Charles Quansah na kesi ya mauaji ya kutisha | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Charles Quansah na kesi ya mauaji ya kutisha

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, May 25, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  May 25, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280

  QUANSAH_charles_ebo_jpg.jpg
  Charles Paapa Kwabena Ebo Quansah

  14391945_295.jpg
  David Asante Apeatu

  59717263.jpg


  Ilikuwa ni mwaka 1998, wakati huo Nchi ya Ghana ikiwa inajiandaa na uchaguzi mkuu wa rais na wabunge wa mwaka 2000, ndipo nchi hiyo ilipokumbwa na kizungumkuti cha mauaji ya kutisha yakilenga wanawake na yakifanyika katika mtindo wa kushangaza.

  Vuvuguvugu la kampeni lilikiwa ndio limeanza na rais aliyekuwa madarakani wakati huo Jerry John Rawlings aliyeingia madarakani kwa uchaguzi huru kupitia chama chake alichokiunda akiwa bado ameshikilia madaraka aliyoyapata kufuatia mapinduzi ya kijeshi hapo mnamo mwaka 1981, ndio alikuwa anamaliza kipindi chake cha utawala.


  Ni baada ya kupata shinikizo kutoka mataifa wafadhili rais huyo alilazimika kuitisha uchaguzi huru unaohusisha vyama vingi ambapo aliunda chama cha National Democratic Congress
  (NDC) hapo mnamo mwaka 1993. Mwaka huo huo wa 1993 Rais Jerry Rawlings alisimama kama mgombea wa urais wa nchi hiyo kupitia chama hicho na kushinda kwa vipindi viwili yaani uchaguzi wa mwaka huo na ule wa kipindi cha pili ambapo alishinda tena mwaka 1996.

  Akiwa katika wakati mgumu kutokana na kubanwa na chama cha upinzani kilichokuwa kimejizolea umaarufu wakati huo cha New Patriotic Party (NPP) kilichokuwa kikiongozwa na John Kofi Agyekum Kufuor, Rais Rawlings ambaye alikuwa haruhusiwi kikatiba kugombea urais kwa mara ya tatu, chama chake kilikuwa kimemsimamisha mgombea mwingine ambaye alikuwa ni makamu wake Dr
  . John Evans Fifii Atta Mills kuwa mgombea wa chama hicho.

  Ni katika kipindi hicho ndipo nchi hiyo ilipokumbwa na mauaji hayo ya kutisha na kuipa wakati mgumu serikali ya nchi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na rais Rawlings. Mauaji hayo yalianzia mwaka 1998 mpaka ilipofika mwaka 2001, baada ya uchaguzi mkuu uliomuingiza rais wa wakati huo
  John Kofi Agyekum Kufuor wa chama cha NPP madarakani ndipo alipokamatwa kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Charles Paapa Kwabena Ebo Quansah aliyekuwa maarufu kwa jina la Charles Quansah ambaye alikuwa ni fundi makenika na dereva wa magari, akihusishwa na mauaji hayo. Awali kijana huyo alikamatwa kwa kutuhumiwa kumuuwa mpenzi wake aliyetajwa kwa jina la Joyce Boateng.

  Je, yalikuwa ni mauaji ya Kishirikina au ya kisiasa…….?


  Charles Quansah alikamatwa kipindi ambacho Idara ya upelelezi ya Polisi ilikuwa na wakati mgumu kuchunguza vifo vya wanawake waliokuwa wanauawa kwa kunyongwa katika maeneo mabalimbali nchini humo. Maeneo kama Spintex Road, Kwabenya, Asylum Down, Kisseman, Teshie, Adenta, Achimota, Adabraka na Dansoman ni miongoni mwa maeneo ambayo miili ya wahanga hao ilitelekezwa. Kitongoji cha Mataheko kilichopo katika jiji hilo la Accra ndicho kilichoathirika zaidi na mauaji hayo. Ilifikia wakati wanawake walikuwa wanaogopa kutoka nje ya nyumba zao ikishafika saa tatu za usiku kwa sababu ilikuwa haijulikani muuaji au wauaji watashambulia wapi na wakati gani. Lakini kilichoishangaza idara ya upelelezi ya nchi hiyo ni namna mauaji yalivyokuwa yakifanyika, kwani miili ya wanawake wote waliouawa ilikutwa ikiwa imelazwa chali upenuni mwa barabara huku ikiwa imepanuliwa miguu na pia ikiwa na mchanganyiko wa damu na mbegu za kiume katika sehemu zao za siri, kuashiria kuwa mhanga alikuwa amebakwa kabla ya kuuawa.

  Mpaka kufikia mwaka 2000 walikuwa wameuawa wanawake wapatao 34 kwa mtindo huo huo na kati ya hao 34, 25 hawakupata kutambuliwa na ndugu zao. Baadae ilibainika kwamba wanawake hao walikuwa ni wageni nchini humo ambao walikuwa wakijishughulisha na biashara ya ukahaba. Baadhi yao walitambuliwa kuwa walitokea katika nchi za Togo, Nigeria na Laiberia. Hata hivyo kutokana na ndugu wa marehemu hao kushindwa kuchukuwa miili ya wanawake hao, ilibidi wazikwe na serikali ili kupunguza msongamano wa maiti katika vyumba vya kuhifadhia maiti. Kutokana na ugumu wa upelelezi wa kesi hiyo ilibidi serikali ya nchi hiyo iombe msaada wa kitaalamu kutoka nchini Marekani ambapo serikali hiyo ilituma wataalamu wake kutoka shirika la upelelezi la nchi hiyo la FBI, ambao walitoka katika kitengo cha upelelezi wa kisayansi (Scientific Investigation Support-SIS)


  Kufuatia ushirikiano huo kutoka FBI ndipo alipokamatwa kijana huyo Charles Quansah 36. Inaelezwa kwamba wakati akihojiwa na Polisi wa upelelezi ndipo alipokiri kumuuwa mwanamke mwingine aliyetajwa kwa jina la Akua Serwaa ambaye mwili wake ulikutwa akiwa amenyongwa na kutupwa karibu na uwanja wa mpira wa Kumasi katika mji huo wa Kumasi uliopo katika mkoa wa Ashanti hapo mnamo Januari 19, 1996. Pia Quansah alikiri kuwanyonga na kuwauwa wanawake wengine 9 kati ya hao 34, katika viunga mbalimbali vya jiji hilo la Accra nchini humo. Inaelezwa kwamba Quansah aliwaongoza Polisi mpaka maeneo ambayo alikuwa akitelekeza baadhi ya miili ya wanawake hao mara baada ya kuwauwa.


  Pamoja na Quansah kukamatwa, lakini bado kulikuwa na maswali mengi ambayo wananchi wa Ghana walikuwa wanajiuliza. Nini hasa sababu ya mauaji hayo? Je ni mauaji ya kishirikina au ya kisiasa………. ? Maswali yote hayo hayakupata majibu na yalibaki kuwa kitendawili ambacho kilitakiwa kiteguliwe na idara ya upelelezi nchini humo.

  Hata hivyo ilielezwa kwamba wataalamu hao wa FBI walikusanya vilelelezo zaidi na kuvipeleka katika maabara yao nchini Marekani kwa uchunguzi wa kitaalamu zaidi ambapo mataokeo ya uchunguzi huo utaambatanishwa na vielelezo vingine ambavyo vilikusanywa kufuatia ushirikianao wa mtuhumiwa Charles Quansah ili iandaliwe hati ya mashitaka na mtuhumiwa afikishwe mahakamani kujibu mashitaka hayo ya mauaji.


  Je huyu Charles Papa Kwabena Ebo Quansah ni nani?


  Kwa nini alikamatwa na kuhusishwa na mauaji hayo ya kutisha? Je kama aliuwa wanawake tisa tu kati ya hao 34, wanawake wengine 25 waliuwawa na nani?

  Naomba ufuatane na mimi katika simulizi hii iliyojaa utata mtupu.


  Charles Papa Kwabena Ebo Quansah, alizaliwa hapo mnamo mwaka 1964 katika mji wa Komenda ulioko katika mkoa Central Region.

  Kwa mujibu wa historia yake iliyotolewa na Polisi wa nchi hiyo, ilionesha kwamba Charles Quansah aliwahi kutumikia kifungo katika jela ya James Fort kwa kosa la ubakaji hapo mnamo mwaka 1986. Baada ya kumaliza kutumikia kifungo chake alikamatwa tena kwa kosa la ubakaji na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na alitumikia kifungo hicho katika jela ya Nsawam hapo mnamo mwaka 1987. Charles Quansah, aliwahi kufungwa tena hapo mnamo mwaka 1996 kwa kosa la ujambazi, alitumikia kifungo chake katika jela ya Nsawam iliyopo katika mji wa Kumasi. Baada ya kumaliza kifungo chake alihamishia makazi yake katika mji wa Accra.


  Quansah alikamatwa nyumbani kwake katika viunga vya Adenta jijini Accra hapo mnamo Februari 2001, baada ya upelelezi mkali uliofanywa na timu maalum. Inaelezwa kwamba Quansah aliwekwa chini uangalizi maalum wa askari wa upelelezi waliokuwa wakifuatilia nyendo zake kwa kipindi cha muda mrefu. Kwa mujibu wa maelezo ya Polisi inalezwa kwamba, wakati akitumikia kifungo chake kwa kosa la ujambazi hapo mnamo mwaka 1996, Quansah alikutana na mtu mmoja aitwae William Bitter, raia wa Lebanon ambapo alimsaidia Quansah kupata kazi katika mji wa Kumasi.
  Baada ya kutoka gerezani mwaka 1996, Quansah alikwenda kuishi katika mji wa Kumasi. Mnamo mwaka 1997 alihamia katika kitongoji cha Dansoman jijini Accra, na ilipofika Septemba 2000, alihamia katika kitongoji cha Adenta katika jiji hilo la Accra.

  Taarifa iliyotolewa na Polisi kwa vyombo vya habari ilieleza kwamba mnamo Mei 8, 2001, Quansah alikiri kwamba, kati ya mwaka 1993 na 2001 alifanya mauaji katika katika mji wa Kumasi na katika viunga vya jiji la Accra ambavyo ni Dansoman, Mataheko, na Adenta, na ilielezwa kwamba aliwauwa wanawake hao kwa kuwanyonga.
  Quansah aliwekwa rumande akisubiri kukamilika kwa upelelezi wa kesi yake kabla ya kufikishwa mahakamani kusomewa mashitaka. Mnamo Machi 15, 2002 Baraza la ushauri la Accra lilitoa hati ya mashitaka na kuamuru mtuhumiwa afikishwe katika mahakama kuu ya jijini la Accra kujibu mashitaka ya kumuuwa Akua Serwaa binti wa miaka 24 ambaye alikuwa ni mtaalamu wa kutengeneza nywele katika mji wa Kumasi.

  Mtuhumiwa afikishwa kizimbani………….


  Mnamo Aprili 16, 2002, Charles Quansah alifikishwa katika mahakama kuu rasmi na kusomewa mashitaka ya mauaji. Katika hati ya mashitaka iliyosomwa pale mahakamani, ilielezwa kwamba hapo mnamo mwaka 1996, wakati akiishi katika mji huo wa Kumasi Quansah alimuuwa kwa kumnyonga Akua Serwaa baada ya kunywa na kulewa sana katika Baa moja maarufu iliyoko karibu na uwanja wa mpira wa Kumasi. Ilielezwa kwamba nia (Motive) ya Quansah kutekeleza mauaji hayo ni kutokana na tabia yake aliyoizoea ya ubakaji, na kutokana na kwamba mara nyingi akibaka hufikishwa kwenye vyombo vya sheria, safari hii aliamua kuwauwa wahanga anaowabaka ili kuwanyamazisha…….. kwani mfu huwa haongei…….!


  Kesi hiyo ambayo ilivuta hisia za watu wengi nchini humo, ilisikilizwa na Mheshimiwa Jaji Agnes Dordzie. Kwa upande wa utetezi, mtuhumiwa alitetewa na wakili maarufu kutoka katika kampuni ya Tetterley Chambers, aliyetajwa kwa jina la Joseph Obliquaye Amui. Huyu aliwahi kuwa mmoja wa wajumbe walioteuliwa wakati fulani katika tume maalum (Special Investigation Board (SIB) ). Tume hiyo iliundwa kuchunguza vifo vya Majaji watatu na Ofisa mmoja mstaafu wa Jeshi, ambao waliuliwa katika mazingira ya kutatanisha.


  Kesi hiyo iliisha kusikilizwa kwake mnamo Agost 7, 2002, na mtuhumiwa Charles Paapa Kwabena Ebo Quansah alihukumiwa kunyongwa hadi kufa kutokana na mauaji hayo.

  Baada ya hukumu hiyo, akiwa katika gereza lenye ulinzi mkali la Nsawam, akisubiri kutekelezwa kwa hukumu yake, Quansah alidai kwamba yeye hakuhusika na mauaji hayo na aliomba iundwe tume maalum ya kuchunguza mauaji hayo ili jina lake lisafishwe. Aliendelea kusema kwamba sheria ilipindishwa makusudi ili apatikane na hatia wakati hakuwahi kukiri hata siku moja kwamba alihusika na mauaji hayo ya kutisha. Quansah aliendelea kusema kwamba, hata hayo maelezo aliyodaiwa kuandikisha baada ya kukamatwa na Polisi hayakuwa yakwake. Alidai kwamba maelezo hayo aliyatoa baada ya Mateso ya kutisha aliyoyapata kutoka kwa askari hao wa upelelezi ambao walishirikiana na wazungu na pia walikuwa mashine fulani ambayo ilidaiwa kuwa ni ya kupima uongo (Lie Ditector). Quansah alidai kwamba askari hao wa upelelezi walipewa amri ya kumtesa kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu wa kitengo cha upelelezi (Criminal Investigation Departiment (CID) ).


  Pamoja na Quansah kuhukumiwa kunyongwa kutokana na mauaji hayo ya kutisha, lakini bado hofu ilikuwa imetanda kwa miongoni mwa wakazi wa maeneo yaliyokuwa yakishambuliwa na muuaji/wauaji hao. Wengi walikuwa wakijiuliza, ikiwa Quansah aliyeripotiwa kuuwa wanawake tisa anadai hana hatia ya kuhusika na mauaji hayo, au hata kama alihusika kweli na mauaji hayo ya watu tisa, hivyo kuna uwezekano wauaji wengine walioshiriki katika mauaji hayo wako mitaani wakisubiri ipatikane nafasi nyingine ya kuendelea na mauaji hayo ambayo hata hivyo wananchi wengi walikuwa hawajui sababu hasa ya mauaji hayo ya kutisha.


  Kwa mujibu wa askari magareza mmoja mbaye hakutaka jina lake litajwe alividokeza vyombo vya habari nchini humo kwamba, maelezo yaliyotolewa mahakamani yakidaiwa ni maelezo ya Quansah akikiri kuhusika na mauaji hayo, hayakuandikishwa na Quansah mwenyewe kama ilivyodaiwa…. Askari huyo alidai kwamba, mtuhumiwa huyo hakuwahi hata siku moja kukiri kuhusika na maauji ya wanawake hao. Aliendelea kusema kwamba, wakati Quansah akiwa gerezani wakati upelelezi wa kesi yake ukiendelea, mara nyingi askari wa upelelezi kutoka makao makuu walikuwa wanakuja hapo gerezani na gari na kumchukuwa Quansah huku wakiwa wamemfunga kitambaa machoni na pingu mikononi na kumepeleka kusikojulikana, ambapo huko walimtesa sana na wakimrudisha alikuwa anatokwa na damu nyingi kila mahali, mdomoni, masikioni na puani. Kutokana na mateso hayo ndipo kile kilichoelezwa na askari hao wa upelelezi kwamba alikiri kuuwa wanawake tisa kilipojitokeza.

  Kwa mujibu wa maelezo yake, Quansah alidai kwamba, kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata mfululizo ndipo siku moja akaropoka, "Nimeuwa 90 na siyo 34 tu." Na ndipo askari wa upelelezi waliokuwa wakimhoji walipokuja na maelezo kwamba, Quansah alikiri kuuwa wanawake tisa kati ya 34.

  Ili kuthibitisha kwamba alikuwa anateswa ili akiri kuhusika na mauaji hayo, Quansah aliwahi kuonyesha makovu manne mgongoni kwake ambayo yalionekana dhahiri kuwa alichomwa na pasi ya kunyooshea nguo. Quansah mara nyingi pia alikuwa na maelezo kwamba wapelelezi hao walikuwa na dhamira yao, ambapo walikuwa wakimshinikiza si akiri tu kuhusika na mauaji hayo, bali pia walimlazimisha awahusishe watu fulani wazito Serikalini kwamba ndio waliohusika kupanga na kumtuma yeye kufanya mauaji hayo, kitu ambacho si kweli.

  Aliendelea kulalamika kwamba, licha ya kukamatwa hapo mnamo mwaka 2001, kwa kuhusishwa na mauaji ya mpenzi wake Joyce Boateng wa Adenta jijini Accra, lakini alifikishwa mahakamni na kushitakiwa kwa kosa la mwanamke mwingine aitwae Akua Serwaa aliyedaiwa kumuuwa na kumtelekeza katika viunga vya uwanja wa mpira wa Kumasi hapo mnamo Januari 19, 1996. Wakati huo huo hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa pale mahakamani kuhusu uhusiano wake na mwanamke huyo.


  Kuhusu kuwapeleka maofisa hao wa upelelezi katika eneo ambalo ndipo alipodai kumuuwa Akua Serwaa, Quansah alikanusha madai hayo na kusema kwamba, wapelelezi walimpeleka mahali ambapo Polisi wa Kumasi walidai kuukuta mwili wa Akua Serwaa ukiwa umetelekezwa hapo. Quansah, alidai kwamba maelezo hayo ya kuteswa kwake yaliwasilishwa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi yake na wakili aliyekuwa akimtetea Joseph O. Amui lakini Mheshimiwa Jaji Agnes Dordzie na baraza la washauri waliyapuuza madai hayo na badala yake akahukumiwa kunyongwa.


  Hata hivyo nakala ya kesi hiyo inaonyesha dhahiri kwamba upande wa mashitaka ulimburuza Jaji na baraza lake la washauri wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo. Pamoja na kutolewa utetezi kwamba, maelezo yaliyodaiwa kutolewa na mtuhumiwa kukiri kuhusikana mauaji hayo, kwamba hayakutolewa kwa hiyari na mtuhumiwa mwenyewe, bali yalitolewa baada ya mtuhumiwa kuteswa kupita kiasi kitu ambacho ni kinyume na haki za binadamu. Shahidi mmoja wa upande wa utetezi aitwae George Yaw Asare Asamoah aliieleza mahakama kwamba, mara nyingi alikuwa anamuona Quansah akichukuliwa na askari wa upelelezi na kurudishwa baadae akiwa amepigwa kiasi cha kuvuja damu mwili mzima.

  Jambo lingine ambalo lililalamikiwa ni kitendo cha kamishina wa Polisi kudharau hati ya kuitwa shaurini iliyotolewa mnamo Julai 9, 2002. Hati hiyo iliyosainiwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa nchi hiyo Mheshimiwa Edward K. Wiredu ikimtaka kamishina huyo (CID) Patrick K. Acheampong ambaye baadae alikuja kuwa Mkuu wa jeshi la Polisi nchini humo (Inspector-General of Police (IGP) ) afike mbele ya Mheshimiwa Jaji Agnes Dordzie akiwa na vielelezo vifuatavyo:


  1. kifaa cha kupimia uongo (polygraph) au (Lie Detector) ambacho kilitumika wakati mtuhumiwa akihojiwa
  2. Maelezo yote yaliyoandikishwa na mtuhumiwa kabla ya Mei 8, 2001
  3. Nakala ya mkanda uliorekodi malezo ya mtuhumiwa kikiri kuhusika na mauaji hayo.

  Pamoja na Acheampong kutofika mahakamanai kama alivyotakiwa na mahakama, lakini hakuchukuliwa hatua yoyote kama sheria inavyotaka iwapo inatokea mtu kudharau hati ya kuitwa shaurini na mahakama. Mwanasheria mmoja akizungumzia kutotokea kwa Achiempong mahakamani alidai kwamba kulitokana na kutingwa na masuala mengine muhimu ya kitaifa. Hata hivyo mwanasheria mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kwamba Mheshimiwa Jaji Agnes Dordzie alitakiwa atoe hati ya kukamatwa kwa Acheampong na kuwekwa ndani. Pia alishangaa, iweje Mheshimiwa Jaji aendelee na kesi bila ya shahidi huyo muhimu kutofika mahakamani na vielelezo kama alivyotakiwa...! kwani ushahidi huo ungesaidia sana kuondoa utata mwingi uliogubika kesi hiyo.

  Wananchi wengi wakizungumzia swala hilo la Acheampong kutotokea mahakamani walisema kwamba, ingekuwa ni vyema kama Aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wakati huo IGP Ernerst Owusu Poku angemlazimisha Acheampong kufika mahakamani kama alivyotakiwa na Mheshimiwa Jaji Dordzie.


  Acheampong akizungumzia madai hayo alidai kwamba, hakumbuki kupata hati ya kuitwa shaurini wakati alipokuwa akifanya kazi katika ofisi hiyo ya CID makao makuu, alisema kwamba huenda hati hiyo haikupelekwa kwake na kitengo chao cha sheria pale makao makuu ya CID kama ilivyoelekezwa. Alipoulizwa kama alikuwa tayari kupeleka vielelezo vilivyotakiwa mahakamani kikiwemo kifaa cha kupimia uongo (Lie Detector), alisema kwamba, Jeshi la Polisi la nchi hiyo halina kifaa kama hicho. Kwa maeneno yake mwenyewe Acheampong alisema, "Ninavyofahamu mimi ni kwamba Polisi CID hawana kifaa hicho cha kupimia uongo (Lie Ditector) na hawajawahi kutumia kifaa hicho wakati wowote tangu alipoanza kulitumikia jeshi hilo la Polisi hapo makao makuu ya CID."


  Wakili aliyekuwa akimtetea Quansah alilalamika kwamba kuna mambo mengi yalikiukwa wakati wa uendeshaji wa kesi hiyo. Aliyataja mambo hayo kuwa ni kitendo cha kuteuliwa Jaji mwanamke kusikiliza kesi hiyo, na kitendo cha kuchapishwa kwa picha nyingi zikimuonesha Quansah na kumuhusisha na Daktari mmoja aliyetajwa kwa jina la Ram Backley ambaye alikuwa na imani za kishirikina ambapo alifungwa kwa kukutwa na viungo vya binadamu. Hayo yalikuwa ni miongoni mwa malalamiko yaliyojitokeza baada ya Quansah kuhukumiwa kunyongwa.


  Wakili huyo alikiri kuona makovu mengi katika mwili wa Quansah ambayo yanaashiria kwamba aliteswa sana. Hata Quansah mwenyewe alimweleza kuwa aliteswa sana wakati akihojiwa na askari wa upelelezi. "Polisi walikuwa na orodha ya wanawake waliouawa na walimpiga sana wakimlazimisha akubali kwamba ni yeye aliyehusika na mauaji hayo. Walitumia koleo kuminya sehemu mbalimbali za mwili wake ili akiri kufanya mauaji hayo" alisema wakili huyo.

  Pia wakili huyo alikanusha madai kwamba Quansah alikuwa mwendawazimu. Wakili huyo aliongeza kwamba, hata maelezo yake ya kukiri kuuwa, (kama yapo) hakuyatoa kwa hiyari yake mwenyewe bali kwa kulazimishwa baada ya kuteswa sana alipokuwa mahabusu. "Kwangu mimi, hakuonekana kuwa alikuwa mwendawazimu, alikuwa na akili zake timamu kabisa."


  Kilichowashangaza wengi ni pale ambapo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo (wakati wa serikali ya NDC) Nii Okaija Adamafio (MB) na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo IGP Peter Namfuri ambao walitangaza majina ya watuhumiwa wa mauaji hayo ya kutisha katika Bunge tukufu la nchi hiyo lakini jina la Quanasah halikuwepo, badala yake jina la Leopold Mawuli Anka lilitajwa kama mtuhumiwa muhimu anayetafutwa kwa kuhusika na mauaji hayo.


  Mkanda aliorekodi Quansah akiwa gerezani waibua mazito................

  Miaka minne baadae tangu alipohukumiwa kunyongwa, Kituo kimoja cha Redio kinachomilikiwa na mtu binafsi, kinachojulikana kwa jina la Radio Gold kilitangaza kupata mkanda uliorekodiwa kwa siri na Quansah akiwa gerezani ambapo kituo hicho kilidai kwamba katika mkanda huo licha ya kukanusha kuhusika na mauaji hayo Quansah pia ameibua tuhuma nzito dhidi ya idara ya upelelezi ya nchi hiyo.

  Quansah amedai kwamba, mmoja wa askari wa upelelezi aliayemtaja kwa jina la Issah, ambaye ndiye aliyekuwa akimtesa kwa kushirikiana na wenzake, alimtaka awataje aliyekuwa rais wa nchi hiyo Jerry Rawlings na mkewe Nana Konadu Agyeman Rawlings kuwa ndio waliomkodi yeye ili kutekeleza mauaji hayo. Aliendelea kudai kwamba Askari huyo wa upelelezi alimwambia, iwapo ataihusisha familia hiyo ya Rawlings na mauaji hayo, mambo yake yatakauwa mazuri na hatashitakiwa kwa mauaji hayo. Quansah alisisitiza katika mkanda huo kwamba alikataa kumhusisha rais huyo mstaafu na mauaji hayo, kwa sababu jambo hilo halikuwa na ukweli wowote. Kwanza alikuwa haifahamau familia hiyo, pili familia hiyo ilikuwa haimfahamu na tatu hakuwahi kutumwa si na Rais huyo tu bali na mtu yeyote kufanya mauaji hayo ambayo pia hakuhusika nayo.


  Quansah hakuishia hapo, aliendelea kudai kwamba, afisa mmoja wa Polisi aliyemtaja kwa jina la Onipa katika mkanda huo, alimtaka pia aongeze jina la Makamu wa Rais wa wakati huo aitwae Aliu Muhama katika orodha hiyo ya watu waliomkodi kufanya mauaji hayo, ambapo pia alikataa kwa sababu alikuwa hamjui huyo Aliu Muhama. Mkanda huo ulirushwa hewani na kituo hicho, na ulikuwa ni wa dakika 60.


  Serikali ya NPP iliyokuwa madarakani ilifahamu kuhusu kuwepo kwa mkanda huo, lakini ilikuwa haijui ni nani aliorekodi mkanda huo na mkanda huo uko wapi. Waziri wa habari wa nchi hiyo chini ya serikali ya NPP Nana Akomea akizungumza na vyombo vya habari hapo mnamo Agost 2003 aliahidi kutoa ripoti ya uchunguzi ambayo itaonyesha ni namna gani chama cha NDC na washirika wake walivyokula njama na Quansah ili kukihusisha chama cha NPP na mauaji ya wanawake zaidi ya 30 yaliyotikisa nchi hiyo. Hata hivyo ripoti hiyo haikuwahi kutolewa hadharani.

  Wana Intelijensia walionyesha wasiwasi wao kwa chama cha NPP kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2004 ambao ulikuwa ufanyike mwaka unaofuata. Kwani majaaliwa ya chama hicho kushinda ni labda kama Charles Quansah angenyongwa kabla ya uchaguzi. Kwani kulikuwa na hofu kwamba Quansah angetoa siri nzito iwapo chama hicho cha NPP kingeshindwa katika uchaguzi huo.


  Wana Intelijensia hao walidai kwamba kutolewa kwa mkanda huo kunaweza kuharakisha kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Kufuor kusaini hati ya kifo na Mwanasheria mkuu wa nchi hiyo kusaini hati ya kunyongwa kwa Charles Quansah ili kumnyamazisha moja kwa moja.


  Mkuu wa upelelezi na mkanda feki wa filamu juu ya mauaji hayo ya kutisha………..


  Mnamo siku ya Ijumaa Novemba 3, 2006, Mkuu wa upelelezi (CID) David Asante Apeatu alidai kwamba ataonyesha mkanda wa filamu wa dakika 45-50 ambao umewahusisha wataalamu mbalimbali wakiwemo wataalamu wa saikolojia, wataalamu wa kesi za mauaji na wataalamu wa uchunguzi wa maiti ambao watathibitisha ni namna gani Charles Quansah alihusika kuuwa wanawake wapatao 31 peke yake kati ya mwaka 1999 na 2000. Pia katika filamu hiyo atakuwepo mtaalamu kutoka nje ambaye ataeleza ni kwa nini, na kwa namna gani, na wakati gani mauaji hayo yalifanyika. Mkuu huyo wa CID aliidai kwamba Quansah alitoa ushirikiano mzuri kwa wapelelezi wa Polisi ambapo alikiri kusika na mauaji hayo.


  Hata hivyo baada ya filamu hiyo iliyoigharimu serikali ya Ghana mamilioni ya pesa kuonyeshwa hadharani, ilibainika kwamba ilikuwa ni ya kutengenezwa. Hata huyo aliyeonyeshwa katika filamu hiyo akihojiwa na askari wa upelelezi na kukiri kuhusika na mauaji ya wanawake 31 kati ya 34 waliouawa ambaye alidaiwa kuwa ni Charles Quansah, hakuwa yeye bali mtu mwingine.Wananchi wengi wa nchi hiyo wanaamini kwamba Charles Quansah ambaye alikamatwa na kushitakiwa kwa mauaji ya wanawake 9 kati ya 34 waliouawa, hakuhusika na mauaji hayo kwa sababu alikamatwa na kuteswa ili kukiri kuhusika na mauaji hayo.


  Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Apeatu alikuwa ni Kiongozi aliyeongoza upelelezi wa kesi hiyo ya mauaji ambapo wakati huo miili ya wanawake ilikuwa ikiokotwa kila uchao.

  Ilionekana dhahiri kwamba Apeatu na watu wake hawakuwa na taarifa zozote kuhusiana na sababu ya mauaji hayo na ni nani wanahusika nayo. Lakini baada ya chama cha NPP kushinda uchaguzi dhidi ya chama tawala cha NDC na kushika madaraka ya nchi hiyo, iliwachukuwa siku sita tu Apeatu na watu wake kufanikiwa kumkamata Charles Quansah kwa kuhusika na mauaji hayo. Lakini pia taarifa zilizovujishwa kutoka katika jeshi hilo, zilidai kwamba Quansah alikamatwa hata kabla ya chama cha NPP kushinda katika uchaguzi huo, ila kukamatwa kwake kulifichwa mpaka serikali mpya ilipoingia madarakani ndipo ikatangazwa kwamba mtuhumiwa wa mauaji ya wanawake 34 ametiwa mbaroni.

  Lakini hata hivyo ndani ya jeshi hilo la Polisi, wengi walikuwa wanajiuliza ni kitu gani Apeatu alikifanyia chama cha NPP ambapo baada ya kushika madaraka walishangaa kuona mwenzao akipanda vyeo mfululizo na kuwapita hata wakubwa wake, na pia kulikuwa na minong'ono kwamba huenda ndiye angekuwa Mkuu wa Polisi (IGP) mtarajiwa.


  Mwandishi mmoja aitwae Atta Kwabenah alizungumzia jambo hilo la David Asante Apeatu kupandishwa vyeo mfululizo kwa namna ya kejeli. Katika moja ya makala zake mwandishi huyo alisema………

  Naomba nimnukuu……….


  "When the NPP came into power, David Asante-Apeatu was then a Chief Superintendent of Police, and the next rank he could have been promoted to was Assistant Commissioner of Police, but because politicians can change a woman into a man, and a man into a woman without going through any medical processes, Asante-Apeatu was frog-jumped and promoted from Chief Superintendent of Police to the rank of Deputy Commissioner of Police. To make matters worse and deepen indiscipline in the Ghana Police Service, Asante-Apeatu was appointed the Director-General of the Criminal Investigation Department (CID) of the Ghana Police Service. Meanwhile, there were more seniors in rank (Assistant Commissioners, Deputy Commissioners, and Commissioners) who were more than qualified to be the head of the CID but the NPP government overlooked them. Can you imagine, the situation when the Assistant Commissioner of Police who was in charge of the Police Forensic Laboratory and Asante-Apeatu's senior in rank now had to report to him (Asante-Apeatu) as the boss, because administratively, the CID boss has oversight responsibility over the Crime Lab? In other words, the head of the Crime Lab under whom Asante-Apeatu served as a junior rank had to say, "Yes Sir Yes Sir" to Asante-Apeatu. What kind of indiscipline was this? What made the whole thing strange and ridiculous was that, hitherto NPP's assumption of power, most of the Schedule Officers who formed the top hierarchy of the Ghana Police Service with the Inspector-General of Police (IGP) were of the rank of Commissioners of Police (COP). There was the Commissioner of Police in charge of Administration, Commissioner of Police in charge of Operations, Commissioner of Police in charge of Welfare, Commissioner of Police in charge of Technical and General Services, Commissioner of Police in charge of the Criminal Investigation Department (CID) among others…………

  Mwisho wa kunukuu……………..

  Inaelezwa kwamba Jeshi la Polisi la nchini humo limekuwa likitumika kisiasa na kwamba Polisi wa nchi hiyo walitumiwa na wanasiasa kumkamata Charles Quansah mtu asiye na makazi maalum, asiyefahamika katika jamii na anayetoka katika familia duni ambayo isingeweza kumpigania katika kesi hiyo aliyozushiwa.


  Pamoja na kuwekwa gerezani akisubiri kutekelezwa kwa hukumu yake, Quansah ameendelea kukanusha kwamba hakuhusika na mauaji hayo, lakini hakuna hata anayesikiliza kilio chake. Wananchi wengi wa nchi hiyo walikuwa wakijiuliza, inawezekana vipi Quansah ashiriki mauaji hayo ya watu 34 peke yake……………..!
   
 2. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #2
  May 25, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Haya wasomaji wa JF, kama kawaida, Ijumaa hii nimehamia anga za Afrika Mgharibi, nikiwa nimejikita nchini Ghana.......
  Katika kesi hii kuna mengi ya kujifunza hasa ukizingatia kwamba siasa na michezo michafu imetamalaki sana katika bara la Afrika. Ngoja niwaachie msome wenyewe na kuweka maoni yenu...........................
   
 3. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #3
  May 25, 2012
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280
  Asante Ngoja nimalizie Gahawa nianze kupitia huu mkasa
   
 4. Ndahani

  Ndahani JF-Expert Member

  #4
  May 25, 2012
  Joined: Jun 3, 2008
  Messages: 14,326
  Likes Received: 1,792
  Trophy Points: 280
  Thanks...kama kawaida kuna kitu cha kujifunza. But after 10 yrs, Attah Mills amekuwa Rais baada ya kuondoka Kuffor
   
 5. Purple

  Purple JF-Expert Member

  #5
  May 25, 2012
  Joined: Feb 9, 2012
  Messages: 2,031
  Likes Received: 228
  Trophy Points: 160
  Mmh nchi za africa zote zinafanana kwa michezo michafu,na siasa imekua source of matatizo mengi..
   
 6. Mvaa Tai

  Mvaa Tai JF-Expert Member

  #6
  May 25, 2012
  Joined: Aug 11, 2009
  Messages: 6,174
  Likes Received: 2,175
  Trophy Points: 280
  Mnhhhh!!!!!!!! nimeharibu siku yangu. Hakuna kitu kinachoumiza kama ukandamizaji wa aina hii
   
 7. TaiJike

  TaiJike JF-Expert Member

  #7
  May 25, 2012
  Joined: Dec 14, 2011
  Messages: 1,475
  Likes Received: 174
  Trophy Points: 160
  mhhhhh........ina maana Quansah mpaka sasa bado anasubiri tu kutekelezwa kwa hukumu yake? inasikitisha sana kwa mtu asiye kuwa na hatia kubebeshwa zigo hili, kwa uelewa wangu mauaji hayo yaliongozwa na polisi chini ya chama kilichokuwa kikitaka kutawala.

  Nadhani hili funzo kubwa sana kwa Policcm yetu kujifunza kutenda wajibu wake kuliko kuongozwa na wanasiasa wetu ambao ndio wanaoiyumbisha nchi hii.
   
 8. E

  Elizabeth Dominic Platinum Member

  #8
  May 25, 2012
  Joined: Dec 7, 2007
  Messages: 4,547
  Likes Received: 52
  Trophy Points: 145
  Asante sana Mtambuzi kwa kesi hii ya kusisimua.
  Kesi inawacha maswali mengi sana na pia inaonyesha jinsi siasa zetu Africa zilivyotawaliwa na hujuma za kutisha..............kama ni ana hatia au sio lakini udhaifu mkubwa wa upelelezi ni wa kusikitisha na hili nadhani pia ni tatizo hapa kwetu jinsi unavyoona wenzetu wa Marekani na kwingine walioendelea wanapofanya uchunguzi kiasi cha kuacha chumba kidogo cha shaka utakuwa amazed of how many people are behind bars ambao hawana hatia kabisa
   
 9. NATA

  NATA JF-Expert Member

  #9
  May 25, 2012
  Joined: May 10, 2007
  Messages: 4,516
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 135
  Thanks Gustavo, kwa kweli it is too sad,
  Inaonyesha ni kwa jinsi gani nchi za kiafrica zote zinafanana kuongoza kimabavu na ukandamizaji.

  Haya mauaji inaonyesha yalikuwa yanafanyika kwa uahodari mkubwa sana na tahadhali ya hali ya juu.

  Kwa kweli binadam ni wanyama wabaya sana, unaua watu bila hatia kwa ajili ya ubinafsi tu.
   
 10. lutayega

  lutayega JF-Expert Member

  #10
  May 25, 2012
  Joined: Feb 29, 2012
  Messages: 1,215
  Likes Received: 61
  Trophy Points: 145
  Hii inathibitisha ule msemo kuwa si wote walio jela wanamakosa. Mtambuzi naomba kama inawezekana utuwekee kesi ya Babu Seya kwani nahisi kama anaweza naye kuwa amebambikiwa kesi kama huyu kijana. Huyu bwana vp ameshanyongwa au bado? asante
   
 11. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #11
  May 25, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  lutayega Bado anasubiri hatima yake akiwa Death Row................................
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 12. Ruttashobolwa

  Ruttashobolwa JF-Expert Member

  #12
  May 25, 2012
  Joined: Feb 22, 2012
  Messages: 43,746
  Likes Received: 12,826
  Trophy Points: 280
  Big up sana Mtambuzi, kweli siasa ni mchezo mchafu. vyombo vya usalama vimekuwa vikitumika kuwanyamazisha watu. hii ina sikikitisha sana, vyombo vya usalama vimepunguza trust kwa wananchi kutokana kutumiwa na wanasiasa,hasa walio madarakani.
   
 13. Ruttashobolwa

  Ruttashobolwa JF-Expert Member

  #13
  May 25, 2012
  Joined: Feb 22, 2012
  Messages: 43,746
  Likes Received: 12,826
  Trophy Points: 280
  Big up sana Mtambuzi, kweli siasa ni mchezo mchafu. vyombo vya usalama vimekuwa vikitumika kuwanyamazisha watu. hii ina sikikitisha sana, vyombo vya usalama vimepunguza trust kwa wananchi kutokana kutumiwa na wanasiasa,hasa walio madarakani.
   
 14. Cantalisia

  Cantalisia JF-Expert Member

  #14
  May 25, 2012
  Joined: Sep 26, 2011
  Messages: 5,229
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 135
  Hakika siasa ni mchezo mchafu,
  nimeamini sio wote walioko jela wana hatia!
   
 15. Ngongo

  Ngongo JF-Expert Member

  #15
  May 25, 2012
  Joined: Sep 20, 2008
  Messages: 12,155
  Likes Received: 3,633
  Trophy Points: 280
  Heshima kwako Mtambuzi,

  Kama kawaida yako unaturusha roho Al Ijumaa.

  Mkuu wangu najua wewe ni mtaalamu wa hii fani hakika sikosi mabandiko yako kila Ijumaa inapowadia tafadhali tufukulie kesi ya Babu Seya nahisi kuna mchezo mchafu.
   
 16. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #16
  May 25, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Ngongo Kesi ya Babu Seya bado naitafuta..........Sijaitia mkononi bado, nikiipata utaisoma hapa LIVE........
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
 17. ossy

  ossy JF-Expert Member

  #17
  May 25, 2012
  Joined: Apr 7, 2011
  Messages: 877
  Likes Received: 28
  Trophy Points: 45
  big ip mkuu,kwa mara nyingine tena u made my day...
  hizi siasa chafu africa zitaisha lini??? pole kwa mshikaji kwa kuangushiwa zigo la kiama..Inasikitisha kwa kweli
   
 18. Asnam

  Asnam JF-Expert Member

  #18
  May 26, 2012
  Joined: Jan 18, 2012
  Messages: 4,268
  Likes Received: 43
  Trophy Points: 135
  nimeamini kweli dunia kigeugeu hii ndo maana ya police;p-polite,o-obedient,l-loyalty,i-intelligent,c-courageous and e-eager to help.But in fact that meaning does not fit and it does not serve the purpose of morden police because they turn to serve politicians and politics rather than to perform their legal duties its amazing,i think even those Songea,Mbeya and Arusha killings was acted under political grounds and their is a need to sue the government it seems like it does'nt care how many people we have lost.BIG UP Mtambuzi we ni mzalendo keep it up
   
 19. Sajunne

  Sajunne Member

  #19
  May 26, 2012
  Joined: Jul 19, 2011
  Messages: 83
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 15
  e'e'e'heee! kisa hiki kinanikumbusha yaliyowahi kujiri tanzania kwa familia nzima kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani, inaumiza sana pale haki inapo gubikwa na ukandamizwaji.
   
 20. MESTOD

  MESTOD JF-Expert Member

  #20
  May 26, 2012
  Joined: Nov 12, 2010
  Messages: 4,641
  Likes Received: 142
  Trophy Points: 160

  Kweli, politician can do anything anytime. Ni wengi sana wametumika hivi kwa tamaa ya mtu mmoja kuwa rais.
  Too sad.
   
  Last edited by a moderator: Jan 4, 2016
Loading...