KAWETELE
JF-Expert Member
- Dec 11, 2015
- 684
- 1,614
ELIMU YA PADRE WA KANISA KATOLIKI
(Sehemu ya Kwanza)
Na. John-Baptist Ngatunga
___________________________
Padre wa Kanisa Katoliki kwa kawaida amesoma na kulelewa kwa katika Mfumo ufuatao kwa hapa Tanzania:
Ieleweke toka mwanzoni kabisa kwamba Mapadre tuliona hapa Tanzania wamegawanyika katika sehemu au Makundi mawili kulingana na Mfumo wao wa Kimalezi:
1. Madre wa Jimbo
2. Mapadre wa Mashirika ya Kimisionari na Kitawa.
Mgawanyo huu wa Mapadre unaenda moja kwa moja pia kwa Maaskofu wetu. Ukiona Maaskofu wameandikwa Majina yao na mbele ya Majina yao ya Pili kuna vifupisho, basi ujue huyo ni Askofu na ni Mtawa au Mmisionari wa Shirika la Kitawa au Kimisionari ndani ya Kanisa. Na hicho kifupisho ni Kifupisho cha Jina la shirika lake. Hapa tunawaona Maaskofu wafuatao:
1. Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya OFMCap - Askofu Mkuu wa Dodoma
2. Askofu Mkuu Yuda Thadei Ruwa'ichi OFMCap - Askofu Mkuu wa Dar es Salaam
3. Askofu Augustine Shao CSSp - Askofu wa Zanzibar
4. Askofu Ludovick Minde ALCP/OSS - Askofu wa Moshi
5. Askofu Joseph Mlola ALCP/OSS - Askofu wa Kigoma
6. Askofu Rogath Kimaryo CSSp - Askofu wa Same
7. Askofu Beatus Urassa ALCP/OSS - Askofu wa Sumbawanga
8. Askofu Lazarus Msimbe SDS - Askofu wa Morogoro
9. Askofu Stephano Musomba OSA - Askofu Msaidizi wa Dar es Salaam
10. Askofu Wolfgang Pisa OFMCap - Askofu wa Lindi
Maaskofu wengine ambao sijawataja ni Maaskofu wa Majimbo. Rejea Orodha ya Maaskofu kama yalivyoandikwa kwenye TAMKO LA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA (TEC).
Turudi kwenye Mfumo wa Malezi ya Mapadre.
Ili kurahisisha uelewa wa hiki ninachotaka kukisema ni naomba nijikite zaidi kwa Mapadre wa Majimbo ambao ndio wengi zaidi kwa hapa Tanzania. Naongelea Mfumo ambao Mapadre wetu wengi wameupitia.
Baada ya Mvulana kuonesha nia ya kutaka kuwa Padre na kufuata taratibu zinazotakiwa kwaajili ya wito huo wa Upadre; Kijana huyo akishamaliza kufanya Mtihani Darasa la Saba anafanya Mitihani Miwili ya Mchujo ya Seminari. Mtihani wa kwanza unakuwa na Mahojiano ya Mdomo (Oral Examination).
Ikifaulu Mtihani huo anafanya Mtihani mwingine wa pili ambao wote waliofaulu Mtihani wa kwanza wanakusanywa pamoja. Mtihani huu wa pili unakuwa ni Mtihani wa kuandika (Written Examination). Masomo yanayoulizwa hapo ni Hisabati, Kiingereza na Dini.
Katika Mitihani hiyo, yanaulizwa Maswali ambayo lengo lake ni kupata Watoto wenye uwezo mkubwa wa uelewa. Maswali yanahitaji Fikra Sahihi. Na hapo hakuna rushwa, Michongo au connection. Anachukuliwa Mtoto aliyekidhi vigezo muhimu vya ufaulu na sio kwa kujuana au kupeana 'shavu'.
Baada ya kufaulu na kupita katika vigezo hivo, anaenda kuanza Rasmi Masomo na Maisha ya Seminari ya Mwaka wa Maandalizi (Preparatory Year) Maarufu kama Pre- Form One. Hapo atasoma kwa muda wa Mwaka 1 akifundishwa Masomo yote ya sekondari na Msisitizo mkubwa ukiwa katika Lugha ya Kiingereza.
Katika Mwaka huo Rekodi za Mitihani, Mazoezi na Majaribio yote ya Mwaka mzima zinatunzwa ili kupata Wastani wa Ufaulu ambao mara nyingi huwa kati ya 50% au 60%. Mwishoni mwa Mwaka huo wa Masomo, hufanya Mtihani wa mwisho ambao Matokeo yake pamoja na Rekodi zake zilizotunzwa zinatafutiwa Wastani.
Kama atafaulu hapo, ataanza Kidato cha Kwanza katika Seminari Ndogo yaani Minor au Junior Seminariy ambayo ni kwaajili ya Kidato I - VI kama ilivyo kwa Mwaka ule wa Pre-Form One.
Katika Masomo yake tangu anapoingia Seminari kuanzia Pre-Form One hadi Form Six Mtindo wa ni mmoja wa kumpima Mseminari huyo. Yaani kinachomfanya Mseminari huyo aendelee kubaki kwenye Mfumo huo wa Malezi yake ili awe Padre ni kuzingatia kwa ukamilifu yote muhimu katika Malezi.
Hapa naomba niseme Nyanja Kuu Tatu zinayozingatiwa sana katika Malezi ya Waseminari ili wawe Mapadre:
1. MALEZI YA KIROHO (Spiritual Formation)
Hapa Mseminari atatakiwa kulelewa katika Misingi ya Kidini yaani Maisha ya Kiroho ya kuwa karibu na Mungu kwa kuishi Maisha ya kiroho, kuwa na hofu ya Mungu, kupokea sakramenti, kushiriki katika Misa Takatifu kila siku, kushiriki katika Ibada na Majitolewa mbalimbali, kuwa katika Uchaji na kujipatia muda wa kutosha kwa Sala binafsi, Mafundisho na Mafungo ya Kiroho.
Atatakiwa alijue, alisome, alitafakari na kuliishi Neno la Mungu (Kila Mseminari ni lazima awe na Biblia Takatifu), kuzishika Amri za Mungu na Amri za Kanisa. Kuishi fadhira za Kimungu yaani Imani, Matumaini na Mapendo. Asome Vitabu mbalimbali vyenye Mafundisho sahihi ya Kiimani. Pamoja na Mambo mengine mengi sana yanayohusu Dini, Imani Katoliki na Maisha ya Kiroho kwa Ujumla wake.
2. MALEZI YA KIELIMU (Intellectual Formation)
Hapa ndio shule yenyewe ilipo. Mseminari atatakiwa kusoma kwa bidii na Maarifa ili aweze kujichotea Maarifa kwa kiwango cha juu sana. Mseminari atafundishwa vizuri na atatakiwa afaulu Mitihani yake vizuri na kukidhi kigezo vyote vya Kitaaluma kwa kufaulu vizuri sana. Atatakiwa ashirikiane na wenzake kimasomo.
Suala la Uaminifu na Uadilifu wakati wa kufanya Mitihani ni Jambo nyeti sana linalozingatiwa katika Usimamizi wake. Mseminari anayeshindwa kufikisha Wastani wa Ufaulu hawezi kuendelea na Masomo yake. Na hapo ndipo utakapokuwa mwisho wa Safari yake ya Malezi ya Upadre.
Licha ya kufaulu Mitihani, Mseminari anatakiwa kuwa na Upeo na uwezo mkubwa wa kufikiri, kuhoji, kidadisi, kuchambua, kuchanganua, kugundua na kuyahusianisha masuala na mambo mbalimbali. Hiki ni kipengele kinachohusu Maendeleo ya Akili na Fikra kwa Ujumla.
Na katika kudhihirisha Mapaji ya Roho Mtakatifu ya AKILI na ELIMU, Kanisa Katoliki linasisitiza sana umuhimu wa Elimu. Ndio maana hata Wamisionari walioleta Ukristo walikuja na kujenga 'Mafiga matatu': KANISA, SHULE na HOSPITALI ili kumkomboa Mwanadamu Kiroho, Kiakili na Kimwili.
Kipimo cha Mtihani kwa Seminari kwa kawaida hakitegemei sana Mitihani ya Kitaifa. Maana mifumo na viwango vya Ufaulu vya Seminari kiko juu kidogo zaidi ya vile vya Sekondari nyingi za hapa nchini. Lengo ni kumwandaa Padre Mtarajiwa kuwa na Upeo wa juu wa ufahamu wa Mambo zaidi ya Waamini wake atakaowaongoza kama KUHANI, NABII na MFALME.
3. MALEZI YA KIBINADAMU (Human Formation)
Katika kipengele hiki Mseminari analelewa katika Maisha ya Kijamii, nidhamu, Heshima kwa watu wote, utii kwa Sheria, kanuni na taratibu za Seminari na Mahali popote atakapokuwa. Anatakiwa kuwa Mkomavu wa Kimwili, Kiakili na Kiroho Mwenye uwezo wa kujizuia na kutunza Siri.
Atatakiwa ajitambue yeye binafsi na awatambue wengine pia na kuishi nao Maisha ya Kijamii (Social life). Atatakiwa ashirikiane na wengine katika Shida na Raha, Michezo, utamaduni, utambuzi, ukuzi na uendelezaji wa vipaji.
Ajibidishe katika Kazi mbalimbali za mikono ili kumjenga katika uwezo wa kujitegemea. Ni kosa kwa Mseminari kuwa Mvivu, Mwizi, kujihusisha na Mahusiano ya aina yoyote ya Kimapenzi, kutumia vilevi au aina yoyote ya Madawa ya kulevya.
ITAENDELEA....... Sehemu ya Pili.