Dkt. R.K Dau anavyomkumbuka Benjamini William Mkapa

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,216
30,582
DR. RAMADHANI KITWANA DAU ANAVYOMKUMBUKA RAFIKI NA KIONGOZI WAKE RAIS MSTAAFU BENJAMIN WILLIAM MKAPA

KWA NINI NAMLILIA MZEE BENJAMIN WILLIAM MKAPA

Dkt. Ramadhani K Dau

Ilikuwa siku ya Ijumaa tarehe 24 Julai 2020 kiasi cha saa 8 na nusu usiku kwa saa za Tanzania nilipopata simu kutoka Accra Ghana kutoka kwa Dkt.

Ken Kwaku aliyekuwa Mshauri wa Rais Mkapa katika masuala ya uchumi kunifahamisha kuwa Mzee Benjamin William Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu amefariki dunia. Kwa hakika nilistushwa sana na taarifa hii kwa sababu mbili.

Kwanza, ni kawaida ya kibinaadamu kuwa kifo hakizoeleki na kila kinapotokea huwa kinastusha. Lakini sababu ya pili ni kuwa jana yake yaani siku ya Alhamisi tarehe 23 Julai 2020 kiasi cha saa 11 jioni kwa saa za Tanzania nilikuwa nazungumza na mtoto wa mama yangu mdogo Bwana Kheri Abdul Mahimbali kuhusu Mzee Mkapa.

Sikujua kuwa kipindi hicho Mzee Mkapa alikuwa hospitali na alibakisha masaa machache kabla ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani aliyoianza tarehe 12 Novemba 1938.

Baada ya kupata taarifa hizo, haraka nikakimbilia kwenye simu yangu ya kiganjani na kukuta ujumbe kutoka kwa rafiki na ndugu yangu Mwanahistoria maarufu Bwana Mohamed Said.

Katika ujumbe wake, Mohamed alisema:

Balozi itakuwa vizuri uandike tazia (sic). Alikuwa rafiki yako na si wengi wanalijua hili.

Mara tu baada ya kupata ujumbe huo pale pale nikajikuta kuwa umeniangukia wajibu wa kuandika Taazia kumuenzi Mzee Mkapa ambaye kwa hakika alikuwa mzee wangu wa karibu sana ambaye ameniongoza na kunisaidia mambo mengi; na kama alivyosema Mohamed si watu wengi walikuwa wanalijua hilo.

Mara ya kwanza kukutana na Mzee Mkapa ilikuwa mwezi Juni 2001 ikiwa ni takriban miezi mitano baada ya kuniteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF tarehe 21 Januari 2001.

Wakati huo tulikuwa Geneva, Uswisi kuhudhuria mkutano wa Shirika la Kazi Duniani yaani ILO.

Mzee Mkapa alikuwa miongoni mwa wageni watatu maalum walioalikwa kuwasilisha mada kuhusu ajira mbaya za utotoni (worse forms of child labour). Baada ya hotuba yake, Mzee Mkapa aliombwa kukutana na wajumbe wa nchi zote za Afrika zilizohudhuria mkutano huo.

Wakati wajumbe wa Afrika walipokuwa wanatoka kwenye chumba kikuu cha mkutano (Plenary Hall) kuelekea kwenye chumba kilichoandaliwa kwa ajili na mkutano na Mzee Mkapa, kipindi hicho Mzee Mkapa aliwekwa kwenye chumba cha muda (holding room) akiwa na wajumbe wote kutoka Tanzania.

Nakumbuka Bwana Naftali Nsemwa, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa PPF alikwenda kumsalimu mahala ambapo Mzee Mkapa alikuwa ameketi akiwa na viongozi waandamizi wa Serikali akiwemo Balozi Ali Mchumo. Katika mazungumzo na Bwana Nsemwa, Mzee Mkapa alimuuliza kuwa amesikia Mkurugenzi Mkuu wa NSSF nae amehudhuria mkutano huo.

Baada ya kusikia hivyo, Balozi Joshua Opanga ambaye alikuwa Mkuu wa Itifaki alitoka na kuja tulipokuwa tumesimama na kutuarifu kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF anatakiwa na Mhe Rais.

Huo ndio ulikuwa mkutano wangu wa kwanza kabisa na Mhe Benjamin Mkapa.

Baada ya mkutano ule wa Geneva, nimekutana na Mzee Mkapa mara kadhaa aidha kwenye sherehe mbalimbali au kikazi kwenye ofisi yake Ikulu.

Idadi ya mikutano yetu iliongezeka sana baada ya Mzee Mkapa kustaafu mwezi Disemba 2005.

Mara nyingi tumekuwa tukikutana nyumbani kwake Sea View na baadae Sea Cliff.

Katika mikutano yetu yote, mkutano ambao ninaukumbuka zaidi kuliko yote ni ule tulioufanya nyumbani kwake Sea View mwezi Aprili 2006.

Mkutano huo ulikuwa ni wa kwanza baina yetu baada ya Mzee Mkapa kustaafu.

Siku hiyo nilikwenda kwa Mzee Mkapa kwa mambo mawili.

Kwanza ni kumjulia hali na kumpongeza kwa kumaliza uongozi wa nchi yetu kwa salama.

Pili ilikuwa kumshukuru kwa imani kubwa aliyoionesha kwangu kwa kuniteuwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi kubwa kama NSSF bila hata kunifahamu.

Nilimwambia Mzee Mkapa kuwa kwa bahati mbaya, katika jamii zetu mtazamo wa watu wengi ni kuwa nafasi nyeti kama hiyo huteuliwa mtu ambaye anafahamika sana au ana ukaribu na Rais kwa namna moja au nyingine.

Nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF si ya kuteuliwa mtu ambaye hafahamiki kabisa kama nilivyokuwa mimi wakati huo.

Aidha nilimkumbusha Mzee Mkapa kuwa wakati ananiteuwa katika nafasi hiyo hakuwa ananifahamu kabisa na mara ya kwanza ya sisi kukutana ilikuwa miezi mitano baada ya uteuzi wangu.

Nilimalizia kwa kumwambia kuwa ni matarajio yangu kuwa nimekidhi mategemeo yake kwangu; nakumbuka kwa Kiingereza nilimwambia I hope I met your expectations.

Baada ya kusema hayo, Mzee Mkapa alizungumza kwa muda mrefu sana na kutoa yake ya moyoni. Kwanza aliniambia kwa maneno yake mwenyewe:

What do you mean you met my expectations. You exceeded my expectations by far!

Kwa tafsiri isiyo rasmi:

Una maana gani kusema umekidhi matarajio yangu. Wewe umevuka matarajio yangu kwa kiasi kikubwa sana.

Kauli yake hii aliithibitisha katika barua binafsi Kumb FP.III/12 aliyoniandikia tarehe 29 Machi 2007, kunishukuru na kunipongeza kwa kazi kubwa niliyoifanya kuibadili NSSF wakati wa uongozi wake.

Kwa maneno yake, Mzee Mkapa alisema:

. . . nimeshangazwa na kufurahishwa zaidi na maainisho ya maendeleo na viwango vya mabadiliko ambayo umeyabuni, umeyaanzisha, umeyatekeleza na kuyasimamia kwa ujasiri na ufanisi mkubwa. Hakika maendeleo hayo ni mapinduzi thabiti katika fani hii ya hifadhi ya jamii katika uchumi wa nchi. Hongera sana. (msisitizo kama ulivyo kwenye barua)

Umenishukuru kwa uteuzi na imani yangu kwako. Kwa upande wangu nakushukuru kwa kudhihirisha waziwazi hivi kwamba tuna hazina kubwa kitaifa ya wataalamu wazalendo, wenye ujuzi mkubwa, waadilifu na wachapa kazi. Matumaini yangu ni kwamba rekodi yako hii ya kazi ya kutukuka itatambuliwa kitaifa.

Katika mkutano wetu wa Aprili 2006, Mzee Mkapa aliniambia maneno ambayo sijapata kumsimulia mtu yoyote.

Katika mazungumzo yetu, Mzee Mkapa aliniambia kuwa katika teuzi zote alizozifanya akiwa Rais, uteuzi wangu ni miongoni mwa teuzi zilizompa taabu sana kutokana na fitna, uzushi na mizengwe dhidi yangu.

Mara ya kwanza alipotaka kuniteuwa, baadhi ya wazee ambao hakuwataja (nami sikuwa na sababu ya kutaka kuwajua) walimwendea na kumshawishi asiniteuwe kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF kwa sababu mimi ni CUF.

Ushahidi wao ni kuwa nyumbani kwa baba yangu mzazi kuna bendera ya CUF.

Mzee Mkapa akawauliza iwapo natumia uCUF wangu kuhujumu Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kazi zangu za Mkurugenzi wa Masoko Mamlaka ya Bandari.

Wazee wakawa hawana majibu.

Akawauliza iwapo CUF ni Chama ambacho kipo kinyume cha Sheria au Chama ambacho kimepigwa marufuku kwa maana ya outlawed organization. Wazee wakawa hawana jibu.

Akawaambia wazee hao kuwa kuwepo kwa bendera ya CUF nyumbani kwa baba yangu si kosa; na hata kama ni kosa, si sahihi kuhukumiwa mimi kwa “kosa” ambalo amefanya baba yangu.

Wazee wakaishiwa hoja na kuondoka. Mzee Mkapa akanisimulia kuwa haikupita muda akaambiwa kuwa asiniteuwe kwenye nafasi hiyo kwa sababu mimi ni Mujahidina.

Ushahidi wao ni kuwa ninaswali ofisini na kwamba kila mwaka mwezi wa Ramadhani naenda Makka.

Mzee Mkapa akahoji iwapo natumia muda wa kazi kuhubiri dini kwenye ofisi za Mamlaka ya Bandari badala ya kufanyakazi niliyoajiriwa.

Jibu likawa hapana.

Mzee Mkapa akauliza iwapo Uislamu wangu unaathiri kazi zangu kama Mkurugenzi wa Masoko wa Mamlaka ya Bandari.

Jibu likawa hapana.

Baada ya kuridhika kuwa zile zote zilikuwa ni fitna, hatimaye tarehe 21 Januari 2001, Mzee Mkapa aliniteuwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF kazi ambayo niliifanya kwa miaka 15 hadi tarehe 15 Februari 2016 wakati Mhe Rais Dkt.

John Magufuli aliponipa heshima ya kipekee ya kuniteuwa kuwa Balozi wake katika nchi saba za Kusini Mashariki ya Asia.

Nchi hizo ni Malaysia, Indonesia, Thailand, Philippenes, Brunei, Cambodia na Laos.

Huo ni mfano mmoja tu kati ya mingi ya uadilifu wa Mzee Mkapa.

Leo najiuliza ni vijana wangapi wamekoseshwa fursa mbalimbali kutokana na fitna na uwongo dhidi yao.

Upo usemi maarufu wa Kiingereza unaosema:

“if you want to kill a dog, give it a bad name”.

Kwa tafsiri isiyo rasmi:

“ukitaka kumuuwa mbwa mpe jina baya”.

Marehemu Mzee Mkapa atakumbukwa kwa mengi sana. Wakati wa utawala wake amefanya mengi ya kuendeleza nchi yetu.

Mengi sana yameandikwa kuhusu mema yake kama mwanadamu na mazuri aliyoyafanyia nchi kama kiongozi.

Lakini yapo mengi ambayo hayajaandikwa au hayapewi uzito ambao ni stahili yake.

Kwa sababu ya ufinyu wa nafasi, leo nitayataja mambo mawili tu.

Kwanza, Mzee Mkapa alikuwa jasiri sana wa kufanya na kusimamia maamuzi yake.

Hapa nitatoa mifano miwili.

Mfano wa kwanza ni uwamuzi wake wa kuwapa Waislamu kilichokuwa Chuo cha TANESCO ili waanzishe Chuo Kikuu chao.

Uwamuzi kama huo unahitaji ujasiri mkubwa.

Alifanya hivyo baada ya kubaini kuwa sehemu kubwa ya raia wake wameachwa nyuma sana kielimu.

Kwa uwamuzi huo, Mzee Mkapa alikuwa anaitakia mema nchi yetu kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu kwa raia wake wengi ili kuharakisha na kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi yetu.

Wapo ambao waliutazama uwamuzi ule kuwa ni wa kidini.

Ukweli ni kuwa uwamuzi wa Mzee Mkapa ulisukumwa na dhamira ya kudumisha ustawi na amani katika nchi.

Ni uwamuzi ambao hoja yake kuu ni ya kiuchumi (economic argument) na pia kuweka mizania sawa katika jamii.

Hakuna nchi duniani ambayo inaweza kuendelea iwapo idadi kubwa ya raia wake wapo nyuma kielimu.

Katika suala hili tunao mfano mzuri wa China.

Nchi hiyo imepiga hatua kubwa sana katika maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa sababu ya kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu kwa raia wake.

Hadi kufikia miaka ya 1980s China ilikuwa na watu chini ya 50 milioni ambao walikuwa na shahada za Chuo Kikuu.

Hivi sasa watu wenye shahada za Chuo Kikuu nchini China wanakadiriwa kufika 500 milioni, idadi ambayo ni zaidi ya watu wote wa Marekani.

Mzee Mkapa aliliona hilo na ndio msingi wa uwamuzi wake wa kuwapa Waislamu Chuo cha TANESCO.

Mfano wa pili wa ujasiri wa Mzee Mkapa ni uwamuzi wake wa kutaka kutatua matatizo ya muda mrefu ya Waislamu baada ya kupokea malalamiko yao wakati wa Baraza la Eid tarehe 19 Januari 1999.

Baadhi tu ya malalamiko hayo ni idadi ndogo ya Waislamu kwenye vyuo vikuu na kwenye ajira katika Taasisi za Umma na Idara za Serikali, kutokuwepo kwa Mahakama ya Kadhi na Tanzania kutojiunga na Organization of Islamic Conference (OIC) licha ya ahadi aliyoitoa Bungeni aliyekuwa Waziri Mkuu Mhe John Malecela mwaka 1993 kuwa Zanzibar inajitoa kwenye OIC ili kuipisha Serikali ya Muungano kujiunga na Umoja huo. Wakati wa uongozi wake, akiwa Mwenyekiti wa CCM, Mzee Mkapa aliliweka suala la Mahakama ya Kadhi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005-2010.

Aidha Serikali ya Mzee Mkapa ilifanya utafiti wa kina kuhusu faida na hasara za kujiunga na OIC na kubaini kuwa kuna faida nyingi kwa Tanzania kujiunga na Umoja huo.

Kuhusu fursa za ajira, Serikali ya Mzee Mkapa iliagiza kufanywa kwa utafiti kwenye Mashirika yote ya Umma na Idara za Serikali kuhusu uwiano wa ajira nchini.

Nakumbuka wakati huo nikiwa Mamlaka ya Bandari, tulitakiwa na Wizara yetu tufanye utafiti huo na kuwasilisha mapendekezo yetu Wizarani kwa ajili ya kupelekwa kwenye Mamlaka za juu kwa hatua stahiki.

Sifa ya pili ya Mzee Mkapa ni kuwa alipenda sana watu wenye kujiamini na kuhimiza kuwa mabadiliko yoyote ya hali za watu ni lazima yaanzie au yatokane na wao wenyewe.

Kwenye suala hili, Mzee Mkapa alikuwa anapenda sana kutumia usemi wake wa sentensi moja ya maneno kumi yenye harufi mbili mbili.

Sentensi hiyo inasema:

if it is to be, it is up to me

Kwa tafsiri isiyo rasmi:

iwapo nataka jambo liwe, basi wajibu ni wangu mwenyewe.

Mfano wa usemi huu umetajwa kwenye Quran, Sura Ra’ad Aya 11 (13:11) ambapo Mwenyezi Mungu Amesema:

Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf-sini mwao.

Mzee Mkapa ameondoka wakati Taifa linamuhitaji sana hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu ipo katika jitihada za kurekebisha uchumi.

Busara za Mzee Mkapa zilikuwa zinahitajika sana katika kipindi hiki kutokana na msimamo wake wa kutumia tofauti zetu kuwa ndio chanzo cha nguvu zetu bila kujali tofauti za mawazo, rangi, dini, kabila nk. kama alivyosisitiza katika hotuba yake aliyoitoa Kigali, Rwanda katika Mkutano wa baadhi ya viongozi wa Afrika uliofanyika kati ya tarehe 19-23 Mei 2014.

Mzee Mkapa alilionesha hili kwa vitendo kwani siku moja mwezi wa Ramadhani wakati wa magharibi Mzee Mkapa alikuwa anamtafuta mmoja kati ya walinzi wake wa karibu.

Baada ya kupewa jibu kuwa ameenda kufuturu, Mzee Mkapa alistuka kwani hakujua kabisa kuwa mlinzi wake wa karibu ambaye amemlinda kwa miaka mingi alikuwa Mwislamu!

Huyo ndio Mzee Mkapa. Kwenye masuala ya kazi na kutoa fursa, Mzee Mkapa alikuwa mwadilifu sana na hakubagua raia wake kwa misingi ya rangi, kabila au dini zao.

Kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla na kwa Waislamu, itakuwa vyema iwapo uongozi wa Chuo cha Waislamu Morogoro ukampa heshima ya kumtunuku Mzee Benjamin William Mkapa Shahada ya Heshima Uzamivu yaani Doctor of Letters (Honoris Causa) posthumously.

Aidha itakuwa vyema iwapo jengo la Utawala (Central Administration) likapewa jina la Benjamin William Mkapa Building.

Kwa upande wa michezo, Mzee Mkapa ametoa mchango mkubwa sana kwa kujenga uwanja mkubwa na wa kisasa. Kwa kuuenzi mchango wake, nashauri Serikali ibadili jina la uwanja wa Taifa na kuitwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Benjamin Mkapa yaani Benjamin Mkapa Memorial Stadium.

Buriani Mzee Benjamin William Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hakika umeitendea haki nchi yako na raia wake. Daima utakumbukwa kwa mema, busara, ujasiri, umahiri, uadilifu na uungwana wako.

Innallillah Wainnaillahi Raajiuun

“Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea” (Quran 2:156).

20200729_084319.jpg
 
Chapisho murua kabisa. Katika kumuelezea mkapa. Asante kwa kumbukizi na exclusive nzuri.

R.I.P Ben
 
Back
Top Bottom