SEHEMU YA 44
Wakawa na hofu kwa kuhisi kwamba mwanaume huyo aliwabadilikia, wakajaribu kuwasiliana naye, simu yake haikuwa ikipatikana, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
Rais Bokasa alipopata safari ya kuelekea nchini Marekani, wakajua kabisa kwamba mwanaume huyo alikuwa akienda kuonana na Mapoto, wakajua kabisa kwamba walibadilikiwa, mtu ambaye walimwamini kwa moyo mmoja, mtu ambaye walimpa dhamana kubwa ya kugombea urais kupitia chama chao, hatimaye aliamua kuwabadilikia na kuungana na chama tawala kinyemela.
“Huu ni usaliti! Sisi kama Tanzania National Party hatutoweza kukubali, ni lazima tulifute jina lake kama mwanachama wa chama hiki,” alisema Edward, alionekana kuwa na hasira sana.
Hilo halikupingwa, kila mmoja akamuunga mkono kwamba ni lazima Mapoto afutwe katika chama hicho. Hawakujua ni hatua gani alizokuwa akipitia nchini Marekani, hawakujua kama mwanaume huyo alikuwa kwenye hali mbaya, kwamba mtoto wake mpendwa, Irene alikuwa hoi kitandani.
Taarifa ya kufutwa kwake uanachama ikatangazwa kwenye vyombo vya habari na baada ya siku mbili, jina lake likakatwa. Kila mtu akahuzunika, wengi hawakuamini kama mwanaume huyo waliyemwamini aliamua kuwasaliti na kujiunga na chama tawala.
Chuki dhidi yake ikaingia mioyoni mwa kila mmoja, kila mtu akamchukia, kuanzia watoto, vijana mpaka wazee wote walionyesha chuki dhidi yake, hawakumpenda, walimuona kuwa msaliti mkubwa, hata habari ya kuumwa kwa Irene hawakuwa wakiijua. Kila mmoja alikubaliana na viongozi wa chama hicho kwamba jina lake lifutwe.
“Yule ni nyoka, ni mtu mbaya sana ambaye huwezi kuvumilia kuwa naye, kama ukiishi naye, anaweza kukuua,” alisema mwanaume mmoja, kwa kipindi hicho, hasa miaka hiyo hakukuwa na mitandao ya kijamii, watu walitegemea taarifa kutoka kwenye televisheni na magazeti, waandishi wa vyombo hivyo hawakujua kilichokuwa kikiendelea, hilo likawafanya wananchi kutokujua lolote lile kuhusu mtoto Irene.