SEHEMU YA 02
Kufuatia kuambiwa hivyo, kijana huyo mweupe, mrefu wa wastani na mwenye vidimponsi vinavyoonekana kila akiongea au kucheka alimjibu fundi Yassin kwamba kwa kuwa alikuwa mtoto wa kiume alikuwa tayari kufanya kazi yoyote.
Licha ya Nelly kupewa ushauri wa kutafuta kazi yoyote ya kufanya, aliumia sana kufuatia bro mmoja ambaye ni mambo safi kumchukua demu wake Careen kwa vile hakuwa na hela.
Msichana huyo aliyeingizwa kwenye ulimwengu wa kimapenzi na Nelly, alikuwa akimpenda sana Nelly lakini alishindwa kudumu naye kwa sababu kila alipohitaji sapoti ya fedha kutoka kwa mpenzi wake huyo ilikuwa zii.
Kila Nelly alipokuwa akikumbuka tukio hilo la kuporwa demu wake na yule bro anayemiliki kampuni ya kutoa mizigo Bandarini aliumia sana, kwa sehemu ishu hiyo ilimfanya akubaliane na ushauri wa baba yake wa kutafuta kibarua chochote cha kufanya.
“Ila Nelly kwa jinsi ninavyokuona sijui kama utaweza kufanya kazi ngumu, kwa kuwa umeamua basi vizuri jiandae ili kesho twende pamoja,” fundi Yassin alimwambia Nelly aliyekuwa akivaa miwani sababu ya kusumbuliwa na macho kwa mbali.
“Fundi Yassin, haina haja ya kusubiri kesho, hivi unavyoniona nipo full, labda niende nikachukue nguo za kufanyia kazi, nimechoka kukaa nyumbani,” Nelly alimwambia fundi Yassin aliyeishia kucheka.
“Haya bwana, nenda kachukue nguo hizo ili nami nijiandae kisha tuanze safari, ukija nitakwambia tunakokwenda,” fundi Yassin alimwambia Nelly.
Baada ya kuambiwa hivyo, kijana huyo wa Kisukuma alikwenda kwao akachukuwa shati kuukuu, suruali ya zamani na raba ambazo hakuwa akizivaa kwa sababu zilianza kuchoka akaziweka kwenye begi.
Wakati Nelly ambaye nimeshakwambia ni handsome boy haswa akijiandaa, nyumbani kwa fundi Yassin mkewe alimwuliza alikuwa akizungumza na nani.
Fundi Yassin alimsimulia kila kitu mkewe, ambaye hakuamini kama kweli Nelly aliyekuwa akimfahamu kwa usmati wake angeweza kufanya kazi ya ujenzi aliyokuwa akiifanya mumewe.
“Yaani baba Tatu, Nelly huyu sharobaro mvaa miwani ataweza kweli kubeba zege, matofali, kuchota maji au kubeba mbao?” mkewe Yassin alimwuliza mumewe.
“Nami nimemuuliza hivyo kaniambia ataweza, wewe ngoja niende naye halafu tukirudi ndiyo nitakueleza kitakachojiri huko,” fundi Yassin alimwambia mkewe, wakacheka.
Wakati fundi Yassin akizungumza na mkewe, nyumbani kwa akina Nelly, baba yake alipomuona kijana wake kabeba begi muda ule wa alfajiri alihisi huenda alikuwa akitoroka kufuatia kumwambia aanze kujitegemea.
“Nelly mbona na begi alfajiri yote hii, unakwenda wapi?” mzee huyo alimwuliza kijana wake.
Baada mama Nelly kuchangamshwa damu asubuhi ile alimshukuru mumewe, akiwa anachekacheka aliamka na kwenda kuandaa maji ya kuoga, wakaoga pamoja kisha alimwandali kifungua kinywa.
Baba Nelly alipomaliza kunywa chai aliondoka kuelekea kwenye pilika za kutafuta riziki, akiwa njiani akawa anamtafakari Nelly aliyemweleza anakwenda kumsaidia kazi fundi Yassim.
“Kama ataweza nitasema kweli amekuwa lakini kwa jinsi ninavyomjua atakapotoka huko ataniambia hatakwenda tena,” mzee huyo aliwaza.
Nelly akiwa na begi lake alipofika nyumbani kwa fundi Yassin, alimkuta akiwa anamsubiri. Hawakupoteza muda, fundi huyo aliamuga mkewe kisha alichukuwa zana zake za kazi na kuanza safari ya kwenda site.
Kwa kuwa bado ilikuwa ni alfajiri walipofika kituo cha daladala lilifika DCM la Mwenge wakapanda, kwa bahati walikaa siti moja.
Wakiwa wanaendelea na safari fundi Yassin ambaye mpaka muda huo alikuwa aamini kama kweli Nelly aliyekuwa akimfahamu vizuri kwa kupenda mambo ya usharobaro aliamua kwenda kufanya kazi za ujenzi.
“Nelly hivi ni kweli umeamua kwa dhati kufanya kazi ngumu ninazofanya?” fundi Yassin alimwuliza .
“Fundi bwana! Sasa kama wewe unaweza mimi nitashindwaje? Mimi mtoto wa kiume bro!” Nelly alimwambia fundi Yassin aliyeishia kucheka.
Katika daladala walilopanda, kiti cha kushoto alikaa kaka mmoja upande wa dirishani na kufuatia demu mmoja mkali ambaye alfajiri hiyo alikuwa akiangalia mambo ya dunia katika simu yake ya kisasa ‘Smartphone.’
Wakati msichana huyo akiwa bize na simu yake, Nelly alikuwa akimtupia macho kwa chati na kumsifia moyoni kwamba kweli Mungu alijua kumuumba na kuishia kusema kama alikuwa ana boyfriend wake basi alikuwa akila vinono.
Hata hivyo, Nelly ambaye alikuwa akiwapenda watoto wazuri alipanga kama demu huyo atashukia Mwenge amuombe namba yake, alipanga kujaribu tu zali la mentali.
DCM walilopanda lilipofika Mwananyamala Hospitali, Yule dada mkali aliinuka moyo wa Nelly ulipiga pa kwani alijua mahesabu yake ya kuomba namba yalifeli, akajisemea moyoni; kudadeki.’
Wakati Nelly akiwa katika wakati huo mgumu, alimuona Yule kaka aliyekaa upande dirishani na yule msichana mkali akasogea dirishani, moyo wa Nelly ukajaa furaha.
“Vipi Nelly naona upo mbali, unawaza kazi za huko site nini?” fundi Yassin alimshtua Nelly ambaye mawazo yake yalikuwa kwa Yule demu.
“Hapana fundi, mambo mengi tu kichwani si unajua hali ilivyo ngumu siku hizi!” Nelly alimwambia fundi Yassin.
Kwa kuwa muda huo wa hakukuwa na jamu, kufumba na kufumbua walijikuta wamefika Makumbusho abiria wakaanza kuteremka kutoka garini, kwenye siti ya akina Nelly alianza yeye, upande wa kushoto Yule demu,
Kufuatia zana za kazi alizokuwa nazo, fundi Yassin ilibidi watu wote washuke ili asiwabughudhi, Nelly na Yule msichana wakiwa chini, kijana huyo handsome boy aliamua kumsalimia na kumsifia kwa jinsi alivyojaaliwa uzuri na alivyopendeza.
Kama ambavyo nimekuwa nisema mara kwa mara kwamba kama kuna mtu hapa duniani akisifiwa huwa hafurahi ujue ana matatizo, Yule dada alimshukuru Nelly na kuachia tabasamu pana.
Je, Nini?