Demokrasia na Maendeleo ya Watu

Mt09

Member
Sep 24, 2021
26
66
Utangulizi
Mwanadamu ameumbwa na vionjo vya asili vya matamanio. Vionjo hivi humuongoza katika kubuni na kujenga mazingira kufikia matamanio yake.

Kwa mujibu wa mwanasaikolojia Abraham Maslow, katika kanuni yake kuhusu mpangilio wa vipaumbele vya mahitaji ya mwanadamu, amebainisha kuwa mahitaji huongezeka kila yanapojitosheleza.
Mahitaji hayo yamegawanyika kuanzia na yale ya Msingi ya kimwili, akili na ya mwisho kwa umuhimu huwa ni yale ya kisaikolojia.
Kwa mfano ni kawaida kwa mtu tajiri kuingia katika mikiki mikiki ya kutaka kuwa kiongozi wa kisiasa kama vile mbunge ama kiongozi wa nchi ilhali mwingine akipigania kupata japo mlo mmoja wa siku. Tofauti hizi za mahitaji ya binadamu katika jamii inaonesha utofauti wa mahitaji tunapozungumzia maendeleo ya watu.

Hivyo mwanadamu amekuwa àkibadilika badilika kifikra na kimtazamo kwa lengo la kutimiza haja za matamanio yake kadiri ya anavyojitosheleza.

Ndio kusema, mazingira huru kwa mtu mmoja mmoja kutumikia maamuzi binafsi ni jambo la msingi sana kwa mstakabali wa maisha na mabadiliko yake na ya wengine.

MAMLAKA ZA DUNIA NA TAWALA ZA WANADAMU

Tawala za Jadi na Maisha.

Mwanadamu anaishi katika makundi. Makundi hayo ni familia ama kaya. Katika tawala za asili, mkusanyiko wa familia mbalimbali zenye nasaba moja hutengeneza ukoo ambao huwa chimbuko la kabila. Kabila huongozwa na ukoo maarufu ambao hutoa uongozi wa kurithi ambye huitwa Chifu au Mtemi wa kabila. Hawa kazi yao kubwa ni kutoa na kusimamia miongozo mbalimbali Ili kudumisha Mila na desturi za jadi ndani ya kabila. Mila na desturi husimamia shughuli za kiuchumi na kijamii katika maisha ya kila siku kama vile utungaji wa sheria kuhusu ndoa na mirathi, umiliki wa rasilimali, elimu, ibada, tiba, mazingira, ulinzi, uongozi, teknolojia n.k. Viongozi hawa wa asili huongoza watu kwa mitazamo ya mila na desturi za jadi zilizotungwa na mababu tangu kale. Hivyo wana nguvu na kinga ya kutohojiwa au kukosolewa. Kwa mfano, katika makabila mengi mwanamke ni kiumbe anayemilikiwa na mwanaume hivyo hana haki za urithi, kumiliki rasilimali na uongozi pamoja na mamlaka ya kuamua hatima kuhusu maisha yake. Kwa kuwa mtazamo mkubwa wa maisha ya jadi ni kulinda na kudumisha mila na desturi za kabila ambazo ndio utambulisho rasmi, juhudi zozote za mabadiliko ni kuvunja miiko ya asili na kwa Imani za kijadi ni chanzo cha mabalaa ndani ya jamii.
Ubaguzi huu wa kijinsia huzuia uhuru wa fikra na Kupunguza muingiliano wa rasilimali na kusababisha hali tegemezi ndani ya jamii.

Tawala za jadi na serikali za kikoloni.
Ujio wa watawala wa kikoloni kuanzia wafanyabiashara wa kiarabu, wapelelezi hadi wakoloni wa kijerumani na waingereza katika pwani ya afrika mashariki walikuta tawala za jadi zikiongoza jamii za waafrika. Wageni hawa hawakuwa na shida na tawala hizi za jadi, bali shida yao kubwa ilikuwa rasilimali zilizokuwa chini ya tawala hizi. Kuanzia nguvu kazi ya binadamu, madini, wanyama na mazao mengine ya misitu.
Wavamizi hao walijenga mahusiano ya kilaghai na watawala hao wa jadi kupitia zawadi mbalimbali kutoka Asia na ulaya ambavyo viliwachanganya akili kutokana na kuwa vipya kwao kuwavutia wenyewe kuliko watu na rasilimali zilizokuwa chini ya himaya zao.
Japokuwa si tawala zote za jadi zilikubaliana na tawala za kikoloni kwa mfano chifu Mkwawa wa wahehe aliyetoa upinzani mkubwa kwa wajerumani, kwa kiwango kikubwa walirahisisha mfumo wa utawala usiokuwa wa moja kwa moja wa wakoloni wa kiingereza.
Kwa mfano serikali za waingereza waliokuwa na mpango uliosomesha watoto wa machifu pekee Ili kurahisisha shughuli za mawasiliano na uenezaji wa propaganda za kikoloni wakati wa utawala usiokuwa wa moja kwa moja.

Tawala za Jadi na Serikali Huru.
Dhana ya serikali huru.

Hizi ni mamlaka zilizoundwa kwa utaratibu wa hiari kwa kuunganisha mamlaka za mtu mmoja mmoja na kupitia itikadi za kisiasa kuunda mamlaka moja ya utawala. Makundi yote ya watu ndani ya jamii yanakubaliana kuunda kanuni, taratibu na miundo ya kiutawala. Hivi ndivyo taifa linavyoundwa. Makubaliano yote huandikwa katika andiko maalum la kitaifa (Katiba) na kuheshimiwa kama mwongozo wa mahusiano ya jamii na maisha ya hapa duniani.

Serikali huru ya Tanganyika
Baada ya kuondoka serikali za kikoloni, baadhi ya serikali zilizoundwa na wazawa mfano serikali ya Tanganyika kwa wakati huo, iliweza kuachana na mfumo wa tawala za Jadi kama mfumo rasmi kiserikali. Mifumo hii ilibaki kama alama za makabila. Huu ulikuwa Mkakati wa kuunganisha makabila ili kuunda jamii ya taifa moja imara na linayotawaliwa na falsafa moja ya uongozi iliyosadifu mazuri ya maisha ya jadi kama vile ushirikiano lakini pia kuendeleza mazuri ya wakoloni kama vile elimu ya kusoma na kuandika, usafi pamoja na teknolojia mpya.
Chini ya mwasisi wa taifa la Tanzania Mwalimu Julius K. Nyerere, falsafa ya ujamaa na kujitegemea iliundwa chini ya Azimio la Arusha kuongoza jamii mpya ya watanzania baada ya serikali za kikoloni na tawala za kichifu.
Kupitia utawala huu mpya Katiba ya nchi iliundwa kukidhi mahitaji ya falsafa iliyoongoza maisha kwa wakati huo.

Dhana ya demokrasia:
Serikali ni mamlaka ya uongozi kwenye eneo linalounganisha asili tofauti za watu. Ili kuzingatia ustawi wa kila mwana jamii, uwazi na ushirikishwaji wa maamuzi ni jambo la msingi. Mfumo huu wa uwazi na ushirikishwaji katika uongozi hujulikana kama demokrasia. Abraham Lincoln Rais wa zamani wa Marekani alitafsiri serikali ya kidemokrasia kuwa ni "serikali ya watu, iliyotokana na watu kwa ajili ya watu". Tafsiri hii inaakisi dhana ya uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya uongozi wa umma.

Demokrasia na maendeleo ya watu.
Mtu anaweza kujiuliza kwanini watu wanahangaika kuzungumzia demokrasia. Kwa kifupi demokrasia ni ushiriki na ushirikishaji wa jamii katika maamuzi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maisha.
Sababu kubwa hasa ya kuhubiri demokrasia ni kurekebisha mapungufu ya kiutawala tuliyorithi kutoka mifumo ya utawala wa jadi ni ule wa kikoloni. Kwa mfano baada ya kupata uhuru serikali ilipanua wigo wa kupata elimu kwa kujenga Shule mpya pamoja na kutaifisha Shule zilizokuwa kwa ajili ya matabaka ya wachache na kuzifanya za umma kwa ajili ya wote. Hii ilikuwa ni utekelezaji wa sera ya elimu kwa wote ambapo elimu kwa watu wazima ilitolewa kwa waliokuwa hawajui kusoma na kuandika.

Dhana ya demokrasia ni Pana. Inahusisha ushirikishaji wa jamii katika kubaini changamoto za jamii, kubuni na kupendekeza njia ya utatuzi, kuweka malengo na vipaumbele, kushiriki utekelezaji na tathmini yake.

Dhana ya demokrasia ni Pana. Kwa mfano changamoto kubwa ya wahitimu kushindwa kujiajiri. Je shida ni elimu yetu, soko la ajira au mifumo yetu ya kiuchumi. Je, ni nani anayefanya maamuzi juu ya ukuzaji mitaala katika elimu yetu. Je, maoni ya wadau wakuu kama soko la ajira, wanafunzi na walimu yanashirikishwa vipi katika mchakato mzima wa Kukuza mtaala. Je, elimu hii yenye changamoto ilitengenezwa na nani? kwa ajili ya nani? na kwa manufaa ya nani? Je, elimu yetu inaenda sambamba na mahitaji ya uchumi wetu?
Haya ni maswali ambayo demokrasia inaweza kuyajibu kwa ufasaha.

Nini kifanyike:
Mageuzi ya kimfumo na kisheria yanahitajika ili kuachana na athari mbaya za utawala wa kikoloni pamoja na kuachana na Mila na desturi zisizoendana na mahitaji ya Karne ya 21 yenye matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia. Lengo ni kujenga jamii yenye misingi ya ushirikishwaji katika kubaini, kupanga, kuamua, kutekeleza, kufanya tathmini na kutoa mrejesho wa mipango ya kiuchumi na kijamii kuanzia ngazi ya familia, shule na vyuo pamoja taasisi za kiutawala.​
 
Back
Top Bottom