Dongo hili zito! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dongo hili zito!

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Aug 27, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Aug 27, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,759
  Likes Received: 82,733
  Trophy Points: 280
  Ni kujenga maisha bora kwa watoto au kujenga jina bora kwao

  Agosti 27, 2008

  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
  Uzitoni Street,
  Bongo.

  Ewe mpenzi
  Mpenzi wa enzi
  Nakupenda kishenzi
  Ili nikuenzi
  Nakuimbia tenzi

  ILA shida ni kwamba nimeishiwa. Aaagh!!

  Vipi mambo ya huko lakini? Pole sana na mihangaiko ya wiki nzima. Naona hatuliwi kidogo. Tunaliwa sana, kama si kulizwa kama alivyosema kipenzi chako Makengeza. Sijui anawezaje kuishi kikawaida na ufyatu wote ule.

  Lakini nilimkumbuka sana Makengeza wiki hii kwa sababu ilibidi nimsindikize Mama Bosi eti yeye anataka kuonyesha anavyopenda watoto yatima hivyo inabidi aende na mikamera kibao na luninga juu. Na, ingawa anajidai kuwapenda sana watoto yatima, hayuko tayari kuonyesha upendo huo kwa kubeba hata katoni moja ya maziwa.

  Ndiyo maana ilibidi niende naye nimbebee msaada wakati anatamba mbele ya mikamera. Hata kumpa mwanafunzi fulana na daftari, ilibidi nitoe na kumpa. Kidogo aniombe nimshike mkono mtoto kwa niaba yake maana naona aliogopa uchafu wa hawa watoto. Lakini mbele ya mikamera isingeonekana vizuri hata kidogo hivyo aliwashika mkono na kusafisha kwa nguvu zote baadaye.

  Ni hapo sasa nilimkumbuka Likengeza maana limelalamika mara mbili hivi inakuwaje watu wakienda kutoa msaada lazima wapigwe picha? Kwanza ni kinyume kabisa cha dini zao. Si misahafu inasema kwamba mkono wa kushoto usijue mkono wa kulia unafanya nani!?

  Sasa iweje watangazie dunia nzima huku wakitamba na nguo za bei iliyooza kabisa mbele ya watoto ambao hawana nguo yoyote ya maana. Wanawatambia nani na minguo hiyo kama si kujionyesha mbele ya luninga? Lengo lao ni kutoa msaada kweli au ni kuonekana wakitoa msaada? Ni kujenga maisha bora kwa watoto au kujenga jina bora kwao. Mimi sielewi kabisa.

  Hata hivyo, kwa kukumbuka alivyosema Makengeza, niliamua kuchukua watoto wachache pembeni na kupiga soga nao wakati wanakula kidogo. Sasa nilipowauliza wanawaonaje watu hawa wanaokuja kutoa msaada mbele ya mikamera, kwanza waliogopa kujibu, au tuseme walinijibu kama ambavyo waliona wanapaswa kujibu. Si mimi nimekuja na mama bosi!

  ‘Oh tunawashukuru sana wafadhili wetu. Kwa kweli tunahitaji msaada sana kwa hiyo Mungu awabariki, Mungu awazidishie neema, Mungu awalipe mara dufu …’

  ‘Lakini kupigwa picha mnaonaje? Hampati shida shuleni?’

  Lo, mpenzi, hapo nilikuwa nimechokoza nyuki kabisa.

  ‘Hapo umesema sista. Yaani, kesho sijui nitajificha wapi huko shuleni. Sijui. Maana watoto si unawajua kabisa?

  ‘Hee! Angalia ombaomba anaingia.’

  ‘Yaani haoni hata haya kuja kuvaa minguo ya msaada …

  Eti anaringa na mitumba …’

  Na maneno mengimengi ya kashfa. Hata mwalimu mara nyingine anaingia.

  ‘Angalia unavyosinzia. Jana wapewa msaada, leo wasinzia tu.’

  Kumbe si ajabu kesho asubuhi hatutakula ndiyo maana …

  ‘Lo pole sana. Sasa mnapendekeza nini?’

  Akasimama dada mmoja ambaye alikuwa na kama miaka kumi na sita hivi.

  ‘Sikiliza sista, sijui wewe ni nani. Sijui kama umekuja kutudadisi au nini. Lakini nakuambia hivi. Analofanya mama yako si sahihi. Si sahihi hata kidogo. Hata ukisoma haki za watoto, tuna haki ya faragha, haki ya mambo yetu kuwa siri ili wengine wasitubague na kutucheka. Kwani tulipenda kuwa yatima! Kwani tunafurahi kuwa walengwa na mtu yeyote anayependa kujionyesha?’

  ‘Usiwe na wasiwasi sista juu yangu. Mimi ni hausigali tu na nilitaka kujua ukweli maana wapo wanaowatetea.’

  ‘Basi waambie waseme, na wasichoke kusema. Waseme na kusema na kusema na kusema hadi wengine wasikie. Waseme hadi UNICEF na Plan na Save na mashirika mengine wanaojidai kuwa watetezi wetu waseme na wao. Waseme hadi watetezi wa haki za binadamu nao waseme. Wawashikie bango wanaodai kwamba wanafuata maadili ya uandishi hadi wasikie. Waseme bila kuchoka maana sisi tumechoka.

  Na hapo nilishangaa mpenzi. Huyu dada, imara, mwenye msimamo, ghafla akaanza kutoa chozi …’

  ‘Nimechoka. Nimechoka jamani. Tutanyanyaswa namna hii hadi lini? Tumekuwa miradi ya wakubwa tu?’

  Nilijaribu kumtuliza kwa kumuahidi kusema lakini hakuwa na raha kabisa. Aliendelea kusema tu.

  ‘Ndiyo, tunahitaji msaada. Lakini si msaada wa kutudhalilisha namna hii.’

  Mwenzake alidakia.

  ‘Sawa iwapo kweli wanatupenda kama wanavyodai, inakuwaje watufanyie hivyo? Kwa nini wasitoe msaada kimyakimya? Au wakitaka kujionyesha, kwa nini wasitengeneze hundi kuuuuubwa na kumkabidhi mkuu wa kituo bila kutubughudhi sisi?’

  ‘Lakini naona shida ni wenye mikamera pia. Hawatulii.’

  ‘Wangetulia kama hatua zingechukuliwa dhidi yao!! Wanavunja maadili ya kazi yao lakini hakuna anayejali kwa kuwa sisi ni yatima. Ni masikini. Hebu fikiria kama wangempiga picha vibaya mnene fulani au kuandika habari za kusikitisha juu yake. Si mnene angewapeleka makahamani. Lakini kwa kuwa sisi ni yatima tu, kila mtu anaweza kututumia kama daraja la kujikweza.

  Hapo aliingilia mvulana mmoja.

  ‘Lakini sista, usituelewe vibaya. Tunawaheshimu sana na tunawashukuru sana kwa kutukumbuka. Tunachotaka ni kwamba wasifikirie tu nini watoe kwetu lakini pia jinsi ya kutoa ili tuongezewe furaha badala ya kuandaliwa matusi na kejeli kwa mwezi mzima unaofuata..’

  Yaani mpenzi, kwa kweli maneno yale yaliniingia moyoni hadi hata mama bosi aligundua wakati tunarudi na gari.

  ‘Vipi Hidaya mbona kimya hivyo. Umesikitika kuona watoto wenye hali mbaya hivyo.’

  ‘Ni kweli mama. Lakini unafikiri ni haki kweli waonyeshwe kwenye luninga?’

  ‘Unasema nini? Wanafurahi sana kuonyeshwa hivyo. Wanawatambia wenzao ambao hawajawahi kuonekana hata siku moja.’

  Nilitaka kunyamaza lakini kila nilipokumbuka maneno ya wale watoto ilibidi nijikaze.

  ‘Lakini mama wakionekana hivyo kesho shule haikaliki. Wenzao wanawabeza, wanawasumbua kwa kila namna.’

  ‘Wivu tu unawasumbua. Lakini mimi najua kwamba wanafurahia msaada wetu na wanafurahia kuonyesha. Na wewe usishikwe na wivu pia.’

  Nakuambia mpenzi. Hakuna kiziwi kama yule ambaye amefunga masikio ili asisikie. MB akanikunjia uso hadi nilinyamaza. Na tulipofika nyumbani alikuwa anajisifu jioni yote kwa jinsi watoto walivyompenda, na shirika lilivyolamba miguu yake katika kumshukuru.

  Naona hata bosi alichoka maana mwisho alienda kuangalia luninga na kuweka sauti ya juu sana eti anataka kusikia wale wa chama tawalapinzani wameibua hoja gani wakati yeye anajenga taifa! Hivyo MB akamgeukia mwanaye hadi yeye pia, kwa mara ya kwanza, akakumbuka ana homework ya kufanya na kwenda kujifungia chumbani mwake. Na mimi nilikimbilia jikoni kwa nguvu zote ili nikoshe vyombo.

  Sasa baada ya muda nilisikia MB akisema.

  ‘Pale! Unaniona? Unaniona?’

  Nilipotoka na kuchungulia niliona sura ya yule dada jasiri aliyelizwa akipokea fulana kutoka kwa mama bosi. Nakuambia mpenzi wangu, sijawahi kuona uso uliojaa mchanganyiko wa huzuni na hasira hivyo. Nilidhani atachana ile fulana vipandevipande hasa yalipoonyesha maneno nyuma ya fulani.

  Tuwawezeshe wasiojiweza.
  Tuwaliwaze wenye mawazo
  Tuwapende yatima

  Yaani kweli amewaliwaza au amewaliza!

  Akupendaye kwa dhati
  Hata akiwa mikononi mwa chatu
  Hidaya wako
   
 2. Mpaka Kieleweke

  Mpaka Kieleweke JF-Expert Member

  #2
  Aug 27, 2008
  Joined: Feb 27, 2007
  Messages: 4,137
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  Huwa wanasoma basi? wakifika kwenye makala kama hizi wanajifanya kunyanyua simu na hatimaye baadae wanasema kuwa wako bize ili wasisome makala hizo.....
   
 3. Pundit

  Pundit JF-Expert Member

  #3
  Aug 27, 2008
  Joined: Feb 4, 2007
  Messages: 3,741
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 135
  He gives best he who gives anonymously - Pundit
   
 4. Ben Saanane

  Ben Saanane Verified User

  #4
  Aug 28, 2008
  Joined: Jan 18, 2007
  Messages: 14,603
  Likes Received: 3,692
  Trophy Points: 280
  Najua hili kombora limeawagusa wengi.wajua hali ya mioyo yao kwa sasa ingawa wataonekana kutabasamu daima
   
 5. L

  Lorah JF-Expert Member

  #5
  Aug 28, 2008
  Joined: Aug 22, 2008
  Messages: 1,193
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  imenigusa sanasana
   
Loading...