Hakuna chama ambacho kimewahi kuumizwa, kuteswa na kutoa gharama kubwa kwaajili ya ustawi wa Tanzania kama CHADEMA.
Sikuwahi kusikia kama Mwingereza aliwahi kuua viongozi wa TANU wakati wa harakati za kupigania uhuru.
CHADEMA, wakati wa utawala wa Kikwete, walirushiwa bomu lililoua watu wengi kule Arusha. Polisi waliwahi kumwua mwanachama wa CHADEMA kule Morogoro. Kiongozi wa CHADEMA kule Arusha alikatwa shingo kwa chainsew. Alphonce Mawazo, Mwenyekiti wa CHADEMA wa mkoa kule Geita, aliuawa kwa mapanga, na Serikali ya CCM ikawazuia watu wasitoe heshima za mwisho kwa Mawazo.
Pamoja na uovu wote huo, ambao hata TANU haikuwahi kufanyiwa na mkoloni mzungu, CHADEMA hawakukata tamaa, japo kwa majonzi makubwa, waliendelea na mapambano ya kutafuta haki zinazogandamizwa na watawala.
Wakati wa Utawala wa Magufuli, viongozi wa CHADEMA, magereza yakageuzwa kuwa nyumba zao, na mahakama kuwa ndiyo sebule zao. Wengine wakapotezwa mpaka leo. Kiongozi wa CHADEMA akamiminiwa risasi zaidi ya hata ngiri anavyoweza kushambuliwa, Ben Sanane akapotea, madiwani wakauawa.
Ni unyama ambao hata Mwarabu hakuwafanyia watumwa alionunua, ni ushenzi ambao hata mkoloni Mwingereza hakuwahi kuutenda, lakini CHADEMA wamefanyiwa. Ni nani katika hali ya kawaida, angeweza kuyamudu mateso na misiba hii? CHADEMA, kwa sababu ya upendo wao kwa Taifa, japo kwa taabu sana, walisonga mbele.
Wakati wa utawala wa Samia, kuingia tu, alichoona ni muhimu na cha haraka, ilikuwa ni kuwakamata na kuwasweka mahabusu mbalimbali viongozi na wanachama wa CHADEMA. Kisha wakaanza kuwatoa mahabusu taratibu. Mwishoni wakambakiza walitemtaka, Mh. Freeman Mbowe (Mungu amjalie afya njema, maisha marefu, moyo mkuu na ujasiri usiokoma), yeye wakambandika na kesi ya ugaidi. Wanaendelea naye mpaka siku watakapokuwa wameridhika.
Ni chama gani ambacho kimeipigania Tanzania ya demokrasia, haki, uhuru wa maoni na uhuru wa habari, uhuru wa Bunge, na haki ya maendeleo kwa Watanzania, kwa gharama kubwa zaidi ya CHADEMA? Hakika hakuna.
CHADEMA, wanachama na wapenzi wake wametoa damu, na maisha yao kwaajili ya Watanzania. Damu hii na maisha ya wenzetu hao, yasiende bure. Katiba mpya ni lazima, Tanzania ya haki, uhuru na demokrasia ni lazima.