Fursa yako ya mabadiliko. Luka 19:1-9

Denis1729

Member
Sep 9, 2021
34
109
Pale shauku ya kutaka kubadilika inapozaliwa ndani yako; unapokea roho ya kupambana na kila kilicho kinyume chako mpaka ukishinde. Hakuna chochote kinachoweza kushindana na mwanaume au mwanamke anayeongozwa na shauku ya mabadiliko, shauku ya mabadiriko ni shauku ya ushindi.

Zakayo alikuwa na shauku ya kutaka kubadilika, Mtu aliyekuwa na jina,
cheo na utajiri, lakini anatafuta kumwona Yesu na kumjua yeye
Lakini hakuweza kumwona Yesu kutokana na watu kuwa wengi, pamoja na ufupi wake.

Pale tu kiu na shauku ya kutaka kubadilika inapozaliwa ndani mwako ndipo vikwazo vitaanza kuzungumza na wewe, Lengo kuu ni kukuvunja moyo na kukuzuia usichukue hatua yoyote,
Sauti ya vikwazo vyako haitadanganya
itasema kweli kukuhusu wewe.

Lengo la vikwazo siyo kukuzuia usifikie malengo yako, bali kukufanya ugundue madhaifu yako na mapungufu ili ujue wapi pa kurekebisha katika maisha yako.

VIKWAZO VINAKUFUNUA WEWE KWAKO MWENYEWE
Zakayo aligundua kwamba hawezi kumwona Yesu na kumjua kama alivyotarajia, lakini hakukata tamaa licha ya vikwazo vyake.

Baadhi ya watu wanapokutana na vikwazo wanakaa chini na kuanza
kulalamika, kulaumu na kuwashutumu wengine, lakini watu wenye nia ya kubadilika hawatetereki mbele ya vikwazo, wanatafuta njia ya kutokea.

Zakayo hakukaa chini na kuanza kulalamika kwa sababu ya wingi wa
watu au ufupi wake, alitafuta njia ya kuitimiza ndoto yake. Biblia inasema alikimbia mbele na kupanda juu ya mti wa mkuyu ili kumwona Yesu. Mti huu wa mkuyu haukuwa pale kwa bahati mbaya, ulikuwa kimkakati na kinabii katika eneo hilo ili kumpa suluhisho Zakayo.

Mti wa mkuyu ulikusudiwa kumpa njia Zakayo ya kutoka katika changamoto yake, Mara zote katika kila tatizo na vikwazo huwa kuna njia ya kutokea,
lakini inahitaji mtu mwenye shauku ya kutaka kubadilika ili kuipata njia hiyo.

KAMATA POINTI HII
Usizungushwe na sauti ya vikwazo vyako, tafuta njia aliyoitoa Mungu, Usikate tama unapokutana na vikwazo hivyo, shauku ya kubadirika ni
shauku ya kushinda.

Pambana mpaka ushinde, mpaka uone badiliko, Unaposhinda vikwazo vyako unajiweka katika nafasi ya kutokuhitaji
kupambana ili umwone yeye, badala yake Yeye atakuwa wa kwanza
kukuona wewe kabla hujamuona.

Zakayo alihitaji kumuona Yesu, lakini baada ya kupambana na kushinda vikwazo, Yesu alianza kumuona yeye. Yesu alimwambia ashuke haraka toka juu ya mti kwa kuwa alihitaji kufika nyumbani kwake.

USIWAPE NAFASI WAPINZANI WAKO KUKUZUIA
Pale tu alipochukua nafasi ya kwenda kumiliki ushindi wake, mambo yaliyopita yalianza kuzungumza. Mara zote unaposhinda ushawishi wa
vikwazo vyako, historia yako itaanza kuzungumza.

Watu walianza kumsema vibaya wakisema kuwa Yesu ameenda kuwa mgeni wa mtu mwenye dhambi, Walishikilia maisha yake yaliyopita.

Pale watu na shetani wanaposhindwa kukuzuia usitimize malengo yako kupitia sauti ya vikwazo vyako, wanaanza kukazia makosa yako ya nyuma ili kukuvunja moyo na kukufanya usiweze kuifikia hatima yako.

Usiruhusu historia yako au makosa yako yaliyopita kukufanya kutotafuta kubadilika, Kila mtu anayo mambo yake yaliyopita lakini utukufu kwa Mungu yeye ameshashughurika nayo pale msalabani
AMEN.
 
Back
Top Bottom