Ni kisasi au chuki...?

Phobia

JF-Expert Member
Mar 29, 2021
1,151
1,783
NI KISASI AU CHUKI...?

"Tulisikia yowe kisha kishindo kikubwa, duuuuf. Baada ya hapo ilisikika sauti ya mwanaume ikipayuka." Ndivyo mashahidi walivyolielezea tukio la kifo cha Anele 'Nelli' Tembe.

Nelli alifariki baada ya kudondoka toka kwenye kibaraza cha ghorofa ya 10 ya hoteli ya Pepperclub iliyopo Cape Town, Afrika kusini. Jumapili ya April 11, 2021.

Saa chache kabla ya kufariki, Nelli akiwa na mchumba wake rapa maarufu wa Afrika Kusini, Kiernan Jarryd Forbes almaarufu kama AKA walionekana kwenye Insta Stories ya AKA wakiwa wanafanya manunuzi kwenye duka la Maxhosa, kabla ya kula mlo wa mchana na marafiki zao na baadaye kuonekana klabu ya Ayeyep Lifestyle, ambako AKA alikuwa anatumbuiza siku hiyo. Nelli alionekana mwenye furaha na raha tele.

Tofauti na wanawake waliopata kuwa na uhusiano na AKA, Nelli aliyekuwa na miaka 22, hakuwa maarufu hapo kabla.

Sasa muda wa alfajiri hivi, ikapigwa simu ya dharura kutokea hoteli ya Pepperclub. Polisi wakafika na gari la wagonjwa likawasili. Watoa huduma ya kwanza wakawa wanapambana kumwokoa Nelli aliyekuwa ameumia vibaya mno hali mwili wake ukiwa mtupu.

Ikashindikana. Na alikuwa hatazamiki kwa namna alivyotawanyika.
Ikatangazwa papo hapo Anele 'Nelli' Tembe ameuma shuka. Kaenda kusikorudika.

Taarifa zikaanza kusambaa mitandaoni. Nelli mchumba wa AKA amejiua kwa kujirusha toka ghorofa ya 10.

Amejiua? Watu wakawa wanang'aka.
Haiwezekani! Watu wakawa bado hawaamini.
Pole zikaanza kumimina kwa rapa AKA. Si kapoteza mchumba wake.
Pole zikadumu kidogo, kabla ya moto kuwashwa na kuwaka.

Kifo cha Nelli kiliacha utatanishi.
Wakati polisi wakilichukulia tukio hilo kama kifo cha kujiua.
Sehemu ya watu mitandaoni ilikataa katakata, walisema kauawa.

Baba yake Nelli, Mfanyabiashara mkubwa 'kigogo' Moses Tembe, wakati wa mazishi alisema kwa uchungu binti yake hajajiua, wala hakuwahi kuwa na dalili za mtu anayefikiria kujiua. Hadi anafikia umri wa miaka 21, Nelli aliyapenda maisha na aliyafurahia. Kusikia binti yake amejiua tena kwa kujirusha toka ghorofani. Naaah! Kuna kitu hakiko sawa.

Wakati baba akiyasema hayo, AKA alikuwa na yake ya kusema.
Nelli aliyemfahamu yeye alikuwa na msongo wa mawazo na alikuwa akitishia kujidhuru mara kwa mara. Siku ya tukio walikuwa wote na walikwaruzana ila wakasema watazungumza. Maana ni kama walishakuwa mke na mume kwa kuwa miezi miwili nyuma AKA alikuwa amemlipia mahari 'lobola', na walikuwa wanajiandaa na harusi.

Kwa mujibu wa AKA, mazungumzo yao chumbani baada ya onesho hayakukaa poa. Walikwaruzana zaidi. AKA akaamua kukodi chumba kingine kuepusha matatizo walau wapumue kwanza hasira zipoe. Anasema, Nelli alivua pete akamrushia. AKA alitoka ila akarudi tena hapo ndipo Nelli akatoa vitisho kwa vitendo.

Kuona hivyo, AKA aliamua kupigia simu walinzi kisha akaenda bafuni. Hajui ni wakati gani Nelli alijirusha; alipokuwa anapiga simu ama alipoenda bafuni. Anachokumbuka, alipotoka bafuni hakumkuta Nelli chumbani. Sachi hapa sachi pale hola! Ndiyo akaamua kuelekea kibarazani na kugundua mchumba wake amejirusha chini.

Wakati akihojiwa, AKA alishangaa na kusikitika, kwa nini Mzee Moses Tembe anahisi mtoto wake ameuawa.

Lakini, mwezi mmoja baada ya kifo cha Nelli, ilivuja video ya AKA akibomoa mlango wa mbao wa chumba alichokuwemo Nelli wakiwa kwao. Inasemekana Nelli alikuwa amejifungia humo kumkwepa AKA. Nelli ndiye aliyerekodi na kumtumia rafiki yake, na inasemekana jamaa alimkung'uta Nelli. Tuhuma ambazo AKA alizikanusha vikali sana japo alikiri zipo nyakati alikuwa toxic na kumnyanyasa Nelli kihisia (Emotional Abuse) mambo anayosema hutokea kwenye mapenzi, uhusiano wao haukuwa perfect, migogoro ilikuwepo ila hakuwahi kumpiga Nelli.

Kesi ya kifo cha Nelli, uchunguzi ulienda doro. Ikaendelea kuchukuliwa kama kifo cha kujiua na si kuuawa. AKA aliyepotea kidogo mitandaoni kwa ajili ya kuomboleza, alirudi na wimbo wa kumkumbuka Nelli na kuzungumzia mapenzi yao - Tears Run Dry.

Inasemekana, Mzee Moses Tembe, alichefukwa barabara. Kwake yeye, AKA alimuua Nelli kwa kumsukuma toka huko ghorofa ya 10. AKA aliyewahi kukiri kutumia madawa ya kulevya kabla ya kuachana nayo, alimkera hasa baba mkwe.

AKA alipitia wakati mgumu sana mitandaoni na kwenye madili yake ya pesa. Baadaye, akasimama na kurejea kuishi maisha yake. Miezi 10 baada ya kifo cha Nelli, Feb, 2022 AKA akauweka wazi uhusiano wake wa kimapenzi na rapa Nadia Nakai.

Alionekana mwenye furaha na raha.
Akaendele na shoo zake kama kawaida.
Akaonekana akiyafurahia maisha na mapenzi na mpenzi wake mpya.
Alifurahia kweli? Hata sijui.

Februari 10, 2023...
Jana hiyo.

AKA alikuwa mwenye bashasha tele, alionyesha pilikapilika zake huku na kule kupitia Insta, akiwa mwenye raha na buraha huku akijiandaa kutumbuiza kwenye klabu moja hivi hapo jijini Durban. Akijiandaa pia kuachia album yake mpya Feb 27.

Saa nne usiku, akiwa nje ya mgahawa mmoja maarufu. Jamaa f'lani wasiojulikana wakiwa kwenye magari mawili, wakamlia mingo wakamchapa mvua ya risasi. Yeye na mtu mwingine, wakafa papo hapo.

Magari yakasepa. Watu wakapigwa na butwaa.

Hivyo, yaani namna hiyo. Kiernan Jarryd Forbes almaarufu kama AKA akaiaga dunia. Kama mzaha tu. Pah Pah Pah! Unaimbiwa niagieni... niagieni... Kifo hiki.

Nelli alifia kwenye jiji la AKA - Cape Town. Naye AKA amefia kwenye jiji la Nelli - Durban.

Inawezekana hiki ni NI KISASI CHA MKWE au NI CHA GENGE LA WAHUNI? Ama NI CHUKI TU ZA WAJA?
 
Wale mbuzi wamemuua Lucky Dube watakuwa na simile kwa huyu Bongo Fleva. Sio watu wale, wanauwana kila siku kama wako Venezuela
 
Sema jamaa alikuwa mtu wa location kila sehemu yeye ni kujitupia tu utoto bado ulikuwa unamsumbua yaani kila mahali alipo lazima atupie picha

Sent from my SM-N950F using JamiiForums mobile app
 
Sema jamaa alikuwa mtu wa location kila sehemu yeye ni kujitupia tu utoto bado ulikuwa unamsumbua yaani kila mahali alipo lazima atupie picha

Sent from my SM-N950F using JamiiForums mobile app
Na hiki ndicho kilimkost jamaa alikuwa akipost anapost na jina la eneo alilopo muda huo jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wako kwa wasiopenda uishi wakamlia timing wakampiga risasi akamfuata mkewe Anele "Nellie" Tembe.
Mwenyezi MUNGU azilaze roho za marehemu hawa mahala pema peponi...Amina!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom