Geita: Ashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuvamia makanisa mawili

Kikwajuni One

JF-Expert Member
Mar 18, 2013
13,142
6,947
Geita. Mkazi wa Chato, John Marore anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo kwa tuhuma za kuvamia makanisa mawili likiwemo la Mtakatifu Bernadetha wa Lurd Parokia ya Nyakato-Buzrayombo na lile la Waadventisti wasabato yaliyopo kata ya Buzrayombo mkoani Geita.

Matukio ya uhalifu kwenye makanisa hayo yalitokea usiku wa Septemba Mosi,2023 na kusababisha Kanisa la Mtakatifu Bernadetha wa Lurd kufungwa kwa siku 30 kutokana na kufuru na najisi iliyofanywa ndani ya Kanisa hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale amethibitisha kukamatwa kwa mtu huyo akidai jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kubaini wote waliohusika ili sheria ichukue mkondo wake.

Katwale amesema katika kukabiliana na uhalifu wamelenga kuimarisha ulinzi shirikishi kuanzia ngazi ya vijiji na kuzitaka taasisi binafsi kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yao ili kuepusha matukio kama hayo kujiridia.

Katika taarifa iliyotolewa Septemba Mosi na Makamu wa Askofu jimbo la Rulenge –Ngara Padri Ovan Mwenge ilieleza watu wasiojulikana walivunja ukuta wa kanisa na kufanya kufuru kwenye sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa kuila ama kuondoka nayo na nyingine kuitelekeza sakafuni ndani na nje ya kanisa.

Taarifa hiyo ilieleza maelekezo na sheria ya Kanisa kanuni ya 1211 -1213 na kwa maelezo ya Askofu Severine Niwemugizi kanisa hilo litafungwa kwa siku 30 ambapo baada ya maboresho na ukarabati mdogo, litabarikiwa na kutakaswa ili liendelee kutumika.

Kwa sasa waumini wanasali nje ya kanisa hilo wakihimizwa kusali, kufunga, kufanya toba na malipizi kwa Mwenyezi Mungu ili aboreshe mioyo ya watu wenye nia ovu kwa mambo matakatifu.

Akizungumzia tukio la kanisa kuvunjwa mlango kisha watu wasiofahamika kuiba vyombo vya muziki Mchungaji wa kanisa la waadiventisti wasabato, Musa Mgema alisema watu hao walivunja mlango wa Kanisa na kuiba vifaa hivyo ikiwemo spika mbili na ‘power mixer’ moja.

Alisema kuibiwa kwa vifaa hivyo kunaathiri huduma za kiroho ya kanisa na kuwa tukio hilo sio la kwanza kwani Agosti mwaka huu katika Kanisa la Kasuzbakaya lililopo Biharamulo watu wasiofahamika walivunja dirisha na kuingia kanisani na kuiba ‘power mixer’ .

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo kuzungumzia tukio hilo hazijazaa matunda baada ya kutokuwa ofisni na hata alipopigiwa simu yake iliita bila kupokelewa.

Tukio hili ni la pili kutokea mkoani Geita ikiwa ni miezi sita imepita baada ya kijana mmoja mkazi wa Geita kudaiwa kuvamia Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo la Geita na kufanya uharibifu uliosababisha hasara ya Sh48.2milioni.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom