Wale wadukuzi mnaohangaika kudukua mawasiliano yetu ya simu kwenye mitandao ya simu ili Mtukufu Mfalme Nebukadreza awasifu na kuwatoa majalalani kisha kuwaweka chini ya meza yake ili awalishe makombo acheni kutumika vibaya kwa ujira wa makombo. Acheni huo UJINGA na unyani, Changamkieni tenda hii kama ninyi ni wadukuzi kweli.
Kampuni ya Apple imetangaza kutoa zawadi shilingi za Tanzania Bilioni 2.3 sawa na dola za Marekani milioni 1 kwa taasisi, kampuni au mtu yeyote atakayeweza kudukua simu za iPhone au kompyuta za Mac, ikiwa ni ongezeko kutoka TZS 460 milioni za awali. Apple imeongeza dau hilo kutokana na wadukuzi kuuza taarifa hizo kwa serikali kwa gharama kubwa zaidi. Tangu Apple watangaze kandarasi hiyo hakuna mdukuzi ambaye ameshafanikiwa kudukua simu ya iPhone, iPad wala Mac OS.
Utakumbuka kuwa December 2015 eneo la San Bernardino, Syed Rizwan Farook na mkewe walifanya shambulio la kigaidi kwa kutumia bunduki na kuwaua zaidi ya watu 14 katika jimbo la California na kisha wao wenyewe kujiua. Baada ya shambulio hilo Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI) walifanikiwa kupata simu ya mshambuliaji huyo iliyotengenezwa na kampuni ya Apple toleo la iPhone 5c. Baada ya FBI kupata simu hiyo wakajaribu kuidukua wakagonga mwamba kutokana na umahiri wa program za simu na vifaa vya kielektroniki vya Apple ikiwemo iPhone.
Farook katika simu yake hiyo alikuwa ameweka pass code (nambari za siri) zenye tarakimu 4 na aliwezesha mfumo wa simu hiyo kufuta data zote zilizomo kwenye simu hiyo ikiwa utakosea kuingiza passcodes mara 10 hapo ndipo FBI walipoishiwa ujanja kabisa.
FBI ikabidi wawashurutishe Apple kufungua simu ya Farook, Apple wakakataa na kuwaambia hawawezi kutoa wala kuingilia faragha za wateja wake jambo ambalo lingewaathiri kibiashara endapo wateja wake wangepoteza imani na Apple na kuhisi kwamba taarifa zao hazipo mikono salama.
Majibizano makali yaliendelea kati ya serikali ya Marekani na kampuni ya Teknolojia ya Apple, baada ya kampuni hiyo kukataa kuisaidia FBI kufungua simu ya mmoja wa washambuliaji waliowauawa watu kwa kuwapiga risasi mwezi Disemba 2015.
Idara ya sheria iliwasilisha ombi Mahakamani ikisema simu ya mshambuliaji huyo huenda ina ushahidi zaidi kuhusu shambulio hilo.
Kampuni hiyo iliendelea kukaidi matakwa ya FBI na serikali ya Marekani ikijitetea na kusema kuwa shirika la ujasusi la FBI linatumia njia za mkato ili kuweza kupata mbinu za kudukua simu zote za wateja wa iPhone kwa kutumia kisingizio cha simu moja ya iPhone ya Farook.
Mapambano ya Kisheria kati ya Taasisi ya Uchunguzi nchini Marekani(FBI) na Kampuni ya uzalishaji wa vifaa vya kieletroniki zikiwemo simu za mkononi Apple yakashika kasi zaidi mahakamani.
FBI ikazidi kuishurutisha Apple kupatiwa taarifa za siri zilizokuwa kwenye simu ya muuaji, Syed Farook aliyewaua kwa risasi watu 14 katika eneo la San Bernardino Desemba 2015.
Katika sakata hilo Jaji aliitaka Kampuni ya Apple kuipatia FBI na mamlaka zote ushirikiano wa kutosha, ambapo Apple walitakiwa kufungua mfumo unaoifunga simu baada ya kufanya majaribio 10 ya kuingiza pass code bila mafanikio.
Apple waligomea agizo hilo la Mahakama na ndipo mabishano ya kisheria yaliposhika kasi. Hapa ilikuwa ni Sheria kwa Sheria, kifungu kwa kifungu na hoja kwa hoja hakuna kutishana, kupeana kesi ya uchochezi, kutekana wala kupewa kesi ya ukwepaji kodi ili kukunyamazisha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Apple, Tim Cook alisema agizo hilo halikubaliki na kama wakiwapatia FBI uwezo wa kuiingilia simu hiyo ya Syed Farook basi FBI hawatashindwa kuziingilia simu nyingine zote za wateja wao. FBI waliendelea kushikilia msimamo wao wa kupatiwa taarifa hizo.
Mkurugenzi huyo akaongeza kuwa sifa muhimu inayoifanya Apple kupendwa licha ya gharama yake kuwa kubwa ni uwezo wake wa ulinzi mkali dhidi ya wadukuzi tofauti na makampuni mengine ya kuunda simu. Hivyo kama watakubali upuuzi wa FBI watakuwa wamepoteza sifa hiyo na hawatokuwa na tofauti na simu zingine jambo ambalo litawaathiri kibiashara.
Apple pia wamewahi kukataa simu ya mteja wake mwingine isidukuliwe. Mahakama ya New York iliwahi kutangaza kukataliwa kwa ombi la kutaka Apple kufungua simu ya iPhone iliyokuwa ikimilikiwa na mlanguzi wa madawa ya kulevya.
Jaji mkuu wa mahakama hiyo James Orenstein alitoa maelezo na kuarifu kwamba serikali ya Marekani haina mamlaka ya kulazimisha uamuzi kama huo bila ya idhini ya kampuni husika ya Apple.
Simu hiyo ya iPhone inashukiwa kuwa na data za siri zinazoweza kusaidia kesi inayoendelea kuhusiana na ulanguzi wa madawa ya kulevya na Apple wamesema abadani asilani hawawezi kuwa sehemu ya kudukua taarifa za wateja wao.
Baada ya mapambano hayo ya Apple na FBI, hatimaye serikali ya Marekani iliamua kutumia mtu wa tatu(Third Party) ili aweze kuingilia simu ya muuaji Syed Farouk na kupata taarifa.
Katika sakata hilo John McAfee mkuu wa kitengo cha kutengeneza ulinzi (Antivirus and software security) kwenye software za kampuni ya McAfee akataka kuonesha umwamba wake wa udukuzi ili kuisaidia FBI kufungua simu hiyo ya Apple ambayo ni iPhone 5c iliyokuwa na passcode. Akajaribu akaangukia pua.
Taarifa ambazo sio rasmi zinasema kuwa hatimaye FBI waliipa kandarasi kampuni ya Israel Cellebrite ambayo ni washirika na Japan kazi hiyo ya kuiingilia simu ya Syed Farouk. Hata hivyo hadi leo FBI hawajawahi kusema ikiwa wakifanikiwa kufanya udukuzi huo. Ila duru zinaarifu kuwa kampuni hiyo ya Israel ilifanikisha udukuzi huo.
Baada ya sakata hilo kampuni hii ya Apple ikaandaa simu isiyoweza kudukuliwa au kupekuliwa na mtu yeyote, Shirika la ujasusi au Serikali yoyote ile duniani. Apple tayari wamefanikisha hilo kwa kuwezesha watumiaji wa iPhone kuzima mfumo wa kuiwezesha iPhone kuwasiliana na computer ambayo ndio njia wadukuzi wa Israel waliitumia kuunganisha simu hiyo na computer iliyokuwa na program maalumu ya udukuzi. Hivyo sasa mtumiaji wa iPhone asipoiruhusu simu yake kuwasiliana na computer mdukuzi hana ujanja mwingine.
Kama hiyo haitoshi teknolojia ya kutumia alama ya Vidole (Fingerprint) katika simu za Apple (iPhone) zina uwezo wa kugundua vidole vya mtu aliyekufa na aliye hai tofauti na makampuni mengine yanayotumia teknolojia ya fingerprints.
Hivyo endapo mtumiaji wa simu akafariki au kuuawa, vidole vyake havitakuwa na uwezo tena wa kufungua simu yake tena.
Makampuni mengine mengi ya kielectroniki na simu hayana teknolojia. Mfano mzuri ni wakati wa uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka 2017 ambapo Mkurugenzi wa kitengo cha Information Technology (IT) cha tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), Christopher Msando alipotakiwa na maharamia kushirikiana nao ili waibe kura za Mgombea Urais kutoka Muungano wa Upinzani (NASA) Raila Odinga alidinda kufanya usaliti na wizi wa Kura ndiposa maharamia walipomteka, kumuua na kisha kukata kidole chake ambacho walikitumia kufungulia na kuingilia (kudukua) mifumo ya kuchakata kura na hatimaye kufanikisha wizi wa Kura uliompa Uhuru Kenyatta ushindi. Matokeo ambayo yalipingwa mahakama ya juu na kisha Mahakama kufutilia mbali uchaguzi huo na kuamuru urudiwe.
Udukuzi kama huo kwa kutumia vidole vya mtu aliyekufa hauwezekani kwa vyovyote vile kwenye vifaa vya kampuni ya Apple iwe ni simu zao za iPhone, iPad au Mac na vinginevyo.
USHAURI
Kama wewe ni mtumiaji wa simu hapa nchini kwa sasa kuwa makini sana na kile unaçhowasilia kupitia simu. Kama una mazungumzo nyeti omba physical appointment na mhusika mfanye mazungumzo ya ana kwa ana. Epuka kupiga simu au kutuma SMS kuhusu jambo nyeti.
Pendelea kupiga simu kutuma ujumbe wa maandishi kwa kwa kutumia program salama zaidi kama Telegram, WhatsApp na Skype miongoni mwa nyingine ambazo server zake ziko ughaibuni kwenye nchi zinazoheshimu haki ya faragha na taarifa za wateja wao. Program hizi ni salama zaidi kwa kuwa zina kile kinachoitwa end to end encryption. Hivyo hakuna mtu wa tatu "third party" au kinyamkera yeyote mwenye uwezo wa kuingilia mawasiliano yako.
Kama wewe sio mtumiaji wa vifaa vya Apple kama iPhone, iPad, miongoni mwa vifaa vyao vingine kama laptop epuka kuhifadhi taarifa nyeti katika simu yako ya kampuni nyinginezo. Zitadukuliwa kwa urahisi sana na wadukuzi.
Hakikisha huwezeshi location service kwenye simu yako bila sababu maalumu.
Hakikisha simu, laptop, memory card, sim card na vifaa vyako vyote vina password au pass code ngumu zisizofanana na unashauriwa kuzibadili angalau kila baada ya wiki moja na ukishindwa basi jitahidi sana kila baada ya mwezi mmoja.
Hakikisha program unazotumia kama Telegram, WhatsApp, Facebook n.k. zina security ya kutosha.
Usimuamini sana mtu wa pili unayezungumza naye hususani katika sensitive issues. Wadukuzi wakishindwa kudukua mawasiliano yako wanaweza kutumia watu wako wa karibu kunasa mazungumzo yako iwe ni kwa kukurekodi au au ku screenshot mazungumzo yenu. Ndio maana huwasisitiza watu kutumia telegram kupitia kipengele cha secret chat.
Kwa maelezo haya nadhani unaweza kuchagua aina na njia za mawasiliano ambazo zitakusaidia katika nchi ambayo UTU, HAKI za faragha na taarifa za mteja haziheshimiwi. Hii ni pamoja na kuchagua kampuni la simu linalojali faragha na taarifa za mteja wake. Sikuambii cha kufanya, jiongeze.
Usingoje kulindwa. Jilinde kabla ya kulindwa.