Diwani CCM aeleza jinsi ‘mabaunsa’ wa Sabaya walivyomsulubu

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,813
4,547
Julai 27, 2021, kesi ya unyang’anyi iliyomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya iliendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Arusha na shahidi wa tano wa Jamhuri, Seleman Msuya (36) aliieleza mahakama alimwona Sabaya akiongoza ‘vijana wake’ kuingia duka la Shaahid Store na kufunga milango yeye akiwa nje ya duka lake.

Alidai Sabaya na vijana waliokadiriwa kuwa kati ya 11 na 12 walishuka katika magari matatu, kisha kuingia dukani hapo na nje ya duka walibaki vijana watatu, kati yao wawili wakiwa na bastola na mmoja akiwa na radio call (redio ya upepo).

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, shahidi huyo ambaye ni mfanyabiashara wa magodoro alidai siku hiyo (Februari 9, 2021), Sabaya alifika Shaahid Store akiwa na magari matatu yenye namba za STL, DFP, huku lingine likiwa na namba za usajili binafsi.

Alidai baada ya Sabaya na kundi lake kuingia dukani humo, mageti yalifungwa na hakujua kilichoendelea ndani na ilipofika saa 12:30 jioni alifunga duka lake na kukaa ndani ya gari lake nje ya duka.

“Wakati nafunga niliona vijana wa Sabaya watatu, wawili wakiwa na bastola na mmoja akiwa na redio call, nikakaa kwenye gari mpaka saa mbili kasoro kutaka kujua kwa jirani yangu kuna nini na nilipompigia mwenye duka sikumpata,” alidai shahidi huyo.

Akihojiwa na Wakili wa utetezi Mahuna, shahidi huyo alidai analifahamu duka la Shaahid Store kwa kuwa alimkuta katika eneo hilo na mkataba wa upangaji wa duka una jina la mmiliki wake, Mohamed Al Saad.

Alidai wakati anasalimiana na Sabaya hakuona akiwa ameshika silaha, badala yake aliwaona vijana wake wawili wakiwa na bastola nje ya duka.

Baada ya Msuya kumaliza kutoa ushahidi, ilifuata zamu ya Diwani wa Sombetini (CCM), Bakari Msangi (36) ambaye alikuwa mlalamikaji katika kesi hiyo.

Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, Msangi alidai alipofika dukani kwa Mohamed Saad, Februari 9,2021 alikuta vijana wawili mlangoni ambao hakuwatambua, kwani walikuwa wamevalia kofia huku kila mmoja akiwa na bastola mkononi.

Alidai alipofungua mlango wa duka hilo na kuingia ndani alikutana na kundi la watu kati ya tisa na 10 na alimtambua Sabaya na msaidizi wake (mshtakiwa wa pili). Alidai Sabaya alimwambia anaingilia kazi aliyotumwa na Rais Magufuli, ya kudhibiti mapato ya Serikali.

Alidai kuwa Sabaya alimwambia wamiliki wa duka hilo ni wahujumu uchumi, wanatakatisha fedha haramu na wanafanya biashara hiyo bila kutoa risiti.

Shahidi huyo alimtambua mshitakiwa wa kwanza (Sabaya) na wa pili (Sylvester Nyegu) na kudai kwa mara ya kwanza alimuona Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM kumpitisha Magufuli kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.

Alidai mara ya pili alimuona Nyegu Dodoma wakati wa kumpitisha Rais Samia kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Shahidi huyo aliendelea kudai akiwa ndani ya duka hilo, Sabaya alimtishia kwa bastola na kuwa amepata tatizo la kusikia vizuri katika sikio la kushoto kutokana na kipigo kikali alichopata kutoka kwa ‘mabaunsa’ baada ya kiongozi huyo kuwaamrisha wampige.

“Baada ya mabaunsa kunizunguka, general (Sabaya) akawa ameshikwa na hasira, akawaambia wale mabaunsa wanisachi nisije kuwa na silaha halafu akaanza kutukana. Akasema mpigeni tero, nikaanza kusachiwa, wakachukua vitu vyangu vyote, wakanipora simu zangu mbili, Sh390,000 na risiti ya vitu vya kununua.

“Ghafla alisema mtoeni wenge, nilipigwa mtama mmoja ambao sijawahi kupigwa tangu nimezaliwa, nikakalishwa chini, nilipigwa kipigo ambacho sijui nahadithiaje, nikawa napigwa makofi ya masikio, wengine wananipiga makofi ya mgongo, nikapiga magoti kumwangukia Sabaya anisaidie vijana wake wasiniue lakini hakusaidia.

“Nikaendelea kupigwa, akashikwa hasira akatoa bastola yake akaninyooshea akaniambia ataniua, nikapiga kelele nikimwambia Sabaya utaniua nina watoto wadogo, nikaenda kumng’ang’ania miguuni mabaunsa wakanitoa kunisogeza mbali,” alidai Msangi.

Alidai Sabaya alipotoa bastola na kumnyooshea kichwani, alimweleza kuwa kiherehere chake ndicho kimempeleka hapo na kwamba nimekuwa nikimfuata fuata.

“Sabaya akaita Bura, nikavutwa akasema funga pingu za miguu na mikononi kwa nyuma, nikapigwa kipigo kizito, nikaona kama napoteza fahamu, nikajiegemeza kwenye kaunta.

“Nilikuwa napigwa funika funua kwenye masikio na baada ya tukio lile ndipo nilipata tatizo la kutokusikia vizuri kwenye sikio la kushoto, ndiyo maana wakati kesi inaanza niliomba tuzungumze kwa sauti, kwani sisikii vizuri,” alidai Msangi

Aangua kilio mahakamani
Julai 28, 2021, Msangi aliendelea kutoa ushahidi na alishindwa kujizuia na kuangua kilio wakati akieleza jinsi alivyotishiwa bastola akiwa amefungwa pingu miguuni na mikononi. Msangi alilia alipoanza kueleza namna alivyotekwa na kiongozi huyo na kundi lake huku akidai alifungwa pingu miguuni na mikononi akiwa ndani ya gari la Sabaya.

Alidai wakati wakitoka katika duka la Saad akiwa ndani ya gari la Sabaya, kiongozi huyo kijana alitoa bastola na kumtisha huku akimwambia ‘unapenda kuingilia mambo yangu.’

Shahidi huyo aliendelea kuieleza mahakama kuwa Sabaya aliendelea kumtukana na kumwambia anayeweza kuongea na yeye (Sabaya) katika nchi hii ni Rais Magufuli na si takataka nyingine huku akijipiga kifuani.
 
“Ghafla alisema mtoeni wenge, nilipigwa mtama mmoja ambao sijawahi kupigwa tangu nimezaliwa''

Hii kauli nimejikuta nacheka kana kwamba mazuri. Ila Sabaya alivimba kichwa aisee
 
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, shahidi huyo ambaye ni mfanyabiashara wa magodoro alidai siku hiyo (Februari 9, 2021), Sabaya alifika Shaahid Store akiwa na magari matatu yenye namba za STL, DFP, huku lingine likiwa na namba za usajili binafsi
Jamaa alikuwa jamaa
 
Back
Top Bottom