SoC02 Elimu ya Upili Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

hellencaren

New Member
Aug 22, 2022
2
1
ELIMU YA UPILI TANZANIA

Elimu ni ujuzi na maarifa juu ya jambo fulani,inayomwezesha binadamu kupata uelewa juu ya dhana tofauti. Elimu ziko za aina mbalimbali,ila hugawanywa katika aina kuu mbili nazo ni, elimu rasmi na elimu isiyo rasmi. Elimu rasmi ni elimu inayowasilishwa katika taasisi mbalimbali yaani shule za awali, msingi, sekondari, vyuo vikuu pamoja na elimu maalum yenye kuongeza utaalamu wa kitaaluma mfano, marubani na madaktari. Elimu asili yaani isiyo rasmi ni elimu inayotolewa na jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine kulingana na utamaduni husika.

Elimu rasmi imegawanywa katika ngazi mbalimbali na ngazi moja wapo iliyo muhimu ni elimu ya upili yaani elimu ya sekondari. Elimu ya sekondari imegawanywa kwanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne. Walimu wa taasisi hii huratibisha masomo kama uraia, hisabati, biolojia, historia, kiingereza, fizikia, kemia na kiswahili. Elimu ya upili ina umuhimu mkubwa sana kwa kijana wa kitanzania nazo ni kama zifwatazo;

Kwanza, elimu huongeza ujuzi na maarifa: Kupitia elimu ya upili, mtu anaweza kupata habari au taarifa mbalimbali juu ya dhana tofauti kama, biolojia na uraia. Bila kuelimishwa binadamu hawezi kujua chochote, sehemu kubwa inayochangia ongezeko la maarifa na ujuzi ni kupitia elimu hii ya upili ambapo watu hujifunza juu ya masomo kama historia, kiingereza pamoja na kujifunza juu ya nchi yetu.

Vilevile,Ni njia ya kuboresha kiwango cha maisha: wengi katika jamii yetu,wameweza kufanikiwa kuwa na maisha bora yenye kiwango cha juu kwasababu ya elimu mbadala mfano marubani, madaktari, walimu na wabunge wamefanikiwa kupata elimu ya upili iliyowapelekea kufika ngazi za juu za elimu na hatimaye kutimiza ndoto zao.

Pamoja na hayo, elimu hii huleta maendeleo katika jamii: kupitia elimu ya upili, wanafunzi wanaweza kupata mwelekeo juu ya kazi na namna ya kutimiza ndoto zao. Elimu hii inawafikisha wanafunzi katika elimu maalamu ambayo husaidia kukidhi mahitaji ya jamii yetu kama wahandisi, walimu, wanasayansi na madaktari .Bila kupata elimu hii jamii hukosa watu walioelimika na hivyo hushindwa kusaidia jamii yetu ya Tanzania.

Hivyo, tunaona namna elimu ya upili ilivyo muhimu, serikali yetu ya Tanzania imejitahidi kuborsha elimu hii na kuhakikisha elimu inatolewa kwa ubora zaidi lakini bado elimu hii inakumbwa na changamoto mbalimbali hasa kwenye taasisi zinazoshughulika na elimu ya upili changamoto hizi ni kama zifuatazo;

Kwanza, mbinu hafifu za ufundishaji: nchi yetu bado inakiwango cha chini cha sayansi na teknolojia. Tatizo hili linakwamisha uwasilishaji wa elimu shuleni kwasababu shule nyingi hazina vifaa vya kisasa na vilivyobora vinavyoendana na teknolojia ya sasa mfano, shule nyingi hasa za serikali hawana tarakilishi, projekta ambazo hutumika sana katika jamii yetu ya sasa Pamoja na hayo, ufundishaji mashuleni sio wa vitendo kwa kiwango chake na hivyo hupelekea wanafunzi kutokuelewa vizuri zaidi na kuishia kukariri.

Pili, elimu yetu huzingatia masomo ya darasani kuliko shughuli zingine za ziada: Muda mrefu hutumika kufundisha darasani, wanafunzi wanakosa muda wa kushiriki katika mambo mbalimbali yanayohusiana n vipaji ili kuvikuza vipaji hivi pamoja na kupumzisha akili ya mwanafunzi, changamoto hii huanzia majumbani ambamo wazazi wengi hawawapi watoto nafasi ya kushiriki kwenye mambo yatakayowawezesha watoto kujenga vipaji kama; mashindano ya midahalo, mziki na uchoraji kulingana na vipaji vya watoto.

Tatu, tatizo la miundo mbinu na vifaa vya shule: shule nyingi hukosa vifaa vilivyo bora ili kusaidia kuelimisha wanafunzi vizuri. Hii ni changamoto kubwa kwani vifaa kama vitabu, maabara, maktaba huhitajika kwa hali na mali mashuleni. Suala la miundombinu pia hushusha ubora wa elimu kwani hupelekea shida tofauti mfano, matatizo ya kiafya kwa wanafunzi hasa shule nyingi vijijini hazina vyoo vya kutosha na hata madarasa ya kuhimili idadi ya wanafunzi hao madarasani.

Pia, umbali wa shule hasa vijijini: wanafunzi wanapata changamoto ya kutembea umbali mrefu kufika shule kwasababu shule ziko mbali na nyumbani .Hivyo hufika shule wakiwa wachovu na kwa kuchelewa. Pamoja na hili, usalama wa mwanafunzi unakuwa hatarini na hupelekea kesi kama za ubakaji, ulawiti, mauaji na ukatili kwa wanafunzi hawa.

Pamoja na hayo, walimu hafifu na haba mashuleni: shule zimekuwa zikiajiri walimu bila kuzingatia vigezo vya kuajiri kama kuwa na cheti cha ualimu na hivyo hupelekea wanafunzi kufundishwa na walimu wasio mahiri katika kazi hii na wasio na ujuzi mzuri. Changamoto hii hushusha ubora wa elimu inayowasilishwa kwa wanafunzi. Pia shule zingine hasa za serikali wanachangamoto ya kuwa na walimu haba kwasababu ya uajiri mdogo wa walimu na serikali pamoja na mishahara midogo isiyowatosheleza walimu hawa.

Pia, adhabu kali shuleni: shule nyingi zimekuwa hazizingatii ukali wa adhabu za kuwapa wanafunzi haswa kwenye adhabu ya fimbo. Adhabu zingine zinapingana na haki za binadamu na hupelekea mateso makali na hata kifo. Hali hii hufanya wanafunzi kuchukia shule, shule haswa za vijijini ni mifano hai za shule zenye hii changamoto ambapo wanafunzi hupewa adhabu kali inayo dhuru afya za wanafunzi, mfano, kifo cha mwanafunzi mmoja mkoani Kagera kwasababu ya kuchapwa fimbo nyingi na mwalimu wake .

Imani na tamaduni potofu: jamii yetu inakumbwa na tamaduni, mila na imani potofu zinazozuia watoto kwenda shuleni. Tamaduni hizi ni kama ndoa za utotoni ambamo wasichana na wavulana wanalazimishwa kuoa na kuolewa katika umri mdogo na kupelekea kuacha shule. Pia jamii zingine mfano wamaasai ,watoto huishia kufanya kazi za nyumbani kama uchungaji wa ng’ombe baadala ya kwenda kusoma. Mila na tamaduni hizi hunyima watoto nafasi ya kuendelea kusoma na kutimiza malengo yao.

Ili kusaidia serikali yetu katika uboreshaji wa elimu ya upili, yafuatayo ni mapendekezo juu ya namna ya kuboresha elimu yetu.

Serikali iongeze bajeti ya elimu :Ili kuweza kutatua matatizo ya umbali wa shule, miundo mbinu, pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia vilevile kuboresha mishahara ya walimu, kuajiri walimu wa kutosha.

Kuipa nguvu zaidi wizara ya elimu katika ngazi ya elimu ya upili: wizara ya elimu iimarishwe na kuweka wazi majukumu ya wizara hii pamoja na TAMISEMI ili iweze kuzingatia uboreshaji ya elimu ya upili kwa kutengeneza taasisi ndogondogo ndani ya wizara hii ili kuhakikisha mitaala huendana na wakati hasa kisayansi na kiteknolojia.

Kwa kuhitimisha, elimu ya upili ni ngazi muhimu sana katika nchi yetu ya Tanzania, hivyo ili kujenga taifa bora, serikali ijitahidi kuimarisha elimu hii kwa kutatua matatizo haya, ili tuweze kuendeleza jamii yetu na kujenga taifa bora lililoelimika la kesho.
 
Back
Top Bottom