SEHEMU YA 11
Hali ilikuwa ni ya mvurugano ndani ya Chama cha Labour, hakukuwa na aliyeona dalili za ushindi mbele yao, Bwana Mapoto alitisha, alikuwa akitikisa kila sehemu na kwenye kila kona ya nchi ya Tanzania, jina lake liliimbwa kwa shangwe huku wengine wakisema kwamba hatimaye Mungu alisikia kilio chao na kumleta mtu aliyeahidi kuleta mabadiliko na kuipeleka Tanzania kuwa nchi yenye nguvu barani Afrika.
“Nimechanganyikiwa kwa furaha! Leo nimemgusa Mapoto,” alisema mwanaume mmoja, alikuwa amevalia kofia ya chama hicho, fulana, kwa jinsi alivyoonekana kuwa na uzalendo na chama hicho, alikuwa kama mtu aliyekunywa maji ya bendera.
“Natamani sana na mimi nikamguse. Huyu ndiye mgombea wa ukweli, ndiye rais wetu ambaye ataweza kututoa hapa tulipokuwa. Maisha yamekuwa magumu sana kisa Labour Party! Huu ndiyo mwisho wao, yaani nikifika kwenye chumba cha kupigia kura, lazima niwachinje,” alisema jamaa mwingine huku akionekana kuwa na kiu ya kuhitaji mabadiliko.
Chama tawala kikachanganyikiwa, hawakuamini kile kilichokuwa kikiendelea. Hawakuona mahali pa kutokea, walizoea kwenda vijijini ambapo waliamini kwamba huko wangechukua watu wengi, kwa mwaka huo kila mmoja aliwashtukia, na walipokanyaga mguu tu, walikuwa wakizomewa na wakati mwingine kupigwa mawe.
“Jamani! Hali imebadilika, hebu zungumza na rais mstaafu,” alisema mwenyekiti wa kampeni, Bwana Edward Mrope.
Simu ikapigwa kwa rais aliyemaliza muda wake, alipewa taarifa juu ya hali ilivyokuwa imebadilika.
Kule vijijini ambapo ndipo walikuwa wakipategemea, palibadilika na kila walipokanyaga, ni jina la Mapoto tu ndiyo lililokuwa likisikika.
“Unasemaje?” aliuliza rais mstaafu.
“Huku hali ni mbaya, kila kona Mapoto, Mapoto, Mapoto tu,” alisema mwenyekiti wa kampeni maneno yaliyomfanya rais huyo kushtuka.
“Haiwezekani!”
“Huo ndiyo ukweli mkuu! Tufanye nini?”
“Nipigie simu baada ya dakika tano,” alisema rais mstaafu na kukata simu.