Dokta mimi siumwi huko

Dokta mimi siumwi huko

DOKTA SIUMWI HUKO-25


ILIPOISHIA
"Mtasha mbona umekuwa mstari wa mbele sana kunizuia mimi nisafanye uhalifu, inakuwaje wewe unashindwa kujizuia?" mume wa Monica alisema akimwita mwenzake huyo kwa jina lake la utani.
Mara, mwenye gari alitokea…
SASA ONDOKA NAYO…


Alishtuka kuona gari lake limeharibika sehemu ya mlango huku timbwili likiendelea…
"Jamani vipi tena?" aliuliza kwa mshangao mkubwa.


Majibu aliyoyapata yalimfanya ajutie lakini akaahidiwa kulipwa fedha ili kwenda kutengeneza gari hilo japokuwa alikubali lakini kwa shingo upande.


Baada ya utulivu kurejea lakini huku wanaume wote wakiwa na hasira ya wivu, waliamua kwenda polisi ambapo Dokta Kisarawe aliwekwa ndani ili kupisha uchunguzi wa madai ya wanaume hao kwamba ametembea na wake zao na kuwapa ujauzito.


Baada ya kuandikisha maelezo, walirudi nyumbani. Wote walifikia nyumbani kwa Mtasha, mume wa Sulee ambapo kikao kilikaa na misimamo ilitolewa…


"Mimi bwana kwa upande wangu nasema wazi kwamba sina haja ya kuwa na mke kama huyu," alisema mume wa Monica huku akimwangalia mkewe kwa macho yaliyojaa uchungu…
"Hata mimi, Sulee nakuandikia talaka zako tatu sasa hivi," alikuja juu Mtasha na kutaka kumpiga tena mke wake kwa hasira…


"Sasa Mtasha si umeshasema unamwandikia talaka si ufanye hivyo, achana na kumpiga bwana," alisema mume wa Monica.


Wanawake hao wawili waliangua kilio huku kila mmoja akimlaumu mwenzake kwamba alimsababishia lakini lawama za Monica kwa Sulee zilikuwa za kweli kwani yeye alipelekwa na shoga yake huyo ambaye alikuwa akiijua tabia chafu ya Dokta Kisarawe…
"Bila wewe Sulee mimi yasingenikuta haya. Ulijua Dokta Kisarawe ni mwingi wa habari ni kwa nini hukuniambia maana hata wewe ulishapitiwa…


"Halafu nilimwambia dokta. Alikuwa akipenda kunishikashika sehemu zisizohusika na matatatizo yangu, nikamwambia dokta mimi siumwi huko yeye hakusikia," alilalama sana Monica…
"Monica ni shetani, hata mimi nilimwambia dokta mimi siumwi huko wakati akipeleka mikono yake kwenye matiti yangu lakini hakutaka kunisikia. Tusameheni jamani."


"Hakuna msamaha hapa… Ala!" wanaume wote walijikuta wakijibu kwa pamoja bila kutaarifiana…
"Kwanza ni muhimu kwenda kupima afya zetu maana kama mna mimba ina maana mlikuwa hamtumii kinga," alisema mume wa Monica…


"Huko kuchepuka kwenu ndiyo faida yake mnaiona sasa," alisema mume wa Sulee huku akikohoa. Hapo alikuwa akisaka karatasi ya kuandikia talaka mara moja.
***
Siku ya pili, Mtasha, yaani mume wa Sulee na mume wa Monica walikwenda kupima virusi vya Ukimwi. Walikutana na wake zao huko wakiwa na shangazi wa Sulee ambaye aliomba kuzungumza na Mtasha kabla ya kuingia kwa dokta. Kwa heshima Mtasha alikubali na akatoka pembeni…


"Baba najua unaniheshimu sana…"
"Kweli shangazi…"


"Mwenzio kanijia na talaka analia. Lakini aliponisimulia kisa hata mimi nilikuunga mkono mwanangu…"
"Nashukuru sana kusikia hivyo shangazi…"
"Enhee, lakini sasa nina ombi moja tu kwako…"
"Lipi hilo shangazi?"


"Msamehe Sulee."
Mtasha palepale alijishika kichwa na kujikuna huku akitumbua macho, akakumbuka mema aliyowahi kuyafanya shangazi huyo kwake maana ana uwezo si wa kitoto.


Kuna mwaka Mtasha alipata kesi mbaya sana, uchumi wake ukayumba sana akajikuta hana hata pesa ya kula. Shangazi huyo wa mkewe akawa ndiye mfadhili wake kwani alikuwa akimpa pesa ya kula na pia alimsimamia kwenye kesi hiyo kwa kumuwekea wakili na akashinda.


Baada ya kushinda alimpatia mtaji akaendelea na miradi yake iliyosimama…
Wakati wa maongezi hayo, shangazi mtu hakumkumbusha kitu chochote Mtasha. Alimwacha ajipime mwenyewe tu…


"Da! Shangazi kusema ukweli umenipa wakati mgumu sana," alisema mume wa Sulee…
"Kwa nini mwanangu? Kusameheana kumewekwa na Mungu na ukimsamehe mwenzako hata Mungu atapenda na kukubariki."


"Ni kweli, lakini shangazi unalionaje hili la ujauzito?"
"Hilo unaweza kuliacha mikononi mwangu nikashughulika nalo."
"Utafanyaje shangazi? Maana mimi kusema kweli siwezi kuishi na mke mwenye ujauzito wa mwanaume mwingine."


"Ndiyo maana nimesema niachie mimi kuhusu hilo."
"Shangazi maamuzi yako ni mema na nakuheshimu wewe sana, je vipi kuhusu kupima Virusi vya Ukimwi?"


Muda wote huo, mume wa Monica alipokuwa amekaa alikuwa akimtumbulia macho mume wa Sulee kama anayemwambia asithubutu kukubali hata siku moja maneno ya shangazi wa Sulee…
"Ndiyo maana tupo hapa! Wewe unadhani Sulee ana virusi?" alisema shangazi mtu huyo…
"Siwezi kusema anavyo au hana, ila kupima ni muhimu shangazi."


"Kwa hiyo kama atakuwa salama utakuwa umepokea ombi langu siyo?
 
DOKTA SIUMWI HUKO-26


ILIPOISHIA
"Siwezi kusema anavyo au hana, ila kupima ni muhimu shangazi."
"Kwa hiyo kama atakuwa salama utakuwa umepokea ombi langu siyo?
SASA JIACHIE MWENYEWE…


"Naamini hivyo."
"Basi turejee kusubiri zoezi likamilike."
Walirudi kwenye fomu. Mume wa Monica akamuuliza mume wa Sulee mazungumzo yao yalihusu nini…
"Shangazi anataka nimsamehe Sulee."
"Uko tayari kwa hilo?"


"Mh! Nimemwambia kama atakuwa hajaathirika naweza."
"We unataka kumrudia Sulee?"
"Unajua nini mshkaji? Huyu shangazi amenisaidia sana katika maisha yangu kuliko mtu mwingine yeyote…"


"Kwa hiyo?"
"Kwa hiyo naweza kuangalia upya cha kufanya."
"Mh! Nadhani sijakuelewa."
"Kivipi?"


"Yaani pamoja na mambo yoote waliyotufanyia hawa Malaya wewe unakubali tuwasamehe, Mungu aniepushie hilo mawazoni mwangu," alisema mume wa Monica na kumfanya mume wa Sulee kuwa na mawazo nusunusu tofauti na alivyoongea na shangazi mtu.
***
Majibu ya vipimo yalitoka, waliitwa mtu mmoja mmoja lakini huku wakiruhusiwa kwenda na watu wao kama wapo walioongozana nao.
Sulee alikwenda na shangazi yake huku akidondosha machozi kwa kuwa muda wa zamu yake ulifika. Alikuwa akitetemeka sana.


Monica, mumewe na mume wa Sulee walibaki nje lakini mume wa Sulee aliuliza kama itakuwa busara na yeye aende kwa vile yanaweza kutoka majibu ambayo yamechakachuliwa na shangazi huyo kwa vile alitaka ndoa ya Sulee iendelee kudumu.


"Noo, achana nao bwana. Wewe mbona hueleweki? Kwanza kama wao walitaka uwazi na ukweli kwa nini wasikwambie muingie wote?" alihoji mume wa Monica mpaka mwenyewe akaona ni kweli, akabaki kwenye fomu.


Baada ya dakika kama kumi, kilio kikubwa kikasikika kutokea chumba cha daktari…
"Uuuwi, Mungu wee nisaidie. Nitakwenda wapi mimi?" ilikuwa sauti ya Sulee…


"Ngoma tayari hiyo mwanangu, hakuna kurudiana wala kwenda mbele," alisema mume wa Monica huku akichekelea. Alijua mpango wa shangazi mtu kuirejesha ndoa hiyo haupo tena.
Kwa upande wake, Monica alionekana kuwa mtu mwenye mchecheto zaidi kwani kila wakati alikuwa akisimama na kukaa. Aliamini kama Sulee ‘aliungua' hata yeye yumo ndani ya ‘moto' huo.


"Mmh! Sasa kama Sulee analia amegundulika kuwa na virusi je mimi? Maana mwanaume aliyemwambukiza yeye ndiyo huyohuyo ametembea na mimi," alisema moyoni Monica huku akimtupia macho ya wizi mumewe.


"Monicaaa…" aliita jina muuguzi kabla hajamalizia, Monica mwenyewe alisimama haraka sana. Mara Sulee na shangazi yake wakatokea huku Sulee akichuruzika machozi.


"Pole Sulee," alisema Monica lakini hakuitikiwa hata shangazi yake hakusema kitu.
"Baba tunaondoka, uamuzi wako ubaki kuwa palepale," alisema shangazi mtu akimwambia mume wa Sulee. Alipita kwenye korido kwa aibu kubwa akiwa amejiinamia mpaka kwenye gari lake akifuatwa na Sulee kwa nyuma.


****
"Eee, thanks God. Asante Mungu, wewe ndiye muweza wa yote. Oooh! Si kwa nguvu zangu bwana bali kwa neema tu. Mimi Monica mimi kwamba sina virusi?" sauti ya Monica ilisikika kutokea kwenye chumba cha daktari.


Ilifika mahali akapiga na vigeregere kufurahia majibu ya vipimo vyake.
Mumewe alianza kuhisi ganzi akiwaza kwamba endapo mkewe yuko fiti halafu yeye akakutwa na ngoma itakuwaje?


"Itakuwa poa tu kwani maisha bado yataendelea," alisema moyoni mume wa Monica huku akiangalia chini kwa mawazo.
"Mkubwa unasikia huko ndani? Shemeji yuko ngangari," mume wa Sulee alisema.
"Eee, ndiyo sherehe inaendelea ndani."
Mara Monica alitokea…


"My dear niko fiti, sina virusi wala vijidudu," alisema Monica huku akirukaruka kwenye miguu ya mumewe…
"Kwa hiyo?" mumewe alimuuliza…
"Heee! Hujapenda?"


"Hata nikipenda, kwani kuna nini? Si umekutwa upo fiti tu."
"Hunisamehi?"
"Haitatokea Monica."


Monica aliangua kilio mbele ya watu huku mumewe naye akiitwa kuchukua majibu yake. Kumbe Sulee na shangazi yake hawakwenda mbali, walikuwa kwenye gari wakisubiri matokeo ya mume wa Sulee, mume wa Monica na Monica mwenyewe.
"Mshkaji mimi nataka twende wote," alisema mume wa Monica baada ya kuitwa jina lake na muuguzi mmoja.


Walizama wote mpaka kwa dokta na wakasema wote wamefika kwa kupima…
"Kwa hiyo majibu mnasikiliziana?" alihoji dokta.
"Ndiyo."
Alianza kwa kuwashauri huku akiweka majibu ya wote sambamba, karatasi ya mume wa Monica ikianza juu.
 
DOKTA SIUMWI HUKO-27


ILIPOISHIA
Alianza kwa kuwashauri kwamba huku akiweka majibu ya wote sambamba, karatasi ya mume wa Monica ikianza juu.
ENDELEA SASA…



"Sasa kwa kuwa mpo wote na wote mmepima na majibu yote yapo hapa baada ya ushauri niliowapa, wote mpo vizuri hakuna mwenye virusi vya Ukimwi," alisema dokta. Walisimama, wakakumbatiana. Wakampa mkono dokta na kutoka nje huku wakicheka kwa furaha…


"Mungu anajua cha kufanya mshkaji, wale wanawake siyo kabisa," alisema mume wa Monica…
"Lakini kama wewe huna na shemeji hana si mnaweza kurudiana?" alihoji mume wa Sulee.
"Na ile mimba?"
"Si utailea tu."


"Mimi nilee mimba ya Dokta Kisarawe?"
"Kwani mshkaji kuna nini?"
"Haitatokea. Mara kumi angenibambika nisijue kuliko kujua."
***
Sulee na Monica walikumbatiana kwenye gari huku wote wakilia. Kilio kikubwa kilikuwa kwa Sulee kwani alikutwa ameungua wakati mwenzake yupo fiti.


"Mwanangu nyie naona mambo mazuri maana naona vicheko," shangazi wa Sulee alimuuliza mumewe…
"Mungu hamtupi mja wake shangazi. Mungu mkubwa bwana," alisema mume wa Monica huku wakiondoka zao kwa mbwembwe wakicheka na kupigiana mikono na wakitembea kwa ujasiri wa hali ya juu.


Wake zao walikuwa wakiwatazama kwa macho yanayoendelea kujaa machozi wasijue la kufanya. Ghafla waliangua vilio mpaka watu wakajaa lakini hakukuwa na jinsi, waume zao walishaamua. Walijuta na kujuta kwa usaliti wakati waume zao walikuwa wakihangaika kusaka maisha.


***********************************MWISHO.*****************************************
Niwashukuru wote mlio fuatilia simulizi hii kwa koment na kimya kimya mkiwa na muongozaji wenu The King Daudi 1 kwa hisani kubwa ya Global publisher, watu wanatafuta namna nyingi ya kuhalalisha lile wanalolifanya ili lionekane halali kwa namna yoyote ile michepuko haifai, tumeona katika simulizi yetu pamoja na kwamba Monica aligundua mumewe hawezi kusababisha mimba lakini alijuutia kitendo chake na hasa baada ya kuambiwa anaachwa, michepuko wapendwa haifai.
 
Michepuko sio dili!Tena bora wanaume tukichepuka huwa tunaingia mguu mmoja.Mwanamke akichepuka anaingia mzimamzima anatoa utamu ambao hata hajawahi kumpa mmewe! ILA ALL IN ALL KUCHEPUKA HAIFAI TUBAKI NJIA KUU JAMANI,MAGONJWA NJE NJE SIKU HIZI!
 
Michepuko sio dili!Tena bora wanaume tukichepuka huwa tunaingia mguu mmoja.Mwanamke akichepuka anaingia mzimamzima anatoa utamu ambao hata hajawahi kumpa mmewe! ILA ALL IN ALL KUCHEPUKA HAIFAI TUBAKI NJIA KUU JAMANI,MAGONJWA NJE NJE SIKU HIZI!
Kweli tubadilike hakuna kitu kinachoumiza moyo kama utagundua mwenzi wako ana mtu mwingine inaumiza sana na hapa mapenzi ndo yanapokuwa machungu
 
Back
Top Bottom