Fursa na vikwazo katika maridhiano kati ya Mbowe na Ikulu

USSR

JF-Expert Member
Jul 15, 2015
9,896
22,664
Fursa na vikwazo katika maridhiano ya kisiasa Tanzania

Kuna msemo unaohusishwa sana na mchezaji mashuhuri wa mchezo wa besiboli nchini Marekani, Lawrence “Yogi” Berra kwamba “ni vigumu kubashiri hasa kwa mambo yajayo”. Nimekumbuka kauli hii mara baada ya mkutano uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam baina ya Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa hapa nchini.

Katika mkutano huo, mambo makubwa matatu ndiyo yamejadiliwa zaidi na wadau. Mosi ni ruhusa ya kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa, pili ni ahadi ya kufanywa kwa marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusu masuala ya kisiasa na tatu ni kuhusu ahadi ya kuukwamua mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Tanzania.

Ni muhimu kufahamu kwamba katika mambo hayo matatu, mawili – kuruhusu mikutano ya kisiasa na kubadili sheria, ni mepesi lakini suala la mchakato wa Katiba ndilo ambalo naliona litabeba nafasi kubwa ya mijadala kuanzia sasa.

Suala la kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa ni suala ambalo halikuwa na msingi wa kisheria bali ni uamuzi uliochukuliwa na serikali ya Rais John Magufuli. Katiba na sheria zilizopo hazikuwahi kukataza mikutano na ndiyo sababu hadi sasa sababu za kuizuia zilikuwa zikitofautiana kuanzia tishio la ugaidi, ukosefu wa askari wa kutosha, kuingiliana na shughuli nyingine na sababu nyingine lukuki.

Kwa sababu hiyo, uamuzi wa kurejesha mikutano hiyo lilikuwa ni la utashi tu wa kisiasa na Rais Samia ametumia utashi wake kurejesha jambo hilo. Ukiangalia suala la marekebisho ya sheria mbalimbali, utaona kwamba kwa sehemu kubwa baadhi ya masuala yalijadiliwa sana wakati mchakato wa maoni ya kutafuta Katiba kupitia Tume ya Jaji Warioba.

Kilichokwamisha kukubaliwa kwa mambo hayo kulikuwa ni suala moja tu la muundo wa Muungano. Hadi sasa, hili ni suala linalogawanya hisia za wengi ingawa Tume ya Warioba ilikuja na mapendekezo ya Serikali Tatu ikieleza ndiyo tafsiri yao ya maoni ya wananchi. Ripoti ilionyesha kwamba ingawa kwa wingi Watanzania wangependa kuendelea na mfumo wa Serikali mbili lakini mahitaji wanayotaka yangeweza tu kutimizwa kupitia mfumo wa Serikali tatu na si mbili.

Wajumbe wa Bunge la Katiba walikubaliana katika mapendekezo mengi ya Tume ya Jaji Warioba ikiwamo mengi ya mabadiliko ya sheria yaliyopendekezwa na wadau kupitia Kikosi Kazi kilichoundwa na Rais Samia. Mijadala mingi kuhusu sheria hizo ilishafanyika tayari na haitarajiwi kwamba kutakuwa na shida kwenye utekelezaji wake.

Rais Samia aliingia madarakani kufuatia kifo cha ghafla cha Rais Magufuli ambaye staili yake ya uongozi ilikuwa tofauti na watangulizi wake wote tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini. Yeye hakuamini katika siasa za ushindani na hadi wakati anafariki dunia, Tanzania ilikuwa imerudi nyuma katika vigezo vyote vya masuala ya demokrasia na utawala bora.

Rais Samia alikuwa na uamuzi wa ama kuendeleza pale alipoachia Magufuli au kufanya mabadiliko kuirejesha Tanzania walau kufikia mahali ilipokuwa kidemokrasia kabla ya urais wa Magufuli. Ingawa hajawahi kutoa kauli yoyote ya kumsema vibaya mtangulizi wake, dalili zinaonyesha kuwa Rais huyu wa kwanza mwanamke ameamua kufuata njia ya demokrasia.

Katika uchambuzi wake wa nini hasa kilisababisha Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789, Alexis de Tocquiville, alisema sababu kubwa ilikuwa ni utawala mpya kuja na mabadiliko makubwa mengi ndani ya muda mfupi. Wachambuzi mbalimbali wanakubaliana pia kwamba Mikhail Gorbachev aliiangusha Urusi kwa sababu mabadiliko yake ya Perestroika na Glasnot ingawa yalikuwa muhimu, yalifanywa kwa haraka na kwa kipindi kifupi.

Uzoefu huu unaonyesha kwamba wakati wa hatari zaidi kwa utawala ulio madarakani ni kipindi kile kifupi kati ya kuondoka madarakani kwa Rais aliyetawala kwa mkono wa chuma na Rais/mtawala mpya, anayetaka kubadilisha mambo ya mtangulizi wake kwa kiasi kikubwa na kwa wakati mfupi.

Pengine hilo ndilo somo ambalo Rais Samia amejifunza na ndiyo sababu mabadiliko yake yanakwenda hatua kwa hatua na si kwa haraka kama ambavyo baadhi ya wakosoaji wake wangetaka. Kuna jambo lingine ambalo amelifanya linalomtofautisha na baadhi ya wafuasi wake.

Kwenye mazungumzo ya Mwafaka wa Zanzibar uliosababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka 2010, kulikuwa na maneno kwamba Rais Amani Karume hakuhusisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) ipasavyo hasa visiwani Zanzibar. Matokeo ya Kura ya Maoni ya Maridhiano yalionyesha kwamba maeneo yanayofahamika kama ngome ya CCM, wanachama hawakuunga mkono mwafaka huo na ndiyo sababu bado unaonekana kusuasua.

Kulikuwa na maelezo pia kwamba mchakato wa kutafuta Katiba Mpya ya Tanzania ulipoanzishwa na Rais Jakaya Kikwete, hakukuwa pia na baraka za chama chake na ndiyo sababu mchakato huo ulikwama mwishoni kwa sababu hiyo.

Rais Samia inaonekana anahusisha chama chake kwenye mchakato mzima. Katika picha zilizosambazwa wiki kazaa na Ikulu, alionekana akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana. Hata kwenye hotuba yake, Rais alieleza namna Kinana alivyoshiriki kikamilifu kwenye mazungumzo ya kuwarejesha mezani CHADEMA.

Zanzibar ambako ACT Wazalendo ndicho chama kikuu cha upinzani, kuliundwa kamati nyingine- kwa maelekezo yake, kwa lengo la kushirikiana na CCM kutafuta maridhiano ya pande zote kama ambavyo Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alivyokuwa sehemu ya mazungumzo Tanzania Bara. Kama CCM ilikuwa haitaki maridhiano katika miaka iliyopita kwa sababu haikuwa ikishirikishwa kikamilifu, staili ya Rais Samia inaondoa doa hilo.

Katiba itakuwa mfupa mgumu

Kihistoria, suala la kuwa na Katiba Mpya, halikuwahi kuwa kipaumbele cha Rais yeyote wa Tanzania aliye madarakani katika awamu yake ya kwanza. Rais Benjamin Mkapa aliahidi kupambana na rushwa, Kikwete akaahidi kasi na ari mpya kwenye kutafuta maendeleo na Magufuli aliahidi kuchapa kazi zaidi.

Sababu kubwa mbili zimesababisha presha kubwa kwa Samia kuleta Katiba mpya kuanzia awamu yake ya kwanza. Mosi ni kwa sababu mchakato ulikuwa umeanza tayari na kufikia hatua karibu na mwisho kabla ya kuwekwa pembeni na mtangulizi wake na pili ni kwa sababu ya madhila waliyopitia Watanzania wakati wa utawala wa Magufuli na Katiba inaonekana kama inaweza kusaidia watu kupata haki zao kuliko ilivyo sasa.

Samia anaelezwa kuwa Rais anayefanya mambo yake baada ya kusikiliza pande zote za shilingi. Kimsingi, wakati alipokuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, sifa yake kubwa ilikuwa ni uwezo wa kusikiliza majadiliano makali bila kuingilia na anapozungumza kuja na hoja inayopita katikati ya mwafaka wa mazungumzo.

Yeye ni Mzanzibari na inaonekana wengi wa Wazanzibari wana shida na aina ya muundo wa Muungano uliopo sasa. Yeye pia ni mwana CCM kindakindaki na kwa chama hicho Muungano wa Serikali mbili ni mojawapo ya hiba (legacy) zake kubwa na haionekani kama yupo mwana CCM mwenye hamu ya kutambulika kama Mwenyekiti aliyesababisha kuvunjika kwa Muungano wa Tanzania. Ni heshima isiyotakiwa kama ilivyo kwa Gorbachev anayeonekana kama Rais aliyeivunja Urusi.

Kwenye mkutano wake , aligusia kidogo kuhusu yapi yanaweza kutokea kwenye mchakato wa Katiba – kuanzia uwezekano wa kumalizia ‘kiporo’ cha mwaka 2014 au kuunda timu itakayotazama mahali mchakato ulipo na kutengeneza njia mpya.

Pasi na shaka, suala la Katiba Mpya ndilo litakuwa gumu zaidi na lenye vikwazo. Itategemea zaidi, muhimu kuliko vyote, nini kinatakiwa zaidi na CCM na upande utakaokuja na hoja nzito zaidi kuhusu mustakabali wa Tanzania kama nchi kufuatia mabadiliko hayo ya Katiba.

Wakati muhimu zaidi wa kupima na kung’amua mwelekeo unaotakiwa ni kipindi cha kati ya sasa na mwaka 2025 wakati kila mmoja – hata wapinzani wake kisiasa, wakiwa wanamwamini kwa sababu ya yale ambayo kayafanya sasa.

Nikiazima maneno ya Yogi niliyoyanukuu mwanzoni mwa uchambuzi huu, kama hatujui nini kiko vichwani na mioyoni mwa vigogo wa CCM kwa sasa, ni vigumu kubashiri nini hasa kitatokea miaka miwili au mitatu ijayo.
 
Back
Top Bottom