Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 4,783
- 14,975
Akizungumza katika uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Sekta ya Viwanda uliofanyika leo, Februari 9, 2026, jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewahimiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa vitendo.
Amesema kuwa ushirikiano kati ya vyuo na sekta ya viwanda ni hitaji la lazima, akitoa wito kwa wadau kutumia ushirikiano huo kufanya tafiti zitakazoongeza tija katika sekta mbalimbali, hususan sayansi na teknolojia.
Aidha, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Ameir akizungumza katika hafla hiyo, amesema kuwa tayari wizara imeshaunda kamati 33 za ushauri wa kitaalamu kwa lengo la kukuza na kuimarisha ushirikiano huo.
Vilevile, baadhi ya wadau waliochangia mjadala uliotangulia uzinduzi wa mpango huo wamesema kuwa, endapo mkakati huo utatekelezwa ipasavyo, utasaidia kukuza ujuzi utakaowawezesha vijana kushindana katika soko la ajira.
Mpango huo umeelezwa kuwa unalenga kuchochea na kukuza ushirikiano kati ya vyuo na sekta ya viwanda, ambazo ndizo waajiri wakuu, ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.