Matokeo kidato cha sita: Wasichana waendelea kushika rekodi
*Kifungilo,Kibosho,Mzumbe, Kilosa vinara
*Potatlal, Maswa, Fidel Castro,Esacs zavuta mkia
Reuben Kagaruki na Said Mwishehe
BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika Februari mwaka huu, ambapo wasichana wameongoza tena kwa kufanya vizuri kuliko wavulana.
Akitangaza matokeo hayo Dar es Salaam jana Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Joyce Ndalichako, alisema ingawa idadi ya wasichana waliofanya mtihani ni ndogo, ikilinganishwa na wavulana, bado wameweza kufanya vizuri hali inayodhihirisha kuwa wakiongezeka watakuwa na nafasi ya kuwazidi wavulana.
Alisema kati ya watahiniwa 47,464 waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni watahiniwa 45,054 waliofanya mtihani. Alisema wanafunzi wa kike waliofaulu ni 14,426 na wavulana ni 25,496 kati ya wote waliofanya mtihani.
"Takwimu hizi zinaonesha kuwa japo wasichana ni wachache lakini wamefanya vizuri kuliko wavulana ingawa idadi yao ni ndogo," alisema Dkt. Ndalichako.
Kuhusu ubora wa kufaulu kwa kuangalia madaraja, alisema takwimu za mwaka huu zinaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 23,415 wamefaulu katika ngazi ya daraja la kwanza hadi la tatu.
Wasichana waliofaulu katika madaraja hayo ni 8,603 na wavulana ni 14.812. Kutokana na matokeo hayo alisema idadi ya wanafunzi waliofaulu kwa madaraja hayo kwa mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 5.83.
Aliongeza kuwa idadi ya watahiniwa katika shule za serikali waliofaulu mtihani huo mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 5.42 huku asilimia ya walioshindwa ikiwa imeshuka kwa asilimia 1.03.
Kwa upande wa shule za Jumuiya alisema kiwango cha kufaulu katika madaraja hayo kimeongezeka kutoka asilimia 57.21 hadi asilimia 71.55 wakati asilimia ya watahiniwa walioshindwa imeshuka kwa asilimia 7.09 kutoka aslimia 13.70 ya mwaka jana
Katika shule za binafsi alisema kiwango cha ufaulu katika madaraja hayo kimeongezeka kwa asilimia 5.03, wakati kiwango cha walioshindwa kimepungua kwa asilimia 0.16 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana.
Pia alisema kiwango cha kufaulu katika shule za seminari katika madaraja hayo kimeongezeka kwa asilimia 0.72 wakati kiwango cha walioshindwa ikipungua kwa asilimia 0.58.
Alisema kiwango cha kufaulu katika shule za Zanzibar kwa madaraja hayo kimepungua kwa asilimia 0.78. Kiwango cha walioshindwa kimepungua kwa asilimia 3.62.
Kwa upande wa shule bora kuanzia zenye watainiwa 25 na kuendelea ambazo idadi yake ni 264, Dkt. Ndalichako alisema Kifungilo ya mkoani Tanga ndio imeoongoza ikifuatiwa na shule ya wasichana Kibosho (Kilimanjaro) na Mzumbe na Kilosa zote za Morogoro.
Nyingine ni Sanu Seminari (Manyara), Maua Seminari (Kilimanjaro), Uru Seminari (Kilimanjaro) Swilla (Mbeya) shule ya wasichana Marian (Pwani) na Nyegezi Seminari (Mwanza).
Kwa upande wa shule kumi za mwisho katika kundi hilo na mikoa zilipo kwenye mabano ni, Popatla (Tanga), shule ya wasichana Maswa (Shinyanga),Fidel Castro (Pemba), Esacs (Dares Salaam), Muslim College na Zanzibar Commercial zote za Zanzibar.
Zingine ni Lake (Mwanza),Rungwe (Mbeya)Ifunda (Iringa) na Shamiani (Pemba). Shule kumi bora zenye watahiniwa chini ya 25 kundi hilo limeongozwa kwa kiwango kikubwa na shule za seminari.
Shule 10 bora katika kundi hilo na mikoa zilipo kwenye mabano ni St. Jemes Kilema seminari (Kilimanjaro), Kaengesa seminari (Rukwa), St. Joseph Kilocha seminari (Iringa)Dungunyi seminari(Singida),Likonde seminari (Ruvuma), Boabab (Pwani), Kaisho (Kagera), Hagafilo (Iringa), Katoke Seminari (Kagera) na Bangala Lutheran Junior (Tanga).
Shule za mwisho katika kundi hilo, Dkt. Ndalichako alizitaja kuwa ni Tweyambe ( Kagera), Mvumi (Dodoma)Dodoma Central (Dodoma), Mount Kilimanjaro (Kilimanjaro), Sunni Madressa (Zanzibar), Besha (Tanga), Dongobesh (Manyara) Arusha Modern (Arusha)EDP Royal (Dar es Salaam) na Mairiva (Arusha.).
Kwa upande wasichana kumi bora na shule watokazo kwenye mabano , Dkt. Ndalichako aliwataja kuwa ni Lulu Edward (Marian), Noelah Lugongo (Mbeya),Wema Kessi (Marian), Haika Malleko (Jangwani)Mercy John (Weruweru),Florencia Kimario (Marian),Zahara Nagri (Shaban Robert), Matilda Kululetera (Marian), Isabela Matandiko (St. Methew) na Jebby Gonza (Kifungilo).
Walioongoza kwa upande wa wavulana katika kundi la kumi bora, Dkt. Ndalichako aliwataja kuwa ni Hussen Hamedu (Feza wavulana), Hajjy Abdul (Mpwapwa), Ibrahimu Shafi (Feza wavulana), Abraham Ambise (Mzumbe), Amani Mwazela (Ilboru),Quizelimana Bwenge (Mzumbe)Dominic Mwita (Pugu)Samson Mwita (Mwenge), Christian Charles (Kibaha) na Ilago Mabelya (Mzumbe).
Alitaja wanafunzi kumi bora katika makundi yote kuwa ni Huseen Hamidu (Feza) huku nafasi ya pili na ya tatu zikishikiliwa na wasichana ambao ni Lulu Edward (Marian) na Noelah Lugongo (Mbeya).
Nafasi ya nne imechukuliwa na Haji Abdul (Mpwapwa) huku msichana mwingine, Wema Kessy (Marian) akijitokeza kushika nafasi ya tano.
Wengine ni Ibrahimu Shafi (Feza wavulana), Abraham Ambise (Mzumbe), Amani Mwazela (Ilboru),Quizelimana Bwenge (Mzumbe)Dominick Mwita.
Alisema NECTA imefuta matokeo ya wanafunzi 54 waliobainika kufanya udanganyifu kati yao 49 ni wa kujitegemea na watano wa shule.
Mbali na hiyo alisema NECTA imesitisha kutoa matokeo ya wanafunzi 170 ambao hawajalipa ada ya mtihani. Alisema baraza limesitisha kutoa matokeo ya watahiniwa wanne wa shule ya Rosemaria kutokana na mkuu wa shule hiyo kutolipa ada ya watahiniwa pungufu ya 25 hivyo yatatolewa baada ya ada hiyo kulipwa.
Katika hatua nyingine, Dkt.Ndalichako alitangaza matokeo ya wanafunzi waliofanya mtihani wa stashahada ya ualimu ambapo watahiniwa 3,282 sawa na asilimi 90.19 kati ya 3,639 wamefaulu masomo yao yote huku wengine 335 wakishindwa baadhi ya masomo hivyo wanatakiwa kurudia. Alisema watahiniwa 22 hawakufaulu kabisa.
majira