JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 3,177
- 7,472
KUHUSU KUSITISHWA KWA SHAMRASHAMRA ZA KUMPONGEZA MGOMBEA URAIS MHE. DOYO HASSAN DOYO NA MGOMBEA MWENZA BI. CHAUSIKU KHATIBU, NA KUOMBA RADHI KWA USUMBUFU WOWOTE ULIOJITOKEZA
Chama cha National League for Democracy (NLD) kinapenda kutoa taarifa rasmi kwa waandishi wa habari na umma kwa ujumla, kufuatia tukio la kusitishwa kwa shughuli za shamrashamra zilizopangwa kwa ajili ya kumpokea Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chetu, Mhe. Doyo Hassan Doyo, pamoja na mgombea mwenza wake, Bi. Chausiku Khatibu tarehe 31, Agosti 2025.
Kwanza kabisa, tunapenda kuweka wazi kuwa, kama chama, tumesikitishwa sana na hali hiyo ya dharura. Hata hivyo, tunalazimika kuheshimu na kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi kama tulivyotia saini kwa hiari yetu. Kwa msingi huo, hatukuwa na budi kufuata taratibu zilizowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, hususan kanuni za uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa ratiba rasmi ya kampeni iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mgombea wa NLD hakuwa na shughuli yoyote ya kampeni jijini Dar es Salaam siku hiyo. Kwa kuzingatia hilo, na kwa kuwa sisi kama chama tunataka kuwa mfano wa kuigwa katika kuheshimu utawala wa sheria na kanuni, tuliamua kusitisha rasmi shamrashamra hizo.
Ni kweli kwamba chama kingine kilikuwa na kampeni siku hiyo katika eneo la kinondoni, lakini hilo halitoi uhalali kwa chama kingine kufanya shughuli yoyote nje ya ratiba yake rasmi, hasa Ngombea urais. Hili ni suala la kisheria, na tunatoa rai kwa vyama na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia kanuni hizi ili kuepusha mkanganyiko.
Kuhusu Mawasiliano kwa Waandishi wa Habari
Kumekuwa na madai ya baadhi ya waandishi kwamba walipokea taarifa za kusitishwa kwa shughuli hizo kwa upendeleo, wengine wakitaarifiwa kwa siri waende kwenye shughuli. Tungependa kufafanua kwamba hakuna muandishi yeyote aliyepigiwa simu kwa nia ya kupendelewa au kwa siri. Changamoto iliyojitokeza ilikuwa ni ucheleweshaji wa ujumbe mfupi (SMS) kufika kwa baadhi ya waandishi, jambo ambalo halikuwa la makusudi.
Pia, tunatambua kuwa wapo waandishi ambao bado hawajajiunga na group hili rasmi la mawasiliano ya chama. Kwa sasa, jitihada zinaendelea kuhakikisha kila muandishi anasajiliwa ipasavyo ili taarifa zote muhimu ziweze kuwafikia kwa wakati ili kuondoa changamoto kama iliojitokeza
Baadhi ya waandishi waliowasili eneo la tukio na kumkuta Mgombea Urais akiwa katika mazungumzo ya kawaida na viongozi wa chama, walielezwa kwa heshima kuhusu kusitishwa kwa shamrashamra. Kwa kuwa walikuwa tayari wamefika na hawakupokea taarifa mapema, hatukuona busara kuwaondoa, ni jambo la kibinadamu, na sisi kama chama tunaheshimu hilo.
Wito kwa Waandishi na Wanahabari Wote.
Tunaomba radhi kwa changamoto iliojitokeza lakini tunatoa wito kwa waandishi wote kuwa na subira, hekima na kutumia lugha ya kujenga katika mijadala ya kikazi. Kukosoana kwa staha ni njia bora zaidi ya kutatua changamoto kuliko kutumia lugha kali au za kejeli. Tujenge mawasiliano ya moja kwa moja, yenye misingi ya heshima na mshikamano.
Nawahimiza pia, kama kuna sintofahamu yoyote, wasiliana nami moja kwa moja kabla ya kuchukua hatua ya kusambaza ujumbe mkali. Kila mmoja wenu ana namba yangu, na nimekuwa nikiwasiliana nanyi bila ubaguzi. Tumejenga mshikamano wa kweli, tumekuwa tukishirikiana hata katika hali ngumu, ikiwemo kugawana nauli ya shilingi 200 kwenye mikutano yatu na waandishi. Hebu tuendeleze moyo huo.
Kwa masikitiko makubwa, tunalazimika pia kugusia suala la baadhi ya wanahabari kuchukua jumbe humu na kutuma jumbe hizo kwa Mgombea Urais, jambo linalosababisha mtafaruku usio wa lazima. Tafadhali tuepuke tabia hii. Chama cha NLD kinapinga tabia hii inayobeba fitina, ubaguzi na mivutano isiyo ya lazima.
Tunaomba la Radhi, Kwa dhati kabisa, tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliosababishwa na kusitishwa kwa shughuli hizo za tarehe 31. Tunaahidi kuboresha mifumo yetu ya mawasiliano ili hali kama hii isijirudie. Dhamira yetu ni njema, na nia yetu ni kuimarisha mshikamano kati ya chama, wanahabari na wadau wote wa habari bila kuleta ubaguzi.
Chama binafsi, kitaendelea kuwa na ushirikiano wa karibu nanyi, na kipo tayari kugawana chochote tulichonacho, hata kama ni kidogo kiasi gani kwa ajili ya mafanikio ya pamoja. Tupo kwenye uratibu wa kuona ni namna gani tutashirikia katika kipindi hichi cha uchaguzi bila kuathiri upande wowote kati yetu.
Asanteni kwa uvumilivu na moyo wa mshikamano.
Imetolewa na
Ombe B. Kilonzo
Afisa Habari, NLD Taifa
01 Septemba 2025