Changamoto za Kilimo

Tougher

JF-Expert Member
Jul 9, 2013
245
65
Kuna msemo unaosema usitazame na kutamani mafanikio ya mtu peke yake, tazama pia na njia alizopitia kufikia mafanikio hayo. Si kwa kilimo pekee ni katika jambo lolote lile ulifanyalo utakumbana na changamoto, mafanikio yako yatategemea mtazamo wako katika changamoto hizo na utayari wako katika kupambana nazo. Nimewaona wengi wakishindwa kuzifikia ndoto zako, lakini pia nimewaona wengi wakifanikiwa kutimiza ndoto zao.

Swali la kujiuliza ni moja; Tofauti kati ya haya makundi ya watu ni nini? Unaweza ukawa na jibu tofauti ila kwangu mimi nimepata jibu moja tu. Wanatofautiana katika mtazamo na maamuzi baada ya kukumbwa na changamoto. Kuna ambao wakianguka huinuka na kujikung'uta vumbi na kuendelea na safari, wengine hulala hapo hapo chini na kuendelea kulalamkia maumivu.

Unaweza kuwashangaa waliokata tamaa,lakini ukiangalia maumivu yao utakubaliana nao na si ajabu ukajiunga nao kuomboleza. Nataka nikutie moyo unapoona giza linazidi kuongezeka tambua kuwa kunakaribia kukucha.

Nilianza rasmi jitihada zangu za kuingia katika kilimo na ufugaji mwaka 2010. Nikaingia katika kilimo cha korosho kule Chinokole, Ruhangwa mkoani Lindi. Mwaka uliofuata nikajitanua na kufungua shamba jingine la korosho Mkuranga, Pwani. Matumaini yalikuwa juu nikaweka jitihada za kuandaa miti yangu vema ili iweze kutoa mazao bora. Matarajio yalikuwa ni kuanza kupata mazao mwaka 2014. Mbali na kilimo cha mikorosho nikaingia pia katika ufugaji wa Kuku, Mbuzi na Ng'ombe.

Hata mimi changamoto hazikuniacha mbali nimekumbana nazo na ninaendelea kukumbana nazo .Namwomba Mungu nizidi kuwa na uwezo wa kujikung'uta vumbi na kusonga;

Changamoto ya Kwanza
Changamoto ya kwanza kukutana nayo kwenye kilimo cha korosho ilikuwa ni bei. Baada ya msimu mzima wa kuandaa mikorosho yangu nilipigwa na simanzi baada ya kupatiwa bei ninayotakiwa kuuzia korosho zangu. Bei ya kilo moja ya korosho ilikuwa Shilingi za kitanzania 800/= (Mia nane tu), ikimaanisha kuwa kwa tani 3 za korosho nitapata Shilingi 2,400,000/=. Kiasi hiki ni kidogo sana ukilinganisha na gharama za uzalishaji wa zao hili.

Gharama za kusafisha shamba pamoja na upuliziaji wa dawa hufikia kiasi cha 1.2 milioni, gharama ya msimamizi wa shamba ni zaidi ya milioni 1. Hapo hujajumuisha gharama za usafirishaji, mwaka huo wa kwanza nilipata hasara. Sikukata tamaa nikaweka dhamira ya kutokuuza tena korosho ambayo haijabanguliwa.

Changamoto ya Pili
Msimu uliofuata nikadhamiria kuhakikisha korosho zangu zinauzwa sokoni baada ya kubanguliwa. Bei ya korosho iliyobanguliwa ni kubwa sana kuliko ile ya korosho ghafi. Kwa soko la mitaani (ukiwauzia vijana maarufu kama machinga) bei ya kilo moja ya korosho iliyobanguliwa ni kati ya shilingi 6,000/- hadi 12,000/- kulingana na ubora wa korosho yenyewe. Bei hii ni zaidi ya 13% ya bei ya korosho ghafi, nikatabasamu kwa kuwa niliona nuru mbele yangu. Ulipofika msimu wa mavuno mwaka 2014 korosho zangu zilionyesha dalili njema ya mazao kuwa mengi.

Lakini baada ya kuvuna kilo 100 tu shamba langu lote likaungua moto na kuteketeza korosho zote zilizokuwemo shambani. Chanzo cha moto ilikuwa ni moto toka shamba la jirani, mwenye shamba aliamua kutumia moto kusafisha shamba lake tayari kwa msimu wa kilimo. Takataka za majani na vichaka toka shambani mwake akavimwaga katika barabara inayotenga shamba langu na lake, na ndipo moto ulipopata kivuko cha kuingia shambani kwangu.

Pigo hili lilikuwa kubwa chakula hakikulika, mdomo ukawa mchachu mithili ya mtu aliyekatika dozi ya malaria. Nimejipa moyo na kuamua kulima tena ila safari hii nimewashawishi majirani wanaonizunguka kulima pia ili kuondoa vichaka mashambani kwao. Natumai kwenye korosho wakati wa mapambazuko utakuwa umefika sasa.

Changamoto ya Tatu
Kama nilivyokueleza awali nikajitosa pia katika ufugaji. Nikafunga safari hadi mkoani Morogoro nikanunua mitamba bora 4 ya ng'ombe wa maziwa, na ndama mmoja dume wa mbegu bora. Kwa kuwa nilitaka kufanya ufugaji wenye tija nikaongeza mitamba wengie 2 wa maziwa aina ya Friesian. Jumla wote ikawa ng'ombe 7, nikaajiri vijana 3 ili waweze kuwatazama ng'ombe hao shambani. Nikahakikisha naweka ufuatiliaji wa makini ili kujiridhisha utendaji wa vijana shambani, hali ilitia moyo sana.

Baada ya muda mambo yakabadilika ghafla, Vijana wakajiingiza katika ulevi na kusahahu kuhudumia mifugo. Vikatokea vifo vya ghafla kwa mifugo ambapo ng'ombe 3, kondoo 3, na mbuzi 5 walikufa ghafla. Afisa mifugo alipofanya postmoterm akaniambia ng'ombe hawa wamekufa kwa uzembe, hawakupewa maji ya kutosha. Nikaumia sana na kuamua kubadili mahali kwa kufugia na kuwarudisha karibu na nyumbani ili uangalizi uwe wa karibu.

Kwa sasa wanaendelea vizuri wamekwisha pandishwa, pia ili kufidia waliokufa na kuweka hai mipango yangu nikaongeza ng'ombe wengine 2 wenye mimba. Matumaini yamefufuka namwomba Mungu changamoto hii isijirudie tena.

Nataka nikutie moyo kuwa changamoto zipo na zitaendelea kuwepo, usikate tamaa. Sikati tamaa na nimejiingiza pia katika unenepeshaji wa ng'ombe wa nyama. Matarajio ni kuwa na ng'ombe 15 watakaokuwa tayari kuuzwa kila mwezi.

CC. Malila, Chasha
 
hongera sana mkuu kwa uzi wa ujasiri katika kupambana na umaskini, mwendo mdundo ni kujikung'uta vumbi na kusonga mbele.
 
Ya mkuu Changamoto huwa ni nyingi sana kuliko tunavyo simuliwa, Ila ni sehemu ya mafunzo na kamwe kama hujapata changamoto huwezi jifunza na hayo mafunzo ulio jifunza kutokana na changamoto usingeweza kufundishwa mahari popote pale,

Kikubwa huwa ni kuto kata tamaa, na hakuna biashara isiyo kuwa na challange na challange zako hazitafanana na challange za mtu mwingine tena ayalima korosho, make mtu mwingine anaye lima korosho anaweza kuja na changamoto zake ukashangaa mbona hazifanani? Sasa makosa tunayo fanya ni kudhania kama mtu fulani alilima au kufuga mifugoi ikafa basi na mimi mifugo itakufa, no wewe Mifugo yako inaweza isife lakini ikaibwa yote,

Mfano Tunao totolesha vifaranga unaweza shangaa mashine in Break Down na kuharibu mayai yote ndani ya mashine, ila mwingine mashine haitaharibika ila umeme utakatika , au umeme utapunguza nguvun na kuharibu.

MKUU HONGERA SANA, KIKUBWA NI KUTO KATA TAMAA KAMWE KWA SABABU THOMASI EDSON ALISHINDWA MARA ZAIDI YA ELFU TISA.
 
Ya mkuu Changamoto huwa ni nyingi sana kuliko tunavyo simuliwa, Ila ni sehemu ya mafunzo na kamwe kama hujapata changamoto huwezi jifunza na hayo mafunzo ulio jifunza kutokana na changamoto usingeweza kufundishwa mahari popote pale,

Kikubwa huwa ni kuto kata tamaa, na hakuna biashara isiyo kuwa na challange na challange zako hazitafanana na challange za mtu mwingine tena ayalima korosho, make mtu mwingine anaye lima korosho anaweza kuja na changamoto zake ukashangaa mbona hazifanani? Sasa makosa tunayo fanya ni kudhania kama mtu fulani alilima au kufuga mifugoi ikafa basi na mimi mifugo itakufa, no wewe Mifugo yako inaweza isife lakini ikaibwa yote,

Mfano Tunao totolesha vifaranga unaweza shangaa mashine in Break Down na kuharibu mayai yote ndani ya mashine, ila mwingine mashine haitaharibika ila umeme utakatika , au umeme utapunguza nguvun na kuharibu.

MKUU HONGERA SANA, KIKUBWA NI KUTO KATA TAMAA KAMWE KWA SABABU THOMASI EDSON ALISHINDWA MARA ZAIDI YA ELFU TISA.

Mkuu unazidi kutufungua macho asante sana
 
Hongera sana mkuu Tougher...
Pia nikupe pole kwa changamoto zilizokukuta, jambo la msingi ni kusimamia msimamo wako, kuwa jasiri... Lazima kitaelewela
 
Last edited by a moderator:
ni kweli huwezi kupiga hatua bila changamoto, we angalia mtoto anapotaka kutambaa au kusimama anakutana na mambo mengi ikiwemo kuanguka,kuumia lakini mwishowe anatembea vizuri
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom