Chumbia binti mpenda vitabu

Ado Shaibu

Member
Joined
Jul 3, 2010
Posts
99
Reaction score
111
CHUMBIA BINTI MPENDA VITABU



Hii ni kwa vijana wanaopenda kuoa! Ukitaka kuoa, chumbia Binti Mpenda Vitabu ( BMV)

Kwa nini?

Wa kazi gani?

Utampata wapi?

Unaweza kumpata Maktaba akihangaika na vitabu vyenye vumbi na harufu kali ichomayo puani; vitabu ambavyo vimeuvaa uajuza na ushaibu kwa kutofunuliwa siku nyingi.

Waweza pia kumkuta kwenye maduka ya vitabu akinunua vitabu. Ukisikia kuna uzinduzi wa kitabu sehemu au mjadala wa Kitabu Nilichosoma, Jongea maeneo hayo kwa vile BMV hawezi kukosa! Nenda tu hata kama hupendi vitabu!

Ukibahatika kukutana naye kwenye daladala, yu nawe siti ya jirani, lazima atakuwa kashika kitabu. Usishangae kwa nini hakusemeshi; kitabu humtia mtu upofu asione cha jirani.

Tafadhali, usimsemeshe mambo yasiyo na kichwa wala maiguu..mara dada habari..waitwa nani..waenda wapi? Hutopata mwitikio mzuri.

Kama wataka kumnasa, msalimie kisha zungumza naye kuhusu kitabu…''Samahani..hii ni fiction au non fiction? Yaelekea ni kizuri eeeh? Kinahusu nini? ''

BMV hupenda kuulizwa mambo ya vitabu. Jitahidi kadiri ya uwezo wako mazungumzo yako yajikite kwenye vitabu. Tupa ndoano ya kuazima kitabu..atakupa mawasiliano. BMV hupenda wapenda vitabu.

Endelea kuwasiliana naye. Nakusihi, kwenye mazungumzo yenu, habari ya vitabu iwe mbele. Mchunguze vitabu avipendavyo. Aweza kuwa mpenzi wa fasihi..Tuchukulie ni mpenzi wa fasihi. Basi jitahidi ujikite hapo.

Ni siku yake ya kuzaliwa. Unapanga kumfanyia nini? Keki? Kadi? Unasema unataka kumnunulia simu ya kisasa halafu umpeleke outing pale Samaki Samaki au Del Monte?

Haya yote ni mazuri lakini hayataacha alama moyoni mwa BMV. Ngoja nikueleze. Unakifahamu kitabu kipya kilichotoka karibuni? Yaweza kuwa amekwishawahi kukitaja kwamba kikiingia madukani atakinunua.

BMV hutumia sehemu ya pesa yake kununua vitabu. Basi chunguza kama hajakinunua. Nenda kakinunue kisha kiweke kwenye bahasha yenye urembo mzuri.

Mwambie kwamba ungependa kutoka naye outing. BMV hupenda pahala tulivu. Mpeleke ufukweni au Soma Book Cafe kwa Demere Kitunga . Amini nakuambia, atafurahi mno kuliko unavyodhani.

Zungumza naye. Kumbuka nilivyokuhusia, mazungumzo yenu yahusu vitabu. Kisha m-suprise kwa zawadi. Mweleze afumbe macho…eeh unataka kumvisha pete? Acha kabisa.

Usifanye hivyo sasa, haraka haraka haina baraka. Toa kitabu ulichonunua kutoka kwenye mkoba wako kisha kiweke mezani. Mwambie kuna zawadi yake mezani, aotee ni zawadi gani. Usidhani ni mbashiri akipata.

BMV ametawaliwa na vitabu kichwani. Mwambie afumbue macho kisha achukue zawadi yake kwenye bahasha! Akifungua na kukuta kitabu chenyewe ni kile akipendacho, tarajia maneno haya ''U're sweet…u're wonderful…Ahsante!

Usishangae, BMV huthamini vitabu kuliko chochote. Acha siku hiyo ipite. Siku nyingine, muombe musome kitabu pamoja au akusimulie kitabu chake pendwa. Fanyeni haya ufukweni.

Siku hiyo, waweza kumueleza kiu yako, kiu ya kuwa naye maishani. Usidhani maneno yako matamu yatamduwaza; ameshasoma mengi.

Ameshasoma vitabuni ahadi za wanaume wanaohadi kutoa milima na mito wakikubaliwa au wale wanaoahidi magari huku wangali makapuku wa kutupwa. Ameshavisoma visa vya wanaume vinga'ng'anizi.

Au umesahau kile kisa cha Mmbu mng'anganizi alichowahi kusimulia Chinua Achebe? Ngoja nikukumbushe! Hapo kale Mbu alimpenda sana sikio…sikio hilihili lililo mwilini mwako.

Basi Mmbu akamwendea sikio na kumweleza kuhusu pendo lake kwa sauti ibembelezayo kwa huba. Mrembo sikio kusikia maneno ya Mmbu akadondoka chini kwa kicheko.

Kisha akarudi pahala pake na kumwambia mbu kwa dharau. ''Wewe mbu kiumbe unayeishi kwa wiki moja kisha unafyekwa na kifo ndiyo unipose mimi?'' Unataka kuniacha mjane halafu anioe nani?''

Mmbu alijaribu kumbembeleza sikio bila mafanikio. Hoja ya sikio ilikuwa ile ile: kwamba Mbu ana maisha mafupi. Basi Mbu akasema kwa huzuni..''Hao waliokuambia kuwa nina maisha mafupi wamekuongopea..nitakuthibitishia hili''.

Kwa hiyo ikawa kila siku mbu anakuja sikioni kwa binadamu na kumweleza sikio kwamba nipo hai. Hata sikioni mwako bila shaka hufika kuendeleza ushawishi wake kwa mnyange sikio.

Ni kwa sababu hujui lugha ya mmbu ndiyo maana uandhani amekuja kukupigia kelele tu! Akija kwa binadamu yoyote, iwe amelala au yu macho, lazima aje kwanza kwa binti sikio kumsalimu. ''Ewe sikio kipenzi, tazama nipo hai, nikubalie'' Kweli Mbu king'ang'anizi!
Kwa hiyo ukiwa na BMV, jua visa vyote hivi amekwisha visoma!

Habari ya kumuota mtu ndotoni au kumuona kwenye glasi achana nayo! Maneno haya yaseme ukiwa na wasichana wengine, si BMV! Mweleze kwamba unampenda. Akikuuliza kwa nini? Mweleze unapenda kila kitu chake.

Usisahau kusema pia unaipenda tabia yake hasa kupenda kwake kusoma vitabu. Hapa BMV atafurahi sana. Furaha yake ni vitabu.
Akikubali, anza uhusiano. Jitahidi nawe uanze kupenda vitabu taratibu.

Akikuuliza unamjua Shaaban Robert usiseme ni shule ya sekondari..sema ni nguli wa fasihi. Akisema kuhusu Andanenga usije dhani ni jina la mzizi fulani..huyo ni malenga mashuhuri almaarufu kama ''Sauti ya kiza''.

Muoe. Kama ndiyo kwanza mnaanza maisha, m-surprise kwa kumnunulia shelf jipya la vitabu. Mukijenga nyumba, usisahau study room, chumba cha kujisomea.

Usishangae usiku akiwa kwenye usingizi mzito akagumia ndotoni…''usimuuue usimuuee!''. Hakuna haja ya kumwamsha; jua anaota ya vitabuni!

Ukirudi nyumbani halafu ukakuta bado hajapika chakula usimfokee wala kumpiga, hiyo ndiyo raha ya BMV. Nenda alipo, yaweza kuwa chumbani kajilaza na kitabu mkononi au nje kwenye bustani akisoma kitabu!

Kwa BMV, vitabu ni popote! Msogelee karibu kisha soma naye hadithi, namaanisha kula naye hadithi kwa sababu huo ndiyo mlo mkuu wa BMV.

Ukiishi na BMV jua haupo peke yako. Mupo waume wawili, wewe na vitabu. Usimuonee wivu mume mwenza kwa sababu kila mmoja ana jukumu la kumfisha BMV kwenye kilele,

Kilele kilojaa raha

Kilele kiso karaha

Kilele chenye furaha

Akawa hajitambui

Hajui yupo ndotoni

Au kapaa mbinguni

Ala raha za peponi

Mrembo hajitambui

Ado Shaibu ( Komredi wa Malenga )
………………………………………………..
NOTE: Tangu kuandikwa kwa mara ya kwanza kwa makala ya ''Don't Date a Girl Who Reads'' ya Charles Warnke, makala nyingi zaidi zimeandikwa kuchukua upande wa mwandishi au upande tofauti. Niliandika post hii baada ya kusoma makala ya Jennifer Souter iitwayo ''You Just Date a Girl who Reads''.


 
Sasa uoe mpenda vitabu ili iweje? Sisi watanzania wengi tuna allergy na aandishi ndio mana hata picha yako umeweka ya mzungu anasoma. Ukioa mzungu napo ndio shida squared..

Mimi nasema oa yeyote ukiona ana sifa za kuwa mke no matter ni bookworm ama no
 
Hii itakuwa siyo ndoa bali jela
 
ngoja nijisosegeze tanganyika library fastaaaaaaa

ning'oe mtoto
 
Inabidi tuongeze hiki kigezo wakati wa kutafta wachumba, "Awe ni mpenda vitabu"
 
Hivi ukiwa unasoma vitabu vya hadithi unakuwa msomaji pia?
 
kusoma ni kipaji sembuse kusoma vitabu mbona janga la taifa hili labda uchepuke uende mashariki ya mbali utakutana nao
 
kusoma ni kipaji sembuse kusoma vitabu mbona janga la taifa hili labda uchepuke uende mashariki ya mbali utakutana nao

Alafu nina zawadi yako ya kitabu cha rasimu ya katiba mpya na kitabu cha cyber crimes...
 
Napenda saana kusoma, sanaaa, lakini siwezi kuowa mwanamke anayependa vitabu, mambo hayatakwenda!
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…