Habari ndiyo hii hapa !
Vyama saba vya upinzani vimeamua kuunda ushirikiano na kumsimamisha mgombea ubunge mmoja katika Jimbo la Mbeya Mjini huku vikitangaza kuwaunga mkono wagombea wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majimbo mawili ya Rungwe Mashariki linalogombewa na Profesa Mark Mwandosya na Kyela linalowaniwa na Dk Harrison Mwakyembe.
Akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari jijini Mbeya, Mwenyekiti wa umoja huo ambaye pia ni Mwenyekiti APPT Maendeleo wilaya ya Mbeya Mjini, Godfrey Devis alisema wameamua kusimamisha mgombea mmoja atakaye pambambana na mgombea wa CCM, kwa lengo la kuweka mbele maslahi ya wananchi wa Mbeya.
Alisema kaulimbiu ya umoja huo ni 'Mbeya kwanza, vyama baadaye' na ndio sababu wanaangalia zaidi uwezo wa mgombea, dhamira ikiwa ni kuwatumikia wananchi wa Mbeya ili kuwaletea maendeleo.
Vyama hivyo vilivyoamua kushirikiana kusimamisha mgombea mmoja wa ubunge katika jimbo la Mbeya Mjini ni Chama cha Wananchi (CUF), NCCR- Mageuzi, UDP, TADEA, SAU, APPT- Maendeleo na TLP.
Devis alisema kwa vile kaulimbiu yao ni Mbeya kwanza na vyama baadaye, wanaamini Dk. Mwakyembe na Profesa Mwandosya ni watu wenye uwezo mkubwa wa kuwaletea wana-Mbeya maendeleo na ni wapambanaji wa vita dhidi ya ufisadi ambao umelitafuna taifa, ndio sababu wamekubaliana kwa kauli moja kuwaunga mkono.
"Tumeamua kwa dhati kushirikiana vyama hivi vyote saba kusimamisha mgombea mmoja mwenye uwezo na nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo," alisema Devis.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Mbeya Mjini, Yasin Mrotwa alisema hivi sasa wanaendelea na mazungumzo na mmoja wa wanachama wa CCM, Prince Mwaihojo kumuomba ili asimame kugombea ubunge wa Mbeya Mjini kwa niaba ya vyama hivyo.
Alisema utafiti wao unaonyesha kuwa Mwaihojo ambaye pia ni mwenyekiti wa mtandao wa wasomi wa Mkoa wa Mbeya anakubalika na umma wa wananchi wa Mbeya hivyo endapo atakubali ombi lao atakuwa ni mtu sahihi wanayeamini kuwa anastaihili kupewa ridhaa ya kuliongoza jimbo la Mbeya Mjini.
Kuhusiana na nafasi za madiwani, Mrotwa alisema wagombea wote watachukua fomu ndani ya vyama vyao na baada ya utafiti watakaofanya, watakuwa wakimuachia mgombea wa chama kinachokubalika zaidi katika kila kata.
Naye Mwenyekiti wa Mipango na Uchumi wa NCCR Mageuzi, Agabo Mwakatobe alisema ushirikiano wa vyama waliouanzisha Mbeya, utakuwa mfano wa kuigwa nchini, kwa sababu kwa mara ya kwanza Mbeya itakuwa na mbunge wa kitaifa anayeungwa mkono na vyama saba.
Mwakatobe alisema wanachama wa vyama vya CCM na Chadema wenye nia ya dhati ya kujikomboa kiuchumi na kimaendeleo pia wanakaribishwa kuingia kwenye ushirikiano huo ili kuongoze nguvu itakayofanya apatikane mbunge wanayemtaka na anayekubalika na wanachi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI