Mawaziri, wabunge kutinga kortini kwa mikopo ya CIS
By Exuper Kachenje
Source: Mwananchi
Date: 2/7/2009
WAKATI vumbi la baadhi ya watuhumiwa wa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), halijatua huenda baadhi ya mawaziri, wabunge na vigogo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakaanza kuburuzwa mahakamani kutokana na kudaiwa kuchota jumla ya Sh199 bilioni za serikali kupitia Mpango wa Uingizaji Bidhaa kutoka Nje (CIS).
Habari ambazo Mwananchi Jumapili inazo zinaonyesha kuwa, miongoni mwa wadaiwa wa mfuko wa CIS wamo mawaziri, wabunge, makada wa CCM na wafanyabiashara wengine maarufu.
Juzi kampuni ya Msolopa Investment Ltd, iliyopewa jukumu la kukusanya fedha zilizochotwa na wajanja kupitia mfuko wa CIS, chini ya mkurugenzi wake, ilitaja kampuni 30 zilizochota fedha za mfuko huo na kueleza kwamba, zitachukuliwa hatua ikiwamo kufikishwa mahakamani ndani ya siku 14.
Habari za ndani ya kampuni hiyo zinathibitisha kuwa miongoni mwa wamiliki wa kampuni zilizojichotea fedha kupitia mfuko huo ni mawaziri, wabunge na makada wa Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mkurugenzi wa kampuni ya Msolopa Investiment Ltd, Ibrahim Msolopa, alikiri baadhi ya wamiliki wa kampuni zinazodaiwa kuwa ni mawaziri, wabunge na makada wa CCM.
"Ni kweli, wamo vigogo walio serikalini, hilo siwezi kuficha, mawaziri, wabunge na wengine ni makada wa Chama Cha Mapinduzi, hiyo sifichi wamo," alisema Msolopa.
Alisema kati ya kampuni 916 zilizokopa fedha hizo tayari kampuni yake imezifikia kati ya kampuni 300 na 400 na kubainisha kwamba, miongoni mwa kampuni hizo zipo zilizoanza kulipa madeni na nyingine zimegoma.
Alifafanua pia baadhi ya kampuni hizo zipo katika mazungumzo na kampuni yake kuhusu utaratibu wa kulipa madeni yao, na kampuni yake itakamata mali za wadaiwa na zisipokidhi madeni yao hatua zaidi zitachukuliwa.
Mkurugenzi huyo alisema wadaiwa wasiolipa ni watu wanaokabiliwa na adhabu kwa kuwa walichofanya ili kujipatia fedha hizo za CIS, ni ugaidi kwa staili ya kukopa fedha za serikali.
"Bahati mbaya watu hawa walikopa fedha za serikali, nategemea tuliowataja watachukua hatua ya kulipa madeni yao katika muda tuliowapa, wasiolipa wanakabiliwa na adhabu, hii si mzaha wameichezea nchi," alisema Msolopa.
Aliongeza kuwa suala hilo ni zito na serikali haifanyi mchezo, pia akaonya kwamba kama ilivyokuwa kwa watuhumiwa wa EPA, wadaiwa wa CIS wasiolipa watapitiwa na mkondo wa sheria.
"Jela si Sheraton, hapafai, ilionekana kama mzaha kwa watuhumiwa wa EPA wakafikishwa mahakamani wakala rumande, na hawa wa CIS sheria haitawakwepa, nawasihi walipe madeni yao waepuke mkono wa sheria," alisema Msolopa.
Alibainisha, zoezi la kutaja kampuni zanazodaiwa linaendeshwa kwa awamu na kwamba, baadaye kampuni yake itatangaza wadaiwa wengine.
Fedha hizo zilitolewa na wahisani mbalimbali ili kuipa uwezo serikali kuimarisha uchumi wake na zilikopwa na wafanyabiashara hao kati ya mwaka 1980 hadi mwaka 1993.
Baadhi ya kampuni zilizotajwa na wakala huyo wa kukusanya madeni ni pamoja na Kiex Trading Limited inayomilikiwa na Rajab Maranda, anayetuhumiwa kuiba fedha za EPA, Dar es Salaam International School Trust Fund, Andrew Traders, K. Agencies International, Chawe Transport, Simba Resources, Shela Beach Investment na Chichi Interprises.