CUF, CHADEMA muendako siko


kilimasera

kilimasera

JF-Expert Member
Joined
Dec 2, 2009
Messages
3,073
Likes
23
Points
135
Age
42
kilimasera

kilimasera

JF-Expert Member
Joined Dec 2, 2009
3,073 23 135
MAANA rahisi ya uwepo wa vyama vya upinzani katika nchi yoyote ile Duniani, ni kuimarisha Demokrasia ya kweli na kuwashinikiza viongozi walio mabadarakani kuwaongoza na kuwatumikia wananchi.
Ni kutokana na hilo, ndio maana siku zote chama tawala hukosa raha na amani pindi chama kimojawapo cha upinzani kinapoanza kupata sauti au nguvu ya kuungwa mkono na wananchi wengi.

Kitendo cha chama cha upizani kuungwa mkono na wananchi wengi humaanisha kuwa na nafasi kubwa ya kukiangusha chama tawala, katika uchaguzi unaofuata.

Hilo ndilo ambalo husababisha chama tawala hukaa chini haraka na kujiuliza wapi walipokosea hata kutoa mwanya kwa wananchi kubadili mwelekeo na kufuata upande wa wapinzani.

Badaa ya kubaini makosa, chama tawala huunda mbinu na mikakati ya kuzima nguvu hiyo ya upinzani, bila kujali kama ni mbinu halali au mbinu chafu.

Kwa hapa Tanzania, baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vya vingi mwaka 1992, hakukuwa na chama cha upinzani kilichoonyesha kuwa na nguvu ya kuitisha CCM.

Hilo lilikuwa wazi na ndio maana viongozi wake waliendelea kulala na kuongoza kwa mazoea yale yale ya kiutawala, dharau, ubabe, vitisho, kulindana na kutumia mali za umma kwa fujo.

Kidogo kujiengua kundini kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi na Naibu Waziri Mkuu, Augustin Mrema na kujiunga na Chama cha NCCR Mageuzi, kukaleta joto kwa CCM, ni kwa sababu kabla ya kujitoa Mrema alifanya kazi iliyokubalika kwa kiasi kikubwa ndani ya jamii ya Watanzania.

Kwa hiyo alikuwa anakubalika, haikuwa ajabu pale alipokuwa akibebwa na vijana wa kihuni au akisukumwa ndani ya gari lake huku akiitwa rais, maisha yaliwachosha na walihitaji mtu wa kuwaletea mabadiliko ambayo waliamini CCM haiwezi.

Ni bahati mbaya kwamba wengi wa vijana wale waliokuwa wakiamini katika mabadiliko hawakujiandikisha kupiga kura hivyo kusababisha kura za Lyatonga kutotosha kumuingiza Ikulu.

Aidha kwa upande wa pili wa Muungano wa Tanzania, sera nzuri za Chama cha Wananchi (CUF), ziliwakuna wananchi na wakajitokeza kwa wingi kukiunga mkono kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo, yakadhihirisha jinsi wananchi wa visiwa hivyo walivyopoteza imani kwa chama tawala, kama sio kukichoka, licha ya kupata ushindi ambao unaendelea kutiliwa shaka hadi leo.

Pamoja na yote hayo, bado serikali ya CCM haikupoteza muda baada ya uchaguzi huo ili kufanya tathmini na kuelewa wapo walipojikwaa na wapi warekebishe ili wafanye vema katika uchaguzi wa mwaka 2000.

Hata hivyo ni dhahiri kwamba, CCM hadi leo haijaketi na kufanya tathmini ya nini wanachokikosea kwa wananchi wa visiwa hivyo kusita kuwapa ushindi wa kishindo ili waongoze.

Kidogo ni kama ninawasifu CCM kwamba baada ya kukabwa koo na Mrema mwaka 1995 wakamuandalia mikakati iliyomaliza kabla ya kufika katika uchaguzi wa mwaka 2000.

Kwa hilo walifanikiwa kwani Mrema wa 1995 hakuwa yule aliyegombea tena mwaka 2000 na hata 2005, alikuwa ni mgombea mpya asiye na mvuto asiyekubalika.

Ni bahati mbaya sana kwamba hata katika vyama vingine hakusimamishwa mgombea mwenye mvuto, mwenye kukubalika mwenye dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko ya takayoleta ahueni kwa wananchi.

Ni katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilipomsimamisha mtu ambaye Watanzania wamekuwa wakimtafuta kwa muda mrefu, walipomsimamisha Dk. Willbrod Slaa.

Wazee kwa vijana, wake kwa waume walijitokeza kwa wingi katika mikutano yake ya kampeni, walimuamini wengi wa wananchi walimuona Dk. Slaa kama mkombozi wa kweli.

Kwa hiyo hawakuishia kujitokeza kwa wingi katika mikutano yake ya kampeni tu, bali walidhihirisha kile wanachokiamini juu yake kwa kujitokeza kwa wingi na kumpigia kura.

Ingawa CCM imeendelea kuongoza dola lakini ni dhahiri kuwa sumu ya Dk Slaa imewaingia, kwa hakika hawakupenda kupoteza majimbo mengi kama ilivyoshuhudiwa.

Ninasikitika kuona kwamba kambi hizi mbili za upinzani zilizoonyesha nguvu kubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, CUF kwa Zanzibar na CHADEMA kwa Tanzania bara, zikianza kutetereka.

Vyama hivi vimepiga hatua kubwa katika kuiondolea CCM, himaya CUF walioanza kumiliki kisiwa cha Pemba safari hii wameonyesha mafanikio kwa kuingia hadi kwenye ngome ya CCM huko Unguja.

CHADEMA wao wamepiga hatua kutoka kwenye majimbo matano ya kuchaguliwa hadi kutwaa majimbo 23 Tanzania bara, likiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 400.

Vyama hivi vilipaswa vikae na kujiuliza kwa nini Watanzania wamewaamini wao hata kuwapa ushindi huo, lakini badala yake tayari kumeanza kuingia virusi kati yao.

Ule umoja waliouunda miaka mitano iliyopita waliuzika kama hiyo haitoshi kwa sasa kila chama kimekuwa na mmomonyoko wa ndani ingawa wanajitahidi kuuficha.

Mabadiliko ya uongozi ndani ya Kurugenzi za CUF na hiki kinachoendelea ndani ya CHADEMA vinanifanya nione kwamba wanakoelekea siko.

Vyama hivi vilipaswa kujiuliza wapi vilikosea na wapi vilipatia hata kupata matokeo hayo waliyopotea na wapi sasa waelekeze nguvu ili kuzidi kuungwa mkono na wananchi wengi.

Suala la kila mmoja kuanza kujiona na kujihesabu kwamba yeye ndiye msafi huku akimnyooshea mwenzake kidole kwamba yu mchafu kutawafikisha pabaya.

Wanapaswa kuwaheshimu wananchi ambao waliwaona wao wote ni wasafi na wakawapa dhamana ya kuwaongoza, aidha walipaswa kukaa na kupanga mikikakati ya kuwatumikia.

Pia kilichokuwa muhimu kwao kwa sasa ilikuwa ni kupanga mikikati endelevu ambayo itautolea jincho na kutoa msukumo wa kipekee katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Nadhani kwa upande wa CUF pia walikuwa na kila sababu za kujiuliza ni kwa nini hadi leo hii, bado hawajaweza kuipiku CCM kwa upande wa Tanzania bara, huku CHADEMA nao wakijiuliza wafanye nini ili waongeze imani kwa wapiga kura.

Vyama hivi ndivyo vinavyoonekana kuichanganya CCM na kuwanyima usingizi wagombea wake wa nafasi mbali mbali za uongozi, hivyo vitapigwa vita.

Ni bahati mbaya sana kwamba vyama hivi vimeanza kuingia katika matatizo madogomadogo yanayotokana na kutaka madaraka zaidi kwa viongozi wao.

Matokeo ya hilo ni kuzaliwa kwa mtoto mbaya aitwaye Chuki, mtoto ambaye huweza kuisambaratisha familia bila kujali ukubwa au uimara wake.

Mtoto huyu ni mbaya hafai kukaribishwa hata kwa jirani achilia mbali ndani kwako, kwa kuwa yupo tayari kuwapokea adui zako na kuwasaidia ili kukuangamiza.

Sihitaji kutolea mifano kwa hili la chuki, kwani naamini CUF na CHADEMA ni mashahidi kwamba katika uchaguzi mkuu uliopita baadhi ya maeneo yaliyokuwa ngome ya CCM, ushindi wao ulitokana na chuki iliyopandikizwa upande wa pili.

Viongozi wa juu hawakuwasikiliza wananchi wanasemaje kuhusu wagombea, walichoamini ni kwamba bado Watanzania wana kasumba ya kupiga kura kwa kumchagua mwenzetu kumbe sivyo.

Watu wanataka wawachague viongozi watakokwenda kuwatumikia pale watakapopewa dhamana za madaraka, kwa hiyo ni mapema mno kwao kwa sasa kutaka kunyoosheana vidole vya ubora, waswahili husema “Kwa shujaa huenda kilio kwa muoga huenda kicheko”.

Wasijidanganye kwamba wanaweza kumtimua au kumtenga mmoja wao halafu kundi likaendelea kuwa na nguvu kama zile za awali, kwa hakika hata kichaa anao wenye kumuunga mkono.

Cha msingi kwa wote ni kukubali kutokubaliana na kukubali kuvumuliana kwa sababu Asilani, hakuna binadamu aliyekamilika, vinginevyo watawakaribisha CCM kupenyeza sumu mbaya kwani kufanya hivyo ndio kujihakikishia kwao kuendelea kula.

Waswahili husema Adui yako Muombee Njaa, hivyo daima CCM inawaombea mabaya CUF na CHADEMA, kwa kuwa haina uhakika wa kuendelea kuongoza iwapo vitazidi kujisogeza na kukubalika zaidi kwa wananchi.

Viongozi wa vyama hivi wajue kuwa wananchi wanatamani mabadiliko, wanataka kuwaingiza madarakani watu watakaowaletea ahueni kimaisha.

Wanawataka viongozi ambao watawakomboa, hivyo kucheza au kuyumba kwenu ni kuiachia CCM kutawala badala ya kuongoza ni kuwanyima wananchi fursa ya kufaidi maana na thamani ya uwepo wa vyama vingi.
 

Forum statistics

Threads 1,235,731
Members 474,712
Posts 29,232,697