[emoji3586]ASIYE BAHATI HABAHATIKI[emoji3586]

mpasta

JF-Expert Member
Jan 17, 2011
917
1,997
Nimemaliza kusoma kitabu cha mchezo wa kuigiza, kinachoitwa "Aliyeonja Pepo" kilichotungwa mwaka 1973 na mtunzi Farouk Topan, nikajikuta nakumbuka kisa cha kweli.maishani kilichomsibu Mzee flani, jina lake kapuni. Mzee huyo, yeye na mkewe wote ni Walalaheri. Wakajaaliwa kupata ghulamu wa kiume. Wakamsomesha mpaka elimu ya Chuo Kikuu, alipofika mwaka wa mwisho chuoni akafurushwa kwa sababu ya mgomo, hivyo akashindwa kuhitimu. Wazazi wake, wakapiga moyo konde, wakampeleka nchi ya ng'ambo kuanza upya kutabahari elimu ya juu. Alipofika mwaka wa mwisho wa masomo yake, akagundulika ni mahamumu wa kansa. Akatibiwa lakini haikufaa kitu aliporejea nchini, haikupita hata nusu mwaka, barobaro wao akatangulia jongomeo.. Ama kweli, kwenye maisha "asiye bahati habahatiki".

Kwenye igizo hili la "Aliyeonja Pepo", mhusika Mkuu ni mswahili, Bwana Juma Hamisi, muuza samaki katika soko la Bagamoyo. Huyu jamaa aliaga dunia kwa kupigwa dafrao na punda akiwa kwenye harakati zake za uchuuzi wa samaki. Kutokana na matendo yake mema aliyoyaishi hapa duniani ikapidi alipofika akhera aingizwe peponi kwenye pandikizi la jumba la anasa mbalimbali. Tahamaki ! kumbe alitolewa roho kimakosa, aliyetakiwa afe siku hiyo ni Mzungu mmoja anaitwa John Houghton anayeishi nchini Uingereza katika Mji wa Bournemouth. Bwana John ahadi yake ya kifo ilitakiwa apate ajali ya kumgonga farasi akiwa kwenye gari lake. Hivyo Malaika mtoza roho, Ziraili alipopitia vitabu vyake vya kumbukumbu ndipo akang'amua makosa yaliyofanywa na wasaidizi wake ya kumuacha hai Bwana John na kumfisha Bwana Juma. Ikabidi kikao kizito cha kujadili kosa hilo kiitishwe, mwisho likaja hitimisho la Bwana Juma atolewe Peponi arudishwe duniani kwa mara ya pili. Ghafla bin vuu Bwana Juma anatolewa kwenye jumba la starehe akiwa kwenye kilele cha starehe, amezungukwa na magashi wa Peponi anakula bata. Akapewa taarifa za yeye kuharakishwa kuletwa akhera kwa mwaka mmoja, hivyo akapewa chaguo la kurudi duniani kwa mwili wa mzungu Bwana John. Hapo ndipo kasheshe lilipoibuka, Bwana Hamisi akapinga waziwazi maamuzi ya yeye kurudishwa duniani. Akajitetea yeye Duniani alikuwa mtu swahilina, hajawahi kunywa mtindi kwa maana haijui ladha ya "John Walker" wala "Chibuku", hafugi mbwa na mengineyo, sasa akirudishwa duniani kwa umbile la mzungu itakuwa mtihani kwake na huenda asiipate tena Pepo.

Hoja zake Bwana Juma mbele ya Malaika zikaonekana zina mashiko hivyo ikaamriwa arudishwe duniani kwa umbile la paka mla shombo za samaki kwenye Soko la Bagamoyo. Hapo akaambiwa hamna kujitetea tena, anarudi duniani kwa umbile la paka, mjadala umefungwa. Wakati wapo njiani wanapaa mawinguni kurudi duniani akawa anaulizia sasa, nitaenda kuwa paka dume au paka jike?. Malaika wakaanguka kicheko hawakumjibu swali lake.

Fasihi andishi za zamani, zilizoandikwa na manguli kama akina Farouk Topan, Amandina Lihamba, Edwin Semzaba, Ndyanao Balisidya, Mobali Muba na wengineo ni tamu sana. Hiki kitabu nimekitafuta kwa miongo kadhaa bila kuchoka, mara ya mwisho nilikisoma nikiwa darasa la 4. Nimejaribu kuwapigia simu wadau wangu kadhaa mpaka nimefanikisha kukipata.

Heavy Metal (Retired Sheikh)
29/05/2023
 
Back
Top Bottom