufyatulia dawa `konkodi'.
"He! Unaweza kuvipata vitu vyote hivi mara hii?"
"Tawire baba!"

""Hebu niambie ngozi ya kondoo dume lililopigwa na radi uliipataje!"
"Ni hadithi ndefu!" alisema mama Mwajey,"kwanza ilinibidi nimuulize Mwajey wanafundishwa nini shuleni kuhusu radi. Mwajey akaniambia radi ni umeme wenye nguvu nyingi sana ambao tungekuwa na teknolojia ya kuuhifadhi radi moja tu ingetosha kuzuia mgao wa umeme kwa mwaka mzima!"
"Enhe!?"

"Mwajey akazidi kunifundisha nilipombishia kwa makusudi. Akasema Mrusi fulani aliuawa na radi alipotengeneza kishada cha bati na kukiunganisha na waya. Lo! Nilichekea tumboni kwa furaha, lakini uso ukabaki umenuna!"
"Enhe, ikawaje" Mganga akazidi kudodosa.

"Nilitengeneza kishada kama cha yule Mrusi nikaenda nacho kijijini kwetu. Nikaenda porini peke yangu na kukifunga kwenye mti mmoja siku fulani ya mvua. Sikukaa hata robo saa radi iliupiga mti ule na kuung'olea mbali. Nilipoona nimefanikiwa, nilikimbia mnadani na kuchukua kondoo dume mmoja na kumpeleka porini. Nikaufunga waya wa kishada kwenye shingo yake, na kuufunga mguu wake wa mmoja wa nyuma kwenye kigingi!"
"Halafu yake?!"

"Hata sikufika mbali, radi ikampiga dafrau na kumuulia mbali! Si unaona mwenyewe ngozi utadhani imechomwa moto?!"
"Ulimchuna mwenyewe?"
"Ndiyo! nilimchuna, japo kikwetu ni mwiko mwanaumke kuchuna ngozi ya mnyama!"
"Na kile kishada?"

"Nilikikata nikakiacha kiruke zake!"
"Hongera sana! sasa lete vitu hivyo vyote nikuchanganyie upate dawa!" alisema mganga.
Baada ya kupayuka maneno mawili matatu na kuchanganya vikorokoro vile, alikata kipande cha ngozi ya kondoo na kumpa mama Mwajey.

"Chukua kipande hiki cha ngozi ya kondoo, uwe nacho muda wote unapofanya biashara!"
Mama Mwajey akakipokea na kukifutika kwenye kanga. Kisha akatoa `bakshish' ya shilingi elfu hamsini kwa mganga.
"Kazi ya kangozi hako itakuwa ni moja tu: Kukukumbusha utumie akili kwenye biashara yako. Kama vile ulivyotumia juhudi na maarifa yote kupata ngozi hiyo, kadhalika ufanye vivyo hivyo kwenye kutafuta wateja, na kuwafanya wateja wasikimbie bidhaa zako.

Sema na wateja vizuri, zingtia kanuni za afya, jifunze mbinu za kisasa za mapishi, na uzingatie ubora wa bidhaa zako!
Ngozi hiyo hivyo ilivyo, haiwezi kukuvutia wateja, na wala hamna dawa nyingine ya biashara!!"
Alisema Mganga Songombingo na kumwacha mama Mwajey donge limemshika.

Alitoka bila kuaga, na akataka kuitupa ngozi ile. Lakini moyo ulisita. Akaamua kukiacha kipande cha ngozi kimkumbushe juhudi na gharama alizoingia kukitafuta.
"Lazima nifanye biashara vizuri ili nirudishe gharama!"

***
Mama Mwajey akaacha kutumia ngano inayookotwa dampo. Akaacha pia kutumia mafuta wateja wasiyoyapenda. Akaongeza iliki kwenye maandazi yake na badala ya kupika maandazi yenye upepo, akapika yaliyojaa. Yote hayo yakiwa ni matokeo ya shule ya Sayansi kimu aliyojifunza kwa njia ya posta.

Kwenye kila andazi hakupata faida kubwa, lakini wateja wengi walinunua kwake na kufanya achume zaidi.
"Wateja wakizoea nitapunguza ubora kidogo nipate faida zaidi!"

Idadi ya wateja ilizidi pale alipoamua kuhifadhi maandazi yale kwenye chombo chenye wavu kuzuia nzi. Ikawa akifika tu, wateja wanaanza kugombea maandazi wasije wakakosa.

"He! Hee! Heeee! kapewa dawa hiyo na Shog'ake mama Mwantum!" wenzake walimng'ong'a.
"Ai babu we! weka maji kidogo kwenye dawa yako, au tugawiye na siye!" Alimtania kwa sauti Mama Hamnazo.
"Hamna dawa yoyote Shoga..."alijitetea mama Mwajey.

"Acha roho mbaya! na Miye utanipeleka kwa mganga wako!" alisisitiza mama Hamnazo.
Mama Mwajey akacheka.
"Utayaweza masharti?"
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…