Jokajeusi
JF-Expert Member
- Jun 1, 2018
- 6,336
- 10,910
Habarini Wakuu!
Eneo lote lilikuwa kimya. Ukimya ule hata ni panya angekuwa akitembea basi sauti yake ingesikika. Giza totoro lilikuwa limetawala. Ukungu mwepesi ulikuwa ukikimbia kwa mwendo wa ado ado na kufanya eneo lile lipoe na majani yalowe kwa umande. Kwa jinsi kulivyokuwa kimya usingefikiri kama kuna kiumbe kilikuwa kinaishi humo. Na kama kipo basi kitakuwa ni kiumbe hatari sana kisichopenda kelele. Itoshe kusema kuwa eneo lile lilifanana kwa ukaribu na kuzimu.
Nilizinduka na fahamu zangu ziliniita baada ya kuhisi baridi. Nilishtuka kuwepo mahali pale. Giza lilikuwa limenikumbatia mpaka kwenye mboni zangu hivyo sikuweza kuona kitu chochote kile. Nilitaka kuamka lakini nilihisi mwili wangu ni mzito na hapo hapo nikaanza kuhisi maumivu maeneo ya mgongoni. Nilipeleka mgongoni mkono wangu wa kulia. Looh!! Lilikuwa ni jeraha kubwa lililokuwa linavuja damu nyingi. Hofu ilipandisha bendera moyoni mwangu. Mapigo ya moyo nayo yalinienda mbio. Masikini Joka Jeusi ni nini kimekupata.
Mguu wangu wa kushoto ulikuwa umevunjika mara mbili hivyo sikuweza kujongea. Nilijikuta nalia huku msitu ukigeuka kasuku kwa kuiga kwikwi yangu. Nilivua shati na kujifunga kwenye mguu ili kuzuia damu isiendelee kutoka. Nilikumbuka nikiwa shule ya msingi tulivyofundishwa jinsi ya kumhudumia mtu anayevuja damu nyingi. Nilijaribu kuvuta kumbukumbu bila mafanikio. Sikukumbuka chochote kile. Nilianza kujivuruza mithili ya Chatu aliyeshiba. Maumivu makali yalizidi na kufanya kichwa kianze kuuma. Licha ya kuwa na baridi kali lakini mwili wote ulilowa kwa jasho. Oooh!! Masikini Mimi.
Kwa mbali nilisikia sauti kama za watu zikija kule nilipokuwepo. Niliacha kulia na kusikiliza kwa umakini. Moyo ulipiga paaa!! baada ya kusikia mmoja wa wale watu akisema: Kichwa chake kitamfanya aamini tumetekeleza kazi. Kauli hiyo ilinifanya nipagawe. Itakuwa ni kichwa cha nani kama si changu. Nilijiuliza kimoyo moyo. "nani huyo anayehitaji kichwa changu ili aamini nimekufa?" Nilinong'ona.
Niliamua kujiburuza bila kujali maumivu makali yaliyokuwa yakinipiga. Tayari niliona lango kuu la kuzimu. Nilijua kuwa nikileta mchezo tuu basi maisha yangu yanaweza kukoma pale. Pumzi iliniisha. Nilikuwa natweta ungedhani ni Bata linalopiga tambo. Nilijiuliza kwani hawa watu wananitafutia nini. Kwani nimefanya nini. Lakini hakuna aliyekuwa ananijibu. Giza na miti ilibaki ikiniangalia kwa huruma bila msaada. Sauti zile nilizisikie tena huku kwa mbali nikiona tochi ikimulika huku na kule kama mtu anayetafuta kitu. Nani mwingine kama si mimi.
Nilijiburuza kwa mara ya mwisho nikijaribu bahati yangu. Moyoni nilihisi kukata tamaa. Mbele yangu nilikabiliwa na mto baada ya kuburuzika kwa kitambo kidogo. Kweli siku ya kufa nyani miti yote inateleza. "Niende wapi sasa?" nikiwa najiuliza hayo nilisikia sauti ikisema: Atakuwa bado hajavuka mto" Hapo hapo niliishiwa na nguvu. Nilianza kukumbuka watu waliokufa zamani nikijua dakika chache zijazo nitaungana nao. Nilimkumbuka Dalana mpenzi wangu aliyekufa miaka mitatu iliyopita. Nilihisi uwepo wake na nilimuona angani akielea kwenye ukungu akiwa ametabasamu. " Joka Mpenzi Nimefurahi kukuona huku" ilikuwa sauti ya Dalana akiwa kwenye ukungu na mavazi meupe pee yaliyofanya eneo lile liwe na nuru. Nilitabasamu nikasimama. Sikujua nimepata wapi nguvu za kusimama. Alishuka chini katikati ya mto akiwa kasimama juu ya Maji kama Yesu. "Njoo! Njoo Mpenzi wangu" Aliongea huku akidengua kwa manjonjo ya kike. Nilipiga hatua na kujikuta nimetumbukia mtoni. Nilibebwa na maji na Dalana alipotea kumbe zilikuwa ni fikra zangu tuu. Nilijitahidi nisibebwe na maji lakini maji yalinishinda. Mwishowe nilipoteza fahamu na rasmi niliingia katika jimbo la kuzimu huko.
Mama Diana akiwa kajipumzisha alishangaa mlango wake ukifunguliwa kwa nguvu. Alishangaa kumuona Devotha akiwa amefura kwa hasira kama mbogo aliyejeruhiwa. Devotha alimsogelea hali iliyomfanya Mama Diana aamke kwenye Sofa alilokuwa kajilaza. Devotha alipiga kibao kikali cha shavu na kumvaa Mama Diana na wote walianguka chini. Muda wote nilikuwa dirishani nachungulia hii vita ya wanawake wawili. Mmoja alikuwa msichana wa miaka 26 na mwingine mama wa miaka 39. Najua unajiuliza ni nini kinafanya wapigane. Si kingine bali ni mapenzi. Mapenzi ni hatari kuliko silaha za kemikali. Yanaunguza kuliko moto. Yananguvu kuliko mauti. Mama Diana alijikurupua pale chini na kukimbia ndani. Devotha alibaki akihema huku akijivunga vizuri kanga yake. Punde si Punde Mama Diana alitoka akiwa ameshikilia Bastola hali iliyomfanya Devotha kuhamaki.
" We malaya yaani unanichukulia Mpenzi wangu na unataka kuniua" Ilikuwa ni sauti ya Devotha aliyekuwa akiongea kwa hasira sana. Niliona Mpenzi wangu Devotha yupo katika hatari kubwa. Nilitoka kule nje dirishani nilipokuwa nachungulia. Nilipofungua tuu mlango nilipokelewa na sauti ya mlio wa risasi. Macho yangu yalimshuhudia Mpenzi wangu Devotha akilamba sakafu huku damu zikmtoka tumboni.
Mama Diana alinigeukia baada ya kusikia mlango ukifunguliwa. Uso wake ulijawa na hofu ya kile alichokifanya kwa Devotha. Kabla sijanyanyua mdomo alinielekezea mdomo wa bastora na kufyatu risasi.
Nilizinduka nikiwa nahema sana. Kumbe ilikuwa ni ndoto baada ya kuzimia kutokana na kubebwa na maji. Pembeni yangu alikuwepo kasima Mzee mmoja wa makamo. Alinisimulia jinsi walivyoniokota usiku ukingoni mwa mto. Sasa nilikumbuka kila kitu baada ya ile ndoto. Nilikumbuka kilichokuwa kimenipata mpaka kufikia kutupwa msituni nikidhaniwa nimekufa. Ni Mama Diana ndiye chanzo cha yote. Yeye ndiye aliyenionjesha mdomo wa kuzimu kwa penzi lake tamu lisiloelezeka. Alinihudumia kwa kunipa pesa za mavazi, chakula pamoja na kunipa gari la kutembelea. Yote hayo aliyafanya kwa siri kubwa bila mume wake kujua lakini yule aliyesema hakuna marefu yasiyo na ncha hakukurupuka. Kwani alizaliwa na mhenga aliyesema siku ya mwizi ni arobaini.
Hapa ninapozungumza ni kuwa nina kilema cha mguu wa kushoto Kwa kupenda Ganda la ndizi kuteleza.
Niite Joka Jeusi
Fasihi huelimisha na kuonya jamii.
Ahsanteni.