Comedy: Mzee Majuto - Heshima ya ndoa

JOTO LA MOTO

JF-Expert Member
Apr 11, 2018
758
555
672431-2dfe13991bcb22eb661d6d4f558c6d76.jpg


2.jpg

TITLE:HESHIMA YA NDOA.
MTUNZI:IMA WA JONI AKA MSANII JOTO LA MOTO.

NYUMBANI KWA MZEE MAJUTO-ASUBUHI.
Mau, kijana machachari, 24, anafika kwenye nyumba moja iliyopo kati kati ya msongamano wa nyumba kadhaa, anasukuma geti dogo la bati, na kwenda pole pole hadi kwenye kona, anamuona Mzee Majuto, mzee wa makamo, 70, kwenye kona barazani akiwa ameketi kwenye ukingo wa baraza, amejiinamia akionekana yupo kwenye dimbwi la mawazo, huku mkononi akiwa na kikombe chenye chai ya rangi, kwenye mkeka kuna sahani yenye maandazi mawili na thermos, Mau anasimama kwa muda akimuangalia Mzee Majuto, ”shikamoo Mzee” Mau anamshtua Mzee Majuto kwa salamu, Mzee Majuto anashtuka na kuinua kichwa kumuangalia Mau, anabaki akimuangalia Mau bila kujibu chochote huku Mau akijongea kwa Mzee Majuto, “na leo umekuja na miguu?” Mzee Majuto anamuuliza Mau, “kumbe ningemuachia nani miguu yangu?” Mau anajibu huku anaketi kwenye mkeka na kuchukua thermos,anaifungua na kumimina chai akitumia kile kikombe kilichokuwa mfuniko wa ile thermos, “nilishakwambia nabana pesa ili nitafute fremu kariakoo” anasema Mau, “nataka nirudi kwenye kazi yangu ya ufundi wa simu” anaongeza Mau huku kwa shida akijaribu kunywa chai ile ya moto, anachukua yale mandazi mawili kwenye sahani na kuyatia mdomoni yote mawili kwa mpigo “umelala njaa?” Mzee Majuto anamuuliza Mau, Mau bila kujibu huku akipambana kutafuna yale maandazi, Mzee Majuto anabaki anamuangalia “alafu Mama yako ameshaulizia kama umefika zaidi ya mara kumi” anasema Mzee Majuto,“sasa ngoja aje akukute umekaa hapa aanze fujo zake ulalamike anakuonea”, anaongeza Mzee Majuto, “mkeo unamuogopa wewe sio mimi”, anajibu Mau, “shika adabu yako kijana” Majuto anamkaripia Mau, “mimi nataka kukusaidia Mzee” anasema Mau, “heshima ya ndoa ni pesa” anasema Mau huku Mzee Majuto anabaki akimshangaa, “pesa” anasema tena Mau kwa sauti ya msisitizo, “ukipata pesa..uwe unarudi nyumbani na mazagazaga haya manyanyaso yote ya mkeo yataisha” Mau anaendelea kusema huku Mzee Majuto ametulia akimuangalia, “ndio maana kuna dili la pesa nataka nikushirikishe” anasema Mau huku anaitoa simu yake na kuibofya, mara wanasikia sauti ya mlango unafunguliwa, wanashtuka “huyo” anasema Mzee Majuto huku akiinuka kwa haraka, Mau naye anainuka na wote wanaondoka kwa kasi kila mmoja akielekea upande wake, Bi Mwenda anafika pale na kusimama, anaangalia vile vikombe themos na sahani pale juu ya mkeka, “hii mifugo ikishakula inaacha kila kitu hapo hapo” Bi Mwenda anaongea mwenyewe kisha anaondoka.


NYUMBANI KWA MZEE MAJUTO-DUKANI-NDANI.
Mau anapanga boksi za viberiti kwenye shelfu, kwenye duka dogo lililopelea bidhaa na kuacha nafasi nyingi wazi kwenye shelfu zake. Anakuja Mtoto dirishani, “madhiwa nusu” sauti ya yule mtoto inamshtua Mau, anasogea na kupokea bilauri na noti ya mia tano kutoka kwa Mtoto,anachukua kikombe na kuchota maziwa kwenye ndoo na kumimina kwenye bilauri, mara anashtuka na kurudisha yale maziwa tena kwenye ndoo, kisha anachukua sado yenye maji iliyokuwa pembeni na kumimina kwenye ile ndoo ya maziwa na kukoroga, kisha anachukua tena kikombe na kupima maziwa kwenye bilauri na kumpatia yule Mtoto, Mtoto anaondoka, Mau anageuka na kushtuka kumkuta Bi Mwenda amesimama mlangoni,“unafanya ujinga gani?” Bi Mwenda anamuuliza Mau, “sikujua kama upo hapo” anasema Mau, “nimekuuliza unafanya ujinga gani?” Bi Mwenda anauliza tena kwa ukali,“nilisahau kuweka maji kwenye maziwa kama ulivyonielekeza..ndio nimekumbuka sasa hivi nimeweka” anajibu Mau, “sasa nilikwambia uwe unaweka mbele ya Mteja shenzi wewe” Bi Mwenda anasema kwa ukali huku akimsogelea Mau na kumkwida,“alafu wewe nilikuwa nakutafuta sana tu” anasema Bi Mwenda huku akimvurumishia Mau ngumi na mbata mfululizo, “na kazini unakuja muda unaotaka kuku wewe” anatamka Bi Mwenda kwa jazba huku akiendeleza kichapo, kelele za Mau, kipigo na vitu vinavyoporomoka pale dukani vinamfanya Mzee Majuto aje mbio pale dukani, anamkuta bado Bi Mwenda akimtandika Mau, “utamuuwa huyo Mtoto wa watu bure Mama Fei” Mzee Majuto anasema kwa upole huku akiwa amesimama pembeni na gazeti lake mkononi, Bi Mwenda anamuachia Mau, “nimechoka kunyanyaswa mimi” anapayuka Mau, “kwa hiyo unataka kufanya nini?” anasema Bi Mwenda, “na hili likazi lenu silitaki tena” anasema Mau huku anaondoka, “kwenda kule unamtisha nani” Bi Mwenda anamwambia Mau, Mzee Majuto anamfuata Mau, “unaenda wapi?” sauti kali ya Bi Mwenda inamshtua Mzee Majuto, anasimama, “kaa pale” kwa ukali Bi Mwenda anamuamuru Mzee Majuto huku akionyesha kigoda kilichopo barazani, Mzee Majuto pole pole anaenda na kuketi kwenye kigoda.


KWA MZEE MAJUTO-BAADAE.
Bi Mwenda na Mzee Majuto wameketi pale barazani kwenye mkeka, Mzee Majuto anasoma gazeti, Bi Mwenda anafuma kitambaa, “house boy ndio ameondoka hivyo..ujiandae kukaa hapo dukani” anasema Bi Mwenda, Mzee Majuto anageuka na kumuangalia Bi Mwenda bila kusema chochote, “na utafute pesa tufufue hilo duka” anaongeza Bi Mwenda huku akiwa makini na sindano yake akifuma kitambaa, Mzee Majuto anageuka tena kumuangalia Bi Mwenda, “hiyo pesa nitoe wapi Mama Fei?” anauliza Mzee Majuto, “utajua wewe” anajibu Bi Mwenda, “wewe ndio kichwa cha nyumba..tafuta pesa” anaongeza Bi Mwenda kwa ukali, “hivi Mama Fei...” anaanza kusema Mzee Majuto, “hodi” kabla ya kukatishwa na sauti ya Bi Hindu, “karibu shoga” Bi Mwenda anapayuka kwa bashasha huku Bi Hindu akiingia getini, “ahsante shoga yangu” anaitikia Bi Hindu, “Mzee Majuto hujambo?” anasalimu Bi Hindu, “sijambo” anaitikia Mzee Majuto, “enhe..lete habari maana nikishakuona tu najua leo mjini kuna jipya” Bi Mwenda anamwambia Bi Hindu, “yapo mengi..kuna za madale” anasema Bi Hindu, “kuna ya Zari” anaongeza Bi Hindu huku akiketi kwenye mkeka, “lete michapo” anasema Bi Mwenda kwa sauti ya juu iliyojaa shahuku, “hebu anza na ya Zari” anaongeza Bi Mwenda, Bi Hindu anageuka kumuangalia Mzee Majuto ambaye ameacha kusoma gazeti na kumkodolea Bi Hindu macho, Bi Hindu anamgusa Bi Mwenda na kumpa ishara amuangalie Mzee Majuto, Bi Mwenda anamuangalia Mzee Majuto, “hivi huoni kuwa tuna maongezi ya kike hapa?” Bi Mwenda anang’aka, Mzee Majuto anashtuka, anainuka na kuweka gazeti chini na kuondoka huku akivua miwani na kuiweka mfukoni, “alafu ukazurure huko urudi hapa mikono mitupu” anasema Bi Mwenda, “dume suruali” anaongeza Bi Mwenda na kumfanya Bi Hindu kuachia kicheko kikubwa huku wakigongeana mikono, “siku hizi kazini haendi?” anauliza Bi Hindu, “ile kazi basi au deiwaka tu” anasema Bi Mwenda, “ni mpaka bosi azidiwe na kazi ndio amuite ampe elfu kumi” anaongeza Bi Mwenda.


NYUMBANI KWA MAU-NJE-MCHANA.
Mzee Majuto anafika kwenye nyumba moja ya udongo ya chumba kimoja iliyojitenga na zingine zilizopo pembeni, anabisha hodi, mlango unafunguka anatoka Mau huku akiwa anajikanda kanda kwa kitambaa chenye maji kwenye paji lake la uso, Mau anashtuka “umefuata nini wewe Mzee na mlitaka kuniua” anauliza Mau kwa ukali, “ningetaka ufe nisingekuja kukujulia hali” anasema Mzee Majuto, huku Mau akienda na kuketi kwenye benchi lililopo pale nje pembeni ya chumba cha chake, “wewe mwenyewe unajua fujo za yule Mama” anasema Mzee Majuto huku naye akijongea kwenda kuketi kwenye lile benchi, wanabaki kimya kwa muda, “na wewe unamuendekeza sana mkeo” anasema Mau, “anakukashifu..anakupiga vibao”, anasema Mau kisha anakatishwa na Mzee Majuto “aaaa..mambo ya nyumba yangu achana nayo” anasema Mzee Majuto, Mau ananyamaza, wanabaki kimya kwa muda kila mmoja akionekana kutafakari la kwake,“alafu nilishakushauri hakikisha Senga anafukuzwa kazi pale uingie wewe..husikii” anasema Mau, Wanabaki kimya kwa muda, Mzee Majuto anashusha pumzi “ile simu yangu umeshairekebisha?” anauliza Mzee Majuto, “ipo tayari” anajibu Mau, kisha anaingia ndani na kutoka na simu moja chakavu ya smart na kumpatia Mzee Majuto, Mzee Majuto anaibofya huku anatabasamu, “mpaka camera imepona?” anauliza Mzee Majuto kwa mshangao, “ndio maana naitwa Maufundi” anajibu Mau,“na wala usinilipe maana najua huna kitu” anaongeza Mau, Mzee Majuto anakatisha tabasamu na kumkata Mau jicho. Zinapita sekunde kadhaa za ukimya “ni dili gani ulisema unataka kunishirikisha?” anauliza Mzee Majuto, Mau anashtuka “kuna meseji nimepata ya jamaa kule mjini anayeuza dili za hela” anasema Mau huku anaitoa simu yake, “dili za pesa?” anahoji Mzee Majuto kwa kushangaa, Mau anaibofya ile simu na kumpatia Mzee Majuto huku akimuonyesha ule ujumbe uliopo kwenye simu, “hii meseji niliipata tangu wiki iliyopita..ndio maana na kazi yenu siitaki tena” anasema Mau huku Mzee Majuto akiitoa miwani mfukoni na kuvaa, anasoma ile meseji, “hawa ni Matapeli” anasema Mzee Majuto baada ya sekunde chache za kusoma, “wala usijisumbue..utalizwa ulie kama Mtoto mdogo” anaongeza Mzee Majuto huku akimrudishia Mau ile simu, “sasa wewe kaa hapo na una shida ya pesa kuliko hata mimi” anasema Mau huku anainuka, “sasa unaenda wapi?” anauliza Mzee Majuto, “wewe si hutaki dili” anasema Mau huku anaondoka na kumuacha Mzee Majuto ameketi pale kwenye benchi, “eti Mtu akuuzie dili” anaongea mwenyewe Mzee Majuto kwa sauti ya chini, mara Mau anarudi tena, “alafu kesho uje umebonyea pua uniambie Bi Mwenda kanitwanga kichwa” anasema Mau kisha anaondoka, Mzee Majuto anabaki ameduwaa kwa muda, “hebu nisubiri wewe mwehu” anasema Mzee Majuto huku anainuka na kumkimbilia Mau.


JIJINI DAR-ES-SALAAM-POSTA-MACHANA.
Mau na Mzee Majuto wanafika maeneo ya Posta, wanasimama wakiangalia huku na kule, “mimi nimekusindikiza tu lakini sitoshiriki huo ujinga wako” anasema Mzee Majuto, Mau anatoa simu na kuibofya, “nimeshafika” anasema Mau kisha anageuka kuangalia kushoto kwenye benchi la msafisha viatu (shoe shine), anamuona Dude,jamaa mtanashati,40, aliyevalia maridadi shati lililonyooshwa vema,tai shingoni na suruali maridadi nyeusi ya kitambaa, akiwa na simu sikioni akiinua gazeti lake juu kama ishara kwa Mau, huku anainuka na kuelekea walipo Mau na Mzee Majuto, “nyie ndio mmekuja kununua dili?” anauliza Dude baada ya kufika walipo Mau na Mzee Majuto, “ndio” anajibu Mau, “mpo pamoja?” anauliza Dude baada ya kumuona Mzee Majuto, “ndio” anajibu Mau, “sasa ni hivi..kuna dili za elfu hamsini laki moja mpaka za milioni kumi” anasema Dude, “sisi tuna elfu hamsini tu kaka” anasema Mau, “lete hiyo hela” anasema Dude, Mau anatoa pesa na kumpa Dude, “sasa sikizeni..kwanza kwa sasa nyie mnajishughulisha na nini?” anauliza Dude, Mau na Mzee Majuto wanaangaliana, “mimi ni dereva kwa mtu” anasema Mzee Majuto, “Mtu gani?” anauliza Dude, “Mfanya biashara mmoja anaitwa JB” anajibu Mzee Majuto, “JB yule tajiri wa mawe wa Arusha?” anauliza Dude, “ndio hyo..umemjuaje?” anajibu Mzee Majuto na kuhoji, "sisi ndio wenye mji Mzee” anajibu Dude “si yule ambae mke wake mdogo anavaa madhahabu na matanzanite ya gharama?” Dude anauliza tena, “ndio huyo?” anajibu Mzee Majuto, “sasa kumbe pesa mnazo alafu mmezikalia” anasema Dude, “una maana gani?” anauliza Mzee Majuto, “ukibeba cheni mbili tu za yule mama unauaga umsikini” anasema Dude, Mzee Majuto na Mau wanabaki wameduwaa “beba cheni mbili tatu peleka kwa Sonara Masawe upewe mamilioni yako” anasema Dude, “ila umwambie Masawe umetumwa na Dude ili asikusumbue” anaongeza Dude, “mimi nimemaliza” Dude anasema huku anaondoka kuelekea usawa wa Feri na kutokomea, Mau na Mzee Majuto wanabaki wamesimama wanaangaliana,“si nilikwambia” anasema Mzee Majuto huku anaondoka, Mau naye anamfuata.


NYUMBANI KWA MAU-NJE-MCHANA.
Mzee Majuto na Mau wanafika pale kwenye benchi na kuketi, wanabaki kimya kwa muda, “kuna wakati huwa najiuliza ni kwa nini Mungu aliumba wajinga” anasema Mzee Majuto huku ameinamisha kichwa, “leo ndio nimejua ni ili wengine waishi” anaongeza Mzee Majuto, Mau anabaki anamkata Mzee Majuto jicho, “ni kama Nyumbu na Simba wanavyoshirikiana porini” anaongeza Mzee Majuto, Mau anashusha pumzi bila kuongea chochote, baada ya kimya kifupi “ningejua unanipeleka kwa mpumbavu kama yule nisingekufuata” Mzee Majuto anamwambia Mau, wanabaki kimya kwa sekunde kadhaa, simu ya Mzee Majuto inaita, anaipokea, “hallow bosi” Mzee Majuto anajibu simu kwa sauti ya utiifu, “uwanja wa ndege?… ok nakuja sasa hivi bosi” Mzee Majuto anasema huku anainuka, “mi ngoja nifukuzie tu hizi elfu kumi kumi zangu..wewe endelea na huyo tapeli wako” Mzee Majuto anasema huku anaondoka, Mau anabaki ameketi akimsindikiza Mzee Majuto kwa macho, “ndio maana mkeo anakudunda” anasema Mau kwa sauti ya chini, Mzee Majuto anarudi, “umesemaje?” Mzee Majuto anamuuliza Mau, “nimesema kila la kheri” anajibu Mau, “nilishakwambia shika adabu yako” Mzee Majuto anamwambia Mau huku akimnyooshea kidole, kisha anaondoka.


JIJINI DAR-ES-SALAAM-UWANJA WA NDEGE-MCHANA.
Gari nyeupe, Toyota Vx, inafika parking ya uwanja wa ndege ikiendeshwa na Mzee Majuto, inafika na kusimama, wanateremka JB, Mzee Majuto, Stiv mtoto wa kiume ,11, na Semi, mtoto wa kike, 13, “fundi Beka atakuja kesho kufanyia hii gari service” anasema JB, “sawa bosi” anajibu Mzee Majuto huku anatoa mabegi kwenye buti, “utarudi Dar lini bosi?” Mzee Majuto anamuuliza JB, “baada ya wiki mbili..kwa nini?” anajibu JB na kuuliza swali, “kuna kitu nilitaka ufahamu bosi” anaongeza Mzee Majuto, “kuhusu nini?” anauliza JB, Mzee Majuto anawaangalia Stiv na Semi wamesimama mita kadhaa kutoka pale, anamsogelea JB, “ni kuhusu yule Dereva Senga” anasema Mzee Majuto kwa sauti ya chini, “amefanya nini?” anauliza JB, “yule jamaa naona kama yupo karibu sana na Mama Stiv” anasema Mzee Majuto, “sina imani nae kabisa” anaongeza Mzee Majuto, JB anabaki anamuangalia Mzee Majuto kwa sekunde kama tano hivi bila kuongea neno, “ina maana unamtuhumu Mke wangu mama Stiv?” anauliza JB kwa mshtuko, “hapana sijasema ni..” Mzee Majuto anajaribu kujieleza kabla kukatishwa na JB, “sikia Mzee” anasema JB, “naomba ufanye kazi yako..yasiyokuhusu achana nayo” JB anasema kwa ukali, “sawa bosi..nimekosa” anasema Mzee Majuto huku anaondoka kwa haraka akikokota Mabegi kuelekea jengo la uwanja wa ndege, JB anabaki anamsindikiza kwa macho makali, “ala" anasema JB kwa ukali, “jitu zima umekalia umbea tu” anasema JB huku bado anamuangalia Mzee Majuto anavyoelekea jengoni..


NYUMBANI KWA JB-MCHANA.
Masai Nyotambofu ameketi ndani ya geti anasinzia, anashtushwa na mlio wa honi ya gari, anakurupuka na kufungua geti kumruhusu Mzee Majuto aingie na gari, Gari inaingia na kusimama, Mzee Majuto anateremka, anafunga mlango na kugeuka barazani anamuona Senga, bwana wa makamo, 48, akiwa amevalia shati na suruali ya kitambaa kwa mtindo maarufu unaoitwa mayenu, akiwa amesimama barazani kwa mikogo na sigara ikiwa mdomoni, Mzee Majuto anasimama kimya kwa sekunde kadhaa akimuangalia Senga kwa hali ya jazba, kisha pole pole anajongea alipo Senga, “alafu wewe mjinga nakwambia mwisho wako utakuwa mbaya sana” anasema Mzee Majuto huku akifika alipo Senga na kusimama, “fuata maisha yako we Mzee achana na mimi” anajibu Senga kwa ukali, kabla Mzee Majuto kutoa neno mlango unafunguka, anatoka Aunty,au Mama Stiv, mke mdogo wa JB,mwanamke mrembo sana, 29, Aunty anamuangalia Mzee Majuto, “nini shida?” anauliza Aunty, “hamna shida madam” anajibu Mzee Majuto kwa sauti ya utiifu huku akiondoka eneo lile, “twende” Aunty anamwambia Senga kisha wanaelekea kwenye gari aina ya Prado, nyeupe iliyopo pale parking, huku Senga akimkata Mzee Majuto jicho kwa dharau na ukali, Aunty na Senga wanaingia kwenye gari,Masai Nyotambofu anafungua geti na gari inatoka,Mzee Majuto anaenda alipo Masai Nyotambofu “huyu pimbi ipo siku nitamzibua mbele ya huyu Mama” Mzee Majuto anamwambia Masai Nyotambofu, “nilimsikia Madam anamuita jamaa mauno feni” anasema Masai Nyotambofu kwa lafudhi yake ya kimasai, “mauno nini?” anauliza Mzee Majuto kwa mshtuko, “mauno feni” anarudia tena Masai Nyotambofu, Mzee Majuto anabaki mdomo wazi akimuangalia Masai Nyotambofu.


NYUMBANI KWA JB-NJE-USIKU.
Saa mbili usiku, Masai Nyota mbofu ameketi ametulia akiimba nyimbo zake za kinyumbani, geti linagongwa, anainuka na kukimbilia getini, “nani?” anauliza Masai Nyotambofu, “mimi” anajibu Senga, “Senga unataka nini saa hizi?” anauliza Masai Nyotambofu kwa ukali, “acha maswali ya kipuuzi” anajibu Senga kwa dharau, “mpigie Msee ndio anipigie nikufungulie” anasema Masai, Senga anashusha pumzi kisha anaitoa simu yake na kuibofya.


NYUMBANI KWA JB-NDANI-USIKU,
Aunty yupo sebuleni kwenye kochi amejilaza akiangalia tamthilia ya kifilipino kwenye TV, simu juu ya meza inaita, anainuka na kuipokea, “hallow” Aunty anajibu simu, “naona huyu Njeree ananizengua hapa getini” sauti ya Senga inasikika kwenye simu, “ok subiri hapo hapo” Aunty anamwambia Senga, huku akiinuka na kwenda jikoni, anachukua glasi, anafungua friji na kutoa geleni yenye juisi na kumimina kwenye glasi ujazo wa robo tatu ya glasi, kisha anachukua sabuni ya maji na kumimina kiasi kidogo kisha anachukua baking powder nusu kijiko na kuweka kwenye glasi, anachukua kijiko na kukoroga kwa nguvu kisha anachukua ile glasi na kutoka.


NYUMBANI KWA JB-NJE-USIKU.
Masai Nyotambofu ameketi akiimba nyimbo za kimasai, “rafiki” Masai Nyotambofu anashtushwa na sauti ya Aunty,“ee” anashtuka na kuitika huku anageuka kumuona Aunty akija na glasi mkononi, “nimekuletea juisi” anaongeza Aunty huku akifika na kumpa Masai Nyotambofu ile glasi, “alijuaje ana kiu kweli leo” anasema Masai Nyotambofu kwa bashasha huku akiinuka na kupokea ile glasi, “mimi nakujali sana eti” anasema Aunty kwa sauti ya upole kisha anageuka na kurudi zake ndani, Masai akiwa mwenye furaha anaketi na kuanza kunywa ile juisi funda baada ya funda huku akiongea mwenyewe maneno ya kikwao yanayoashiria kuwa anaburudika vilivyo na kinywaji kile, Aunty anafika ndani na kusimama dirishani akimchungulia Masai.
Zinapita dakika kadhaa, Masai Nyotambofu anaanza kukunja uso huku anajishika tumbo akionekana ni mtu mwenye maumivi makali,anainuka na kuelekea nyuma ya nyumba kwa mwendo wa kasi.
Aunty anatoka na kwenda getini kufungua geti, Senga anaingia, wanakumbatiana kisha wanaelekea ndani.


NYUMBANI KWA JB-NJE-ASUBUHI.
Mzee Majuto anafika, anasukuma geti na kuingia, anasita kidogo huku akiangalia huku na kule, “Masai” anaita Mzee Majuto huku akizidi kuangalia huku na kule, “Masai” anaita tena Mzee Majuto na kuelekea nyuma ya nyumba, anafika na kumuona Masai amelala kwenye majani pembeni ya kilipo choo cha nje, “Masai” Mzee Majuto anaita, “umevimbiwa?” anauliza Mzee Majuto huku akijongea pale alipolala Masai Nyotambofu, Nyotambofu anagugumia maumivu, Mzee Majuto anashtuka, “Masai vipi?” anauliza Mzee Majuto, “tumbo imefuruga kweli usiku yote” anajibu Masai Nyotambofu kwa sauti dhoofu, “nini kimetokea?” anauliza Mzee Majuto huku akiinama ple kwa Masai “sijui” anajibu Masai Nyotambofu, “hii hali yako sio nzuri” anasema Mzee Majuto huku akimuinua Masai na kumkokota kutoka nje ya geti, wanatoka na kusubiri kidogo, inapita Bajaji, Mzee Majuto anapunga mkono, Bajaji inasimama, anamsaidia Masai kuingia kwenye Bajaji na kuondoka.


NYUMBANI KWA JB-NJE-SAA TANO USIKU.
Mzee Majuto ameketi kwenye kiti pembeni ya geti akisinzia, honi ya gari inamshtua, anakurupuka kwa mshtuko na kuanguka kutoka pale kitini huku anatoa macho, anainuka na kutulia kwa sekunde chache, honi inalia tena, Mzee Majuto anakwenda getini na kufungua geti, anamuona Aunty akishuka kutoka kwenye taxi, Aunty anaingia getini akiwa anaonekana amelewa, “hee..mbona wewe ndio uko huku saa hizi?” Aunty anauliza kwa sauti ya kuvuta maneno kuashiria amekolea kinywaji, “Masai leo amepumzika hajisikii vizuri” anajibu Mzee Majuto, “mbona ajanijulisha?” Aunty anauliza, “ameanza kucheza na kazi sio?” anaongeza Aunty huku akitembea kwa shida kuelekea mlangoni, anafika mlangoni na kuanza kuhangaika kufungua mlango, Mzee Majuto anasimama akimuangalia kwa muda kisha anaenda na kumsaidia kufungua huku akimshika mkono na kumsaidia kuingia.


NYUMBANI KWA JB-NDANI-USIKU.
Mzee Majuto anamshika Aunty kumsaidia mpaka pale sebuleni, anamuachia na Aunty anajikongoja kuelekea mlango wa chumbani, anafika mlangoni na kuanza tena kuhangaika kuufungua mlango wa chumba, Mzee Majuto anabaki akimuangalia kwa muda kisha anaenda tena kumsaidia, anafungua mlango na kumsaidia Aunty mpaka kilipo kitanda na kumkalisha juu ya kitanda, Aunty anajilaza kitandani akiwa amelegea mwili mzima, Mzee Majuto anashusha pumzi na kutikisa kichwa kwa kusikitika, kisha anageuka na kuangalia kwenye dressing table, anaona mikufu kadhaa ya dhahabu, Tanzanite, silver ikiwa juu ya ile meza, anabaki ameduwaa,anaisikia ile sauti ya Dude kichwani, anageuka na kumuangalia Aunty pale kitandani, Aunty yupo kwenye usingizi mzito akikoroma, Mzee Majuto anasogea mezani na kubeba mikufu mitatu ya dhahabu na polepole anatoka na kuufunga mlango.


KWA SONARA MASAWE-ASUBUHI.
Mzee Majuto akiongozana na jamaa mmoja, wanafika mita kadhaa kutoka ulipo mlango ulioandikwa SONARA MASAWE, “ni pale” anasema Jamaa huku akionyesha kidole ulipo mlango, “nashukuru sana mwanangu” anasema Mzee Majuto huku akielekea ulipo mlango, “buku yangu Mzee?” anauliza Jamaa, “kafanye kazi acha ujinga” anasema Mzee Majuto huku anafika mlangoni na kuingia, Jamaa anabaki amejishika kiuno, “hawa Wazee wa siku hizi sio kabisa” Jamaa anaongea mwenyewe kisha anashusha pumzi na kuondoka.
Mzee Majuto anafika, Sonara Masawae, jamaa aliyeshiba na kitambi kikubwa na upara, 30, “Mzee karibu” anasema Masawe, “nina mzigo” anasema Mzee Majuto huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa mikufu mitatu ya dhahabu na kuipitisha kwenye kadirisha kadogo, Masawe anaipokea na kuiangalia kwa muda akitumia vifaa vilivyopo mezani kisha anamuangalia Mzee Majuto, “umeipata wapi?” Masawe anamuuliza Mzee Majuto, Mzee majuto anashtuka na kubaki kutoa macho, “nimeagiziwa na yule jamaa yako Dube” anasema Mzee Majuto kwa kigugumizi, Masawe anabaki kimya akimuangalia Mzee Majuto, "Dude" anasema Masawe, "huyo ee" anasema Mzee Majuto “nakupa milioni tatu kwa yote” Masawe anamwambia Mzee Majuto, Mzee Majuto anabaki kimya ameduwaa, “au vipi uondoke nayo” anasema Masawe, “sawa” Mzee Majuto anajibu kwa haraka kabla Masawe kumalizia alichokuwa anasema, Masawe anaingia chumba kilichopo pembeni, zinapita sekunde kadhaa kisha anarudi akiwa na maburungutu kadhaa ya pesa, anaweka kwenye mashine ya kuhesabu iliyopo pale mezani, baada ya kuhesabau “ona” anasema Masawe huku akimuonyesha Mzee Majuto namba zinazoonekana kwenye screen ya mashine, Mzee Majuto anaangalia zile tarakimu na kutikisa kichwa akiashiria amekubaliana nayo, Masawe anazitoa pesa kwenye mashine na kuzifunga kwenye mafungu matatu ya milioni moja moja, anamuangalia Mzee Majuto kuhakikisha haoni kwa chini, anachukua chip mfano wa simcard ya simu na kuichomeka kati kati ya bunda moja la pesa, “una kwa kubebea?” Masawe anamuuliza Mzee Majuto, “hapana” anajibu Mzee Majuto, Masawe anainama chini na kutoa begi moja dogo la mgongoni, anaziweka zile pesa na kumpatia Mzee Majuto lile begi, Mzee Majuto anaondoka, Masawe anachukua simu na kuibofya kisha anaiweka sikioni, “Dude..Muzee ya kazi” anasema Masawe, “sema mkubwa Masawe” inasikika sauti ya Dude kwenye simu, “sasa kuna boya mmoja ulimuagiza kwangu..nimempa m tatu sasa hivi” anasema Masawe, “nimeweka ile GPS tracker..kwa hiyo kazi kwako kutrack mzigo” Masawe anamwambia Dude kwenye simu, “kumbuka kurudisha chip yangu” anaendelea Masawe, “usikonde mkubwa” inasikika sauti ya Dude kwenye simu, “kila la kheri” anasema Masawe kisha anaitoa simu sikioni, mlango wa pembeni unafunguka, anatoka Moze, Moze anaangalia ile mikufu pale mezani, “huu mzigo ndio umempa m tatu?” Moze anamuuliza Masawe, “mjini hapa..Mzee mwenyewe boya boya tu” Masawe anamwambia Moze, Moze anacheka kwa sauti ya juu, “Masawe nimekukubali” anasema Moze huku akiendelea kucheka na kuondoka kurudi chumba alichotoka.


NYUMBANI KWA MAU-MCHANA.
Mzee Majuto anafika akiwa na begi lake mgongoni, “Mau” Mzee Majuto anaita kwa sauti ya juu, huku akisukuma mlango na kuingia, Mau yupo mezani akichokonoa moja ya smart phone iliyochambuliwa juu ya meza yake ndogo, “kuna nini?” anauliza Mau kwa mshtuko huku anainuka, Mzee Majuto anatoa lile begi mgongoni, anasogea na kusukuma mlango kuhakikisha umefungwa, anafungua begi na kumimina mabunda juu ya kitanda, Mau anapatwa na mshangao mkubwa, “umepata wapi?” anauliza Mau kwa mshangao huku akibaki ameduwaa,”ule ushauri wa mikufu” anasema Mzee Majuto, “duh” anasema Mau, wanabaki kimya kwa sekunde chache,“sasa tusipaniki” anasema Mau, “tukae tupange mikakati” anasema Mau, Mzee Majuto anashtuka na kumuangalia Mau, “upange na nani?” anauliza Mzee Majuto, “si mimi na wewe” anajibu Mau, “mikakati bila mke wangu?” anasema Mzee Majuto, “mke wako?” anauliza Mau kwa mshtuko, “Yule kichwa cha panzi anajua nini zaidi ya kupiga domo?” anasema Mau, Mzee Majuto anabaki kimya kama aliyepatwa na shoti ya umeme akimuangalia Mau, “we si nilishakukanya kuhusu kumsema mke wangu vibaya?” anasema Mzee Majuto, “ok sorry” anasema Mau, huku Mzee Majuto pole pole anaketi kitandani kama Mtu anayehisi uchovu wa mwili, “unajua kabisa yule Mwanamke ndiye barafu ya moyo wangu?” Mzee Majuto anasema kwa sauti ya upole iliyojaa hisia, “si nimeshakuomba msamaha mzee” anasema Mau kwa upole, Mzee Majuto anainuka na kukusanya zile pesa na kuzirudisha kwenye begi, “Mke wangu ndiye atatoa mwongozo wa hizi pesa” anasema Mzee Majuto huku anafunga zipu ya begi, Mau anabaki ameduwaa, Mzee Majuto anajishika tumbo, “maneno yako mabaya mpaka yamefanya tumbo langu linakata” Mzee Majuto analalamika huku akijishika tumboni, “nielekeze msalani kwanza” anasema Mzee Majuto huku ameinama kuashiria ana maumivu, “hapo nje upande wa kulia” anasema Mau, Mzee Majuto anatoka, Mau anabaki ameduwaa kwa muda, “yaani pesa nimeshaziona alafu zitoke kwenye upeo wa macho yangu?” Mau anaongea mwenyewe, anainuka, anachukua begi anafungua zipu, anainua godoro na kumimina pesa zote chini ya kitanda, “huyu Mzee hanijui” anasema Mau huku akikusanya matambara na makaratasi yaliyopo pale chumbani na kuweka ndani ya begi, kisha anaketi na kutulia.


BARABARANI-MCHANA.
Dude na Mpoki wapo juu ya Pikipiki, Mpoki anaendesha huku Dude yupo nyuma akitumia simu yake ya smart kutafuta uelekeo wa chip,“tunakaribia..ongeza mwendo” Dude anamuhimiza Mpoki, “usikonde baba” anasema Mpoki huku akiongeza mwendo.


NYUMBANI KWA MAU-MCHANA.
Mau ameketi juu ya kitanda, Mzee Majuto anaingia, “uko fiti?” anauliza Mau, Mzee Majuto anashusha pumzi, “kiasi afadhali” anasema Mzee Majuto huku anainua lile begi, anasita kidogo akijaribu kutikisa lile begi kuhisi uzito, Mau anaonekana na wasiwasi huku akimuangalia Mzee Majuto kwa kuibia, Mzee Majuto anaweka begi mgongoni, "nitakupa mrejesho baada ya kujadiliana na mke wangu" anasema Mzeee Majuto na kutoka, Mau anatulia kwa sekunde kadhaa, anainuka na kwenda kufungua mlango na kuchungulia nje, anafunga mlango na kuweka komeo kisha anarudi na kuinua godoro, anatoa bunda moja na kuliangalia huku anatabasamu kwa bidii, mara mlango unagongwa, Mau anashtuka na kutoa macho, kwa haraka anarudisha lile bunda chini, anarudishia godoro na kuinuka, “nani?” anauliza Mau kwa uoga, kabla ya kupata jibu mlango unapigwa teke na kufunguka, anaingia Dude na Mpoki wakiwa wamevaa viziba uso na kuacha macho tu, Mpoki ana bastola mkononi “pesa ziko wapi?” anauliza Dude, “pesa gani?” anauliza Mau, Mpoki anampiga Mau ngumi ya kichwa, Mau anapata kizunguzungu kikali na kwenda chini kama mzigo, Dude akiwa na simu yake mkononi ikitoa mlio kuashiria chip ipo karibu, anaenda na kupekua juu ya kitanda, anainua godoro, “bingo” Dude anapayuka huku kwa haraka anainua shuka kutoka kitandani na kukusanya maburungutu na kuyazungushia kwenye shuka ile na kutoka kwa haraka, Mpoki anamuinua Mau pale chini na kumtandika tena ngumi mbili zote kwenye paji la uso na kumuachia Mau akienda chini mzima mzima, "siku nyingine ukitembelewa na Wanaume onyesha ushirikiano Ndezi wewe" anasema Mpoki kisha anatoka.


NYUMBANI KWA MZEE MAJUTO-NDANI-MCHANA.
Mzee Majuto anaingia akiwa na begi lake mgongoni, Bi Mwenda yupo sebuleni ameketi akiweka tambi kwenye jiko la mchina, “ulikuwa wapi siku nzima” Bi Mwenda anashtuka na kumuuliza Mzee Majuto, Mzee Majuto anatabasamu, Bi Mwenda anamshangaa, “usikute umekunywa pombe maana sikuelewi” Bi Mwenda anamwambia Mzee Majuto, huku Mzee Majuto kwa mikogo analitoa begi mgongoni na kumpatia Bi Mwenda, “fungua mwenyewe” Mzee Majuto anamwambia Bi Mwenda, Bi Mwenda huku bado anamshangaa Mzee Majuto, anachukua lile begi na kufungua, anaangalia ndani huku amebaki na mshangao, anageuza begi na kumimina makaratasi na matambara chini huku akikung’uta lile begi, Mzee Majuto anabaki amekodoa macho, anaanguka na kupoteza fahamu.


NYUMBANI KWA MAU-SIKU NYINGINE-NJE-MACHANA.
Mau na Mzee Majuto wameketi wakiwa na sahani yenye mihogo na vikombe vya maji kila mmoja, Mau akiwa amevimba jicho na uvimbe mkubwa kwenye paji la uso, “sifanyi tena wizi” anasema Mzee Majuto, “bahati haikuwa yetu” anasema Mau, “yale sijui ni mazingaombwe?” anasema Mzee Majuto, wanabaki kimya kwa muda, “unasema umeangukiwa na nini?” anauliza Mzee Majuto, “nimeng’atwa na nyigu” anasema Mau, “pole sana” anasema Mzee Majuto, wanabaki kimya kwa muda, “kilichobaki sasa ni kumshughulikia tu yule Mwehu pale kwa JB” anasema Mzee Majuto, “tena kuhusu huyo jamaa yako kuna mbinu nimeipata” anasema Mau, “mbinu gani?” anauliza Mzee Majuto, “nina Camera ya smartphone..tukaifunge pale ndani kwa JB” anasema Mau, Mzee Majuto anabaki anamuangalia Mau kwa muda kisha anatabasamu, “inawezekana?” anauliza Mzee Majuto kwa bashasha, “mimi ndio Maufundi baba” anasema Mau kwa mikogo.


KATIKATI YA JIJI-WIKI MBILI BAADAE-SK HOTEL.
JB, Mzee Majuto na Mau wapo mezani, JB akiwa na Lap Top mbele yake, Mzee Majuto na Mau wakiwa na sahani zilizosheheni maakuli, wakiwa bize na uma na kisu huku JB anaangalia Lap top na kujifuta machozi kwa leso, “yaani hiki ndio kinachoendelea ninapokuwa sipo?” anasema JB kwa sauti ya uchungu, “na hapo ni vile tuliweka hiyo camera sebuleni" anasema Mzee Majuto,"tungeiweka kule chumbani ungekufa kwa presha” anaongeza Mzee Majuto, “huyo jamaa anaitwa mauno feni” anasema Mzee Majuto, JB anabaki ameduwaa mdomo wazi, “na tumetumia hiyo mbinu kwa sababu nimeona nikikwambia kwa mdomo huniamini” anazidi kusema Mzee Majuto, JB anabaki kimya akitafakari, Mzee Majuto na Mau wanaendelea kufakamia msosi. “kuanzia leo wewe Mzee utachukua ile kazi ya huyu mjinga” anasema JB, Mzee Majuto anatabasamu, “na jioni nitawapatia milioni tatu tatu..kwa sababu mmeniepusha na janga kubwa sana” anaongeza JB, Mzee Majuto na Mau wanaangaliana na kutabasamu, “na yule mwehu lazima nitamnyoosha ashike adabu” anasema JB kwa hisia kali.


NYUMBANI KWA MZEE MAJUTO-JIONI.
Bi Mwenda ameketi barazani akipata maakuli ya ugali na dagaa, anashtushwa na mngurumo wa Bajaji nje, mara anaingia Mzee Majuto akiwa na mifuko miwili iliyosheheni mazagazaga pamoja na kibegi kimoja cha ukubwa wa wastani alichokikumbatia vilivyo kwenye kwapa lake, Mzee Majuto anaweka mifuko ile mbele ya Bi Mwenda kisha anafungua kile kibegi kidogo kumuonesha Bi Mwenda, kwa sekunde kadhaa Bi Mwenda anabaki ameduwaa akiangalia mabulungutu kwenye lile begi, Bi Mwenda anainuka na kumkumbatia Mzee Majuto, “mume wangu” anasema Bi Mwenda huku akipiga vigelegele na kutumia kanga yake kumfuta Mzee Majuto jasho usoni, “pumzika mume wangu jamani” anasema Bi Mwenda kwa sauti iliyojaa mahaba huku akimuongoza Mzee Majuto na kumketisha kwenye kiti, “nikupikie nini?” anauliza Bi Mwenda, “kwenye mfuko kuna mchele..kuna nyama” anasema Mzee Majuto, Bi Mwenda anachukua ile mifuko na kuingia ndani akimuacha Mzee Majuto na tabasamu kali usoni, akijinyoosha na kuchukua gazeti kutoka mfukoni kwake na kuanza kulisoma.
Sekunde chache baadae anakuja Bi Mwenda na kikombe cha chai, Mzee Majuto anaangalia kikombe, “nani kakutuma chai” anasema Mzee Majuto, “si nimeona upashe kwanza wakati unasubiri chakula” anasema Bi Mwenda kwa unyenyekevu, “niwekee maji ya kuoga..sitaki chai mimi” anasema Mzee Majuto, “haya mume wangu” anasema Bi Mwenda huku akichukua kile kikombe na kuondoka, Mzee Majuto anarudi kusoma gazeti lake.


MTAANI-MIEZI KADHAA BAADAE-MCHANA.
Mzee Majuto anaenda ilipo gari aina ya Prado, anafungua mlango wa nyuma, “we zoba” anaita Mzee Majuto, anakuja Senga akiwa na tambara na ndoo mkononi,“hivi ndio umeosha” anasema Mzee Majuto kwa sauti ya ukali, “nimeosha Mzee” anasema Senga kwa unyonge, “hebu osha vizuri la sivyo sikulipi” anasema Mzee Majuto kwa ukali, Senga anaingiza tambara kwenye ndoo ya maji na kufuta gari, “ala” anasema Mzee Majuto huku ameweka mikono mfukoni, “unadhani hela zinaokotwa sio” anasema Mzee Majuto huku akienda huku na kule kwa mikogo.


MWISHO.
 
Wakati tunamuombea Mzee wetu apate matibabu mema na arudi salama kusukuma gurudumu...tuburudike na hii kutoka kwa Msanii joto la moto.
 
Back
Top Bottom