Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,329
- 33,138
Profesa Ibrahim Lipumba
Chama cha Wananchi (CUF), kimetangaza kwamba kitasimamisha mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo, katika mkutano na waandishi wa habari ambao aliutumia kutangaza kuanza rasmi mchakato wa kushiriki Uchaguzi Mkuu.
Katika kujipanga kuelekea uchaguzi huo, CUF imetoa ratiba ya kura za maoni ya kuwapata wagombea wa udiwani, ubunge wa majimbo, ubunge viti maalum na urais katika uchaguzi huo kwa upande wa Tanzania Bara na kutangaza tarehe ya kuchukua na kurejesha fomu kwa wanachama wanaotaka kugombea urais kuwa ni Mei 1-5, mwaka huu.
Kwa kauli hiyo sasa CUF itakuwa imesimamisha mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa mara ya nne mfululizo; wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, 2000 na 2005, chama hicho kilimsimamisha Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, Profesa Lipumba mara zote hizo amekuwa akishindwa na wagombea wanaosimamishwa na CCM, kuanzia Rais Mstaafu Benjamin Mkapa mwaka 1995 na 2000, kisha Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005.
Katika mkutano huo uliofanyika makao makuu, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Mketo pia alisema wamefikia uamuzi huo ili kukata kiu ya wananchi wengi waliokuwa wakitaka kujua iwapo CUF itasimamisha mgombea urais katika uchaguzi huo.
Jambo la muhimu, ambalo tungependa wananchi wajue ni kwamba, CUF imedhamiria kushinda uchaguzi huu na kwamba wengi wamekuwa wakihoji iwapo tutaweka mgombea urais au la.
Kwa kinywa kipana kabisa CUF itaweka mgombea wa urais na ndiye atakayekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2010-2015, alisema Shaweji na kuongeza:
Haiwezekani katika kipindi ambacho nchi imekumbwa na ombwe la uongozi, hali ya maisha ya Watanzania imezidi kuwa mbaya, uchumi wa taifa umezidi kudidimia, migawanyiko katika jamii inaongezeka kwa kasi ya kutisha ambayo inatokana na serikali kushindwa kuwajibika, kutoweka kwa maadili ya taifa na hata kufutika kwa utu wa watu, jamii iendelee kukikumbatia Chama Cha Mapinduzi.
Aliwataka wanachama wa CUF wenye sifa za kugombea wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya chama kuwania uongozi katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Pia, aliwaomba Watanzania kujiandaa kuchagua viongozi makini watakaotetea maslahi ya taifa.
Kwa mujibu wa ratiba ya kura za maoni, wanachama wanaotaka kugombea urais wametakiwa kuchukua na kurejesha fomu hizo kwa makatibu wa wilaya, ambapo Mei 6 -10 fomu za wagombea urais zitafikishwa kwa Katibu Mkuu.
Shaweji alisema fomu za kugombea udiwani na ubunge (ikiwamo viti maalum) zilizoanza kuchukuliwa Februari 23, zimetakiwa ziwe zimerejeshwa kwa makatibu wa tawi ifikapo Aprili 13, mwaka huu.
Alisema Aprili 14 - 20, itakuwa ni kipindi cha kurejesha fomu za wagombea udiwani na ubunge (ikiwamo viti maalum) kwa makatibu wilaya, wakati Aprili 27 - Mei 6 itakuwa ni kipindi cha mikutano ya wilaya ya kura za maoni kwa wagombea udiwani na viti maalum.
Mei 13 - 20 matokeo ya kura za maoni kwa wagombea ubunge na viti maalum kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu, wakati Mei 29 - 30 Baraza Kuu la Uongozi la Taifa litafanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea ubunge.
Alisema Juni 2, Mkutano Mkuu wa Taifa wa kura za maoni kwa wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na urais Zanzibar na Juni 3 maandalizi ya kampeni.
CHANZO: NIPASHE