KIVURUGE WA TANDALE 22
ILIPOISHIA:
“Hapana, mpaka kesho,” alisema huku akigeuka na kuanza kutembea kwa maringo kuelekea getini, huwezi kuamini kwa mara ya kwanza nilijisikia wivu wa kupindukia kwenye moyo wangu, nikatamani nimfuate lakini nikaona nishai, nikabaki nimeduwaa tu pale mlangoni kama msukule. Mara nikasikia mlango wa mama mwenye nyumba ukifunguliwa.
SASA ENDELEA...
“Vipi ulikuwa unaongea na nani?”
“Huyu dada mgeni alikuwa ananiomba nifunge mlango anatoka,” nilimdanganya mama mwenye nyumba, akasogea mpaka getini na kuhakikisha kama kweli ametoka.
“Mbona sasa hujafunga?”
“Nilikuwa nataka kuja kufunga ndiyo nikakusikia unafungua mlango,” nilizidi kuutetea uongo wangu, akaufunga mlango na kunisogelea.
“Mtoto mshenzi huyu, anaenda kwenye biashara zake saa hizi kurudi mpaka asubuhi!”
“Biashara gani?”
“Hee! Kumbe hujui... anafanya biashara ya kujiuza pale Kona, Sinza Afrika Sana, kila siku asubuhi mimi ndiyo namfungulia mlango, alisema mama mwenye nyumba, moyo ukanilipuka paah! Japokuwa kulikuwa na baridi, kijasho chembamba kilianza kunitoka.
“Changudoa?” niliuliza nikiwa ni kama siamini.
“Ndiyo, hawa wasichana wa siku hizi mchana ukimuona utadhani mtu wa maana kweli, ngoja giza liingie,” alizidi kushindilia msumari mama mwenye nyumba.
Hata sikumbuki tuliagana naye vipi, nilikuja kujikuta nimekaa sebuleni nikiwa nimejikunyata, mawazo tele yakipita ndani ya kichwa changu.
Pamoja na ujanja wangu wote, hakuna kitu nilichokuwa nakiogopa kama kutoka na machanguoa, kibaya zaidi ni kwamba nilipokutana na Khazija nilikuwa nimeuza mechi. Niliingia mzimamzima bila tahadhari yoyote.
Kama umewahi kupiga gemu na mtu halafu baadaye ukaanza kuwa na hofu kuhusu usalama wako, unaweza kuelewa ni hofu kiasi gani niliyokuwa nayo. Nilibaki nikiwa nimejikunyata kwa muda mrefu, yaani nimekaa tu! Sitazami runinga wala sisikilizi redio, muda wote natetemeka tu.
Mpaka inafika saa saba za usiku, nilikuwa nimekaa tu pale sebuleni, mawazo mengi yakiendelea kukisumbua kichwa changu. Nilikuwa nikipiga picha jinsi nitakavyokonda, jinsi nitakavyokuwa nakohoa na kutokwa na madonda mwili mzima. Hakika yajayo yalikuwa yakitisha.
Hata sijui nilipitiwa na usingizi saa ngapi, nilipokuja kuzinduka ilikuwa ni tayari saa kumi na mbili alfajiri na kilichoniamsha ni baada ya kusikia mlango wa geti ukifunguliwa, nikakurupuka na kusogea dirishani, nikawa nachungulia nje.
Kweli alikuwa ni Khazija, alikuwa akitembea kwa kuyumbayumba, mkononi akiwa ameshika chupa ya pombe kali. Nilimuona mama mwenye nyumba akipita haraka na kurudi kwake, Khazija akawa anahangaika kufungua mlango wa chumba chake.
“Kwa nini umeniua Khazija? Kwa nini? Why?” nilijikuta nikijisemea huku machozi yakianza kunitoka, donge kubwa lilinikaba kooni, machozi yakawa yanamwagika kwa wingi na kuulowanisha uso wangu.
Niliona kama nitaendelea kukaa ndani naweza hata kuchukua uamuzi wa kujidhuru, nikaona bora nijiandae na kwenda kazini labda kidogo nitachangamka. Basi nilitoka na kwenda bafuni kinyonge, nikajimwagia maji huku nikiendelea kuumia mno ndani ya moyo wangu.
Nilijikuta namchukia sana Khazija na nikajiapiza atakapokuja kunishibokea tena, naweza hata kumtia makofi.
Nilirudi ndani na kujiandaa, muda mfupi baadaye nikatoka kimyakimya, sikutaka hata mtu yeyote anione, nafsi yangu ilikuwa inanisuta mno na nikiri kwamba sijawahi kuwa kwenye majuto kwenye moyo wangu kama kuanzia nilipopewa taarifa kwamba Khazija ni changudoa.
Kwa kawaida kila ninapoondoka kwenda kazini nawasalimu majirani zangu, washkaji na watu wote ninaowafahamu lakini siku hiyo tangu natoka ndani mpaka nafika kituoni, sikuwa nimemsemesha mtu yeyote, muda wote nilikuwa natembea huku nimeinamisha kichwa chini, machozi yakinilengalenga.
Hakuna kitu nilichokuwa nakiogopa kama kufa kwa Ukimwi, nikawa natamani kila kilichotokea kiwe ndoto. Nilijuta kumfahamu Khazija na kubwa zaidi nilijuta mno kumvamia mtu nisiyemjua, tena bila kutumia kinga.
nilipofika kazini, ilibidi kwanza nitafute sehemu na kutulia kabla sijapanda ngazi kuelekea juu ofisini, kwa sababu nilikuwa na hali mbaya sana. Nilinunua maji na kunawa usoni ili hata mtu akinitazama asijue kwamba nilikuwa nalia.
Baada ya kuhakikisha nipo sawa, nilipanda ngazi mpaka juu, mtu wa kwanza kukutana naye alikuwa ni Salma wa mapokezi. Aliponiona tu, aliacha kila kitu alichokuwa anafanya, akanikimbilia na kunikumbatia kwa nguvu huku akinibusu shingoni.
“Kwa nini hupatikani hewani? Halafu hata ukiwa unapatikana mbona unakuwa mzito kupokea simu zangu?” Salma aliniuliza kwa sauti ya chini iliyojaa mahaba na upole, tofauti kabisa na jinsi alivyokuwa siku zote.
“Bado naumwa, nimejikaza tu kuja kazini!”
“Ooh! Maskini pole, hata uso wako unaonesha unaumwa,” alisema huku akiniachia, mwili wangu wote ukabaki na harufu ya pafyumu aliyokuwa amejipulizia. Sikuzungumza naye mambo mengi, nikapita na kwenda ofisini kwangu.
Bado kazi nilizoziacha zilikuwa palepale, kompyuta kadhaa zilizokuwa zinahitaji marekebisho, simu za ofisi na vifaa vya kuunganishia intaneti, vyote vilikuwa vinanisubiri. Nikaweka begi langu sehemu yake na kuchukua vifaa vyangu vya kazi. Niliamua kuelekeza nguvu kwenye kazi nikiamini nitasahau majanga niliyokuwa nayo.
Niliifungua kompyuta ya kwanza na kuanza kuitengeneza, nilibadilisha ‘hard drive’ na kuweka nyingine mpya, nikarekebisha na vitu vingine muhimu kisha nikaichomeka kwenye umeme, nikaiwasha lakini haikuwaka.
Nilirudia kuikagua tena na tena, nikarekebisha kila nilichokuwa nadhani ndiyo tatizo lakini kila nilipokuwa naiwasha, bado ilikuwa ikigoma. Nikaachana nayo na kuanza kuitengeneza nyingine, nayo nikarekebisha kila kitu lakini nilipoiwasha, haikuwa ikiwaka.
Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kichwa changu hakipo sawa kwa sababu kwa jinsi nilivyobobea kwenye masuala ya teknolojia ya mawasiliano, hata kama kompyuta ni mbovu kiasi gani, ikishafika kwangu lazima itapona. Nilivyoona kompyuta zote mbili zimenishinda, niliamua kuachana nazo, nikawa nafanya kazi nyingine.
Niliingia kwenye website ya kampuni na kuanza kukagua baadhi ya mambo kama ilivyokuwa kawaida yangu, vitu vingi havikuwa sawa na kila nilichokigusa kwa lengo la kurekebisha, nilijikuta nazidi kuharibu, nikaamua kuachana nayo.
“Sasa nitafanya kazi gani leo?” nikiwa nado najiuliza, simu ya mezani iliita. Nilipoipokea alikuwa ni Salma, akaniambia bosi ananiita ofisini kwake, nilishusha pumzi ndefu na kujifuta jasho, nikaacha kila kitu na kwenda mpaka ofisini kwa Madam Bella.
Nilipofungua mlango tu, aliacha kila alichokuwa anakifanya na kusimama, akaja mbiombio na kunikumbatia kwa mahaba, tukagusanisha ndimi zetu huku mikono yake ikifanya utalii wa ndani kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wangu.
“Nimekumiss jamani mume wangu,” alisema baada ya kuniachia, akanibusu tena na kunikaribisha kiti.
“Mbona umepooza namna hiyo, tatizo nini?” alisema Madam Bella huku akinikazia macho, nikamuungia humohumo kwamba nilikuwa naumwa sana na kwamba nimejilazimisha kuja kazini.
“Pole mume wangu, nakuona kabisa hauna furaha! Basi we nenda tu kapumzike, tutawasiliana baadaye, nikitoka naweza kuja kukuona nyumbani mgonjwa,” alisema Madam Bella, akanibusu mdomoni na kuifuata pochi yake. Alitoa noti tano za shilingi elfu kumikumi na kuniwekea kwenye mfuko wa shati, akanibusu tena.
Nilimshukuru na kutoka, nikaenda ofisini kwangu na harakaharaka nilichukua begi langu na kutoka mpaka mapokezi. Nikamuaga Salma ambaye alibaki ananishangaa.
“Naenda hospitali, nisije nikakufia bure,” nilimtania, akacheka na kunibusu kwa mbali, nikateremka kwenye ngazi na muda mfupi baadaye nilikuwa nimeshafika chini.
“Ebwana kuna mgeni wako anakutafuta kwelikweli.”
“Nani?”
“Yule dada uliyekuwa naye siku ile mkakaa pale, anasema hupatikani hewani kila akikupigia,” alisema mlinzi.
“Dah! Yuko wapi kwani?”
“Yule amekaa pale mlipokuwa mmekaa siku ile, tena naona amekuona maana anasimama,” alisema mlinzi, nikageukia kule alikokuwa ananionesha. Alikuwa ni Nancy, nilimfuata na kuzungumza naye juujuu, nikamwambia naumwa sana na naenda hospitali.
Kwa jinsi uso wangu ulivyobadilika, kweli aliamini naumwa, akataka anisindikize lakini nilimkatalia, nikaondoka huku akionesha wazi kwamba hakufurahishwa na nilichokifanya. Niliingia kwenye Bajaj na kumuelekeza dereva sehemu ya kunipeleka.
“Nipeleke Muhimbili.”
“Hospitali au?”
“Ndiyo,” nilisema huku nikishusha pumzi ndefu. Niliamua liwalo na liwe, lazima nikapime nijue mbivu na mbichi.
Je, nini kitafuatia?