CHADEMA wameweza kurusha ngumi. Je, wanao uwezo wa kuhimili ngumi?

Mindi

JF-Expert Member
Apr 5, 2008
3,523
4,991
Kuna simulizi la mpiganaji ngumi maarufu, ambaye alikuwa amepigana (sio ulingoni) mara ishirini. Katika hizo, alishindwa mara moja tu. Alikuwa ni mpigaji ngumi mzuri sana. Kwa leo nitamuita Kulwa. Katika hilo pambano aliloshindwa, Kulwa alimmiliki vema mpinzani wake, na kumrushia makonde mazito na yalikuwa yanatua. Tatizo ni kwamba huyo aliyekuwa ananyeshewa mvua ya makonde, aliweza kuinuka baada ya kuanguka, na ijapo aliumizwa sana usoni na sehemu nyingine, alimudu kuendelea na pambano. Ilifika wakati huyu Kulwa akachoka kurusha ngumi. Hapo ndipo mpigwaji akageuka kuwa mpigaji. Na akaonesha kwamba anaweza pia kurusha ngumi tena nzito. Kulwa alitandikwa kwelikweli, na baada ya kuanguka mara chache na kuinuka, hakuweza tena kuinuka wala kuendelea na pambano, akawa ameshindwa.

CHADEMA wamejenga hoja nzito na watanzania wamezikubali na kuwapa kura kwa wingi. Pamoja na uchakachuaji na vurugu zingine, bado performance ya CHADEMA ni nzuri kupita yoyote iliyowahi kupatikana na chama cha upinzani katika historia ya Tanzania. Lakini mafanikio waliyopata yanakuja na gharama zake. Inabidi sasa CHADEMA ioneshe kwamba inaweza kuongoza, inaweza kujenga hoja na kuzisimamia na kuzitekeleza. Inaweza kushughulikia kero na matatizo yaliyopo ndani ya chama kwa kutumia vikao na taratibu za kichama, na kuyamaliza. Ni jambo moja kukosoa utendaji kazi wa CCM, kufichua ufisadi, kufichua maovu mbalimbali ya serikali iliyoko madarakani. Ni jambo lingine kabisa kubuni mikakati na kuitekeleza, kuwa chama kikubwa cha upinzani chenye nguvu, kinachounganisha watu wa aina mbalimbali na kada mbalimbali.

CHADEMA walirusha makombora kwa CCM, na wameiumiza. Sasa CCM ikianza kurusha makombora yake, CHADEMA itamudu kusimama na kuendelea na pambano? Au ndio itakuwa hadithi ya Kulwa? Maana hivi juzi tu mwezi wa June 2010 CHADEMA haikuwa tishio sana kwa CCM. Wala CCM haikuwa na haja ya kusuka mashambulizi dhidi ya CHADEMA. Lakini sasa hivi CCM wanayo kila sababu ya kuishambulia CHADEMA. Katika thread ya MMJ, alijenga hoja juu ya makamanda wa CCM ambao wanao uwezo wa kutumia mbinu za kijeshi. Pamoja na kwamba bado hawajaonesha umahiri wao, haifai kuwadharau. Wanayo nafasi ya kujipanga na hata kutumia majeshi ya kukodiwa ili mradi waimalize CHADEMA. Inafaa CHADEMA wajipange na kuepuka maradhi yaliyovikuta vyama vingi vya “ukombozi”, ambavyo vilikuwa mahiri kupambana na ukoloni, lakini vilipopewa nchi, vikashindwa kuwa vyama vya kujenga nchi.

Ni wakati wa kuonesha kwamba CHADEMA ni chama kikubwa kilichokomaa. Kwa mfano, tumesikia habari ya viti maalum, kwamba uteuzi ulifanywa kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa. Lakini nadhani kuna haja ya CHADEMA kuangalia kwa makini. Hii ni siasa, siyo fizikia, na ina mahitaji yake ya kisiasa, ambayo ni zaidi ya vigezo vilivyoainishwa. Mfano kama wabunge wengi wa viti maalum wanatoka sehemu moja tu ya Tanzania, unawezaje kukwepa lawama za ukabila? CHADEMA wanayo dhamana ya watanzania, na wamepewa nafasi kuonesha njia. Sio kosa kufanya kosa. Kosa ni kurudia kosa, kutorekebisha kosa, au kufumbia macho kosa. Hilo ndio kosa. Bado CHADEMA ipo kwenye honeymoon, waitumie vizuri kujipanga na kusafisha nyumba yao.
 
Back
Top Bottom