Wako wapi wale 'wachambuzi mahiri' wa soka walioshutumu, kudhihaki na kudhalilisha hatua za Yanga kumsajili Okwi? Ina maana zile hoja zao zote zilikuwa ni uchwara na batili? Walikiamini walichokuwa wakikiandika, waliandika ili kuvutia wasomaji, au waliandika kutokana na ushabiki wao tu dhidi ya Yanga? Mojawapo ya lolote kati ya hayo, maana yake ni kwamba tunalazimika kutokubaliana tena na uchambuzi wao ujao.
Wako wapi wale wanaosifiwa kwa kujua 'fitna za mpira' waliotoa viapo vinavyokaribiana na vya kufukua makaburi ya wapendwa wao iwapo Okwi angeichezea Yanga msimu huu? Ina maana vile viapo vyao vyote vilikuwa ni vya mdomoni tu, au waliamini walichokuwa wakikiapia? Maana yake ni kwamba hawataaminika tena mbele ya waliokariri viapo vyao, hasa wanachama, wapenzi na washabiki wa timu yao (ingawa hii si mara ya kwanza).
Wako wapi wale waliolumbana kwenye JF kwa kebehi na kejeli dhidi ya hoja zetu sahihi kwamba swala la Okwi kuichezea Yanga halihusiani hata kidogo na uhamisho wake wa Villa wala na madeni ya Simba kwa Etoile, kama vile kusivyokuwa na uhusano baina ya kisiki alichojikwaa mwendaji wa miguu na mahali alikoangukia? Maana yake ni kwamba kuna tofauti baina ya malumbano na mjadala. Mjadala hautumii fikira za utashi (wishful thinking) wa mtu, bali uhalisia wenye malengo (objective facts). Inshalla watajirudi kwenye mijadala ijayo ili isigeuke kuwa malumbano.
Wako wapi wale waliosema kwa vinywa vipana kwamba kulikuwa na mchezo mchafu kwenye swala zima la uhamisho wa Okwi kwenda Yanga, licha ya hoja bayana na mifano timamu kutoka kwa wahusika ambao bila ya shaka wana uelewa zaidi na kwa hivyo ndio wa kuaminiwa kuhusu swala hili kuliko wababaishaji wetu waliojivika majoho ya weledi wa mambo waliyoyadandia ukibwani ili kuganga njaa zao?
Yote kwa yote, tujifunze kupima ukweli wa mambo kwa uzito wa hoja zitolewazo na si kwa ukubwa wa vinywa (midomo) vya watoa hoja.