MBINU zinazosukwa na vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Edward Lowassa na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Mwigulu Nchemba ili kukidhohofisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Mwanza zimefichuka.
Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) na Mwigulu wanatajwa kutaka kutumia harambee ya kuchangia wafanyabiashara wadogo (Machinga) eneo la Makoroboi jijini hapa leo ili kufanikisha hujuma zao hizo za kisiasa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Magharibi, Peter Makere, kupitia idara yao ya usalama wamefanikiwa kunasa mikakati hiyo ya kutaka kuwadhoofisha.
Alisema kuna baadhi ya makada wa CCM wamejipanga kuhujumu kadi na baadhi ya vifaa vya uenezi vya CHADEMA kwa ajili ya kuvirudisha kwenye harambee hiyo ili kuhadaa umma kuwa chama hicho hakikubaliki.
Makere alisema kuwa mgeni rasmi wa harambee hiyo, ametajwa kuwa ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Lowassa ambaye ataongozana na makada wengine wa CCM, akiwemo Mwigulu.
CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi, imebaini mbinu chafu na ovu zinazopangwa na makada wa CCM kuhujumu kadi na vifaa vyetu. Hujuma hizi zinaandaliwa ili kuuhadaa umma eti CHADEMA haikubaliki. Vifaa hivi vimepangwa kurudishwa kwenye harambee ya kuchangia machinga itakayoongozwa na Lowassa, alisema.
Alisema kuwa CHADEMA kama chama makini na chenye dira thabiti ya kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye makucha ya CCM yaliyojaa umasikini, wanaomba umma upuuze hujuma hizo na kuendeleza mapambano ya kuiondoa madarakani 2015.
Aidha, Makere aliwaomba wamachinga na wananchi wa Jiji la Mwanza bila kujali itikadi zao wapokee fedha za CCM na waongeze ujasiri na mbinu za kuiondoa madarakani katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema muda huu ni wa msimu, kwani baadhi ya viongozi wa CCM wanaotafuta urais kwa gharama kubwa kupitia makanisa na misikitini, wameanza kujipendekeza ili waungwe mkono, hivyo ni vema Watanzania wakawaogopa watu hao kama ukoma.
CCM lazima ibadilike, iachane na siasa uchwara, hadaa, ghiliba na mazingaombwe. CHADEMA tunataka chama hicho kupitia viongozi wake kiwaambie Watanzania kimewafanyia nini katika sekta za elimu, afya, maji, ajira kwa zaidi ya miaka 50 ya uhuru, alisema Makere.
Source:Tanzania Daima Ijumaa